Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 46
  • Mwanamke Aligusa Vazi Lake

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwanamke Aligusa Vazi Lake
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Mwanamke Aligusa Vazi Lake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Aponywa kwa Kugusa Vazi la Yesu
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Yesu Anafufua Wafu
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Tunaweza Kufufuliwa!
    Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 46

Sura 46

Mwanamke Aligusa Vazi Lake

HABARI za kurudi kwa Yesu kutoka Dekapoli zinafika Kapernaumu na umati mkubwa unakusanyika kando ya bahari kumlaki anaporudi. Bila shaka wamesikia jinsi alivyoituliza dhoruba na kumponya wanaume waliokuwa wamepagawa na roho waovu. Sasa, anapokanyaga pwani, wanakusanyika kumzunguka, wakiwa na hamu na tazamio.

Mmoja wa hao walio na hamu nyingi ya kumwona Yesu ni Yairo, ofisa msimamizi wa sinagogi. Anaanguka miguuni pa Yesu na kumsihi tena na tena: “Binti yangu mdogo yuko katika hali mahututi. Unaweza tafadhali kuja umwekelee mikono yako ili apate kupona akaishi?” Kwa kuwa yeye ndiye mtoto wake pekee na ana umri wa miaka 12 tu, hasa ni wa thamani sana kwa Yairo.

Yesu anaitikia na, umati ukiandamana pamoja naye, anaelekea kwenye kao la Yairo. Twaweza kuwazia jinsi watu hao wanavyosisimuka huku wakitazamia muujiza mwingine. Lakini mwanamke fulani katika umati ule amekaza fikira zake kwenye tatizo lake mwenyewe lililo zito sana.

Kwa muda mrefu wa miaka 12, mwanamke huyo ametaabishwa na mtiririko wa damu. Ameenda kwa daktari mmoja baada ya mwingine, akitumia pesa zake zote kwa matibabu. Lakini hajasaidiwa; bali tatizo lake limezidi tu kuwa baya.

Kama unavyoweza kuthamini, zaidi ya kumdhoofisha sana, ugonjwa wake pia unamfadhaisha na kumvunjia heshima. Kwa kawaida mtu hawezi kuzungumza waziwazi juu ya ugonjwa kama huo. Tena, chini ya Sheria ya Musa mtoko wenye kutiririka wa damu unafanya mwanamke awe asiye safi, na yeyote mwenye kumgusa yeye au mavazi yake yenye madoa ya damu anatakwa kuoga na kuwa asiye safi mpaka jioni.

Mwanamke huyo amesikia juu ya miujiza ya Yesu na sasa amemtafuta akampata. Kwa sababu ya ukosefu wake wa usafi, anajisukuma katikati ya umati huo kwa njia ya kutoonekana kadiri iwezekanavyo, akijiambia hivi: “Nikigusa tu mavazi yake ya nje nitapona.” Anapofanya hivyo, mara anahisi kwamba mtiririko wake wa damu umekauka!

“Ni nani aliyenigusa?” Lo! lazima maneno hayo ya Yesu yamshtue kama nini! Yeye angeweza kujuaje? ‘Mfunzi,’ anateta Petro, ‘umati huu unakuzunguka na kukusonga, nawe wasema, “Ni nani aliyenigusa?”’

Akitazama pande zote ili amwone mwanamke yule, Yesu anaeleza: “Mtu fulani alinigusa, kwa maana nilihisi ya kuwa nguvu zimetoka kwangu.” Kweli kweli, si mguso wa kawaida tu, kwa sababu kuponywa kunakotokea kunapunguza nguvu za Yesu.

Anapoona kwamba hakuepuka kujulikana, mwanamke huyo anasonga mbele na kuanguka mbele ya Yesu, akiwa na hofu na kutetemeka. Mbele ya watu wote anamweleza ukweli wote juu ya ugonjwa wake na jinsi ameponywa sasa hivi.

Akisukumwa na ungamo lake kamili, Yesu anamfariji kwa huruma: “Binti, imani yako imekuponya. Enda kwa amani, na uwe na afya njema utokwe na ugonjwa wako wenye kuhuzunisha.” Jinsi lilivyo jambo zuri kujua kwamba yule ambaye Mungu amechagua kuitawala dunia ni mtu mchangamfu na mwenye huruma jinsi hiyo, anayewajali watu na pia ana uwezo wa kuwasaidia! Mathayo 9:18-22; Marko 5:21-34; Luka 8:40-48; Walawi 15:25-27, NW.

▪ Yairo ni nani, na kwa nini yeye anamjia Yesu?

▪ Mwanamke mmoja ana tatizo gani, na kwa nini kumjia Yesu ili apate msaada ni jambo gumu sana kwake?

▪ Mwanamke huyo anaponywaje, naye Yesu anamfariji jinsi gani?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki