Maisha na Huduma ya Yesu
Mwanamke Aligusa Vazi Lake
HABARI za kurudi kwa Yesu kutoka Dekapoli zinafika Kapernaumu na mkutano mkubwa unakusanyika kando ya bahari ili kumlaki anaporudi. Bila shaka wamesikia jinsi alivyoituliza dhoruba na kumponya mwanamume aliyekuwa amepagawa na mashetani. Sasa, anaposhuka pwani, wanakusanyika kumzunguka, wakiwa na shauku na tazamio.
Mmoja wa wale ambao wana hamu ya kumwona Yesu ni Yairo, afisa msimamizi wa sinagogi. Anaanguka miguuni pa Yesu na kumsihi tena na tena: “Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi.” Msichana huyo ana thamani sana kwa Yairo, kwa kuwa ni mtoto wake wa pekee na ana umri wa miaka 12 tu.
Yesu anaitikia na, akifuatwa na kutano lile, anaelekea nyumbani kwa Yairo. Twaweza kuwazia jinsi watu wanasisimuka huku wakitazamia muujiza mwingine. Lakini mwanamke fulani katika kutano lile amekaza fikira zake kwenye tatizo lake mwenyewe lililo zito sana.
Kwa miaka 12 mwanamke huyo ametaabishwa na mtiririko wa damu. Ameenda kwa daktari mmoja baada ya mwingine, akitumia pesa zake zote kwa matibabu. Lakini badala ya kusaidiwa, tatizo lake limezidi tu kuwa baya.
Kama unavyoweza kuthamini, zaidi ya kumdhoofisha sana, ugonjwa wake pia unamfadhaisha na kumvunjia heshima. Kwa kawaida mtu hawezi kuzungumza waziwazi juu ya ugonjwa kama huo. Tena, chini ya sheria ya Musa mtoko wenye kutiririka wa damu unafanya mwanamke awe asiye safi, na ye yote mwenye kumgusa yeye au mavazi yake yenye madoa ya damu anatakwa kuoga na kuwa asiye safi mpaka jioni.
Mwanamke huyo amesikia juu ya miujiza ya Yesu na sasa amemtafuta akampata. Kwa sababu ya ukosefu wake wa usafi, anajisukuma katika kutano lile kwa njia ya kutoonekana kwa kiasi kiwezekanacho, akijiambia: “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.” Anapofanya hivyo, mara anahisi kwamba mtiririko wake wa damu umekauka!
“Ni nani aliyenigusa!” Bila shaka maneno hayo ya Yesu yanamgutusha sana! Angeweza kujuaje? ‘Mwalimu,’ anateta Petro, ‘makutano haya wanakuzunguka na kukusonga, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa?’
Akitazama pande zote ili amwone mwanamke yule, Yesu anaeleza: “Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.” Kwa kweli, huo si mguso wa kawaida tu, kwa sababu kuponya kunakotokea kunapunguza nguvu za Yesu.
Anapoona ya kwamba hakuepuka kujulikana, mwanamke huyo anasonga mbele na kuanguka mbele ya Yesu, akiwa na hofu na kutetemeka. Mbele ya watu wote anamweleza ukweli wote juu ya ugonjwa wake na jinsi ameponywa sasa hivi.
Akivutwa na ungamo lake kamili, Yesu anamfariji kwa huruma: “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani.” Jinsi lilivyo jambo zuri kujua kwamba yule ambaye Mungu amechagua kuitawala dunia ni mtu mchangamfu na mwenye huruma jinsi hiyo, anayewajali watu na ana uwezo wa kuwasaidia! Mathayo 9:18-22; Marko 5:21-34; Luka 8:40-48; Walawi 15:25-27.
◆ Yairo ni nani, na kwa sababu gani yeye anamjia Yesu?
◆ Mwanamke mmoja ana tatizo gani, na kwa sababu gani kumjia Yesu ili apate msaada ni jambo gumu sana kwake?’
◆ Mwanamke anaponywaje, naye Yesu anamfariji kwa njia gani?