Sura 48
Kuondoka Kwenye Kao la Yairo na Kuzuru Tena Nazareti
SIKU imekuwa yenye shughuli nyingi kwa Yesu—safari ya baharini kutoka Dekapoli, kuponya yule mwanamke mwenye mtiririko wa damu, na kufufua binti Yairo. Lakini siku haijaisha bado. Kwa wazi Yesu anapokuwa akiondoka kao la Yairo, wanaume wawili vipofu wanamfuata nyuma, wakipaaza sauti hivi: “Uturehemu sisi, Mwana wa Daudi.”
Kwa kumwita Yesu “Mwana wa Daudi,” kwa njia hiyo wanaume hao wanaonyesha imani kwamba Yesu ndiye mrithi kwenye kiti cha ufalme cha Daudi, na hivyo kwamba yeye ndiye yule Mesiya aliyeahidiwa. Hata hivyo, yaelekea Yesu anapuuza vilio vyao vya kutaka msaada, pengine ili kujaribu uendelevu wao. Lakini wanaume hao hawaachi. Wanamfuata Yesu kwenda mahali anakokaa, na anapoingia ndani ya nyumba, wanamfuata na kuingia ndani.
Humo Yesu anauliza: “Je! nyinyi mna imani kwamba mimi naweza kufanya hili?”
“Ndiyo, Bwana,” wanajibu kwa uhakika.
Hivyo, akigusa macho yao, Yesu anasema: “Na itukie kulingana na imani yenu.” Kwa ghafula wanaweza kuona! Ndipo Yesu anapowaagiza kwa mkazo hivi: “Mwone kwamba hakuna yeyote anayepata kujua hilo.” Lakini wakijawa na nderemo, wanapuuza amri ya Yesu na kuongea habari zake kote kote katika sehemu za mashambani.
Mara wanaume hao waondokapo, watu wanaleta mwanamume aliyepagawa na roho mwovu ambaye roho mwovu huyo amemnyang’anya usemi wake. Yesu afukuza roho mwovu huyo, na mara hiyo yule mwanamume aanza kuongea. Umati wastaajabia miujiza hii, wakisema: “Jambo lolote kama hili halijapata kuonwa kamwe katika Israeli.”
Mafarisayo wapo pia. Hawawezi kukana miujiza ile, lakini katika ile hali yao mbovu ya kutoamini wanarudia shtaka lao kuhusu chanzo cha kazi zenye nguvu za Yesu, wakisema: “Ni kwa nguvu za mtawala wa roho waovu kwamba yeye hufukuza roho waovu.”
Muda mfupi baada ya matukio hayo, Yesu arudi kwenye mji wa nyumbani kwake Nazareti, wakati huu akiambatana na wanafunzi wake. Mwaka mmoja hivi mapema, yeye alikuwa amezuru sinagogi na kufundisha huko. Ijapokuwa mwanzoni watu walistaajabia maneno yake yenye kupendeza, baadaye walichukizwa na fundisho lake na wakajaribu kumuua. Sasa, kwa rehema, Yesu anafanya jaribio jingine la kuwasaidia hao ambao hapo zamani walikuwa majirani wake.
Ingawa mahali pengine watu wanamwendea Yesu makundi-makundi, kwa wazi hapa hawafanyi hivyo. Basi, katika Sabato, yeye anaenda kwenye sinagogi ili akafundishe. Walio wengi wa wale wanaomsikia wanashangaa. “Mtu huyu alitoa wapi hekima hii na kazi hizi za nguvu?” wanauliza. “Je! huyu si mwana wa yule seremala? Mama yake si yule aitwaye Mariamu, na ndugu zake Yakobo na Yosefu na Simoni na Yuda? Na dada zake, je, wote hawapo pamoja nasi? Basi, mtu huyu alitoa wapi mambo haya yote?”
‘Yesu ni mwenyeji tu kama sisi,’ wanasababu. ‘Sisi tulimwona akikua, nasi twajua jamaa yake. Yeye angewezaje kuwa ndiye Mesiya?’ Kwa hiyo ujapokuwa uthibitisho wote—hekima yake kubwa na miujiza—wao wanamkataa. Kwa sababu ya kumjua kwa undani sana, hata watu wake mwenyewe wa ukoo wanajikwaa juu yake, wakisababisha Yesu kukata maneno hivi: “Nabii hakosi kuheshimiwa isipokuwa katika eneo la nyumbani kwake na miongoni mwa watu wa ukoo wake na katika nyumba yake mwenyewe.”
Kweli kweli, Yesu anastaajabia ukosefu wao wa imani. Kwa hiyo yeye hafanyi miujiza yoyote huko isipokuwa kuwekelea watu wachache wagonjwa mikono yake na kuwaponya. Mathayo 9:27-34; 13:54-58; Marko 6:1-6; Isaya 9:7, NW.
▪ Kwa kumwita Yesu “Mwana wa Daudi,” wale wanaume vipofu wanaonyesha wanaamini nini?
▪ Mafarisayo wamechagua kutoa elezo gani kwa miujiza ya Yesu?
▪ Kwa nini ni wonyesho wa rehema kwa Yesu kurudi kusaidia wale walio katika Nazareti?
▪ Yesu anapokewaje katika Nazareti, na kwa nini?