Kutazama Baadhi ya Miujiza ya Yesu
UNAPOLISIKIA neno “mwujiza,” waonaje? Waona kwamba watu wanaoishi leo hawawezi kukubali kuna miujiza? Hayo ni maoni ya watu wengi.
Walakini, Biblia Takatifu, inayokubaliwa na mamia ya mamilioni ya watu kuwa Neno la Mungu aliloliongoza kwa roho yake, yasimulia miujiza mingi sana iliyofanyizwa na uwezo wa kimungu. Kati ya miujiza hiyo, iliyofanywa na Yesu Kristo ndiyo inayotokeza zaidi.
Je! masimulizi hayo ya Biblia juu ya miujiza iliyotukia maelfu ya miaka iliyopita yanafaidi watu leo? Tukitazama baadhi ya miujiza ya Yesu twaweza kusaidika tujibu ulizo hilo.
MIUJIZA YA KUPONYA
Yesu alitenda mambo ya ajabu yasiyokuwa na kifani katika historia yote ya wanadamu, ya kuponya watu. Je! alifanya matendo hayo kukiwa na sherehe za ushirikina, kwa kutoa hotuba za kupigapiga makelele, au kwa kukusanya sadaka, kama wanavyofanya “waponyaji” wa leo? Na tuangalie lililotukia mwaka 33 W.K., wakati wa safari ya mwisho ya Yesu ya kwenda Yerusalemu:
“Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma: wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.”—Luka 17:11-14.
Mwujiza huo haukufanywa kwa kutia ndani mambo mengi ya kiajabu. Ni amri nyepesi tu iliyotolewa kwamba wanaume hao wenye ukoma wakajionyeshe kwa makuhani. Walipona walipokuwa njiani, bila ya Yesu kuwapo. Nyakati nyingine Mwana wa Mungu alifanya miujiza kama hiyo ya kuponya akiwa mbali.—Mt. 8:5-13; Yohana 4:46-54.
Mfano mmoja wa mapozo ya mwujiza yasiyokuwa yametangulia kuonekana wapatikana katika Yohana 9:1-7:
“Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake. . . . Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.”
Je! kweli Yesu aliponya upofu ambao mtu huyo alizaliwa nao? Ikiwa hakuponya, hiyo ingekuwa nafasi bora ya Mafarisayo, waliokuwa wapinzani wa Yesu wa kidini, kukana tukio lote hilo na kumwonyesha wazi kuwa mdanganyifu. Lakini ndivyo walivyofanya?
Masimulizi ya Injili yaendelea kusema: “Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona. Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa? Wazazi wake wakawajibu, wakasema. Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho.”—Yohana 9:9:18-21.
Alipoulizwa na Mafarisayo, mtu huyo aliyeanza kuona alijibu: “Hii ni ajabu! kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho! . . . Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.”—Yohana 9:30-33.
Hakuna cho chote katika masimulizi hayo kinachoonyesha ni ya uongo. Hakuna maelezo yenye kuonyesha ni hadithi tu. Bali, tumetajiwa watu, mahali na mazungumzo yaliyokuwa ya kawaida katika Palestina wakati wa karne ya kwanza W.K.
WAFU WAFUFULIWA
Kati ya miujiza yote ya Yesu, yenye kutokeza sana ni ya kufufua wafu. Biblia yasimulia visa vitatu ambapo Yesu alifufua watu. Ufufuo wa kwanza ulifanywa Naini katika Galilaya na ulihusu mwana pekee wa mwanamke mjane. Twasoma hivi:
“Na alipokaribia lango la mji [wa Naini], hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.”—Luka 7:11-15.
Vivyo hivyo, Yesu alimfufua binti wa Yairo, mmojawapo maafisa wasimamizi wa sinagogi katika Kapernaumu. (Mt. 9:18-26; Marko 5:21-43; Luka 8:40-56) Ufufuo wenye kustaajabisha sana aliofanya Yesu ni ule wa rafiki yake mkubwa Lazaro. Injili ya Yohana yausimulia hivi:
“Yesu alipofika, alimkuta [Lazaro] amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. . . . Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.” Yohana 11:17, 38-44.
Tena, masimulizi ya Biblia hayaonyeshi maneno ya kiuchawi yalitumiwa. Ni amri nyepesi tu iliyotolewa: “Lazaro, njoo huku nje.” Miujiza ya Yesu yafanyiza sehemu kubwa ya maandishi ya Injili yanayosifiwa mara nyingi kuwa “historia sahihi.” Hata hivyo, watu wengine huona si jambo la akili kuamini miujiza. Kwa sababu gani wanakuwa na maoni hayo?
MIUJIZA NA UJUZI WAKO
Watu wengi husema, “Kuona ni kuamini.” Wengine hupita kiasi katika maoni hayo. Katika mambo fulani wanakataa kuamini mambo ambayo wao wenyewe hawajayaona. Ni hekima kuwaza hivyo?
Ni jambo la maana kukumbuka kwamba, dunia yetu, sayari nyingine, na nyota zenye kufanya kazi kwa utaratibu na mapatano, zaonyesha yuko Muumba mwenye akili na uwezo usiowazika. (Rum. 1:20) Ingekuwa vigumu mno Muumba asiweze kugeuza kawaida za vitu vya asili kwa ajili ya kusudi la pekee? Mtu ye yote akikataa hilo atakuwa amekosa maarifa na atakisia-kisia mambo kipumbavu.
Ujuzi wako wafika wapi? Ni watu wachache wamepata nafasi ya kujifunza mambo moja kwa moja, wao wenyewe, wakati wa maisha yao mafupi. Kwa mfano, je! wewe mwenyewe umejionea namna mbalimbali karibu 800,000 za wadudu ambao wamegunduliwa na wanasayansi? Ikiwa waishi katika nchi ya Afrika, je! umepata kutembea Uhindini, kwenye visiwa vya bahari au mahali penginepo pa mbali, ukajionea mwenyewe watu wenye kupendeza wanaoishi huko, desturi zao za ajabu na mazingira yenye kutazamisha? Inaelekea hujatembea; lakini waamini vyepesi kwamba wadudu hao, watu hao na mahali hapo ni halisi. Kwa sababu gani? Kwa sababu wewe hukubali ushuhuda wa wengine katika mambo ya kila siku. Maarifa mengi uliyo nayo umeyapata hivyo, bila ya kujitegemea wewe mwenyewe. Je! ni jambo la akili kukataa ushuhuda wa namna iyo hiyo ati kwa sababu unahusu miujiza?
USHUHUDA USIO WA BIBLIA
Tumeona kwamba Biblia inaeleza miujiza ya Yesu kwa wepesi na unyofu. Je! ulijua kwamba ushuhuda kama huo wapatikana katika maandishi yasiyo ya Biblia, hata katika mengine yaliyoandikwa na wenye kupinga Ukristo? Angalia:
Katika The Ecclesiastical History, Eusebius wa Kaisaria aonyesha usemi mmoja wenye kupendeza wa mtu mmoja aitwaye Quadratus, aliyemwandikia Hadrian, mfalme aliyetawala Rumi kutoka mwaka 117 mpaka 138 W.K., “kuomba radhi” kwa ajili ya Ukristo. Quadratus asema: “Sikuzote kazi za Mwokozi wetu zilionekana wazi, kwa maana zilikuwa halisi. Wale walioponywa, na wale waliofufuliwa kwa wafu, walionekana, si walipokwisha kuponywa au kufufuliwa tu, bali pia muda mrefu zaidi baada ya hapo; si wakati tu alipokuwa duniani, bali pia muda mrefu baada ya kuondoka kwake: hata wengine wao wameishi mpaka nyakati zetu.”
Kwa habari ya vile watu walivyoiona miujiza iliyofanywa na Yesu, mitume kumi na wawili wake na Wakristo wengine wa karne ya kwanza W.K., kitabu Lectures on the Evidences of Christianity chasema:
“Miaka sabini ilipita kati ya kuanza kwa huduma ya Kristo na kufa kwa mtume wa mwisho. Kipindi chote hicho, karama za miujiza zinazotiliwa mashaka zilitumiwa. Sasa, kwa kuwa tendo la uongo linaporudiwa kila mara linazidi kuwa katika hatari ya kugunduliwa kwamba ni la uongo, na jinsi wakati uzidivyo kupita ndivyo inavyokuwa vigumu zaidi kuficha mpango wa hila, kuna ushuhuda unaoonyesha kwamba miujiza inayotajwa na Injili ilikuwa ya kweli, kwamba iliendelea kufanywa na kuchunguzwa muda wa miaka mingi. Lakini adui hao wakali, wasiochoka kuchunguza Ukristo sikuzote, hawakuona hata kosa moja wala udanganyifu.”
Kwa habari ya adui za Ukristo, T. H. Horne asema katika An Introduction to the Critical Study and Knowledge of the Holy Scriptures: “Wayahudi na waabudu wa miungu ya kishenzi walilazimika kuikubali [miujiza]; ingawa walisema ililetwa na vitu mbalimbali . . . Ingawa kulikuwa na vithibitisho vya karibuni visivyoweza kupingwa, Celsus, Porphyry, Hierocles, Julian, na adui wengine, walikubali ilitukia, lakini wakasema ilikuwa ya kiuchawi, walikataa kukubali kwamba aliyeifanya aliagizwa na Mungu. Lakini hata wawe walisema ni kitu gani kilichofanya itukie, kukubali kwao kwamba miujiza hiyo ilitukia, kwaonyesha bila ya wao kutaka kwamba miujiza ilikuwa na kitu fulani [kisicho na nguvu za asili].”
Miujiza ilitimiza kusudi la pekee kwa habari ya Yesu na wanafunzi wake. Mungu alitabiri kwamba Masihi aliyeahidiwa angekuwa ‘nabii kama Musa.’ (Kum. 18:15-19) Kwa kuwa Musa alifanya miujiza kuhakikisha kwamba Mungu alikuwa akimsaidia, Wayahudi walimtazamia Masihi afanye vivyo hivyo. (Kut. 4:1-9) Kwa hiyo, wakati watu “walipoiona ishara aliyoifanya [Yesu], walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.” (Yohana 6:14) Vilevile, miujiza ambayo wanafunzi wa Yesu walifanya ilihakikisha kwamba Mungu alikuwa ameondoa upendeleo wake katika taifa la Israeli wa asili akalipa kundi la Kikristo. (Mt. 21:43) Jambo hilo lilipokwisha thibitishwa, Wakristo hawakuhitajiwa tena wafanye miujiza, kwa maana ilikwisha kulingana na kusudi la kimungu.—1 Kor. 13:8-10.
KUJIFUNZA KUTOKANA NA MIUJIZA YA YESU
Je! leo watu wanaweza kufaidika kutokana na masimulizi yanayoeleza miujiza ya Yesu? Fikiria wakati alipomfufua mwana wa mwanamke mjane wa Naini. Yesu aliongozwa na nini afanye hivyo? Masimulizi ya Injili yasema: “Bwana alipomwona alimwonea huruma.” (Luka 7:13) Yesu alionyesha huruma iyo hiyo alipomfufua Lazaro. (Yohana 11:33, 35, 36) Hiyo ni sifa nzuri sana ambayo watu wote wapaswa kuiga ili wawachukue wenzao ifaavyo.—Yohana 13:15.
Masimulizi ya kuponywa kwa wenye ukoma kumi na kuponywa kwa upofu ambao mtu alizaliwa nao yafundisha watu wanaotaka kumpendeza Mungu somo jingine la maana. Wenye ukoma walipaswa kwanza watii maagizo ya Yesu wakajionyeshe kwa makuhani. (Luka 17:14) Naye kipofu alipaswa kwenda zake akanawe katika birika la Siloamu. (Yohana 9:7, 11) Kwa kuwa hakuna kati ya watu hao aliyeponywa kabla ya kutimiza matakwa hayo, walipaswa kuamini kwamba Yesu alikuwa na nia na uwezo wa kuwaponya.
Hilo latuhusuje leo? Kulingana na Biblia, miujiza ya Yesu ilionyesha mapema faida ambazo atamiminia wanadamu wote wakati wa utawala wake wa miaka elfu utakaokuwa duniani pote. Maandiko yatabiri kwamba wanadamu wataponywa magonjwa yote wakati wa utawala huo wa mileani. (Ufu. 21:4; Isa. 33:24) Vilevile, wakati huo “wote waliomo makaburini,” si watu wachache tu, “wataisikia sauti yake. Nao watatoka.” (Yohana 5:28, 29) Je! wewe unaamini kwamba ahadi hizo zitatimizwa? Je! utahakikisha imani yako kwa kujifunza Maandiko na kutii matakwa aliyotoa Mungu kwa ajili ya siku hizi?
Miujiza ya Yesu ni ya maana sana kwa watu leo. Inaonyesha wazi kwamba ahurumia wanadamu na kupendezwa wawe na hali njema, na kwamba ana uwezo wa kuondoa ole wote unaopata wanadamu, kutia na kifo. Maandishi ya Injili yanayohusu miujiza ya Yesu yaonyesha pia uhitaji wa kumtumaini kabisa Yesu Kristo kama mjumbe wa Mungu na “Wakili Mkuu wa uzima.” (Matendo 3:15, NW) Kwa kuwa miujiza ya Yesu i kati ya matukio yenye kuthibitishwa sana ya historia ya mwanadamu, kuna msingi imara wa kumwamini.