Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 129
  • Yesu Atokea Mara Zaidi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yesu Atokea Mara Zaidi
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Mitokeo Zaidi ya Yesu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Yesu Aliyefufuliwa Awatokea Wengi
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Ndani ya Chumba Kilichofungwa
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Yesu Yuko Hai!
    Biblia—Ina Ujumbe Gani?
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 129

Sura 129

Yesu Atokea Mara Zaidi

WANAFUNZI wangali wameshuka moyo. Hawafahamu maana ya lile ziara (kaburi) tupu, wala hawaamini habari za wale wanawake. Basi baadaye Jumapili, Kleopa na mwanafunzi mwingine waondoka Yerusalemu kwenda Emau, umbali wa karibu kilometa 11.

Wakiwa njiani, wanapozungumza matukio ya siku hiyo, mtu wasiyemjua ajiunga nao. “Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea?” auliza.

Wanafunzi hao wasimama, nyuso zao zikiwa na huzuni, naye Kleopa ajibu hivi: “Je! wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?” Auliza: “Mambo gani?”

“Mambo ya Yesu wa Nazareti,” wao wajibu. “Wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha [wakamtundika mtini, NW]. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli.”

Kleopa na mwandamani wake waeleza matukio ya kustaajabisha ya siku hiyo—ile habari juu ya kuonekana kusiko kwa kawaida kwa malaika na lile ziara tupu—halafu waungama kwamba wametatanishwa na maana ya mambo hayo. Mtu huyo wasiyemjua awakemea hivi: “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?” Halafu awafasiria vifungu vya kutoka maandishi matakatifu ambavyo vyamhusu Kristo.

Mwishowe wafika karibu na Emau, na mtu yule wasiyemjua afanya kana kwamba asonga mbele na safari yake. Wakitaka kusikia zaidi, wanafunzi wahimiza hivi: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha.” Basi yeye akaa apate mlo. Asemapo sala na kumega mkate na kuwapokeza, wao watambua kwamba yeye kwa kweli ni Yesu akiwa katika mwili wa kibinadamu aliouvaa. Kisha atoweka.

Sasa wao waelewa ni jinsi gani mtu huyo wasiyemjua alivyojua mengi sana! “Je! mioyo yetu haikuwaka ndani yetu,” wao wauliza, “hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?” Bila kukawia, wao wainuka na kufanya haraka wakishika njia yote kurudi Yerusalemu, ambako wawakuta mitume na wale waliokusanyika pamoja nao. Kabla Kleopa na mwandamani wake hawajaweza kusema kitu, wale wengine watoa habari hii kwa msisimuko: “Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni.” Halafu wawili hao wasimulia jinsi Yesu alivyowatokea pia. Hiyo yafanya ziwe ni mara nne katika mchana huo ambazo amewatokea wanafunzi wake tofauti-tofauti.

Ghafula Yesu atokea mara ya tano. Hata ingawa milango imefungwa kwa kufuli kwa sababu wanafunzi wawahofu Wayahudi, aingia, na kusimama mle mle katikati yao, na kusema: “Amani iwe kwenu.” Wao waogopa mno, wakiwazia kwamba wanaona roho fulani. Basi, akieleza kwamba yeye si mzuka, Yesu asema hivi: “Mbona mnafadhaika? na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni-shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.” Bado, wao hawataki kuamini.

Ili kusaidia akili zao zifahamu kwamba kwa kweli yeye ni Yesu, auliza hivi: “Mna chakula cho chote hapa?” Baada ya kukubali kipande cha samaki aliyekaangwa na kukila, asema hivi: “Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi.”

Akiendeleza kile ambacho, kwa kweli, ni sawa na funzo la Biblia pamoja nao, Yesu afundisha hivi: “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.”

Kwa sababu fulani Tomaso hayupo penye mkutano huo muhimu wa Jumapili jioni. Basi katika siku zifuatazo, wale wengine wamwambia kwa shangwe hivi: “Tumemwona Bwana.”

“Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari,” Tomaso akanusha, “na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.”

Basi, siku nane baadaye wanafunzi wanakutana tena ndani ya nyumba. Safari hii Tomaso yu pamoja nao. Ingawa milango imefungwa kwa kufuli, Yesu asimama kwa mara nyingine katikati yao na kusema: “Amani iwe kwenu.” Halafu, akimgeukia Tomaso, amwalika hivi: “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini.”

“Bwana wangu na Mungu wangu!” Tomaso apaaza sauti kwa mshangao.

‘Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki?’ Yesu auliza. “Wa heri [wenye furaha ni, NW] wale wasioona, wakasadiki.” Luka 24:11, 13-48; Yohana 20:19-29.

▪ Mtu wasiyemjua awauliza maulizo gani wanafunzi wawili walio njiani kwenda Emau?

▪ Mtu huyo wasiyemjua asema nini ambalo lafanya mioyo ya wanafunzi iwake ndani yao?

▪ Wanafunzi hao watambuaje mtu huyo wasiyemjua ni nani?

▪ Wakati Kleopa na mwandamani wake wanaporudi Yerusalemu, ni habari gani ya kusisimua wanayosikia?

▪ Ni kupi kutokea kwa Yesu kwa mara ya tano kwa wanafunzi wake, na ni nini latukia wakati huo?

▪ Ni nini latendeka siku nane baada ya Yesu kuwatokea wanafunzi wake mara ya tano, na mwishowe Tomaso asadikishwaje kwamba Yesu yu hai?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki