Maisha na Huduma ya Yesu
Mitokeo Zaidi ya Yesu
WANAFUNZI wangali wameshuka moyo. Hawaufahamu umaana wa ziara tupu, wala hawaamini habari za wale wanawake. Basi baadaye Jumapili, Kleopa na mwanafunzi mwingine waondoka Yerusalemu kwenda Emau, umbali wa karibu kilometa 11.
Njiani, wakiwa wanazungumza matukio ya siku hiyo, mgeni ajiunga nao. “Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea?” auliza.
Wanafunzi hao wasimama, nyuso zao zikiwa na huzuni, na Kleopa ajibu hivi: “Je! wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?”
“Mambo gani?” auliza.
“Mambo ya Yesu wa Nazareti,” wao wajibu. “Wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha [wakamtundika, NW]. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli.”
Kleopa na mwandamani wake waeleza matukio ya kustaajabisha ya siku hiyo—ile habari juu ya muonekano usio wa kikawaida wa malaika na lile ziara tupu—lakini ndipo waungama kwamba wametatanishwa na maana ya mambo haya. Mgeni huyo akemea hivi: “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?” Halafu awafasiria vifungu vya kutoka maandishi matakatifu ambavyo vyamhusu Kristo.
Mwishowe wafika karibu na Emau, na mgeni yule asonga kana kwamba asonge mbele na safari. Wakitaka kusikia zaidi, wanafunzi wahimiza hivi: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha.” Basi yeye akaa apate mlo. Asemapo sala na kumega mkate na kuwapokeza, wao watambua kwamba yeye kwa kweli ni Yesu akiwa katika mwili wa kibinadamu uliovaliwa. Lakini ndipo atoweka.
Sasa wao waelewa ni jinsi gani mgeni huyo alijua mengi sana! “Je! mioyo yetu haikuwaka ndani yetu,” wao wauliza, “hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?” Bila kukawia, wao wainuka na kufanya haraka wakishika njia yote kurudi Yerusalemu, ambako wawakuta mitume na wale waliokusanyika pamoja nao. Kabla Kleopa na mwandamani wake hawajaweza kusema kitu, wale wengine watoa habari hii kwa msisimuko: “Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni”! Halafu wawili hao wasimulia jinsi Yesu alivyowatokea. Hii yafanya ziwe ni mara nne katika mchana huo ambazo amewatokea wanafunzi wake tofauti-tofauti.
Hata ingawa milango imefungwa kwa kufuli kwa sababu wanafunzi wawahofu Wayahudi, kwa ghafula Yesu afanya mtokeo wake wa tano. Asimama pale pale katikati yao na kusema: “Amani iwe kwenu.” Wao waogopa mno, wakiwazia kwamba wanaona roho. Basi, akieleza kwamba yeye si mzuka, Yesu asema hivi: “Mbona mnafadhaika? na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni-shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.” Bado, wao hawataki kuamini kwa sababu kuwa kwake hai kwaonekana kuwa jambo zuri mno hata lisiwe la kweli.
Ili kuwasaidia washike akilini kwamba kwa kweli yeye ni Yesu, auliza hivi: “Mna chakula cho chote hapa?” Baada ya kukubali kipande cha samaki aliyekaangwa na kukila, aanza kuwafundisha, akisema: “Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi.”
Akiendeleza kile ambacho, kwa kweli, ni sawa na funzo la Biblia pamoja nao, Yesu afundisha hivi: “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.”
Kwa sababu fulani Tomaso hayupo penye mkutano muhimu huu wa Jumapili jioni. Basi katika siku zifuatazo, wale wengine wamwambia kwa shangwe hivi: “Tumemwona Bwana”!
“Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari,” Tomaso akanusha, “na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.”
Basi, siku nane baadaye wanafunzi wanakutana tena ndani ya nyumba. Safari hii Tomaso yu pamoja nao. Ingawa milango imefungwa kwa kufuli, Yesu asimama kwa mara nyingine katikati yao na kusema: “Amani iwe kwenu.” Halafu, akimgeukia Tomaso, amwalika hivi: “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.”
“Bwana wangu na Mungu wangu!” Tomaso apaaza mshangao.
“Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki[?],” Yesu auliza. “Wa heri [wana furaha, NW] wale wasioona, wakasadiki.” Luka 24:11, 13-48; Yohana 20:19-29.
◆ Ni maulizo gani ambayo mgeni afanya kwa wanafunzi wawili walio njiani kwenda Emau?
◆ Mgeni huyo asema nini ambalo lafanya mioyo ya wanafunzi iwake ndani yao?
◆ Wanafunzi hao watambuaje kwamba mgeni huyo ni Yesu?
◆ Wakati Kleopa na mwandamani wake warudipo Yerusalemu, ni habari gani ya kusisimua wasikiayo?
◆ Ni mtokeo gani wa tano ambao Yesu afanyia wanafunzi wake, na ni nini litukialo wakati wa mtokeo huo?
◆ Ni nini litendekalo siku nane baada ya mtokeo wa tano wa Yesu, na mwishowe Tomaso asadikije kwamba Yesu yu hai?