Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • pr seh. ya 2 kur. 6-10
  • Nani Awezaye Kutuambia?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nani Awezaye Kutuambia?
  • Ni Nini Lililo Kusudi la Uhai?
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je! Uhai Ulijitokeza kwa Nasibu?
  • Ubuni Hutaka Mbuni
  • Yale Ambayo Biblia Husema
  • “Nimeumbwa Kiajabu”
  • Jinsi Tunavyoweza Kujua Kwamba Kuna Mungu
    Je, Kweli Mungu Anatujali?
  • Vutiwa na Ubuni Jifunze Kumhusu Mbuni
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Ubuni Pasipo Mbuni?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Je! Kuna faida ya Kumwamini Mungu?
    Furaha​—Namna ya Kuipata
Pata Habari Zaidi
Ni Nini Lililo Kusudi la Uhai?
pr seh. ya 2 kur. 6-10

Sehemu ya 2

Nani Awezaye Kutuambia?

1 Ni nani awezaye kutuambia ni nini hasa lililo kusudi la uhai? Ikiwa ungemzuru mbuni wa mashine na ukamwona akibuni mashine iliyo tata ambayo hungeweza kuitambua, wewe ungeweza kujuaje kusudi la mashine hiyo? Njia iliyo bora zaidi sana kwako ingekuwa ni kumuuliza mbuni.

2 Vipi kuhusu ubuni wa ajabu tunaoona kila mahali duniani, kama vile katika viumbe vyote hai, kutia ndani chembe hai iliyo ndogo zaidi sana? Hata molekyuli na atomu ndogo sana zilizomo katika chembe hai zimebuniwa kwa njia ya ajabu na ni zenye utaratibu. Vipi pia, kuhusu ubongo wa kibinadamu uliobuniwa kiajabu? Na vipi kuhusu mfumo wa jua, na galaksi yetu ya Njia ya Maziwa, na ulimwengu wote mzima? Je! si ubuni huo wote wenye kustaajabisha mno ulihitaji Mbuni? Hapana shaka kwamba yeye aweza kutuambia kwa nini alibuni vitu hivyo.

Je! Uhai Ulijitokeza kwa Nasibu?

3 Buku The Encyclopedia Americana lilieleza kuhusu “kiwango kikubwa ajabu cha utata na utaratibu katika viumbe” na likasema: “Uchunguzi wa hali ya juu wa maua, wadudu, au mamalia huonyesha mpangilio wa visehemu ulio sawasawa kabisa kwa jinsi ya kustaajabisha.” Mstadi Mwingereza wa nyota na anga Sir Bernard Lovell, akirejezea mfanyizo wa kikemikali wa viumbe vilivyo hai, aliandika hivi: “Uwezekano wa . . . tukio la kinasibu linaloongoza kwenye mfanyizo wa molekyuli ya protini iliyo duni sana ni mdogo mno. . . . Hasa haiwezekani.”

4 Vivyo hivyo, mstadi wa nyota na anga Fred Hoyle alisema: “Muundo mzima wa biolojia sanifu bado hushikilia kwamba uhai ulitokea bila mpango. Hata hivyo wanabiolojia-kemia wanapovumbua zaidi na zaidi utata wenye kustaajabisha mno wa uhai, ni wazi kwamba uwezekano wao kuwa ulitokea kwa aksidenti ni duni sana hivi kwamba waweza kukataliwa kabisa. Uhai haungeweza kuwa ulianza kwa nasibu.”

5 Biolojia ya molekyuli, mojawapo nyanja za sayansi za hivi karibuni zaidi, ni masomo juu ya viumbe vilivyo hai kwenye kiwango cha jeni (urithi-tabia), molekyuli, na atomu. Mwanabiolojia wa molekyuli Michael Denton atoa maelezo juu ya yale ambayo yamepatikana: “Utata wa aina ya chembe sahili zaidi ijulikanayo ni mkubwa mno hivi kwamba haiwezekani kukubali kwamba kitu kama hicho kingaliweza kuwa kilitupwa pamoja kwa ghafula na namna fulani ya tukio la kiajabu, lisiloelekea kutukia hata kidogo.” “Lakini si ule utata tu wa mifumo hai ambao ni mgumu sana kufahamika, pia kuna ule ufundi wa ajabu ambao mara nyingi sana hudhihirishwa na ubuni wayo.” “Ni katika kiwango cha molekyuli ambapo . . . akili ya ubuni wa kibiolojia na ukamilifu wa malengo yaliyotimizwa huonekana wazi zaidi.”

6 Denton aendelea kusema hivi: “Kila mahali tutazamapo, iwe ni kwa kina gani tunachotazama, tunapata uzuri na ufundi unaopita mwingine wote kabisa, jambo linalodhoofisha sana wazo la nasibu. Je! kweli inaweza kukubalika kwamba mambo yaliyotukia bila mpango yangeweza kuunda vitu halisi, ambavyo sehemu ndogo zaidi yavyo—protini tendaji au jeni—ni tata sana kupita uwezo wetu wenyewe wa kuunda vitu, vitu halisi ambavyo ni kinyume kabisa cha nasibu, ambavyo ni bora sana katika kila pande kupita chochote kilichotokezwa na akili ya mwanadamu?” Yeye pia asema: “Kati ya chembe hai na mfumo usio wa kibiolojia wenye utaratibu wa juu zaidi, kama vile fuwele au chembe ya theluji, kuna pengo kubwa sana na pana kwa kadiri iwezekanayo kuwaziwa.” Na profesa wa fizikia, Chet Raymo, asema: “Ninavutiwa sana . . . Kila molekyuli inaonekana ilibuniwa kimuujiza kwa ajili ya kazi yayo.”

7 Mwanabiolojia wa molekyuli Denton amalizia kwamba “wale ambao bado huunga mkono kishupavu kwamba uhalisi huu wote mpya ni tokeo la nasibu tu” wanaamini ngano. Kwa kweli, yeye aita nadharia ya Darwini kuhusu viumbe hai kutokea kwa nasibu kuwa “ngano kubwa ya nadharia ya asili ya ulimwengu wote mzima ya karne ya ishirini.”

Ubuni Hutaka Mbuni

8 Uwezekano wa kwamba vitu visivyo na uhai vingeweza kuwa hai kwa nasibu, kwa aksidenti isiyo na mpango wowote, ni duni sana hivi kwamba haiwezekani. La, viumbe hai vyote duniani vilivyobuniwa kiajabu havingeweza kuwa vilitokea kwa aksidenti, kwa kuwa kila kitu ambacho kimebuniwa lazima kiwe na mbuni. Je! unajua juu ya vitu vyovyote visivyopata kubuniwa? Hakuna hata kimoja. Na kadiri ubuni ulivyo tata zaidi, ndivyo mbuni alivyo mwenye uwezo zaidi.

9 Labda tutoe kielezi cha jambo hili hivi: Tunapoona mchoro, tunaukubali kuwa uthibitisho kwamba kuna mchoraji. Tunaposoma kitabu, tunakubali kwamba kuna mtungaji. Tunapoona nyumba, tunakubali kwamba kuna mjenzi. Tunapoona taa za kuongoza magari barabarani, tunajua kwamba kuna baraza la kutekeleza sheria. Vitu hivyo vyote vilifanyizwa kwa kusudi fulani na wale waliovifanyiza. Na ingawa huenda tusielewe kila kitu kuhusu watu waliovibuni, hatuna shaka kwamba watu hao wako.

10 Vivyo hivyo, uthibitisho wa kuwako kwa Mbuni Mkuu Zaidi Sana waweza kuonwa katika ubuni, utaratibu, na utata wa viumbe hai duniani. Vyote vinaonyesha kwamba kuna Akili Kuu Zaidi ya Zote. Ndivyo ilivyo na ubuni, utaratibu, na utata wa ulimwengu wote mzima pamoja na mabilioni ya magalaksi yao, kila moja ikiwa na mabilioni ya nyota. Na maumbo yote ya kimbingu hudhibitiwa na sheria sahihi, kama zile za mwendo, joto, nuru, sauti, sumakuumeme, na nguvu za uvutano. Je! kunaweza kuwa na sheria bila mfanyiza sheria? Mwanasayansi wa roketi Dakt. Wernher von Braun alisema hivi: “Sheria za asili za ulimwengu wote mzima ni sahihi kabisa hata kwamba hatutatiziki kuunda chombo cha angani kiruke kwenda kwenye mwezi na twaweza kupangia mruko huo wakati kwa usahihi kabisa wa kisehemu cha sekunde. Lazima sheria hizo ziwe ziliwekwa na mtu fulani.”

11 Ni kweli, hatuwezi kumwona Mbuni Mkuu Zaidi Sana na Mpaji-Sheria kwa macho yetu halisi. Lakini je, sisi hukana kuwako kwa vitu kama vile nguvu za uvutano, usumaku, umeme, au mawimbi ya redio eti kwa sababu tu hatuwezi kuviona? La, hatukani, kwa vile twaweza kuona matokeo yavyo. Basi kwa nini tukane kuwako kwa Mbuni Mkuu Zaidi Sana na Mpaji-Sheria eti kwa sababu tu hatuwezi kumwona, ilhali tunaweza kuona matokeo ya kazi yake ya ajabu?

12 Paul Davies, profesa wa fizikia, amalizia kwamba kuwako kwa mwanadamu si tukio tu la ajali. Yeye asema hivi: “Kwelikweli sisi twakusudiwa kuwa hapa.” Na anasema hivi kuhusu ulimwengu wote mzima: “Kupitia kazi yangu ya sayansi, nimekuja kuamini kwa dhati zaidi na zaidi kwamba ulimwengu wote mzima tunaoona umewekwa pamoja kwa ufundi unaostaajabisha sana hivi kwamba siwezi kuamini kuwa jambo tu lisilo la akili. Kwangu mimi, inaonekana ni lazima kuwe na ufafanuzi wenye kina kirefu zaidi.”

13 Hivyo, uthibitisho unatuambia kwamba ulimwengu wote mzima, dunia, na viumbe hai duniani havingaliweza kuwa vilitokea kwa nasibu tu. Vyote vinatoa ushuhuda wa ukimya juu ya Muumba mwenye nguvu, aliye na akili ya hali ya juu sana.

Yale Ambayo Biblia Husema

14 Biblia, kitabu cha zamani zaidi cha ainabinadamu, hutoa mkataa uo huo. Kwa kielelezo, katika kitabu cha Biblia cha Waebrania, kilichoandikwa na mtume Paulo, tunaambiwa hivi: “Kila nyumba hujengwa na mjenzi fulani—na Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.” (Waebrania 3:4, Habari Njema kwa Watu Wote) Kitabu cha mwisho cha Biblia, kilichoandikwa na mtume Yohana, pia husema hivi: “Umestahili wewe, Bwana [Yehova, New World Translation] wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.”—Ufunuo 4:11.

15 Biblia huonyesha kwamba ingawa Mungu hawezi kuonwa, tunaweza kujua yeye ni Mungu wa aina gani kwa yale ambayo ameumba. Hiyo husema hivi: “Sifa zisizoonekana [za Muumba], yaani nguvu na uabudiwa wake wa milele, zimedhihirika kwenye jicho la ufikiri, tangu wakati ule ulimwengu ulipoanza, katika mambo ambayo amefanya.”—Warumi 1:20, The New English Bible.

16 Kwa hiyo Biblia hutupeleka sisi kutoka tokeo hadi kwenye kisababishi. Tokeo—vitu vyenye kustaajabisha mno vilivyofanywa—ni uthibitisho wa Msababishi mwenye nguvu, na mwenye akili: Mungu. Pia, tunaweza kushukuru kwamba yeye hawezi kuonekana, kwa kuwa yeye akiwa Muumba wa ulimwengu wote mzima, bila shaka ana nguvu kubwa mno hivi kwamba wanadamu wenye nyama na damu hawawezi kutarajia kumwona waendelee kuishi. Na hivyo ndivyo Biblia husema hasa: “Mwanadamu hataniona [mimi Mungu] akaishi.”—Kutoka 33:20.

17 Wazo juu ya Mbuni Mkubwa, Mtu Mkuu Zaidi Sana—Mungu—lapaswa kuwa la maana sana kwetu. Ikiwa tulifanywa na Muumba, basi kwa hakika lazima awe alikuwa na sababu, kusudi fulani, katika kutuumba sisi. Ikiwa tuliumbwa ili tuwe na kusudi maishani, basi kuna sababu ya kutumaini kwamba mambo yatakuwa bora zaidi kwetu wakati ujao. Ama sivyo, twaishi tu na kufa bila tumaini. Kwa hiyo ni jambo la maana sana kwamba tupate kujua kusudi la Mungu kwetu sisi. Ndipo tunaweza kuchagua kama tunataka kuishi kupatana na kusudi hilo au la.

18 Pia, Biblia husema kwamba Muumba ni Mungu mwenye upendo ambaye hujali sana juu yetu. Mtume Petro alisema hivi: “Yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (1 Petro 5:7; ona pia Yohana 3:16 na 1 Yohana 4:8, 16.) Njia mojawapo ambayo twaweza kuona ni kwa kadiri gani Mungu hujali ni kwa kufikiria njia ya ajabu ambayo kwa hiyo ametufanya sisi, kiakili na kimwili.

“Nimeumbwa Kiajabu”

19 Katika Biblia mtunga zaburi Daudi alikiri hivi: “Kwa njia yenye kutia hofu mimi nimeumbwa kiajabu.” (Zaburi 139:14, NW) Kwa hakika, hiyo ndiyo kweli, kwa kuwa akili na mwili wa binadamu zilibuniwa kwa njia ya kustaajabisha na yule aliye Mbuni Mkuu Zaidi Sana.

20 Mathalani, ubongo wako ni tata zaidi ya kompyuta yoyote. Buku The New Encyclopœdia Britannica lasema hivi: “Mpitisho wa habari katika mfumo wa neva ni wenye utata zaidi ya mifumo mikubwa zaidi ya mawasiliano ya simu; uwezo wa ubongo wa kibinadamu kutatua matatizo hupita kwa mbali uwezo wa kompyuta zenye nguvu zaidi.”

21 Mamia ya mamilioni ya habari na taswira za akilini huwekwa katika ubongo wako, lakini hiyo si ghala tu la habari. Kwa huo unaweza kujifunza jinsi ya kupiga mbinja, kuoka mkate, kusema lugha za kigeni, kutumia kompyuta, au kupurusha eropleni. Unaweza kuwazia jinsi likizo litakavyokuwa au jinsi tunda litakavyokuwa na ladha tamu. Unaweza kuchanganua na kufanyiza mambo. Unaweza pia kupanga mambo, kuthamini, kupenda, na kuhusianisha mawazo yako ya kale, ya sasa, na ya wakati ujao. Kwa kuwa sisi binadamu hatuwezi kubuni kitu kama vile ubongo wa kibinadamu wenye kustaajabisha, basi bila shaka Yule aliyeubuni ana hekima na uwezo unaopita kwa mbali ule wa binadamu yeyote.

22 Kuhusu ubongo, wanasayansi wanakiri hivi: “Hatujui hata kidogo jinsi kazi hizi zinavyotimizwa na chombo hiki kilichojawa na maajabu, ambacho kilitengenezwa kwa ufundi mwingi sana, kwa utaratibu na kwa njia ya kustaajabisha sana. . . . Huenda wanadamu wasiweze hata siku moja kutatua mambo mbalimbali yenye kuwatatanisha yanayotokezwa na ubongo.” (Scientific American) Na profesa wa fizikia Raymo asema hivi: “Kusema kweli, bado sisi hatujui mengi kuhusu jinsi ubongo wa kibinadamu huweka habari, au jinsi unavyoweza kukumbuka mambo yanapotakwa. . . . Kuna chembe za neva zipatazo bilioni mia moja katika ubongo wa binadamu. Kila chembe huwasiliana, kupitia sainapsi zilizo kama mti, pamoja na maelfu ya chembe nyinginezo. Uwezekano wa kuungana pamoja ni wenye kutatana kwa njia yenye kustaajabisha.”

23 Macho yako ni yenye usahihi kabisa na yenye kubadilikana zaidi ya kamera yoyote; kwa kweli, hayo ni kamera zinazojiendesha zenyewe, zikijirekebisha zenyewe ili kuona vizuri, na kuona sinema za rangi-rangi. Masikio yako yaweza kusikia aina mbalimbali za sauti na yakupatie uwezo wa kwenda utakako na ujisawazishe. Moyo wako ni pampu yenye uwezo ambao wahandisi walio bora kabisa hawajaweza kufanyiza namna yayo. Pia sehemu nyinginezo za mwili ni za ajabu: pua yako, ulimi, na mikono, pamoja na mifumo yako ya mzunguko wa damu na usagaji chakula, kutaja sehemu chache tu.

24 Hivyo, mhandisi aliyeajiriwa kubuni na kujenga kompyuta kubwa alitoa sababu hivi: “Ikiwa kompyuta yangu ilihitaji mbuni, vipi basi kuhusu ile mashine tata ya kifizikia-kemia-biolojia ambayo ni mwili wangu wa kibinadamu—ambao nao ni sehemu duni mno ya ulimwengu wote mzima wenye utaratibu ambao karibu hauna mpaka?”

25 Kama vile tu ambavyo watu huwa na kusudi akilini wanapotengeneza eropleni, kompyuta, baiskeli, na vitu vingine, ndivyo lazima Mbuni wa ubongo na mwili wa binadamu awe alikuwa na kusudi katika kutubuni sisi. Na Mbuni huyo lazima awe mwenye hekima inayopita ile ya binadamu, kwa kuwa hakuna yeyote kati yetu anayeweza kufanyiza namna inayofanana na ubuni wake. Basi ni jambo la akili kwamba, Yeye ndiye anayeweza kutuambia kwa nini alitubuni sisi, kwa nini alituweka duniani, na kule tunakoelekea.

26 Tukiisha kujua mambo hayo, basi ubongo na mwili wetu wa ajabu ambao Mungu alitupatia vyaweza kutumiwa katika kutimiza kusudi letu maishani. Lakini ni wapi tunakoweza kujifunza juu ya makusudi yake? Ni wapi anakotupatia habari hiyo?

[Maswali ya Funzo]

1, 2. Ni njia gani bora zaidi ya kujua kusudi la kitu kinachobuniwa?

3, 4. Kuna uwezekano gani kwamba uhai ulianza kwa nasibu?

5-7. Biolojia ya molekyuli inathibitishaje kwamba viumbe hai haviwezi kutokea kwa nasibu?

8, 9. Toa kielezi kuonyesha kwamba kila kitu kilichobuniwa lazima kiwe na mbuni.

10. Ni uthibitisho gani wa Mbuni Mkuu Zaidi Sana unaoweza kuonwa?

11. Kwa nini hatupaswi kukana kuwako kwa Mbuni Mkuu Zaidi Sana kwa sababu tu hatuwezi kumwona?

12, 13. Uthibitisho wasema nini juu ya kuwako kwa Muumba?

14. Biblia hutoa mkataa gani juu ya Muumba?

15. Tunaweza kujuaje baadhi ya sifa za Mungu?

16. Kwa nini twapaswa kufurahi kwamba binadamu hawawezi kumwona Mungu?

17, 18. Kwa nini wazo juu ya Muumba liwe la maana kwetu?

19. Ni kweli gani ambayo mtunga zaburi Daudi aleta kwenye uangalifu wetu?

20. Ensaiklopidia moja hufafanuaje ubongo wa binadamu?

21. Tunapoona yale ambayo ubongo waweza kufanya, twapaswa kutoa mkataa gani?

22. Wanasayansi hukiri nini juu ya ubongo wa binadamu?

23, 24. Taja majina ya baadhi ya sehemu za mwili zilizobuniwa kiajabu, na mhandisi mmoja alitoa maelezo gani?

25, 26. Mbuni Mkubwa anapaswa aweze kutuambia nini?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Njia bora kabisa ya kujua kwa nini kitu fulani kilibuniwa ni kumuuliza mbuni

[Picha katika ukurasa wa 8]

Utata na ubuni wa viumbe hai waweza kuonekana katika molekyuli DNA

[Picha katika ukurasa wa 9]

“Uwezo wa ubongo wa kibinadamu kutatua matatizo hupita kwa mbali uwezo wa kompyuta zenye nguvu zaidi”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki