Somo la 3
Yesu Kristo Ni Nani?
Kwa nini Yesu anaitwa Mwana “mzaliwa wa kwanza” wa Mungu? (1)
Kwa nini anaitwa “Neno”? (1)
Kwa nini Yesu alikuja duniani akiwa binadamu? (2-4)
Kwa nini alifanya miujiza? (5)
Yesu atafanya nini wakati ujao ulio karibu? (6)
1. Yesu aliishi mbinguni akiwa mtu wa roho kabla ya kuja duniani. Alikuwa uumbaji wa kwanza wa Mungu, na kwa hiyo anaitwa Mwana “mzaliwa wa kwanza” wa Mungu. (Wakolosai 1:15; Ufunuo 3:14) Yesu ndiye Mwana pekee ambaye Mungu aliumba mwenyewe. Yehova alimtumia Yesu kabla hajawa binadamu, kuwa “stadi [wake] wa kazi” katika kuumba vitu vingine vyote mbinguni na duniani. (Mithali 8:22-31; Wakolosai 1:16, 17) Mungu alimtumia pia kuwa msemaji Wake mkuu. Hiyo ndiyo sababu Yesu anaitwa “Neno.”—Yohana 1:1-3; Ufunuo 19:13.
2. Mungu alimtuma Mwana Wake duniani kwa kuhamisha uhai wake hadi katika tumbo la uzazi la Mariamu. Kwa hiyo Yesu hakuwa na baba wa kibinadamu. Hiyo ndiyo sababu yeye hakurithi dhambi wala kutokamilika kokote. Mungu alimtuma Yesu duniani kwa sababu tatu: (1) Kutufundisha kweli kumhusu Mungu (Yohana 18:37), (2) kudumisha uaminifu mkamilifu wa maadili, akitutolea sisi kigezo cha kufuata (1 Petro 2:21), na (3) kudhabihu uhai wake ili kutuweka sisi huru kutoka katika dhambi na kifo. Kwa nini hilo lilihitajiwa?—Mathayo 20:28.
3. Kwa kutotii amri ya Mungu, binadamu wa kwanza, Adamu, alifanya ile ambayo Biblia huita “dhambi.” Kwa hiyo Mungu alimhukumia kifo. (Mwanzo 3:17-19) Yeye hakufikia tena viwango vya Mungu, kwa hiyo hakuwa mkamilifu tena. Polepole alizeeka akafa. Adamu alipitisha dhambi kwa watoto wake wote. Hiyo ndiyo sababu sisi pia tunazeeka, tunakuwa wagonjwa, na tunakufa. Wanadamu wangeweza kuokolewaje?—Warumi 3:23; 5:12.
4. Yesu alikuwa binadamu mkamilifu kama vile Adamu. Lakini tofauti na Adamu, Yesu alikuwa mtiifu kikamilifu kwa Mungu chini ya hata lile jaribu kubwa kupita yote. Kwa hiyo yeye angeweza kudhabihu uhai wake mkamilifu wa kibinadamu ili kulipia dhambi ya Adamu. Hicho ndicho kinachorejezewa na Biblia kuwa “fidia.” Hivyo watoto wa Adamu wangeweza kuachiliwa kutoka katika hukumu ya kifo. Wote wawekao imani yao katika Yesu waweza kusamehewa dhambi zao na kupokea uhai udumuo milele.—1 Timotheo 2:5, 6; Yohana 3:16; Warumi 5:18, 19.
5. Alipokuwa duniani Yesu aliponya wagonjwa, alilisha wenye njaa, akatuliza dhoruba. Hata aliwafufua wafu. Ni kwa nini alifanya miujiza? (1) Alihisi sikitiko kwa ajili ya watu waliokuwa wakiteseka, naye akataka kuwasaidia. (2) Miujiza yake ilithibitisha kwamba alikuwa Mwana wa Mungu. (3) Ilionyesha yale ambayo atawafanyia wanadamu watiifu anapotawala akiwa Mfalme juu ya dunia.—Mathayo 14:14; Marko 2:10-12; Yohana 5:28, 29.
6. Yesu alikufa akafufuliwa na Mungu akiwa kiumbe cha roho, naye akarudi mbinguni. (1 Petro 3:18) Tangu wakati huo, Mungu amemfanya awe Mfalme. Karibuni Yesu ataondoa uovu na kuteseka kote kutoka dunia hii.—Zaburi 37:9-11; Mithali 2:21, 22.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Huduma ya Yesu ilitia ndani, kufundisha, kufanya miujiza, na hata kutoa uhai wake kwa ajili yetu