Sura ya 2
Baba Mwenye Wana Waasi
1, 2. Eleza jinsi ambavyo Yehova amekuja kuwa na wana waasi.
ALIWALEA watoto wake kwa njia nzuri, kawaida ya mzazi yeyote mwenye upendo. Kwa miaka mingi alihakikisha kuwa wanapata chakula, mavazi, na makao. Aliwatia nidhamu ilipohitajika. Lakini adhabu yao haikupita kiasi kamwe; sikuzote ilitolewa “kwa kadiri inayofaa.” (Yeremia 30:11, NW) Basi twaweza kuwazia tu uchungu anaohisi baba huyu mwenye upendo alazimikapo kutoa taarifa hii: “Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi.”—Isaya 1:2b.
2 Wana waasi wanaorejezewa hapa ni watu wa Yuda, na Yehova Mungu ndiye baba anayesikitika. Ni jambo lenye kuhuzunisha kama nini! Yehova amewalisha Wayudea na kuwainua juu ya mataifa. “Nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa hariri,” awakumbusha baadaye kupitia nabii Ezekieli. (Ezekieli 16:10) Hata hivyo, kwa jumla, watu wa Yuda hawathamini yale ambayo Yehova amewafanyia. Badala yake, wanaasi.
3. Kwa nini Yehova aziita mbingu na dunia zishuhudie uasi wa Yuda?
3 Kwa kufaa basi, maneno ya Yehova kwa wanawe waasi yaanza kwa taarifa hii: “Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena.” (Isaya 1:2a) Karne nyingi mapema mbingu na dunia zilisikia kitamathali Waisraeli wakipokea maonyo ya wazi kuhusu matokeo ya kutotii. Musa alisema: “Nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki.” (Kumbukumbu la Torati 4:26) Sasa katika siku ya Isaya, Yehova aziita mbingu zisizoonekana na dunia inayoonekana zishuhudie uasi wa Yuda.
4. Yehova aamua kujidhihirishaje kwa Yuda?
4 Hali hiyo mbaya sana yahitaji kukabiliwa moja kwa moja. Ingawa hivyo, yapasa izingatiwe—nayo yasisimua—kuwa hata katika hali hizi mbaya mno Yehova ajidhihirisha kwa Yuda kuwa mzazi mwenye upendo badala ya mmilikaji ambaye amewanunua. Kwa kweli, Yehova anawasihi watu wake wafikirie jambo hilo kwa maoni ya baba anayehangaikia wanawe waliopotoka. Labda hata wazazi fulani katika Yuda wamepatwa na hali kama hiyo, nao wachochewa na kielezi hicho. Kwa vyovyote vile, Yehova anakaribia kuleta mashtaka yake juu ya Yuda.
Wanyama Wasio na Akili Ni Afadhali
5. Kinyume cha Israeli, ng’ombe na punda huonyeshaje hali fulani ya uaminifu?
5 Kupitia Isaya, Yehova asema: “Ng’ombe amjua bwana wake, na punda ajua kibanda cha bwana wake; bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.” (Isaya 1:3)a Watu wanaoishi Mashariki ya Kati wanawafahamu ng’ombe na punda, wanyama wavutao mizigo. Kwa hakika, Wayudea hawangeweza kukanusha kwamba hata wanyama hao wa hali ya chini huonyesha hali fulani ya uaminifu, ufahamu wenye kina kwamba wao ni mali ya bwana-mkubwa fulani. Kuhusu hilo, fikiria aliloshuhudia mtafiti fulani wa Biblia jioni moja katika jiji moja huko Mashariki ya Kati: “Mara kundi lilipoingia ndani ya kuta, likaanza kutawanyika. Kila fahali alimjua mwenyewe kikamilifu na njia ya kwenda nyumbani kwake, wala hakutatanishwa hata kidogo na vijia vingi vilivyopindika-pindika. Punda naye alienda moja kwa moja hadi mlangoni, na kuingia katika ‘hori ya bwana-mkubwa wake.’”
6. Watu wa Yuda wameshindwaje kutenda kwa kufikiri?
6 Kwa kuwa mandhari kama hizo zajulikana katika siku ya Isaya, lengo la ujumbe wa Yehova ni wazi: Iwapo hata mnyama asiye na akili hutambua bwana-mkubwa wake na hori yake, mbona watu wa Yuda wamwache Yehova? Kwa kweli “hawafikiri.” Ni kana kwamba hawafahamu kwamba ufanisi wao na hasa uhai wao humtegemea Yehova. Kwa kweli Yehova anawaonyesha rehema yake kwa kuendelea kuwaita Wayudea “watu wangu”!
7. Twaweza kuonyesha uthamini wetu kwa maandalizi ya Yehova katika njia zipi?
7 Hatungependa kamwe kutenda bila ufahamu kwa kukosa kuthamini yote ambayo Yehova ametufanyia! Badala yake, twapaswa kumwiga mtunga-zaburi Daudi, aliyesema: “Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.” (Zaburi 9:1) Kuendelea kutwaa ujuzi juu ya Yehova kutatutia moyo kwa habari hii, kwa maana Biblia yataarifu kwamba “kumjua Mtakatifu ni ufahamu.” (Mithali 9:10) Kutafakari kila siku juu ya baraka za Yehova kutatusaidia kuwa wenye shukrani wala si kumpuuza Baba yetu wa mbinguni. (Wakolosai 3:15) “Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza,” asema Yehova, “naye autengenezaye mwenendo wake, nitamwonyesha wokovu wa Mungu.”—Zaburi 50:23.
Dharau Kubwa kwa “Mtakatifu wa Israeli”
8. Kwa nini watu wa Yuda waweza kuitwa “taifa lenye dhambi”?
8 Isaya aendelea na ujumbe wake wenye maneno makali kwa taifa la Yuda: “Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.” (Isaya 1:4) Matendo maovu yaweza kuongezeka na kuwa mzigo wenye kulemea sana. Katika siku ya Abrahamu Yehova alizifafanua dhambi za Sodoma na Gomora kuwa “nzito sana.” (Mwanzo 18:20, Zaire Swahili Bible) Hali kama hiyo sasa ni dhahiri kwa watu wa Yuda, kwa maana Isaya asema kwamba ‘wanauchukua mzigo wa uovu.’ Kwa kuongezea, awaita “wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu.” Naam, Wayudea ni kama watoto wahalifu. “Wamefarakana [na Baba yao] na kurudi nyuma.”
9. Usemi “Mtakatifu wa Israeli” una umuhimu gani?
9 Watu wa Yuda wanaonyesha dharau kubwa kwa “Mtakatifu wa Israeli” kwa mwenendo wao mpotovu. Usemi huu unaopatikana mara 25 katika kitabu cha Isaya una umuhimu gani? Kuwa mtakatifu kwamaanisha kuwa safi na mwenye kutakata. Yehova ni mtakatifu kwa kadiri kuu. (Ufunuo 4:8) Waisraeli wakumbushwa jambo hilo kila mara wayaonapo maneno yaliyoandikwa katika bamba la dhahabu lenye kung’aa kwenye kilemba cha kuhani wa cheo cha juu: “Utakatifu ni wa Yehova.” (Kutoka 39:30, NW) Basi, kwa kumrejezea Yehova kuwa “Mtakatifu wa Israeli,” Isaya akazia uzito wa dhambi ya Yuda. Kwani, waasi hawa wanakiuka moja kwa moja amri hii waliyopewa babu zao: “Takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu”!—Mambo ya Walawi 11:44.
10. Twaweza kuepukaje kumdharau “Mtakatifu wa Israeli”?
10 Lazima Wakristo leo waepuke kwa hali na mali kufuata kielelezo cha Yuda cha kumdharau “Mtakatifu wa Israeli.” Ni lazima wauige utakatifu wa Yehova. (1 Petro 1:15, 16) Nao wahitaji ‘kuuchukia uovu.’ (Zaburi 97:10) Mazoea machafu kama vile ukosefu wa adili katika ngono, ibada ya sanamu, wizi, na ulevi yaweza kufisidi kutaniko la Kikristo. Hiyo ndiyo sababu wale wanaokataa kuyaacha mambo hayo hutengwa na ushirika wa kutaniko. Hatimaye, wale wanaofuata mwenendo mchafu bila kutubu hawatakuwa miongoni mwa wale watakaopata shangwe ya baraka za serikali ya Ufalme wa Mungu. Kwa kweli, kazi zote mbovu kama hizo ni dharau kubwa kwa “Mtakatifu wa Israeli.”—Waroma 1:26, 27; 1 Wakorintho 5:6-11; 6:9, 10.
Wagonjwa Tokea Kichwa Mpaka Wayo
11, 12. (a) Fafanua hali mbaya ya Yuda. (b) Kwa nini hatupaswi kusikitikia Yuda?
11 Kisha Isaya ajitahidi kusababu na watu wa Yuda kwa kuwatajia hali yao dhaifu. Asema hivi: “Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi?” Kwa maneno mengine Isaya anawauliza: ‘Kwani hamjateseka vya kutosha? Kwa nini mjiletee madhara zaidi kwa kuendelea kuasi?’ Isaya aendelea: “Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia. Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake.” (Isaya 1:5, 6a) Yuda iko katika hali yenye kuchukiza, ya ugonjwa—ugonjwa wa kiroho tangu kichwa hata wayo. Dalili yenye kuhuzunisha kama nini!
12 Je, tuisikitikie Yuda? Hasha! Karne kadhaa mapema taifa zima la Israeli lilionywa ipasavyo juu ya adhabu ya kutotii. Waliambiwa hivi kwa sehemu: “BWANA atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.” (Kumbukumbu la Torati 28:35) Kitamathali, Yuda sasa inapata matokeo hayohayo ya mwenendo wake wa ukaidi. Hayo yote yangeweza kuepukwa iwapo tu watu wa Yuda wangemtii Yehova.
13, 14. (a) Yuda imepata majeraha gani? (b) Je, mateso ya Yuda huifanya iache mwenendo wake wa uasi?
13 Isaya aendelea kufafanua hali yenye kusikitisha ya Yuda: “Bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.” (Isaya 1:6b) Hapa nabii huyo arejezea aina tatu ya majeraha: majeraha (kukatwa, kama vile kwa upanga au kisu), machubuko (uvimbe unaosababishwa na pigo), na vidonda (vidonda vya hivi karibuni, vilivyo wazi na vinavyoonekana kuwa haviwezi kupona). Wazo linalotolewa ni la mtu ambaye ameadhibiwa vikali kwa njia zote ziwezekanazo, na mwili wake wote umepata madhara. Hakika Yuda iko katika hali ya kukata tamaa.
14 Je, hali yenye taabu ya Yuda huifanya imrudie Yehova? La! Yuda ni kama mwasi anayetajwa katika Mithali 29:1: “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, atavunjika ghafula, wala hapati dawa.” Yaonekana taifa hilo haliwezi kupona. Kama asemavyo Isaya, majeraha yake ‘hayakufungwa, hayakuzongwa-zongwa wala kulainishwa kwa mafuta.’b Kwa njia fulani, Yuda yafanana na kidonda kilicho wazi, kisichofungwa bendeji, na kilichoenea kotekote.
15. Twaweza kujilindaje dhidi ya ugonjwa wa kiroho?
15 Twapaswa kujifunza kutokana na Yuda, na tujilinde dhidi ya ugonjwa wa kiroho. Sawa na ugonjwa wa kimwili, ugonjwa huo waweza kudhuru yeyote kati yetu. Kwani, ni nani kati yetu asiyeweza kupatwa na tamaa za kimwili? Pupa na tamaa ya kupata raha kupita kiasi zaweza kusitawi mioyoni mwetu. Basi twahitaji kujizoeza ‘kukirihi lililo ovu’ na ‘kuambatana na lililo jema.’ (Waroma 12:9) Twahitaji pia kukuza matunda ya roho ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku. (Wagalatia 5:22, 23) Tukifanya hivyo, tutaepuka janga lililopata Yuda—hali ya kuwa wagonjwa kiroho tangu kichwa mpaka wayo.
Nchi Iliyoachwa Ukiwa
16. (a) Isaya afafanuaje hali ya ardhi ya Yuda? (b) Kwa nini wengine husema kwamba labda maneno hayo yalitamkwa wakati wa utawala wa Ahazi, lakini twaweza kuyaelewaje?
16 Sasa Isaya aacha mifano yake ya kitiba na kugeukia hali ya ardhi ya Yuda. Akiwa kama atazamaye nchi tambarare yenye alama za vita, asema hivi: “Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni.” (Isaya 1:7) Wasomi fulani husema kuwa ingawa maneno haya yapatikana mwanzoni mwa kitabu cha Isaya, huenda yalitamkwa baadaye maishani mwa nabii huyo, labda wakati wa utawala wa Mfalme Ahazi mwovu. Wao husisitiza kuwa utawala wa Uzia ulikuwa na ufanisi mwingi mno usiweze kustahili ufafanuzi huu usio na tumaini. Ni kweli, haiwezi kusemwa kwa hakika iwapo kitabu cha Isaya kilitungwa kwa utaratibu wa matukio. Hata hivyo, maneno ya Isaya yahusuyo ukiwa yamkini ni ya unabii. Kwa kutamka taarifa iliyo juu, yaelekea Isaya anatumia mbinu inayopatikana kwingineko katika Biblia—ile ya kufafanua tukio la wakati ujao kana kwamba limekwisha tendeka, hivyo ikikazia hakika ya utimizo wa unabii huo.—Linganisha Ufunuo 11:15.
17. Kwa nini ufafanuzi wa unabii wa ukiwa haupaswi kuwashangaza watu wa Yuda?
17 Kwa vyovyote vile, ufafanuzi wa unabii wa ukiwa wa Yuda haupaswi kuwashangaza watu hawa wakaidi na wasiotii. Karne kadhaa mapema, Yehova aliwaonya dhidi ya jambo ambalo lingetendeka iwapo wangeasi. Alisema: “Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia. Nanyi nitawatapanya-tapanya katika mataifa, nami nitaufuta upanga nyuma yenu; na nchi yenu itakuwa ni ukiwa, na miji yenu maganjo.”—Mambo ya Walawi 26:32, 33; 1 Wafalme 9:6-8.
18-20. Maneno ya Isaya 1:7, 8 yatimizwa lini, na Yehova ‘huachaje mabaki machache’ wakati huo?
18 Yaonekana maneno ya Isaya 1:7, 8 hutimizwa wakati wa uvamizi mbalimbali wa Ashuru unaosababisha kuharibiwa kwa Israeli na uharibifu na kuteseka kulikoenea kotekote katika Yuda. (2 Wafalme 17:5, 18; 18:11, 13; 2 Mambo ya Nyakati 29:8, 9) Hata hivyo, Yuda haiangamizwi kabisa-kabisa. Isaya asema: “Binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa.”—Isaya 1:8.
19 Katikati ya maangamizi hayo yote, “binti Sayuni,” Yerusalemu, ataachwa amesimama. Lakini hatakuwa salama hata kidogo—kama vile kibanda katika shamba la mizabibu au upenu wa mlinzi katika shamba la matango. Akisafiri katika Nile, msomi mmoja wa karne ya 19 alikumbuka maneno ya Isaya alipoona vibanda kama hivyo, anavyovitaja kuwa kama “kitu kinachofanana na ua unaokabili upepo wa kaskazi.” Uvunaji ulipokwisha katika Yuda, vibanda hivi viliachwa vianguke na kuharibika. Ingawa hivyo, Yerusalemu lijapoonekana dhaifu machoni pa jeshi la uvamizi la Waashuri, litaokoka.
20 Isaya amalizia taarifa hii ya unabii, akisema: “Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.” (Isaya 1:9)c Hatimaye Yehova ataipa Yuda msaada dhidi ya Ashuru yenye nguvu. Tofauti na Sodoma na Gomora, Yuda haitafutiliwa mbali. Itaokoka.
21. Baada ya Babiloni kuliharibu Yerusalemu, kwa nini Yehova ‘aliacha mabaki machache’?
21 Zaidi ya miaka 100 baadaye, Yuda ilikuwa hatarini tena. Watu hawakuwa wamejifunza kutokana na nidhamu waliyopewa kupitia Ashuru. “Waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake.” Kwa hiyo, “ghadhabu ya BWANA [ikazidi] juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.” (2 Mambo ya Nyakati 36:16) Nebukadreza mtawala wa Babiloni alishinda Yuda, na wakati huo hakukubaki chochote “kama kibanda katika shamba la mizabibu.” Hata Yerusalemu liliharibiwa. (2 Mambo ya Nyakati 36:17-21) Na bado, Yehova ‘aliacha mabaki machache.’ Hata ingawa Yuda ilivumilia miaka 70 uhamishoni, Yehova alihakikisha kuwa taifa hilo laendelea na hasa nasaba ya Daudi, ambayo ingetokeza Mesiya aliyeahidiwa.
22, 23. Katika karne ya kwanza, kwa nini Yehova ‘aliacha mabaki machache’?
22 Katika karne ya kwanza, Israeli ilikabili mgogoro wake wa mwisho ikiwa watu wa agano la Mungu. Yesu alipojitokeza akiwa Mesiya aliyeahidiwa, taifa hilo lilimkataa, naye Yehova akawakataa. (Mathayo 21:43; 23:37-39; Yohana 1:11) Je, huo ulikuwa mwisho wa Yehova kuwa na taifa la pekee duniani? La. Mtume Paulo alionyesha kuwa Isaya 1:9 lingekuwa na utimizo mwingine tena. Akinukuu tafsiri ya Septuagint, aliandika hivi: “Kama vile Isaya alivyokuwa amesema wakati wa mbele: ‘Isingekuwa Yehova wa majeshi alikuwa ametuachia sisi mbegu, tungalikuwa kama Sodoma, nasi tungalifanywa kama vile Gomora.’”—Waroma 9:29.
23 Mara hii wenye kuokoka walikuwa Wakristo watiwa-mafuta, waliomwamini Yesu Kristo. Mwanzoni kabisa, hao walikuwa Wayahudi waamini. Baadaye waamini wasio Wayahudi wakajiunga nao. Wote pamoja wakafanyiza Israeli mpya, “Israeli wa Mungu.” (Wagalatia 6:16; Waroma 2:29) “Mbegu” hiyo iliokoka uharibifu wa mfumo wa mambo wa Kiyahudi mwaka wa 70 W.K. Kwa kweli, taifa la “Israeli wa Mungu” lingali nasi leo. Sasa mamilioni ya watu mmoja-mmoja wenye imani kutoka kwa mataifa, wanaofanyiza “umati mkubwa, ambao hakuna mtu [awezaye] kuuhesabu, kutoka katika mataifa yote na makabila na vikundi vya watu na lugha” wamejiunga nalo.—Ufunuo 7:9.
24. Wote wanaotaka kuokoka mgogoro mkuu wa mwanadamu wapaswa kuzingatia nini?
24 Hivi karibuni ulimwengu huu utakabiliwa na vita ya Har–Magedoni. (Ufunuo 16:14, 16) Ingawa huo utakuwa mgogoro mkubwa kuliko uvamizi wa Ashuru au wa Babiloni katika Yuda, mkubwa hata kuliko ukiwa uliosababishwa na Roma katika Yudea mwaka wa 70 W.K., kutakuwako wenye kuokoka. (Ufunuo 7:14) Basi, ni muhimu kama nini wote wafikirie kwa uzito maneno ya Isaya kwa Yuda! Hayo yaliokoa waaminifu wa wakati huo. Nayo yaweza kuokoa wenye imani leo.
[Maelezo ya Chini]
a Katika muktadha huu, “Israeli” hurejezea ufalme wa Yuda wa makabila mawili.
b Maneno ya Isaya yadhihirisha mazoea ya kitiba ya siku yake. Mtafiti wa Biblia E. H. Plumptre ataarifu hivi: “Utaratibu uliojaribiwa kwanza ni ‘kufunga’ au ‘kuminya’ kidonda ili kuondoa usaha; kisha, kama katika kisa cha Hezekia (sura ya 38:21), ‘kilizongwa-zongwa,’ na dawa ya kupaka, kisha mafuta fulani au marhamu yenye kutuliza, labda kama katika Luka 10:34, mafuta na divai vilitumiwa kusafisha kidonda hicho.”
c Kichapo Commentary on the Old Testament, cha C. F. Keil na F. Delitzsch, chasema hivi: “Hapa pana kituo katika hotuba ya nabii huyo. Nafasi iliyoachwa kwenye maandishi kati ya mstari wa 9 na 10 yaonyesha hakika ya kwamba imegawanywa katika sehemu mbili mahali hapa. Mtindo huu wa kugawanya sehemu kubwa au ndogo, ama kwa kuacha nafasi au kwa kugawanya mstari, ni wa zamani kuliko ule wa alama za vokali na za lafudhi, nao hutegemea desturi bora ya zamani za kale.”
[Picha katika ukurasa wa 20]
Tofauti na Sodoma na Gomora, Yuda haitabaki ukiwa milele