Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • be funzo 2 uku. 86-uku. 88 fu. 3
  • Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi
  • Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
  • Habari Zinazolingana
  • Tumia Vizuri Nguvu za Ulimi Wako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Sema Lililo “Jema kwa Ajili ya Kujenga”
    “Jitunzeni Katika Upendo wa Mungu”
  • “Upatano Wenye Kulingana Kabisa”
    Amkeni!—1997
  • Je, Wewe Ni “Mfano Mzuri . . . Katika Kusema”?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2022
Pata Habari Zaidi
Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
be funzo 2 uku. 86-uku. 88 fu. 3

SOMO LA 2

Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi

Unahitaji kufanya nini?

Sema kwa njia inayoeleweka kwa urahisi. Hiyo inatia ndani (1) kutumia vizuri viungo vya usemi na (2) kuelewa muundo wa maneno.

KWA NINI NI MUHIMU?

Unaposema kwa njia inayoeleweka wazi, wengine wanaweza kukuelewa. Watu huchukua kwa uzito maneno yanayoeleweka wazi.

NI SHARTI useme kwa njia inayoeleweka ili watu wakuelewe vizuri. Huenda ikawa unataka kusema jambo linalopendeza, au hata muhimu sana, lakini ni kazi bure kulisema ikiwa maneno yako hayaeleweki kwa urahisi.

Watu hawachochewi na maneno ambayo hawaelewi vizuri. Hata kama una sauti kubwa inayosikika vizuri, lakini kama maneno yako si wazi, wengine hawatachochewa kutenda. Ni kana kwamba unaongea lugha ya kigeni ambayo haieleweki. (Yer. 5:15) Biblia inatukumbusha hivi: “Tarumbeta ikivuma wito usio dhahiri, nani atajitayarisha kwa ajili ya pigano? Katika njia hiyohiyo pia, nyinyi msipotamka usemi wenye kueleweka kwa urahisi kupitia hiyo lugha, linalosemwa litajulikanaje? Kwa kweli, mtakuwa mkisema hewani tu.”—1 Kor. 14:8, 9.

Ni Nini Ambacho Hufanya Usemi Usiwe Dhahiri? Huenda ikawa tatizo ni kutofumbua kinywa vizuri. Ikiwa misuli ya utaya haitaki kusogea na ikiwa midomo haifumbuki vizuri, maneno yanaweza kukosa kuwa dhahiri.

Pia inaweza kuwa vigumu kueleweka ikiwa unaongea haraka-haraka. Hiyo ni kama kuweka kaseti yenye mazungumzo icheze haraka kuliko inavyokusudiwa. Maneno yanasemwa, lakini hayafaidi.

Katika hali nyingine, maneno yasiyo dhahiri husababishwa na kasoro katika viungo vya usemi. Lakini hata wale ambao wamelazimika kukabili tatizo hilo wanaweza kutumia madokezo ya somo hili ili kujitahidi kuboresha usemi wao.

Hata hivyo, mara nyingi maneno yasiyo dhahiri husababishwa na hali ya kusema upesi hivi kwamba inakuwa vigumu kueleweka. Huenda tatizo likawa kuruka silabi fulani au kuruka herufi muhimu au kutotamka herufi za mwisho za maneno. Mtu anapoongea upesi, wale wanaomsikiliza wanaweza kushika tu maneno fulani lakini watakisia tu maneno mengine. Kwa hiyo, kutosema maneno yanayoeleweka wazi kunaweza kufanya ufundishaji wako usiwe na matokeo.

Jinsi ya Kusema kwa Njia Inayoeleweka Wazi. Jambo moja ambalo litakusaidia kusema maneno yanayoeleweka wazi ni kufahamu muundo wa maneno ya lugha yenu. Katika lugha nyingi, maneno hufanyizwa kwa silabi. Silabi ni herufi moja au zaidi zinazotamkwa pamoja. Katika lugha kama hizo, kila silabi hutamkwa unapoongea, ingawa silabi zote hazitamkwi kwa mkazo uleule. Ikiwa unataka kusema kwa njia inayoeleweka wazi, punguza mwendo wako wa kusema na ujitahidi sana kutamka kila silabi. Mwanzoni, huenda ikaonekana unakazia sana kila neno kupita kiasi, lakini ukiendelea kufanya mazoezi, hatua kwa hatua utarudia kuzungumza kwa mfuatano wa kawaida. Ufasaha unaweza kufanya uzungumze upesi, lakini tunapaswa kuepuka kufanya hivyo ikiwa kuna uwezekano wa maneno mengine kutoeleweka wazi.

Lakini tahadhari: Ili uzoee kusema kwa njia inayoeleweka, unaweza kufanya mazoezi ya kusema na kusoma kwa kutaja kila neno kwa hususa kabisa. Lakini usiache hiyo iwe njia yako ya kawaida ya kusema. Itaonekana kana kwamba huongei kwa njia ya kawaida na unajifanya.

Ikiwa husemi kwa njia inayosikika wazi, jifunze kuinua kichwa chako ili kidevu chako kisiwe karibu na kifua chako. Unaposoma Biblia, uiinue juu kwa kiasi cha kwamba utainua kichwa kidogo tu kuwatazama wasikilizaji. Hiyo itafanya maneno yako yatokee bila kuzuiwa.

Pia, kujifunza kutulia kunaweza kuboresha usemi wako. Inajulikana kwamba mkazo kwenye misuli ya uso au kwenye misuli inayoongoza jinsi unavyopumua unaweza kuathiri usemi wako. Mkazo kama huo huzuia upatano uliopo kati ya akili, viungo vya usemi, na jinsi unavyopumua. Kwa kawaida kuna upatano mzuri sana kati ya viungo hivyo.

Misuli ya utaya inahitaji kulegea ili ubongo uweze kuiongoza kwa urahisi. Pia midomo inapasa kutulia. Midomo inapaswa kuwa tayari kupanuka na kujifinya haraka ili iweze kutokeza vizuri sauti nyingi zinazotoka kinywani na kooni. Ikiwa utaya na midomo zina mkazo, kinywa hakitafumbuka vizuri, na sauti italazimishwa kupitia meno. Hiyo itatokeza sauti yenye kukwaruza isiyosikika wazi. Lakini kutuliza utaya na midomo hakumaanishi kwamba tuwe wazembe katika usemi wetu. Tunapaswa kusawazisha jambo hilo na kusema maneno kwa njia inayoeleweka wazi.

Unapojichunguza kuhusiana na jambo hili, ingefaa usome kwa sauti. Chunguza kwa makini jinsi unavyotumia viungo vyako vizuri ajabu vya usemi. Je, wewe hufumbua midomo yako wazi ili sauti iweze kutoka bila kuzuiliwa? Kumbuka kwamba mbali na ulimi kuna viungo vingine pia vinavyohusiana na usemi, hata ingawa ulimi ni mojawapo ya viungo vya usemi vyenye utendaji zaidi. Shingo, utaya wa chini, midomo, misuli ya uso, na misuli ya koo, zote zinachangia usemi. Wakati unapoongea, je, huonekana kana kwamba uso wako hausongi? Ikiwa ndivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba husemi kwa njia inayoeleweka wazi.

Kama una ukanda wa kunasa sauti, rekodi sauti yako unapoongea kama kawaida, kama ambavyo ungezungumza na mtu katika huduma ya shambani. Rekodi mazungumzo yako kwa dakika kadhaa. Ukisikiliza sauti yako uliyorekodi, utaweza kuona tatizo lolote ambalo unaweza kuwa nalo la kutosema maneno fulani kwa njia inayoeleweka wazi. Kwa mfano, sikiliza pindi ambazo umesema haraka mno, au pindi ambazo umekosa kutamka maneno wazi, au pindi ambazo umekata-kata maneno, na ujaribu kutambua kwa nini unafanya hivyo. Mara nyingi unaweza kurekebisha udhaifu huo kwa kufuata madokezo ambayo yametajwa hapo juu.

Je, una tatizo fulani la usemi? Jizoeze kufumbua kinywa chako zaidi kidogo kuliko jinsi ambavyo umekuwa ukifanya na ujaribu kutaja kila neno kwa hususa zaidi. Vuta pumzi, kisha uzungumze polepole. Kufanya hivyo kumewezesha wengi wenye matatizo ya kusema waseme kwa njia inayoeleweka zaidi. Kama huwezi kutamka vizuri s na z, jaribu kuvuta ulimi wako mbali na meno yako ya mbele unapozitamka. Hata ingawa huenda hiyo isiwe suluhisho kabisa, usikate tamaa. Kumbuka kwamba ijapokuwa labda Musa alikuwa na tatizo la usemi, Yehova alimchagua atangaze ujumbe muhimu kwa Waisraeli na pia Farao wa Misri. (Kut. 4:10-12) Ukitaka, atakutumia pia, na atakubariki upate mafanikio katika huduma yako.

JINSI YA KUFAULU

  • Sema na kusoma neno moja moja kwa njia inayoeleweka wazi—kwa kutaja kila neno vizuri, kwa sauti inayofaa, na kwa mwendo unaofaa.

  • Sema kila neno kwa njia inayoeleweka wazi na usiongee upesi hata wasikilizaji wakakosa kukuelewa vizuri.

  • Inua kichwa, na ufumbue kinywa vizuri unapozungumza.

  • Jizoeze kutuliza shingo, utaya, midomo, misuli ya uso na misuli ya koo.

MAZOEZI: Zungumza kama kawaida. Unafumbua kinywa chako kadiri gani? Je, unahitaji kufumbua kinywa zaidi kwa kiasi na kutumia zaidi misuli ya uso? Fanya mazoezi ya kufumbua kinywa zaidi kwa kiasi unaposoma kwa sauti Mathayo 8:23-27. Hakikisha kwamba umeinua kichwa na ujaribu kutuliza misuli ya utaya.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki