Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • be funzo 12 uku. 121-uku. 123 fu. 2
  • Ishara za Mwili na za Uso

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ishara za Mwili na za Uso
  • Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
  • Habari Zinazolingana
  • Shauku
    Boresha Uwezo Wako wa Kusoma na Kufundisha
  • Kutoa Hotuba kwa Njia ya Maongezi
    Boresha Uwezo Wako wa Kusoma na Kufundisha
  • Kuzungumza kwa Hisia
    Boresha Uwezo Wako wa Kusoma na Kufundisha
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
Pata Habari Zaidi
Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi
be funzo 12 uku. 121-uku. 123 fu. 2

SOMO LA 12

Ishara za Mwili na za Uso

Unahitaji kufanya nini?

Unahitaji kutumia mikono, mabega, au mwili wote kuonyesha mawazo yako, hisia zako, au mitazamo yako.

Tumia macho, mdomo, na kichwa kukazia jambo unalosema na kuonyesha jinsi unavyohisi.

Kwa Nini Ni Muhimu?

Ishara za mwili na za uso hukazia zaidi maneno yako kwa sababu watu wanakutazama na kuona hisia zako. Ishara hizo zinaweza kuchochea hisia zako na kuzidisha uchangamfu wako.

WATU wa malezi fulani-fulani hutumia ishara zaidi kuliko watu wa malezi mengine. Lakini, karibu kila mtu hutumia ishara za uso na ishara fulani za mwili wanapoongea na watu wengine au wanapohutubia watu.

Yesu na wanafunzi wake wa mapema walizoea kutumia ishara. Pindi moja, mtu fulani alimwambia Yesu kwamba mama yake na ndugu zake wanataka kuongea naye. Yesu alijibu: “Ni nani mama yangu, na ni nani ndugu zangu?” Biblia inaendelea kusema: “Akinyoosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema: ‘Tazama! Mama yangu na ndugu zangu!’” (Mt. 12:48, 49) Biblia inaonyesha katika Matendo 12:17 na 13:16 kwamba mtume Petro na mtume Paulo pia walitumia ishara, na kuna marejeo mengine kama hayo.

Mbali na sauti, ishara za mwili na za uso huonyesha pia mawazo na hisia. Mtu asipotumia ishara hizo vizuri, watu wanaweza kudhani hajali. Lakini mtu akitumia vizuri sauti yake pamoja na ishara, hotuba yake inakuwa bora sana. Hata kama unazungumza na mwingine kwa simu, ikiwa unatoa ishara nzuri za mwili na za uso, sauti yako itaonyesha zaidi umuhimu wa ujumbe wako na jinsi unavyohisi kuhusu jambo unalosema. Basi, kama unatoa hotuba kwa njia ya maongezi au unasoma, iwe wasikilizaji wanakuangalia au wanaangalia Biblia zao, ni muhimu kutumia ishara za mwili na za uso.

Ishara za mwili na za uso zinapasa kutokea kwa njia ya kawaida, na isionekane ni kama umeziiga kwenye kitabu. Hukujifunza jinsi ya kucheka au kuudhika. Vivyo hivyo ishara zinapasa kuonyesha hisia zako za ndani. Inatakikana ishara zitokee zenyewe zaidi na zaidi.

Kwa ujumla kuna aina mbili za ishara za mwili: ishara za ufafanuzi na za mkazo. Ishara za ufafanuzi huonyesha tendo au ukubwa na pia mahali. Unaposhughulikia ishara katika shule, usitumie ishara moja au mbili tu. Jaribu kutoa ishara kwa njia ya kawaida katika hotuba yote. Kama unashindwa kutoa ishara, unaweza kutafuta maneno yanayoonyesha mahali, umbali, ukubwa, au maneno yanayolinganisha mahali fulani na mahali pengine. Hata hivyo, mara nyingi unahitaji tu kutoa hotuba kwa moyo wako, bila kujali watu wanakuonaje, lakini ukiongea na kufanya mambo kama kawaida yako. Mtu akitulia, ishara zake hutokea zenyewe tu.

Ishara za mkazo huonyesha hisia na usadikisho. Ishara hizo hukazia mambo nazo ni muhimu. Lakini jihadhari! Ni rahisi sana ishara za mkazo ziwe mazoea yasiyotakikana. Ikiwa unatumia ishara ile ile moja kila wakati, inaweza kujitokeza na kuwa jambo kuu badala ya kuboresha hotuba yako. Mwangalizi wa shule akionyesha una tatizo hili, jaribu kutumia ishara za ufafanuzi pekee kwa muda fulani. Baadaye anza kutumia tena ishara za mkazo.

Ili ujue kadiri unavyopasa kutumia ishara za mkazo na mikazo inayofaa, wafikirie wale unaowahutubia. Wasikilizaji wanaweza kufadhaika ukiwanyoshea kidole. Katika jamii fulani-fulani mwanamume hawezi kutumia ishara fulani kuonyesha mshangao, kama vile kufunika mdomo wake kwa mkono kwa sababu kufanya hivyo huonwa kuwa tabia ya kike. Katika sehemu nyingine za ulimwengu, mwanamke hawezi kutumia sana ishara za mkono kwa sababu watu watafikiri hana adabu. Basi katika sehemu kama hizo, hasa akina dada wanahitaji kutumia zaidi ishara za uso. Na katika karibu kila sehemu ya ulimwengu, kutoa ishara zenye kupita kiasi mbele ya watu wachache kunaweza kuonwa kuwa vioja vya kuchekesha.

Unapoendelea kupata ujuzi na kuzoea kutulia unapotoa hotuba, ishara zozote za mkazo unazotumia zitaonyesha hisia zako za ndani, usadikisho wako na unyofu wako. Zitafanya maneno yako yawe na maana.

Ishara ya Uso Wako. Mara nyingi uso wako huonyesha jinsi unavyohisi kwelikweli kuliko sehemu nyingine yoyote ya mwili wako. Macho yako, umbo la mdomo wako, na kichwa chako vinahusika. Pasipo neno lolote, uso unaweza kuonyesha kutojali, machukizo, kutatanika, mshangao, au furaha. Ukionyesha ishara kama hizo unapoongea, zitakazia mambo unayosema. Muumba ameweka zaidi ya misuli 30 usoni mwako. Karibu nusu ya misuli hiyo hutumika unapotabasamu.

Iwe unatoa hotuba jukwaani au unahubiri shambani, unajaribu kuwaeleza watu ujumbe unaopendeza ambao unaweza kufurahisha mioyo yao. Tabasamu ya kutoka moyoni huthibitisha jambo hilo. Kwa upande mwingine, ikiwa uso wako hauonyeshi hisia yoyote, watu wanaweza kutia shaka kama kweli unaamini mambo unayosema.

Na zaidi, tabasamu huonyesha wengine kwamba unawapenda. Tabasamu ni muhimu sana hasa siku hizi ambapo watu huwaogopa wale wasiowafahamu. Tabasamu inaweza kuwastarehesha na kufanya watake kusikiliza zaidi.

MAMBO YA KUKUMBUKA

  • Ishara bora zaidi za mwili na za uso hutoka moyoni. Tazama wafanyavyo wengine, lakini usijaribu kuwaiga katika kila jambo.

  • Chunguza hotuba yako mpaka ikuingie vizuri. Uielewe kabisa, uitie akilini, utumie sauti, mikono, na uso kuitoa.

MAZOEZI: (1) Soma Mwanzo 6:13-22. Kwa maneno yako, fafanua jinsi safina ilivyojengwa na jinsi wanyama walivyokusanywa. Usijali mambo madogo-madogo; jaribu tu kusimulia mambo unayokumbuka. Tumia ishara za ufafanuzi unaposimulia mambo hayo. Mwambie mtu mwingine akutazame kisha akuambie maoni yake. (2) Zungumza kana kwamba unamhubiria mtu kuhusu Ufalme wa Mungu na baraka zake. Hakikisha uso wako unaonyesha jinsi unavyohisi kuhusu mambo unayomwambia.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki