“Hawakujali”
KUPUUZA maonyo kunaweza kusababisha msiba.
Mnamo mwaka wa 1974, wakazi wa Darwin, nchini Australia, walikuwa wakijitayarisha kusherehekea sikukuu, waliposikia milio ya ving’ora ikiwaonya kuhusu kimbunga kilichokuwa kikikaribia. Lakini miaka 30 hivi ilikuwa imepita tangu jiji la Darwin liharibiwe na kimbunga. Mbona liharibiwe wakati huu? Wakazi wengi walipuuza hatari hiyo hadi upepo mkali ulipoanza kung’oa paa na kubomoa kuta za nyumba ambamo watu walisongamana. Kufikia asubuhi jiji hilo lilikuwa magofu.
Mnamo Novemba 1985, mlima mmoja wa volkeno ulilipuka huko Kolombia. Theluji na barafu ziliyeyuka na kuporomosha matope yaliyozika zaidi ya wakazi 20,000 wa mji wa Armero. Je, kulikuwa na maonyo yoyote ya mapema? Mlima huo ulitetemeka kwa miezi mingi. Hata hivyo, wakazi wengi wa Armero hawakujali kwa sababu hilo lilikuwa jambo la kawaida. Wenye mamlaka walionywa kwamba kungekuwa na msiba karibuni, lakini hawakujishughulisha kuwaonya watu. Matangazo ya redio yalitolewa ili kujaribu kuwatuliza watu. Kipaza-sauti cha kanisa kilitumiwa kuwasihi watu watulie. Kulikuwa na milipuko miwili mikubwa sana wakati wa jioni. Je, wewe ungeacha mali yako na kukimbia? Ni watu wachache tu waliofanya hivyo, lakini kwa wengi ilikuwa kuchelewa mno.
Mara nyingi wataalamu wa miamba hutabiri kwa usahihi sana mahali ambapo matetemeko ya nchi yatatokea. Lakini ni mara chache sana wanapotabiri kwa usahihi yatatokea lini. Katika mwaka wa 1999, matetemeko ya nchi yaliwaua watu wapatao 20,000 ulimwenguni pote. Wengi wa waliokufa hawakudhani jambo hilo lingeweza kuwapata.
Wewe Huitikiaje Maonyo Yanayotolewa na Mungu Mwenyewe?
Biblia ilieleza waziwazi mapema mambo ambayo yangetukia siku za mwisho. Inapofafanua mambo hayo, Biblia inatuhimiza tufikirie “siku za Noa.” “Katika siku hizo kabla ya gharika,” watu walikuwa wakijishughulisha sana na mambo ya kawaida ya maisha hata ingawa walifadhaishwa na jeuri iliyokuwa imeenea. Mungu aliwaonya kupitia mtumishi wake Noa, lakini “hawakujali mpaka gharika ikaja na kuwafagilia mbali wote.” (Mathayo 24:37-39) Je, wewe ungetii onyo hilo? Je, unafanya hivyo sasa?
Vipi kama ungeishi Sodoma, karibu na Bahari ya Chumvi, katika siku za Loti, mpwa wa Abrahamu? Sehemu za mashambani zilikuwa kama paradiso. Jiji hilo lilikuwa lenye ufanisi. Watu waliishi raha mustarehe. Katika siku za Loti, “walikuwa wakila, walikuwa wakinywa, walikuwa wakinunua, walikuwa wakiuza, walikuwa wakipanda, walikuwa wakijenga.” Watu hao pia walikuwa na maadili mapotovu sana. Je, ungetii onyo la Loti aliposhutumu mazoea hayo maovu? Je, ungemsikiliza ikiwa angekwambia kwamba Mungu ameazimia kuliharibu jiji la Sodoma? Au ungedhani ni mzaha, kama walivyodhani wana-wakwe za Loti? Je, labda ungeanza kukimbia kisha kutazama nyuma kama alivyofanya mke wa Loti? Ingawa wengine hawakuchukua onyo hilo kwa uzito, siku ambayo Loti alitoka Sodoma, “kulinyesha moto na kiberiti kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote.”—Luka 17:28, 29.
Katika nyakati zetu, watu wengi hawajali. Lakini mifano hiyo imeandikwa katika Neno la Mungu ili kutuonya sisi na kututia moyo TUENDELEE KUKESHA!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]
Je, Kweli Kulikuwa na Gharika ya Ulimwenguni Pote?
Wachambuzi wengi wanasema Hapana. Lakini Biblia inasema Ndiyo.
Yesu Kristo mwenyewe alizungumzia gharika hiyo, naye alikuwa hai mbinguni na aliiona ilipotukia.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]
Je, Kweli Majiji ya Sodoma na Gomora Yaliharibiwa?
Vitu vya kale vilivyochimbuliwa vinathibitisha tukio hilo.
Vitabu vya historia vinataja tukio hilo.
Yesu Kristo alithibitisha tukio hilo, na limetajwa na vitabu 14 vya Biblia.