Mfano wa Kuigwa—Mshulami
Msichana Mshulami anajua kwamba anahitaji kuwa na akili timamu katika mambo ya mahaba. Anawaambia wenzake: “Nimewaapisha ninyi, . . . msijaribu kuamsha au kuwasha upendo ndani yangu mpaka wenyewe utake.” Mshulami anajua kwamba hisia zinaweza kulemea akili kwa urahisi. Kwa mfano, anajua kwamba huenda wengine wakamsukuma akubali kutongozwa na mtu asiyemfaa. Hata hisia zake mwenyewe zingeweza kupumbaza akili zake. Kwa hiyo Mshulami anaazimia kuwa kama “ukuta.”—Wimbo wa Sulemani 8:4, 10.
Je, maoni yako kuhusu upendo yanaonyesha ukomavu kama wa Mshulami huyo? Je, unaweza kutumia akili badala ya kuvutwa tu na hisia? (Methali 2:10, 11) Nyakati nyingine, huenda wengine wakakusukuma uanzishe urafiki na mtu fulani kabla hujawa tayari. Huenda hata hisia zako mwenyewe zikakusukuma. Kwa mfano, unapoona mvulana na msichana wakitembea wakiwa wameshikana mikono, je, unatamani sana kuwa katika uhusiano kama huo? Je, ungekubali kuwa na urafiki na mtu ambaye imani yake ni tofauti na yako? Msichana Mshulami alionyesha ukomavu katika mambo ya mahaba. Wewe pia unaweza kuonyesha ukomavu!