Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • lfb somo la 38 uku. 92-uku. 93 fu. 2
  • Yehova Alimfanya Samsoni Awe na Nguvu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yehova Alimfanya Samsoni Awe na Nguvu
  • Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Habari Zinazolingana
  • Mwanamume Mwenye Nguvu Kuliko Wote
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Samsoni Ashinda kwa Nguvu za Yehova!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Mtegemee Yehova Kama Samsoni Alivyofanya
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2023
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
Pata Habari Zaidi
Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
lfb somo la 38 uku. 92-uku. 93 fu. 2
Samsoni anasukuma nguzo za hekalu la Dagoni na jengo linaanguka

SOMO LA 38

Yehova Alimfanya Samsoni Awe na Nguvu

Wengi kati ya Waisraeli walianza tena kuabudu miungu ya uwongo, hivyo, Yehova akaruhusu watawaliwe na Wafilisti. Hata hivyo, kulikuwa na baadhi ya Waisraeli ambao walimpenda Yehova. Mmoja wao aliitwa Manoa. Yeye na mke wake hawakuwa na watoto. Siku moja, Yehova alimtuma malaika kwa mke wa Manoa. Malaika alimwambia hivi: ‘Utazaa mwana. Atawakomboa Waisraeli kutoka kwa Wafilisti. Naye atakuwa Mnadhiri.’ Je, unajua Wanadhiri walikuwa nani? Walikuwa watumishi wa pekee wa Yehova. Wanadhiri hawakuruhusiwa kunyoa nywele.

Baada ya muda, walipata mtoto nao wakamwita Samsoni. Alipokuwa mtu mzima, Yehova alimfanya kuwa mwenye nguvu nyingi. Samsoni angeweza kuua simba kwa mikono yake tu. Wakati fulani, Samsoni aliua Wafilisti 30 akiwa peke yake. Wafilisti walimchukia na walitafuta njia za kumuua. Usiku mmoja, Samsoni alipokuwa amelala huko Gaza, Wafilisti walimsubiri kwenye lango la jiji ili itakapofika asubuhi wamkamate na kumuua. Hata hivyo, katikati ya usiku, Samsoni aliamka, akaenda kwenye lango la jiji na kuling’oa. Kisha, akalibeba lango hilo mabegani mwake mpaka kwenye kilele cha mlima ulio karibu na Hebroni!

Baadaye, Wafilisti walimwendea Delila, mchumba wa Samsoni, na kumwambia: ‘Tutakupa maelfu ya vipande vya fedha ukituambia siri ya nguvu za Samsoni. Tunataka kumkamata na kumfunga gerezani.’ Delila alikubali kwa sababu alitaka pesa. Mwanzoni, Samsoni alikataa kumwambia chanzo cha nguvu zake. Hata hivyo, Delila aliendelea kumsumbua hadi akamfunulia siri ya nguvu zake. Alimwambia hivi: ‘Sijawahi kunyolewa nywele, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri. Nikinyolewa tu, sitakuwa na nguvu tena.’ Samsoni alikosea sana kumfunulia siri yake, sivyo?

Mara moja, Delila akawaambia Wafilisti: ‘Ninajua siri yake!’ Akamlaza Samsoni katika paja lake, halafu akamwita mtu amnyoe nywele. Kisha, Delila akasema kwa sauti kubwa: ‘Samsoni, Wafilisti wamekuja!’ Samsoni akaamka, lakini hakuwa na nguvu. Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho na kumfunga gerezani.

Siku moja, maelfu ya Wafilisti walikusanyika katika hekalu la mungu wao Dagoni wakishangilia na kusema, ‘mungu wetu amemtia Samsoni mikononi mwetu! Mleteni Samsoni nje ili atutumbuize.’ Wakamsimamisha katikati ya nguzo mbili na kuanza kumdhihaki. Samsoni akasali hivi: ‘Ee Yehova, tafadhali nitie nguvu, mara hii moja tu.’ Wakati huo, nywele za Samsoni zilikuwa zimekua tena. Samsoni akasukuma nguzo za hekalu kwa nguvu zake zote. Jengo lote likaanguka na kuwaua watu wote waliokuwemo kutia ndani Samsoni.

“Kwa mambo yote nina nguvu kupitia yule anayenipa nguvu.”—Wafilipi 4:13

Maswali: Kwa nini Samsoni alikuwa mwenye nguvu sana? Samsoni alipatwa na nini alipomwambia Delila chanzo cha nguvu zake?

Waamuzi 13:1–16:31

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki