SOMO LA 62
Ufalme Unaofananishwa na Mti Mkubwa
Usiku mmoja, Nebukadneza aliota ndoto yenye kuogopesha. Akawaita wanaume wake wenye hekima ili wamwambie maana yake. Lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumweleza maana yake. Mwishowe, mfalme akazungumza na Danieli.
Nebukadneza akamwambia hivi Danieli: ‘Katika ndoto yangu, niliona mti. Mti huo ulikua hadi urefu wake ukafika mbinguni. Nao ungeweza kuonekana kutoka sehemu yoyote ya dunia. Ulikuwa na majani mazuri na matunda yake yalikuwa mengi. Wanyama walipumzika chini ya kivuli chake, na ndege wa mbinguni walijenga viota kwenye matawi yake. Kisha malaika akaja kutoka mbinguni. Akapaaza sauti hivi: “Ukateni na kuuangusha mti huu, yakateni matawi yake. Lakini kiacheni kisiki na mizizi yake ardhini kati ya majani ya shambani, kikiwa na pingu ya chuma na ya shaba. Moyo wake na ubadilishwe usiwe wa mwanadamu, nacho kipewe moyo wa mnyama, na acheni nyakati saba zipite. Watu walio hai wajue kwamba Aliye Juu Zaidi ni Mtawala katika ufalme wa wanadamu na kwamba yeye humpa ufalme huo yeyote anayetaka kumpa.”’
Yehova alimfunulia Danieli maana ya ndoto hiyo. Danieli alipoelewa maana ya ndoto hiyo, akaogopa sana. Akasema hivi: ‘Ee mfalme, laiti ndoto hiyo ingewahusu adui zako, lakini inakuhusu wewe. Mti mkubwa uliokatwa ni wewe. Utapoteza ufalme wako, nawe utakula majani kama mnyama wa mwituni. Lakini kwa sababu malaika alisema kisiki kiachwe pamoja na mizizi yake, utakuwa mfalme tena.’
Mwaka mmoja baadaye, Nebukadneza alikuwa akitembea juu ya paa la jumba lake la kifalme, na kuonea fahari Babiloni. Akasema hivi: ‘Tazama jiji hili la kifahari nililojenga. Ona jinsi nilivyo mkuu!’ Alipokuwa akisema maneno hayo, sauti kutoka mbinguni ikasema hivi: ‘Nebukadneza! Sasa umepoteza ufalme wako.’
Wakati huohuo, Nebukadneza akapatwa na wazimu na kuwa kama mnyama wa mwituni. Naye akalazimika kutoka katika jumba lake la kifalme akaishi na wanyama wa mwituni. Nywele za Nebukadneza zikawa ndefu kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.
Miaka saba ilipopita, Nebukadneza akarudiwa na akili timamu na Yehova akamfanya tena kuwa mfalme wa Babiloni. Kisha Nebukadneza akasema hivi: ‘Ninamsifu Yehova, Mfalme wa mbinguni. Sasa ninajua kwamba Yehova ndiye Mtawala. Anawanyenyekeza wenye kiburi, na humpa ufalme huo yeyote yule anayetaka kumpa.’
“Kiburi hutangulia kuanguka kwa kishindo, na roho ya majivuno hutangulia kujikwaa.”—Methali 16:18.