RANGI
Maneno yanayofafanua rangi katika Biblia hayatumii ufafanuzi hususa kama maneno ya kisasa yanayofafanua rangi. Waandikaji wa Biblia walifafanua rangi kulingana na kitu kilichokuwa kinazungumziwa, au kwa kulinganisha vitu wasivyovihahamu na vitu walivyovifahamu. (Kut 16:31; Ufu 1:14) Vitu vinavyofahamika kama vile damu, theluji, aina fulani ya ndege, moto, mawe yenye thamani, na kadhalika vilitumiwa kufafanua rangi. (2Fa 3:22; Zb 51:7; Wim 5:11; Mt 16:2, 3; Ufu 9:17) Rangi zilitumiwa pia kwa njia ya mfano, na wakati mwingine jambo hususa lilihusianishwa na rangi fulani.
Rangi nyeusi inatumiwa kufafanua nywele (Law 13:31; Mt 5:36), farasi (Zek 6:2, 6), ngozi (Ayu 30:30), na jua (Ufu 6:12). Kwenye Ufunuo 6:5, 6, farasi mweusi anafananisha njaa. Vilevile Maandiko yanataja ‘marumaru nyeusi’ na “rangi nyeusi.”—Est 1:6; Yer 4:30.
Rangi ya bluu inafananisha vitu mbalimbali vilivyotiwa rangi, kama vile nyuzi, vitambaa, na joho. (Kut 26:4, 31, 36; 39:22; Hes 4:7) Kila vazi la Mwisraeli lilipaswa kuwa na uzi wa bluu juu ya upindo wa nyuzinyuzi. (Hes 15:38, 39) Bluu ya hayasinthi ni mojawapo ya rangi maridadi zinazopamba mabamba ya kifuani yanayotajwa kwenye Ufunuo 9:17.
Rangi ya kahawia inatumiwa tu kuwafafanua kondoo.—Mwa 30:32, 33, 35, 40.
Rangi ya moto inatumiwa kwa njia ya mfano kufafanua mwonekano wa joka mkubwa, Shetani Ibilisi. (Ufu 12:3) Farasi wa rangi hiyo anatumiwa kufananisha vita kati ya mataifa, kama inavyoonyeshwa kwenye Ufunuo 6:4.
Rangi ya kijani inatajwa katika Maandiko, lakini mara nyingi hairejelei rangi. Badala yake, inaleta wazo la ubichi na uhai wa mimea. (Mwa 1:30; Ayu 39:8; Yoe 2:22) Mchanganyiko wa rangi ya manjano na kijani unatumiwa kuhusu madoa ya ukoma kwenye vitambaa na kwenye nyumba zenye kuta za mawe au kufafanua dhahabu bora.—Law 13:49; 14:37; Zb 68:13, maelezo ya chini.
Rangi ya zambarau inatajwa mara nyingi katika Maandiko, ingawa hakuna ufafanuzi kuhusu aina tofauti za rangi ya zambarau zinazotengenezwa kwa njia mbalimbali. (Kut 25:4; Hes 4:13; Eze 27:7, 16; Da 5:7, 29; Mr 15:17, 20; Lu 16:19; Ufu 17:4) Kwa sababu ya gharama yake, mara nyingi rangi hii ilihusianishwa na utajiri, heshima, na ukuu wa kifalme.
Rangi nyekundu ilitumiwa kwenye vitu vya bei ghali vilivyotiwa rangi. (2Nya 2:7, 14; 3:14; Nah 2:3) Vilevile dhambi zinalinganishwa na rangi nyekundu iliyokolea.—Isa 1:18.
Rangi nyekundu na hudhurungi zimetumiwa kufafanua vitu mbalimbali kama vile nywele (Mwa 25:25), ngozi za kondoo zilizotiwa rangi (Kut 25:5), wanyama (Hes 19:2; Amu 5:10; Zek 1:8), mavazi (Isa 63:2), na anga la jioni (Mt 16:2, 3). Neno la Kiebrania linalotafsiriwa “nyekundu” (ʼa·dhomʹ) linatokana na neno dam, linalomaanisha “damu.”—Mwa 25:30; 9:6.
Rangi nyekundu inatajwa kuhusiana na kamba au nyuzi, vitambaa na majoho; na pia dhambi. (Mwa 38:28, 30; Hes 4:8; Yos 2:18; Yer 4:30; Mt 27:28; Isa 1:18) “Mnyama wa mwituni” anayefafanuliwa kwenye Ufunuo 17 ana rangi nyekundu (mst 3), inayomtofautisha na “mnyama wa mwituni” anayetajwa kwenye sura ya 13. Kahaba aliyeketi juu ya mnyama wa mwituni mwenye rangi nyekundu amepambwa kwa rangi ya zambarau na nyekundu. (Ufu 17:3-5) Kwa hiyo, maono hayo yanaonyesha mamlaka ya yule “mnyama wa mwituni” na vilevile anasa na hali ya kifalme anayofurahia mwanamke aliyeketi juu yake.
Rangi nyekundu (Yer 22:14; Eze 23:14) inarejelea rangi inayotokana na mchanganyiko wa kemikali ya chuma au risasi. Inaonekana Wafoinike ndio waliokuwa wa kwanza kuitumia baada ya kuisafirisha kutoka katika migodi ya Kaskazini mwa Afrika. Baadaye migodi kama hiyo ilianzishwa Mashariki ya Kati.
Rangi nyeupe ndiyo rangi inayotajwa mara nyingi katika Maandiko. Licha ya kufafanua rangi, inatumiwa pia kwa njia ya mfano kuwakilisha uadilifu na usafi wa kiroho. (Ufu 3:4; 7:9, 13, 14) Farasi mweupe, kama inavyoonyeshwa kwenye Ufunuo 6:2 na 19:11, anawakilisha vita safi ya uadilifu inayoongozwa na Yesu Kristo.
Mavazi meupe yalivaliwa na maskini na pia watu wenye vyeo. Pindi zote mavazi ya malaika yanatajwa kuwa meupe. (Mr 16:5; Yoh 20:12; Ufu 19:14) Vitu vingine vinavyotajwa kuwa vyeupe ni nywele (Law 13:3; Mt 5:36), ngozi (Law 13:16), mashamba ya nafaka yaliyo tayari kuvunwa (Yoh 4:35), na kiti cha ufalme cha Mungu cha hukumu ya uadilifu (Ufu 20:11). Yesu aliwalinganisha waandishi na Mafarisayo na makaburi yaliyopakwa chokaa. (Mt 23:27) Mfano wake ulihusiana na desturi ya kupaka chokaa makaburi yaliyokuwa karibu na Yerusalemu kabla ya Pasaka ili kuwalinda watu waliokuwa wakija kusherehekea Pasaka wasiwe najisi kwa kugusa makaburi. Biblia inataja aina mbalimbali za rangi nyeupe, kwa mfano, mchanganyiko wa rangi nyekundu na nyeupe (Law 13:19, 24) na ambayo si nyeupe sana.—Law 13:39.
Rangi ya manjano na manjano ya kiberiti zinatajwa pia.—Law 13:30, 32, 36; Ufu 9:17.
Mchanganyiko wa rangi. Mbali na rangi hususa, Biblia inafafanua kwamba vitu fulani vilikuwa na rangi zisizo hususa au mchanganyiko wa rangi—kwa mfano: mabakamabaka (Mwa 30:32, 33), rangi zinazong’aa (Isa 63:1), rangi nyingi (Yer 12:9), mabaka (Zek 6:3, 7), mistarimistari, madoadoa (Mwa 31:10, 12; Zek 6:3, 6), rangi mbalimbali (Eze 16:16; 17:3; 27:7, 16, 24).—Tazama KUTIA RANGI.
Joho la Kristo. Rangi ya joho ambalo Yesu Kristo alivishwa siku aliyouawa limefanya baadhi ya watu waseme kwamba kuna kasoro katika masimulizi ya Biblia kuhusu vazi hilo. Mathayo alisema kwamba wanajeshi ‘walimvisha joho jekundu’ (Mt 27:28), huku Marko na Yohana wakisema lilikuwa la zambarau. (Mr 15:17; Yoh 19:2) Hata hivyo, badala ya kuiona kuwa kasoro, tofauti hiyo ya ufafanuzi wa rangi ya vazi hilo unathibitisha kwamba vitabu vya Injili viliandikwa na watu tofauti na kwamba hawakushauriana. Mathayo alilifafanua vazi hilo kwa maoni yake, yaani kulingana na jinsi alivyoelewa rangi, na alikazia mwonekano wa rangi nyekundu wa vazi hilo. Yohana na Marko waliiona rangi hiyo kuwa zambarau. “Zambarau” inaweza kuhusianishwa na rangi yoyote yenye mchanganyiko wa bluu na nyekundu. Kwa hiyo, Marko na Yohana walikubaliana na Mathayo kwamba vazi hilo lilikuwa jekundu kwa kadiri fulani. Bila shaka, mandhari na mwangaza ulioakisi vazi hilo huenda ulifanya lionekane kwa njia tofauti. Bahari inaweza kuonekana kuwa na rangi mbalimbali nyakati tofauti, ikitegemea rangi ya anga na mwangaza. Basi, tunapochunguza mambo hayo, inaonekana kwamba waandikaji wa vitabu vya Injili hawakutofautiana kuhusu rangi ya joho ambalo wanajeshi Waroma waliomdhihaki Kristo walimvisha siku aliyouawa.