Upofu wa Kutopambanua Rangi Kasoro Yenye Kustaajabisha
ULIKUWA mshtuko gani kwa washiriki wa dhehebu la Wakweka wenye akili timamu walipoona soksi ndefu za John Dalton zilizokuwa nyekundu-nyangavu! Kwa kuwa kwa kawaida alivalia kwa rangi zisizo nyangavu—kijivu, kijani-kibichi, na nyeusi—waliona mvalio wa John ukiwa wenye kushtua, bila kutaja mengineyo! Ni nini kilichokuwa kimetendeka?
Dalton, aliyezaliwa 1766 katika Eaglesfield, Uingereza, aliieleza damu kama “rangi nzito ya kijani-kibichi” na akaonelea kwamba jani la mti loreli wa Ulaya “ni sawa na lakiri [nyekundu].” Ndiyo, Dalton, ambaye alikuja kuwa maarufu kwa elimu ya dawa, aliugua kutoweza kupambanua rangi nyinginezo, au hususa zaidi, kasoro ya kutokuona rangi.
Kwa Dalton, nyekundu ilionekana kama kijivu na si tofauti sana na kijani-kibichi. Si ajabu kwamba rafiki yake mwenye vitendo vya mzaha angeweza kubadilisha soksi ndefu zake na kusababisha hasira kubwa sana! Kwa kupendeza, katika nchi fulani za Ulaya, kasoro ya kutoweza kupambanua rangi inaitwa Udaltoni.
Tatizo la Ulimwengu Mzima
Katika 1980, Dkt. Janet Voke wa Chuo Kikuu cha Jiji, London, alikadiria kwamba watu zaidi ya milioni mbili katika Uingereza wana kasoro ya kutopambanua rangi. Katika jamii za sehemu za mbali, kwa kulinganisha ni wachache ambao wana kasoro hii. Katika Fiji, mtu mmoja tu katika kila 120 ana kasoro ya kutopambanua rangi mbalimbali, hali katika Kanada, kila mtu wa 9, kwa wastani, anapungukiwa upambanuzi ule wa kawaida wa rangi.
Uwezo wa kupambanua unatofautiana kwa mtu na mtu. Kulingana na nadharia inayokubaliwa na watu wengi, uwezo wako wa kuona ni wa kawaida ikiwa unaona nyeupe wakati miale mitatu ya nuru—kila mmoja ukiwa mwekundu, kijani-kibichi, na buluu—inapochanganywa kwa uwiano ulio sawasawa. Wakati miale hiyo mitatu inapochanganywa kwa kadiri zinazotofautiana, namna nyingine za rangi zile zile za msingi ambazo kwa kawaida wewe huwa wazifahamu zaweza kutokezwa.
Ikiwa, hata hivyo, namna zote za rangi unazoweza kuziona zinaweza kuwa sawa kwa kuchanganya rangi mbili za msingi, na ongezo la rangi ya tatu halileti badiliko lolote lenye kuonekana kwa urahisi, basi uwezo wako wa kuona rangi una kasoro. Wewe ni yule ambaye huitwa daikromati (asiyepambanua rangi mbili zenye ukaribiano). John Dalton alikuwa daikromati kipofu wa kutopambanua rangi nyekundu.
Kasoro zinazoathiri wale wanaoitwa monokramati (wasiopambanua hata rangi moja) ni mbaya hata zaidi. Wale wenye hali hii hawawezi kubagua rangi. Kwa wamonokramati (wasiopambanua hata rangi moja), televisheni ya rangi huenda ionekane kwao kama televisheni isiyo ya rangi.
Wengi wenye upofu wa kutopambanua rangi huwa ni watraikomati wenye kasoro (wenye kukosa kupambanua rangi tatu za msingi). Zile namna mbalimbali za aina ya rangi moja ambazo huweza kuziona huwa bado ni mchanganyiko wa rangi tatu kuu, lakini watraikomati wenye kasoro wanatofautiana katika kadiri ya rangi za msingi ambazo wanaweza kutambua. Ikiwa hili ndilo tatizo lako, kurekebisha usawaziko wa rangi katika televisheni yako huenda kukatokeza malalamiko kama “Hiyo ni nyekundu mno!” au “Ni yenye kijani mno!” kutoka kwa wenzi wako wasio na kasoro ya rangi.
Visababishi
Ni nini husababisha kasoro kama hizo? The New Encyclopaedia Britannica yatambulisha kisababishi kimoja kuwa ni “vyombo vya kubagua urefu-mawimbi.” Kila moja la macho yako lina vipokea-nuru kama milioni 130 katika ngozi yenye wavu wa neva (retina), lakini ni milioni 7 tu ya hivi hukupa uwezo wa kuona rangi. Hivi vipokea rangi vinaitwa koni (pia) kwa sababu ya umbo lake kama koni.
Watu wenye uwezo wa kawaida wa kuona rangi wana aina tatu za koni. Koni fulani huitikia vizuri zaidi ikiwa marefu-ya-mawimbi ya nuru (mekundu) ni marefu zaidi. Kikundi cha pili huhisi marefu-ya-mawimbi ya kiwango cha kati (ya kijani-kibichi), na wale wengine marefu-ya-mawimbi yaliyo mafupi zaidi (buluu). Ikiwa kikundi cha koni hakipo au kinakosa kuitikia vizuri kuona rangi nyekundu, kwa mfano, utaona tofauti ndogo sana ya badiliko la rangi wakati nyanya inapoiva kutoka kijani-kibichi kuwa rangi ya chungwa hadi nyekundu.
Kuharibiwa kwa neva za macho za mwono ambao huathiri ujumbe wa koni unaoenda hadi kwenye ubongo kunaweza kuanzisha upofu wa kutopambanua rangi. Hata namna fulani za utibabu, kama vile dawa fulani za kuzuia malaria, zimejulikana kuwa zadhuru uwezo wa kutambua rangi. Tembe fulani zinazomezwa kuzuia uzazi zimeripotiwa kwamba zaweza kudhuru uwezo wa kutambua namna mbalimbali za buluu, namna mbalimbali za kijani-kibichi, na namna mbalimbali za kimanjano. Katika kitabu Colour Vision Testing, Dkt. Voke aorodhesha tumbako na kileo kuwa visababishi vya kasoro za kudumu za upofu wa kutopambanua nyekundu na kijani-kibichi.
Uzee pia ni kisababishi, hasa kwa uwezo wa mtu wa kuona nuru ya buluu. Mtafiti R. Lakowski asema kwamba uwezo wa kubagua rangi hufikia kilele wakati wa ubalehe, na huendelea kuwako hadi umri wa 35. Halafu uwezo huo wa kubagua rangi huisha polepole, hasa baada ya umri wa miaka 60.
Ingawa kasoro ya uwezo wa kuona rangi mbalimbali unaweza kumpata mtu katika wakati wa maisha yake, wengi wa wale walio na kasoro hii wako hivyo tangu kuzaliwa kwao. Kwa nini?
‘Kama Babu, Kama Mjukuu’
Uwezo wa kawaida wa kibinadamu wa kuona rangi mbalimbali ni zawadi ya pekee. Wakati koni zako zifanyapo kazi sawasawa na neva za macho zinapopelekea ubongo kwa uaminifu ujumbe uliorekodiwa, ndipo wewe unaona rangi kamili. “Jicho la kibinadamu lililozoezwa linaweza kutambua kufikia namna 150 za rangi,” charipoti kitabu How Animals See. “Wanyama wengi . . . labda hawaoni rangi kama sisi tuzionavyo. Lakini hali hiyo ni ya kawaida machoni pao, haina kasoro,” chasema The World Book Encyclopedia.
Ikiwa uwezo wako wa kuona umekuwa na kasoro wakati wote, hakuna shaka ulirithi kasoro hiyo. Kutoka kwa nani? Kichapo Health and Disease hueleza kwamba kasoro hii ya upofu wa kutopambanua rangi “hutokezwa na wanawake lakini kwa kawaida huja kutokea-tokea tena katika vizazi vya baadaye vya wanaume.” Kwa hiyo, mara nyingi, mambo huwa ni ‘kama babu, kama mjukuu.’
Je! Una Upofu wa Kutopambanua Rangi? Jinsi ya Kujua
Unashuku kwamba watoto wako ni vipofu wa kutopambanua rangi? “Ukitambua kwamba mtoto wako wa miaka 5 au 6 ana shida ya kutambulisha rangi; ikiwa huwa anavalia soksi zisizopatana; au ikiwa hawezi kuchukua kalamu ya rangi ifaayo kutoka kwenye kijisanduku aombwapo kuchagua moja kulingana na rangi yake, “basi, kitabu Childcraft kinasema,” unapaswa kumpeleka achunguzwe uwezo wake wa kuona.” Namna gani?
Moja ya njia zilizo maarufu za kuchunguza uwezo wa kuona rangi ni ule mtihani wa Ishihara. Mchunguzi humwonyesha mtoto wako mfululizo wa kadi zenye vitonetone vya namna nyingi za rangi. Kati ya madoa hayo kuna violezo na namba zenye kutambuliwa na wale tu ambao huona rangi zote kikawaida. Mtoto wako apaswa kusema ni kiolezo au namba gani anayoona. Kwa kuangalia chati moja, mtoto asiyeweza kuona rangi nyekundu huona “6,” mtoto asiyeweza kuona rangi ya kijani-kibichi huona “9.” Ikiwa mtoto wako anaona “96,” uwezo wake wa kuona rangi ni wa kawaida, kulingana na sehemu hiyo ya mtihani.
Kukiwa na ongezeko la utumizi wa rangi katika vifaa ambavyo vinatumika katika kufunzia watoto, ni jambo la hekima kujua kama uwezo wa watoto wako wa kuona rangi zilizo tofauti una kasoro. Lakini kwa kuwa ukosefu uliorithiwa wa kuona rangi hauwezi kubadilishwa au kutibiwa kwa sasa, je! waweza kufanya lolote kuhusu hilo?
Tahadhari za Kuchukuliwa
Hazel Rossotti, mtunzi wa kitabu Colour, kwanza apendekeza uchunguzi wa mapema. Halafu mtu yule mtu mwenye upofu wa kutopambanua rangi aweza ‘kufahamishwa hali ambazo zaelekea kusababisha mvurugo iwezekanapo, na kufunzwa kutegemea mambo mengine badala ya kutegemea rangi zisizofahamika wazi.”
Unaweza kumfunza mtoto wako aliye kipofu wa kutopambanua rangi maana ya ishara za barabarani zenye rangi. Ingawa huenda ikawa aweza kupambanua ishara nyekundu ya kusimama yatofautiana na ile ya kijani-kibichi ya “nenda” kulingana na kikao chayo, msaidie atambue nguvu au mng’aro wa kila taa. Halafu, awapo peke yake, atasoma ishara hizo kwa usahihi hata gizani.
Ikiwa wewe una upofu wa kutopambanua rangi, ni vema kutokutegemea rangi peke yake wakati wa kufanya maamuzi. Kwa kuwa ubongo waweza kujazia kasoro za uwezo wa kutofautisha rangi, uongezee habari unazoupa kwa kuwa mwangalifu zaidi kwa uangavu, kikao, na umbo la kitu. Usisite kuwaomba msaada marafiki na watu wa ukoo wako walio na uwezo wa kawaida wa kutofautisha rangi.
Katika kufanya maamuzi ya maana, kama aina ya kazi utakayofanya, utakuwa mwenye hekima ukizingatia madhara ambayo upofu wa kutopambanua rangi huleta. Katika aina za kazi fulani, upofu wa kutopambanua rangi ni mzigo mkubwa. Kwa mfano, ni kizuizi kwa wenye ujuzi wa dawa, wataalamu wa kuunga na kutoa madawa, wapiga chapa za rangi, na wapiga picha. Uwezo mzuri wa kuona rangi tofauti ni msaada mkubwa kwa madaktari wa meno wanapolinganisha meno bandia. Pia, wauza nyama na walio katika uchumi wa kutoa chakula wanaweza kuwa chonjo zaidi kwa mabadiliko katika hali ya chakula wakati wanapokuwa na uwezo mzuri wa kuona rangi tofauti. Ukosefu wa kutambua rangi unaweza kufanya iwe vigumu zaidi kwa wauguzi na madaktari kudhihirisha hali ya afya ya wagonjwa wanapowapima.
Kila mtu anayeona vizuri ana mali ya thamani. Ikiwa uwezo wako wa kuona rangi mbalimbali ni wa kadiri tu, unapaswa uwe mwangalifu zaidi. Kwa mfano, unapaswa utambue kwamba kutumia dawa zisizohitajiwa, kutumia kileo kupita kiasi, au kutumia tumbako kunaweza kuzorotesha uwezo wa kutambua rangi. Ikiwa una uwezo wa kuona rangi tofauti-tofauti, basi una zawadi isiyo na kifani ya kuthamini sana.