Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 8/8 kur. 14-15
  • Dawa za Kulevya kwa Ajili ya Raha—Kwa Nini Sivyo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dawa za Kulevya kwa Ajili ya Raha—Kwa Nini Sivyo?
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo Yenye Kudhuru na ya Kufisha
  • Mwili Wako—‘Dhabihu Iliyo Hai’
  • Je! Dawa za Kulevya Zinaleta Maisha Bora?
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
  • Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001
  • Jinsi Ambavyo Dawa za Kulevya Haramu Huathiri Maisha Yako
    Amkeni!—1999
  • Matumizi ya Dawa za Kulevya Yatakomeshwa!
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 8/8 kur. 14-15

Maoni ya Biblia

Dawa za Kulevya kwa Ajili ya Raha—Kwa Nini Sivyo?

“KOKENI . . . labda ndiyo dawa ya kulevya iliyo pole kupita dawa zote haramu zinazotumiwa kwa mweneo mkubwa na ndiyo yenye raha sana.”

Ndivyo alivyosema Dkt. Peter Bourne katika 1974. Miaka minne baadaye akiwa kama mshauri wa miongozo ya kiafya ya White House kwa ajili ya Rais Jimmy Carter, Dkt. Bourne alilazimika kujiuzulu kwa sababu ya mashtaka ya utumizi haramu wa dawa za kulevya. Kama wengine wengi, labda alifikiri angetetea kwamba ni haki kutumia dawa za kulevya kwa kupata raha.

Katika wakati mmoja kokeni ilipatikana kwa urahisi kwa kila mtu karibu kila mahali—katika maduka ya vyakula, majumba ya kunywea vileo, na kutoka kwa wachuuzi wa maagizo ya barua. Katika miaka ya 1880 na 1890, ingeweza kuvutwa ikiwa katika muundo wa sigareti iliyofungwa kwa majani. Ingeweza kunywewa katika michanganyo mbalimbali ya divai na vinywaji visivyo vikali. Hata yule mpelelezi wa kubuniwa wa Kiingereza anayejulikana sana Sherlock Holmes anaelezwa akiwa anatumia kokeni “mara tatu kwa siku kwa miezi mingi.”—The Sign of Four, na Sir Arthur Conan Doyle.

Kokeni ilistahiwa kwa uwezo wayo wa kuponya na ilisifiwa kama dawa ya maumivu ya kichwa, ugonjwa wa pumu, homa iletwayo na mavumbi ya maua, na maumivu ya meno. Kwa watu wengi ikaja kuwa kinywaji kitamu chenye dawa. Kwa mfano, katika 1884 Sigmund Freud kijana aliandika: “Nimeyajaribu matokeo haya ya koka, ambayo huondoa njaa, usingizi, na uchovu na kufanya mtu awe shupavu katika uwezo wa akili, mara kadhaa nikiyajaribu kwangu mimi mwenyewe . . . Kipimo cha kwanza na hata vipimo kadhaa vinavyofuatana vya koka havitokezi tamaa yenye nguvu ya kutumia kichocheo hicho zaidi.”—Über Coca.

Katika miaka iliyofuata, maelezo kama hayo yametolewa kuhusu marijuana, ambayo yalifanya watu wengine waamini kwamba utumizi wa dawa za kulevya ulikuwa hauna madhara. Hata hivyo leo unaweza kusoma ithibati ya kitiba iliyo kama mlima ikionyesha vingine. Kwa kweli, utumizi wa dawa za kulevya kama vile marijuana, kokeni, kraki (aina ya kokeni), heroini, amfitamini, na babitureti unadhuru sana mwili.

Matokeo Yenye Kudhuru na ya Kufisha

Wachunguzi wanadai kwamba watumiaji wa marijuana wanaweza kutazamia vitoto vidogo zaidi, aksidenti nyingi zaidi, na mapafu yaliyoharibika. Kokeni na kitokezo chayo kraki vimeunganishwa na ugonjwa wa akili wa kushuku mambo bila sababu na dalili nyingine za kuwazia mambo yasiyokuwako, kupoteza hamu ya kula, kutoweza ngono, kuudhika-udhika sana, ugonjwa wa kifafa, ugonjwa wa moyo, magonjwa ya ghafula, ubadilifu wenye kudhuru wa tishu chini ya ngozi, au malengelenge, kupoteza mikono au miguu na vidole, kasoro za uzazi, maambukizo ya sehemu ya juu ya kupumua, kupoteza uwezo wa kunusa, na kifo. Kulingana na mwandishi mmoja wa kisayansi, “kama utumizi wa kokeni wakati wa mimba ungekuwa ni ugonjwa, uzito wa matokeo yao kwa vitoto vichanga ungefikiriwa kuwa hatari kubwa kwa utunzaji wa afya ya kitaifa.”

Aina fulani za watumizi wa dawa za kulevya pia wamo katika hatari kubwa ya kuambukizwa UKIMWI. (Ona ukurasa wa 25.) Na matatizo mengi ya afya yameshirikishwa na utumizi mbaya wa dawa za kulevya zisizo za asili, kama vile amfitamini, babitureti, dawa za utulizaji, na “dawa za mwenye kubuni” za kutoka nchi za nje.

Bado, hata kukiwa na hasara zinazojulikana, watu bado wanashawishwa kutumia dawa za kulevya. Watumizi wa mara kwa mara wanaona dawa kama hizo zikifurahisha. Hata hivyo, hatari ni halisi sana. Ni kama kuendesha meli inayochukua shehena ya mafuta juu ya miamba iliyo chini ya maji—maafa ni hakika.

Mwili Wako—‘Dhabihu Iliyo Hai’

Kanuni inayoelezwa na mtume Paulo katika Warumi 12:1 ina uelekezo wenye nguvu katika jambo hilo. Hiyo husema: “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana [utumishi mtakatifu, NW].” Wakristo wanatoa dhabihu zenye umaana mkubwa kuliko dhabihu za wanyama ambazo taifa la kale la Israeli lilitakiwa litoe.

Wenye kustahili kuangaliwa ni utumizi wa Paulo wa neno la Kigiriki linalotafsiriwa “dhabihu iliyo hai, takatifu” (thysiʹan zoʹsan ha·giʹan). Kulingana na wanachuo mbalimbali wa Biblia, maneno haya yanachukua maana ifuatayo: Mwisraeli alitoa dhabihu ya mnyama aliyekufa. Haingetolewa tena. Kwa kutofautiana, Mkristo anajitoa mwenyewe pamoja na nishati zake zote za uhai, ‘zilizo hai.’ (Kitenzi cha Kigiriki kinachotafsiriwa “hai” kinaweza wakati mwingine kumaanisha “kuwa hai katika afya.”) Na kama vile Mwisraeli alivyokatazwa kutoa kile ambacho kimelemaa au chenye kasoro yoyote ya umbo, Mkristo hutolea Mungu vitivo vyake vilivyo bora zaidi. Na kwa sababu mwili wa Mkristo ndicho kisafirishi kinachompeleka kwenye matendo yake, vitendo vyake vyote na fikira pamoja na chombo chake—mwili wake—vinawekwa wakfu kwa Mungu peke yake. Hiki kinakuwa kitendo cha kujiweka wakfu kamili. Yeye hadai kitu kingine chochote kwake mwenyewe. Hivyo, uhai wake, si desturi ya ibada, ndiyo dhabihu ya kweli.

Kwa hiyo, Paulo alikuwa akiwatia moyo Wakristo wa karne ya kwanza, hali wakiwa hai duniani, watumie nishati zao, afya yao, majaliwa yao au zawadi zozote walizo nazo katika utumishi wa nafsi yote kwa Mungu. (Wakolosai 3:23) Wangepaswa kumpa Yehova kile kilicho bora zaidi kimwili na kiakili. Mungu angependezwa na dhabihu kama hizo.

Hata hivyo, Mungu angalitendaje kama wangalijiingiza kwa kutaka katika mazoea ambayo yalididimisha uwezo wao wa kimwili na kiakili na hata yakafupisha uhai wao? Je! Wakristo wangependa kuvunja sheria na wawe katika hatari ya kupunguza kufaa kwao katika huduma ya Mungu? Mazoea machafu yangeweza kuwaondolea ustahili wasiwe wahudumu na hata yatokeze kuondoshwa kwao katika kundi la Kikristo.—Wagalatia 5:19-21.

Leo, ni zoea la kawaida ulimwenguni mwote watu kutumia vibaya dawa za kulevya. Je, mtu aweza kutumia dawa kama hizo kwa ajili ya raha na bado atoe mwili wake kama “dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kumpendeza Mungu”? Si uchunguzi wa kitiba tu na mambo yaliyoonwa yenye matokeo ya hasara kubwa bali pia kanuni za Biblia zinatoa jibu lililo wazi—sivyo!

[Picha katika ukurasa wa 14]

“The Opium Smoker”—by N. C. Wyeth, 1913

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki