Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • it uku. 520
  • Agano

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Agano
  • Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Habari Zinazolingana
  • Mtakuwa “Ufalme wa Makuhani”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
  • Agano Jipya la Mungu Lakaribia Kutimizwa
    Usalama Ulimwenguni Pote Chini ya “Mwana-Mfalme wa Amani”
  • Baraka Kubwa Zaidi Kupitia Agano Jipya
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Yehova ni Mungu wa Maagano
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
Pata Habari Zaidi
Ufahamu wa Kina wa Maandiko
it uku. 520

AGANO

Ni makubaliano kati ya watu wawili au zaidi ya kutenda au kujiepusha na tendo fulani; mapatano; mkataba. Neno la Kiebrania berith′, ambalo asili yake si hakika, linaonekana zaidi ya mara 280 katika Maandiko ya Kiebrania; zaidi ya mara 80 kati ya mitajo hiyo imo katika vitabu vitano vya Musa. Kwamba maana yake ya msingi ni “agano,” linalofanana na neno letu “mkataba” la kisheria la kisasa, inaonyeshwa na mabamba ya maandishi ya kikabari yaliyopatikana katika 1927 huko Qatna, jiji fulani la kale lisilo la Kiisraeli Kusini-Mashariki mwa Hamathi. “Yaliyomo katika mabamba hayo mawili [kati ya 15 yaliyopatikana] ni sahili. Bamba A lina orodha ya majina . . . Bamba B ni orodha ya posho . . . kwa hiyo Orodha A ni mapatano ambayo katika hayo wanaume husika . . . wanakubali kumtumikia mtu fulani au kutimiza wajibu fulani mbalimbali. Kisha Orodha B, iliyoandikwa na mwandishi huyo mmoja, inaonyesha aina ya mapatano hayo; nao wanaume hao wangepokea maposho hususa kwa ajili ya utumishi wao. . . . wazo la Kiisraeli la berit, ‘agano,’ lilikuwa habari kuu ya msingi katika theolojia ya Yahwe. Humu mna mtajo wa kwanza wa neno hilo wa nyakati za kale wenye kuonekana nje ya Biblia—si wa baada ya thuluthi ya kwanza ya karne ya kumi na nne Kabla ya Kristo.”—Bulletin of the American Schools of Oriental Research, Februari 1951, ukur. 22.

Katika baadhi ya tafsiri za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo neno di·a·the′ke linatafsiriwa katika njia mbalimbali kama “agano,” “wasia,” “testamenti” (testamentum, Vg). Hata hivyo, Cyclopaedia ya M’Clintock and Strong (1891) yasema, chini ya “Agano”: “Hata hivyo, inaonekana hakuna sababu ya kuanzisha neno jipya [kando na “agano”] lenye kutokeza wazo jipya. Kwa Sept[uagint] kutafsiri [berith′] (ambalo kamwe halimaanishi wasia au testamenti, bali sikuzote ni agano au mapatano) kwa kutumia [di·a·the′ke] kotekote katika A.K. bila kigeugeu, hivyo huenda ikadhaniwa kwa kulichukua neno hilo, wale waandikaji wa A.J., walikusudia kuwasilisha kwa wasomaji wao, wengi wao wakiwa wanafahamiana na A.K. la Kigiriki, wazo lile moja. Isitoshe, katika visa vingi, kitu kile kimoja ambacho kimeitwa ‘agano’ (berith′) katika A.K. kinarejezewa katika A.J. (k.m. 2Kor. 3, 14; Ebr. 7, 9; Ufu. 11, 19); na katika muktadha ule mmoja neno na kitu kile kimoja katika Kigiriki huwakilishwa wakati mwingine katika Kiingereza [tafsiri ya KJ] na ‘agano,’ na wakati mwingine na ‘testamenti’ (Ebr. 7, 22; 8, 8-13; 9, 15).”—Ona pia NW (Kiingereza) nyongeza, kur. 1584, 1585.

Kwa kurudia-rudia katika kitabu cha Waebrania (Ebr 7:22; 8:6, 8, 9, 10; 9:4, 15, 16, 17, 20) mwandikaji anatumia neno di·a·the′ke bila shaka kurejezea agano katika ile maana ya zamani ya Kiebrania, hata akinukuu kutoka Yeremia 31:31-34 na kurejezea “sanduku la agano.” Katika kutafsiri mistari hii ya Yeremia, Septuagint ya Kigiriki inatumia di·a·the′ke kwa berith′ la Kiebrania cha kale, linalomaanisha “agano.” Pia, Waebrania 9:20 hunukuu Kutoka 24:6-8, ambapo pasipo shaka lolote agano linazungumziwa.

Utekelezaji wa Ahadi. Sikuzote maagano yalihusisha wahusika wawili au zaidi. Yangeweza kuwa ya upande mmoja (ambapo mhusika katika upande mmoja angeweza kuwa na daraka la yeye pekee kutimiza masharti hayo) au ya pande mbili (ambapo wahusika katika pande zote mbili walikuwa na masharti ya kutimiza). Kando na yale maagano ambayo katika hayo Mungu ni mhusika, Biblia ina maandishi ya maagano yaliyofanywa kati ya wanadamu, na kati ya makabila, mataifa, au vikundi vya watu. Kuvunja agano kulikuwa ni dhambi nzito.—Eze 17:11-20; Ro 1:31, 32.

Neno “agano” linatumiwa kuhusu sheria yenye uhakika, kama lile linalohusu mkate wa wonyesho (Law 24:8), au kuhusu uumbaji wa Mungu unaoongozwa na sheria zake, kama vile mfuatano usioweza kuwa na kigeugeu wa mchana na usiku (Yer 33:20); pia linatumiwa kwa njia ya mfano, kama vile katika usemi “agano pamoja na Kifo.” (Isa 28:18) Pia Yehova anasema juu ya agano kuhusiana na wanyama-mwitu. (Ho 2:18) Mapatano ya ndoa yanaitwa agano. (Mal 2:14) Usemi “wenye (wamiliki) agano” una maana ya “washiriki,” kama vile kwenye Mwanzo 14:13.

Hivyo basi, ahadi yoyote iliyofanywa na Yehova ni agano; hakika itatimizwa, inaweza kutegemewa kwa uhakika kuwa itatimizwa. (Ebr 6:18) Agano linatumika maadamu masharti yake yanatenda kazi na wajibu wa kutenda uko juu ya mhusika mmoja au wote wawili. Matokeo au baraka zinazoletwa na agano zaweza kuendelea, hata milele.

Njia za Kufunga Agano. Mara nyingi Mungu alitajwa kuwa shahidi. (Mwa 31:50; 1Sa 20:8; Eze 17:13, 19) Kiapo kililiwa. (Mwa 31:53; 2Fa 11:4; Zb 110:4; Ebr 7:21) Nyakati nyingine wanadamu walipanga kuwe ishara au ushahidi, kama vile zawadi (Mwa 21:30), nguzo au rundo la mawe (Mwa 31:44-54), au kupaita mahali fulani jina (Mwa 21:31). Pindi moja Yehova alitumia upinde wa mvua. (Mwa 9:12-16) Njia moja ilikuwa ni kuua na kugawana wanyama, wahusika wenye kufanya agano wakipita katikati ya hivyo vipande; ile nahau ya Kiebrania sanifu ‘kata agano’ ilitokana na desturi hii. (Mwa 15:9-11, 17, 18, klz-chn; Yer 34:18, klz-chn, 19) Nyakati nyingine sherehe ziliambatana na kufanywa kwa miungano. (Mwa 26:28, 30) Pengine chakula cha ushirika kingeliwa, kama vile kuhusiana na kufanywa kwa lile agano la Sheria. (Ob 7; Kut 24:5, 11) Pengine yule mhusika mkuu angemkabidhi yule mwingine sehemu fulani ya mavazi au silaha zake. (1Sa 18:3, 4) Baadhi ya mataifa ya kipagani yalifuata desturi ya mtu kunywa damu ya mwenzake au damu iliyochanganywa na divai (ikiwa ni kuvunja sheria ya Mungu aliyowapa watu wote akiwakataza hilo, kwenye Mwanzo 9:4, na kupewa Israeli chini ya ile Sheria), na wenye kufanya agano walimtamkia laana zilizo nzito zaidi mhusika ambaye baadaye angelivunja agano.

Biblia hutumia usemi “agano la chumvi” ili kuonyesha kudumu na kutoweza kugeuzwa kwa agano. (Hes 18:19; 2Nya 13:5; Law 2:13) Kati ya vikundi vya watu wa kale ilikuwa ni ishara ya urafiki kula chumvi pamoja na ilionyesha uaminifu na ushikamanifu wenye kudumu; ulaji wa chumvi pamoja na dhabihu za ushirika ulifananisha ushikamanifu wa kudumu.

Vifaa Vilivyoandikwa. Zile Amri Kumi ziliandikwa juu ya jiwe kwa “kidole cha Mungu” (Kut 31:18; 32:16); Yeremia aliandika hati-miliki, akatia muhuri, na kuchukua mashahidi (Yer 32:9-15); mabamba ya udongo ya vikundi vya watu wa kale yamegunduliwa, ambayo yanaonyesha masharti ya mikataba. Mara nyingi hii ilifungwa ndani ya bahasha za udongo.

Ahadi ya Edeni. Kwenye Mwanzo 3:15, Yehova Mungu alitaja kusudi lake kwa njia ya unabii katika bustani ya Edeni mbele za Adamu, Hawa, na yule “nyoka.”

Kuhusiana na kitambulisho cha wale wanaohusika katika ahadi na unabii huu: Njozi aliyopewa mtume Yohana, kwenye Ufunuo 12:9, inatujulisha kwamba yule “nyoka” ni Shetani Ibilisi. Uthibitisho unaonyesha kwamba “uzao” wa “mwanamke,” uliotafutwa kwa muda mrefu na wanadamu waadilifu, unatambulishwa kuwa “uzao” wa Abrahamu, Yesu Kristo. (Gal 3:16; Mt 1:1) “Uzao” huo ungepondwa kwenye kisigino na nyoka. Yesu Kristo aliuawa, jeraha ambalo hata hivyo halikuwa la kudumu, kwa maana Mungu alimfufua Yesu. Lakini, nao, “uzao” huo ungeponda kichwa cha nyoka, na hivyo kumshinda daima.

“Mwanamke” anayehusika kwenye agano hilo ni nani? Hakika si Hawa, ambaye alikuwa amekuwa adui ya Mungu. Ili ushinde, ‘uangamize’ huyo kiumbe wa roho Shetani Ibilisi, ingehitajika “uzao” huo usiwe wa kibinadamu, bali wa roho. (Ebr 2:14) Yesu alipozaliwa alikuwa Mwana wa Mungu wa kibinadamu, lakini wakati wa ubatizo wa Yesu, Mungu alimtambua kuwa Mwana Wake, akashusha juu yake roho yake takatifu. Hapo Yesu akawa Mwana wa Mungu aliyezaliwa kwa roho. (Mt 3:13-17; Yoh 3:3-5) Baadaye, kwenye ufufuo wake, yeye ‘alifanywa kuwa hai katika roho.” (1Pe 3:18) Basi, ni nani aliyekuwa “mama,” si wa yule mtoto mchanga wa kibinadamu Yesu bali wa Mwana wa Mungu aliyezaliwa kwa roho? Mtume Paulo anasema kwamba Abrahamu, Sara, Isaka, Hagari, na Ishmaeli walihusika katika drama ya mfano, ambayo katika hiyo Isaka aliwakilisha wale waliokuwa na matumaini ya kimbingu, kutia ndani Paulo mwenyewe. Kisha Paulo anasema kwamba “mama” yao ni “Yerusalemu la juu.” Yesu Kristo anawaita hao “ndugu” zake, kuonyesha kwamba wana mama yule mmoja. (Ebr 2:11) Hilo linatupa msingi wa kumtambua “mwanamke” wa Mwanzo 3:15 kuwa ni “Yerusalemu la juu.”—Gal 4:21-29.

Masharti ya ahadi hiyo yanadokeza mpito wa wakati ambao katika huo yule “nyoka” angetokeza “uzao” na uadui ungesitawi kati ya ‘mazao’ hayo mawili. Miaka 6,000 hivi imepita tangu taarifa ya ahadi hiyo. Pindi fupi tu kabla ya Utawala wa Miaka Elfu wa Kristo huyo “nyoka” atatupwa ndani ya abiso ya kutotenda, na kufuatia mwisho wa hiyo miaka elfu yeye ataangamizwa milele.—Ufu 20:1-3, 7-10; Ro 16:20.

Agano Pamoja na Noa. Yehova Mungu alifanya agano pamoja na Noa, aliyewakilisha familia yake, kuhusiana na kusudi Lake la kuhifadhi uhai wa binadamu na wanyama huku akiuharibu ulimwengu mwovu wa siku hiyo. (Mwa 6:17-21; 2Pe 3:6) Noa alianza kupata wana baada ya kuwa na umri wa miaka 500. (Mwa 5:32) Wakati Mungu alipomfunulia Noa kusudi hili, wanawe walikuwa wamekuwa watu wazima na kuoa. Kwa upande wake Noa, alipaswa ajenge safina na kuingiza humo mke wake, wanawe, na wake za wanawe, vilevile wanyama na chakula; Yehova angehifadhi mwili duniani, wa binadamu na wanyama. Matokeo ya Noa kutimiza kwa utiifu masharti ya agano hilo, yalikuwa ni Yehova kuhifadhi uhai wa kibinadamu na wanyama. Agano hilo lilitimizwa kikamili katika 2369 K.W.K., baada ya Gharika, wakati kwa mara nyingine binadamu na wanyama waliweza kuishi tena juu ya ardhi na kuzaa aina yao.—Mwa 8:15-17.

Agano la Upinde wa Mvua. Agano la upinde wa mvua lilifanywa kati ya Yehova Mungu na mwili wote (wa kibinadamu na wanyama), wakiwakilishwa na Noa na familia yake, katika 2369 K.W.K., katika milima ya Ararati. Yehova alisema kwamba hangeharibu tena kamwe mwili wote kwa njia ya gharika. Kisha upinde wa mvua ukatolewa kuwa ishara ya agano hilo, ambalo linadumu maadamu binadamu wanaishi duniani, yaani, milele.—Mwa 9:8-17; Zb 37:29.

Agano Pamoja na Abrahamu. Inaelekea agano pamoja na Abrahamu lilianza kufanya kazi wakati Abramu (Abrahamu) alipovuka Frati akiwa njiani kwenda Kanaani. Agano la Sheria lilifanywa miaka 430 baadaye. (Gal 3:17) Yehova alikuwa amezungumza na Abrahamu alipokuwa akiishi Mesopotamia, katika Uru la Wakaldayo, akamwambia asafiri kwenda kwenye nchi ambayo Mungu angemwonyesha. (Mdo 7:2, 3; Mwa 11:31; 12:1-3) Kutoka 12:40, 41 (LXX) kinatuambia kwamba kwenye mwisho wa miaka 430 ya kukaa Misri na katika nchi ya Kanaani, “siku hiyo hiyo” Israeli, ambao walikuwa wamekuwa katika utumwa Misri, wakatoka. Siku waliyokombolewa kutoka Misri ilikuwa ni Nisan 14, 1513 K.W.K., tarehe ya Pasaka. (Kut 12:2, 6, 7) Inaelekea jambo hilo ni kama linaonyesha kwamba Abrahamu alivuka Mto Frati kuelekea Kanaani mnamo Nisani 14, 1943 K.W.K., na kwa wazi ni wakati huo ambapo agano pamoja na Abrahamu lilianza kufanya kazi. Mungu alimtokea Abrahamu tena baada ya yeye kuwa amesafiri na kuingia Kanaani hadi Shekemu na kuifafanua zaidi ahadi hiyo, akisema, “Nitaupa uzao wako nchi hii,” hivyo akaonyesha uhusiano wa agano hili pamoja na ile ahadi katika Edeni, na kufunua kwamba ule “uzao” ungepitia njia ya kibinadamu, yaani, ungepitia nasaba ya kibinadamu. (Mwa 12:4-7) Mafafanuzi zaidi yalisemwa baadaye, kama ambavyo imeandikwa kwenye Mwanzo 13:14-17; 15:18; 17:2-8, 19; 22:15-18.

Ahadi za agano hilo zilipitishwa kwa vizazi vya Abrahamu vya baadaye kupitia Isaka (Mwa 26:2-4) na Yakobo. (Mwa 28:13-15; 35:11, 12) Mtume Paulo anasema kwamba Kristo (akiwa wa kwanza) na wale walio katika muungano na Kristo ndio “uzao” wa kweli.—Gal 3:16, 28, 29.

Mungu alifunua kusudi na mambo yenye kutimizwa na agano la Abrahamu, akisema kwamba kupitia Abrahamu, uzao wa ahadi ungekuja; uzao huo ungemiliki lango la maadui zake; uzao wa Abrahamu kupitia Isaka ungekuwa idadi kubwa, isiyoweza kuhesabiwa na binadamu wakati huo; jina la Abrahamu lingefanywa kuwa kuu; uzao huo ungeimiliki Nchi ya Ahadi; familia zote za dunia zingejibariki kupitia uzao huo. (Ona maandiko yaliyoko juu kutoka Mwanzo.) Kulikuwa na utimizo wa kihalisi wa mambo hayo, uliokuwa ufananisho wa utimizo mkubwa zaidi kupitia Kristo. Paulo anatoa habari ya ziada kuhusu namna ya ufananisho na ya kinabii ya masharti ya agano hili anaposema kwamba Abrahamu, Sara, Isaka, Hagari, na Ishmaeli waliigiza drama ya mfano.—Gal 4:21-31.

Agano pamoja na Abrahamu ni “agano la mpaka wakati usio na kipimo.” Masharti yake yanataka kwamba liendelee hadi uharibifu wa adui zote wa Mungu na familia zote za dunia ziwe zimebarikiwa.—Mwa 17:7; 1Ko 15:23-26.

Akizungumza juu ya agano la Abrahamu na lile la Sheria, Paulo alitaja kanuni kwamba “hakuna mpatanishi mahali ambapo ni mtu mmoja tu anayehusika,” na kisha akaongeza kwamba “Mungu ni mmoja tu.” (Gal 3:20; ona MEDIATOR.) Yehova alifanya agano pamoja na Abrahamu likihusisha upande mmoja. Kwa kweli hilo lilikuwa ni ahadi, naye Yehova hakuweka masharti ambayo ilikuwa lazima Abrahamu atimize ili ahadi hiyo itimizwe. (Gal 3:18) Kwa hiyo, hapana mpatanishi aliyehitajiwa. Kwa upande mwingine, lile agano la Sheria lilihusisha pande mbili. Lilifanywa kati ya Yehova na taifa la Israeli, na Musa akiwa mpatanishi. Waisraeli walikubali masharti ya agano hilo, wakatoa ahadi takatifu kuwa wataitii Sheria hiyo. (Kut 24:3-8) Agano hili la baadaye halikulitangua lile agano pamoja na Abrahamu.—Gal 3:17, 19.

Agano la Tohara. Agano la tohara lilifanywa katika 1919 K.W.K., Abrahamu alipokuwa na umri wa miaka 99. Yehova alifanya agano hilo pamoja na Abrahamu na uzao wake wa asili; watu wote wa kiume wa nyumba yake, kutia ndani watumwa, walipaswa kutahiriwa; yeyote aliyekataa alipaswa kukatiliwa mbali na watu wake. (Mwa 17:9-14) Baadaye, Mungu alisema kwamba mkaaji-mgeni yeyote aliyetaka kula pasaka (mtu aliyetaka kuwa mwabudu wa Yehova pamoja na Israeli) angepaswa kutahiri watu wa kiume wa nyumba yake. (Kut 12:48, 49) Tohara ilitumika kama muhuri wa uadilifu ambao Abrahamu alikuwa nao kupitia imani alipokuwa katika hali ya kutotahiriwa, nayo ilikuwa ni ishara ya kimwili ya uhusiano wa agano wa wazao wa Abrahamu kupitia Yakobo, ambao walikuwa nao na Yehova. (Ro 4:11, 12) Mungu aliikubali tohara hadi mwisho wa agano la Sheria, katika 33 W.K. (Ro 2:25-28; 1Ko 7:19; Mdo 15) Japo tohara ya kimwili iliendelezwa chini ya ile Sheria, Yehova alirudia kuonyesha kwamba yeye alipendezwa zaidi na maana yake ya mfano, akiwashauri Israeli ‘watahiri govi la mioyo yao.’—Kum 10:16; Law 26:41; Yer 9:26; Mdo 7:51.

Agano la Sheria. Agano la Sheria kati ya Yehova na taifa la Israeli wa asili lilifanywa katika mwezi wa tatu baada ya wao kuondoka Misri, katika 1513 K.W.K. (Kut 19:1) Hilo lilikuwa ni agano la kitaifa. Mtu aliyezaliwa akiwa Mwisraeli wa asili aliingia ndani ya agano la Sheria pale alipozaliwa na kwa hiyo alikuwa ndani ya uhusiano wa pekee pamoja na Yehova. Sheria hiyo ilikuwa kwa namna ya orodha, ikiwa imepangwa kwa utaratibu, sheria zake zikiwa zimewekwa katika vifungu-vifungu. Sheria hiyo, iliyowasilishwa kupitia malaika kwa mkono wa mpatanishi, Musa, ilifanywa ikaanza kutenda kazi kupitia dhabihu za wanyama (badala ya Musa, aliyekuwa mpatanishi, au “mfanya-agano”) kwenye Mlima Sinai. (Gal 3:19; Ebr 2:2; 9:16-20) Wakati huo Musa alinyunyiza juu ya madhabahu nusu ya damu ya wanyama waliotolewa dhabihu, kisha akawasomea watu kitabu cha agano, nao wakakubali kuwa watiifu. Baadaye alinyunyiza ile damu juu ya kile kitabu na juu ya watu hao. (Kut 24:3-8) Chini ya sheria, ukuhani ulisimamishwa katika nyumba ya Haruni, wa familia ya Kohathi wa kabila la Lawi. (Hes 3:1-3, 10) Ukuhani mkuu ulipitishwa kwa vizazi kutoka kwa Haruni hadi kwa wanawe, Eleazari akimfuata Haruni, Finehasi akimfuata Eleazari, na kadhalika.—Hes 20:25-28; Yos 24:33; Amu 20:27, 28.

Masharti ya agano la Sheria yalikuwa kwamba ikiwa Waisraeli wangelishika agano hilo wangekuwa kikundi cha watu kwa ajili ya jina la Yehova, ufalme wa makuhani na taifa takatifu, wakiwa na baraka Zake (Kut 19:5, 6; Kum 28:1-14); kama wangelivunja agano, wangelaaniwa. (Kum 28:15-68) Makusudi yake yalikuwa ni: kudhihirisha makosa (Gal 3:19); kuwaongoza Wayahudi kwa Kristo (Gal 3:24); kuwa kivuli cha mambo mazuri ya baadaye (Ebr 10:1; Kol 2:17); kuwalinda Wayahudi kutokana na dini ya uongo ya kipagani na kuhifadhi ibada ya kweli ya Yehova; kulinda nasaba ya uzao ulioahidiwa. Likiwa pamoja na lile agano lililofanywa pamoja na Abrahamu (Gal 3:17-19), lilipanga kitengenezo taifa-uzao wa asili wa Abrahamu kupitia Isaka na Yakobo.

Agano la Sheria lilipanua baraka zifikie wengine wasiokuwa Israeli wa asili, kwa maana wao wangeweza kuwa wageuzwa-imani, watahiriwe, na kupokea nyingi kati ya zile faida za Sheria.—Kut 12:48, 49.

Ni jinsi gani agano la Sheria likaja ‘kuchakaa’?

Hata hivyo, agano la Sheria ‘lilichakaa’ katika maana fulani wakati Mungu alipotangaza kupitia nabii Yeremia kwamba kungekuwa na agano jipya. (Yer 31:31-34; Ebr 8:13) Katika 33 W.K. agano la Sheria lilifutwa kwa msingi wa kifo cha Kristo juu ya mti wa mateso (Kol 2:14), mahali pake pakachukuliwa na agano jipya.—Ebr 7:12; 9:15; Mdo 2:1-4.

Agano Pamoja na Kabila la Lawi. Yehova alifanya agano pamoja na kabila la Lawi, kwamba kabila zima linapasa kuwekwa kando wawe watumishi waliofanywa kuwa tengenezo wa lile hema, kutia ndani ukuhani. Hili lilifanyika kwenye nyika ya Sinai, katika 1512 K.W.K. (Kut 40:2, 12-16; Mal 2:4) Haruni na wanawe, wa familia ya Kohathi, wangekuwa makuhani, zile familia nyingine za Lawi zitunze kazi nyinginezo, kama vile kusimamisha hema, kulihamisha, na mambo mengine. (Hes 3:6-13; sura 4) Baadaye, walitumikia vivyo hivyo kwenye hekalu. (1Nya 23) Shughuli za utumishi wa kuweka ukuhani zilifanywa Nisani 1-7, 1512 K.W.K., nao wakaanza kutumikia Nisani 8. (Law sura 8, 9) Walawi hawakuwa na urithi katika nchi hiyo, bali walipokea zaka kutoka kwa yale makabila mengine, nao walikuwa na majiji waliyotengewa ya kuishi. (Hes 18:23, 24; Yos 21:41) Kwa sababu ya bidii ya Finehasi ya kujitoa kikamili kwa Yehova, Mungu alifanya agano la amani pamoja naye, agano kwa ajili ya ukuhani hadi wakati usio na kipimo kwa ajili yake na wazao wake. (Hes 25:10-13) Agano pamoja na Lawi liliendelea kutenda kazi mpaka mwisho wa lile agano la Sheria.—Ebr 7:12.

Agano Pamoja na Israeli Huko Moabu. Pindi fupi tu kabla ya Israeli kuingia Nchi ya Ahadi, katika 1473 K.W.K., Yehova alifanya agano pamoja na Israeli wa asili huko Moabu. (Kum 29:1; 1:3) Hapa sehemu kubwa ya ile Sheria ilitajwa tena na kuelezwa na Musa. Kusudi la agano hilo lilikuwa liwatie watu moyo wawe waaminifu kwa Yehova na kufanya marekebisho na kuweka sheria fulani zilizokuwa za lazima kwa Waisraeli walipokuwa wakifanya badiliko kutoka kwenye maisha ya kutanga-tanga hadi kwenye maisha ya ustakimu katika nchi hiyo. (Kum 5:1, 2, 32, 33; 6:1; linganisha Law 17:3-5 na Kum 12:15, 21.) Agano hili lilimalizika wakati agano la Sheria lilipoondolewa, kwa maana hilo lilikuwa sehemu ya msingi ya hiyo Sheria.

Agano Pamoja na Mfalme Daudi. Agano pamoja Daudi lilifanywa pindi fulani wakati wa utawala wa Daudi katika Yerusalemu (1070-1038 K.W.K.), wahusika wakiwa ni Yehova na Daudi akiwa anawakilisha familia yake. (2Sa 7:11-16) Masharti ya agano hilo yalikuwa kwamba mwana fulani kutoka kwa wazao wa Daudi angerithi kiti cha ufalme milele, na kwamba mwana huyu angejenga nyumba kwa ajili ya jina la Yehova. Kusudi la Mungu katika agano hilo lilikuwa ni kuwapa Wayahudi nasaba ya kifalme; kumpa Yesu, akiwa mrithi wa Daudi, haki ya kisheria ya kiti cha ufalme cha Daudi, “kiti cha ufalme cha Yehova” (1Nya 29:23; Lu 1:32); na kuandaa kitambulisho kwa ajili ya Yesu akiwa Masihi. (Eze 21:25-27; Mt 1:6-16; Lu 3:23-31) Agano hili halikutia ndani ukuhani wowote; ukuhani wa Walawi ulitumika ukishirikiana na wafalme wa nasaba ya Daudi; chini ya ile Sheria, ukuhani na ufalme vilitenganishwa kabisa. Kwa kuwa Yehova anaukubali ufalme huo naye anafanya kazi kupitia huo milele, agano hilo linadumu milele.—Isa 9:7; 2Pe 1:11.

Agano la Kuwa Kuhani Kama Melkizedeki. Agano hilo linatajwa kwenye Zaburi 110:4, na mwandikaji wa kitabu cha Biblia cha Waebrania analitumia kumhusu Kristo kwenye 7:1-3, 15-17. Ni agano ambalo limefanywa na Yehova pamoja na Yesu Kristo peke yake. Inaonekana Yesu alilirejezea alipokuwa akifanya agano kwa ajili ya ufalme na wafuasi wake. (Lu 22:29) Kwa kiapo cha Yehova, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu wa kimbingu, angekuwa kuhani kulingana na ile namna ya Melkizedeki. Melkizedeki alikuwa mfalme na kuhani wa Mungu duniani. Yesu Kristo angeshikilia vyeo vyote viwili vya kuwa Mfalme na Kuhani Mkuu huko mbinguni, wala si duniani. Yeye aliwekwa akae daima kwenye cheo baada ya kupanda mbinguni. (Ebr 6:20; 7:26, 28; 8:1) Agano hilo ni lenye kutenda kazi milele, kwa kuwa Yesu atatenda akiwa Mfalme na Kuhani Mkuu milele chini ya mwelekezo wa Yehova.—Ebr 7:3.

Agano Jipya. Yehova alitabiri kuhusu agano jipya kupitia nabii Yeremia katika karne ya saba K.W.K., akieleza kwamba halingekuwa kama agano la Sheria ambalo Waisraeli walilivunja. (Yer 31:​31-34) Yesu Kristo alipoanzisha mwadhimisho wa Mlo wa Jioni wa Bwana katika usiku wa Nisani 14, 33 W.K., alitangaza kwamba agano jipya lingehalalishwa kwa dhabihu aliyotoa. (Lu 22:20) Siku 50 baada ya ufufuo wake na siku 10 baada ya kupaa kwenda kwa Baba yake, alimimina roho takatifu aliyopokea kutoka kwa Yehova juu wanafunzi wake waliokuwa wamekusanyika katika chumba cha juu huko Yerusalemu.​—Mdo 2:​1-4, 17, 33; 2 Ko 3:​6, 8, 9; Ebr 2:​3, 4.

Washiriki wa agano jipya ni Yehova na “Israeli wa Mungu,” waliozaliwa kwa roho katika muungano na Kristo ambao wanafanyiza kutaniko lake au mwili wake. (Ebr 8:10; 12:​22-24; Gal 6:​15, 16; 3:​26-28; Ro 2:​28, 29) Agano jipya linatendeshwa kwa damu iliyomwagwa (dhabihu ya uhai wa mwanadamu) ya Yesu Kristo, na aliwasilisha thamani yake mbele za Yehova baada ya kupaa kwenda mbinguni. (Mt 26:28) Mtu anapochaguliwa na Mungu na kupokea mwito wa kwenda mbinguni (Ebr 3:1), Mungu anamfanya mtu huyo awe mshiriki wa agano Lake kwa msingi wa dhabihu ya Kristo. (Zb 50:5; Ebr 9:​14, 15, 26) Yesu Kristo ndiye mpatanishi wa agano jipya (Ebr 8:6; 9:15) na ndiye sehemu kuu ya Uzao wa Abrahamu. (Gal 3:16) Kwa kuwapatanisha kwa njia ya agano jipya, Yesu anawasaidia wale walio kwenye agano hilo kuwa sehemu ya uzao halisi wa Abrahamu (Ebr 2:16; Gal 3:29) kupitia msamaha wa dhambi zao. Yehova anawatangaza kuwa waadilifu.​—Ro 5:​1, 2; 8:33; Ebr 10:​16, 17.

Hawa ndugu watiwa-mafuta wa Kristo, waliozaliwa kwa roho, wanakuwa makuhani wadogo wa yule Kuhani Mkuu, “ukuhani wa kifalme.” (1Pe 2:9; Ufu 5:9, 10; 20:6) Wao wanafanya kazi ya kikuhani, “utumishi wa watu wote” (Flp 2:17), na wanaitwa “wahudumu wa agano jipya.” (2Ko 3:6) Ni lazima hawa walioitwa wafuate kwa ukaribu sana hatua za Kristo, kwa uaminifu, hadi kutoa maisha zao katika kifo; kisha Yehova atawafanya kuwa ufalme wa makuhani, awafanye kuwa washiriki wa asili ya kimungu, na kuwathawabisha na hali ya kutoweza kufa na kutoharibika wakiwa warithi-wenzi mbinguni pamoja na Kristo. (1Pe 2:21; Ro 6:3, 4; 1Ko 15:53; 1Pe 1:4; 2Pe 1:4) Kusudi la agano hilo ni kutwaa kikundi cha watu kwa ajili ya jina la Yehova wakiwa sehemu ya “uzao” wa Abrahamu. (Mdo 15:14) Wanakuwa “bibi-arusi” wa Kristo, nao ni jamii ya watu ambao Kristo huingiza katika agano kwa ajili ya Ufalme, watawale pamoja Naye. (Yoh 3:29; 2Ko 11:2; Ufu 21:9; Lu 22:29; Ufu 1:4-6; 5:9, 10; 20:6) Lile kusudi la agano jipya linataka kwamba liendelee kutenda kazi mpaka “Israeli wa Mungu” wote wawe wamefufuliwa wakiwa na hali ya kutoweza kufa mbinguni.

Agano la Yesu Pamoja na Wafuasi Wake. Kwenye usiku wa Nisani 14, 33 W.K., baada ya kusherehekea Mlo wa Jioni wa Bwana, Yesu alifanya agano hili pamoja na mitume wake waaminifu. Yeye aliwaahidi mitume wake waaminifu 11 kwamba wangeketi juu ya viti vya ufalme. (Lu 22:28-30; linganisha 2Ti 2:12.) Baadaye, alionyesha kwamba ahadi hiyo iliwahusisha ‘washindi’ wote waliozaliwa kwa roho. (Ufu 3:21; ona pia Ufu 1:4-6; 5:9, 10; 20:6.) Kwenye siku ya Pentekoste yeye aliwazindulia agano hili kwa kuwatia mafuta kwa roho takatifu wanafunzi wale waliokuwapo katika chumba cha juu katika Yerusalemu. (Mdo 2:1-4, 33) Wale ambao wangeshikamana naye kupitia majaribu, wafe kifo cha aina aliyokufa (Flp 3:10; Kol 1:24), wangetawala pamoja naye, waushiriki utawala wake wa Ufalme. Agano hilo linaendelea kutenda kazi milele kati ya Yesu Kristo na wafalme hawa wenzi.—Ufu 22:5.

Maagano Mengine Mbalimbali. (a) Yoshua na wakuu wa Israeli pamoja na wakaaji wa jiji la Gibeoni kuwaruhusu kuendelea kuishi. Ingawa wao walikuwa Wakanaani waliolaaniwa, ambao Waisraeli walipaswa kuwaharibu, hata hivyo agano lilionwa kuwa lenye kufunga sana hivi kwamba Wagibeoni wakaruhusiwa waishi, lakini laana hiyo ikatekelezwa kwa kuwafanya wawe wakusanya-kuni na wateka-maji kwa ajili ya kusanyiko la Israeli. (Yos 9:15, 16, 23-27) (b) Yoshua pamoja na Israeli kumtumikia Yehova. (Yos 24:25, 26) (c) Wanaume wazee wa Gileadi pamoja na Yeftha huko Mispa kumfanya awe mkuu wa wakaaji wa Gileadi ikiwa Yehova angempa ushindi juu ya Waamoni. (Amu 11:8-11) (d) Kati ya Yonathani na Daudi. (1Sa 18:3; 23:18) (e) Yehoyada kuhani pamoja na wakuu wa walinzi wa Wakari na wa wakimbiaji. (2Fa 11:4; 2Nya 23:1-3) (f) Israeli pamoja na Yehova kufukuza wake wageni. (Ezr 10:3) (g) Yehova kutoa mtumishi wake awe agano la (kwa ajili ya) watu. (Isa 42:6; 49:8) (h) Daudi pamoja na wanaume wazee wote wa Israeli, huko Hebroni. (1Nya 11:3) (i) Agano la watu, wakati wa utawala wa Asa, kumtafuta Yehova kwa moyo wao wote na nafsi. (2Nya 15:12) (j) Yosia pamoja na Yehova kutunza amri za Yehova, kulingana na ile Sheria. (2Nya 34:31) (k) Wale “wenye kujigamba” waliotawala Yerusalemu walikuwa wanafikiria kimakosa walikuwa salama katika “agano pamoja na Kifo.”—Isa 28:14, 15, 18.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki