Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • it kur. 121-123
  • Mwadhimisho wa Miaka 50

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwadhimisho wa Miaka 50
  • Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Habari Zinazolingana
  • Yehova Ameandaa Njia ya Kukuweka Huru
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2019
  • Yubile ya Yehova—Wakati Wetu Kufurahi Sana
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Mwadhimisho wa Miaka 50 na Uhuru wa Wakati Ujao
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2021
Pata Habari Zaidi
Ufahamu wa Kina wa Maandiko
it kur. 121-123

MWADHIMISHO WA MIAKA 50

Mwadhimisho huo ulifanywa mwaka uliofuata mzunguko wa vipindi saba vya miaka 7, nao ulihesabiwa kuanzia wakati Waisraeli walipoingia kwenye Nchi ya Ahadi. Neno la Kiebrania yoh·velʹ (au, yo·velʹ) linamaanisha “pembe ya kondoo dume,” na linarejelea kupuliza pembe ya kondoo dume katika mwaka wa 50 ili kutangaza uhuru katika nchi yote.​—Law 25:9, 10; onaPEMBE.

Tangu taifa la Israeli lilipoingia katika Nchi ya Ahadi, Waisraeli walipaswa kuhesabu miaka sita ya kulima, kupanda mbegu, na kuvuna; lakini mwaka wa saba ulipaswa kuwa mwaka wa sabato, nchi haikupaswa kulimwa mwaka huo. Mwaka wa saba hawakupaswa kupanda au kupunguza matawi ya mimea. Hata hawakupaswa kuvuna nafaka iliyoanguka na kuota baada ya mavuno ya mwaka uliotangulia wala kuchuma zabibu kutoka kwenye mizabibu ambayo haikuwa imepunguzwa matawi. Mwenye shamba, watumwa wake, wafanyakazi wake waliokodiwa, wakaaji wageni, na maskini wangekula nafaka na matunda yaliyomea yenyewe. Wanyama wa kufugwa na wa mwituni waliruhusiwa pia kula nafaka na matunda hayo. (Law 25:2-7; Kut 23:10, 11) Walipaswa kuhesabu vipindi hivyo saba vyenye urefu wa miaka saba (7 x 7 = 49), na mwaka uliofuata, mwaka wa 50, ulikuwa mwaka wa Mwadhimisho wa Miaka 50.

Mwaka wa mwadhimisho wa miaka 50 ulifanana na mwaka wa sabato. Kwa mara nyingine tena nchi ilipata pumziko kamili. Walifuata maagizo yaleyale kuhusu mazao ya nchi. (Law 25:8-12) Kwa hiyo, mavuno ya mwaka wa 48 katika kila kipindi cha miaka 50 yaliliwa mwaka huo na zaidi ya miaka miwili hivi iliyofuata mpaka walipopata mavuno ya mwaka wa 51, yaani, mwaka uliofuata Mwadhimisho wa Miaka 50. Kwa sababu ya baraka za pekee za Yehova katika mwaka wa sita, walipata mavuno ya kutosha kuliwa mwaka wote wa Sabato. (Law 25:20-22) Vivyo hivyo, Wayahudi walipotii Sheria yake, Yehova aliwapa mavuno mengi ya kutosha katika mwaka wa 48 ambayo yangeliwa na taifa hilo mwaka wote wa Sabato, mwaka wa Mwadhimisho wa Miaka 50, na hadi wakati wa mavuno ya mwaka uliofuata.

Mwaka wote wa Mwadhimisho wa Miaka 50 ulikuwa mwaka wa sherehe, mwaka wa uhuru. Waisraeli walipofanya mwadhimisho huo walionyesha kwamba wana imani katika Mungu wao Yehova na pia ulikuwa wakati wa kushukuru na kufurahia maandalizi yake.

Pembe (shoh·pharʹ, au sho·pharʹ, pembe ya mnyama iliyopindika) ilipigwa siku ya kumi ya mwezi wa saba (mwezi wa Tishri), Siku ya Kufunika Dhambi, ili kutangaza uhuru nchini kote. Siku hiyo, watumwa Waebrania, ambao wengi wao walijiuza wenyewe kwa sababu ya madeni waliwekwa huru. Kwa kawaida waliwekwa huru mwaka wa saba wa utumwa (Kut 21:2), lakini Mwadhimisho wa Miaka 50 ulipofika hata wale waliotumikia chini ya miaka sita waliwekwa huru. Ardhi yote ya urithi iliyokuwa imeuzwa (mara nyingi kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi) ilirudishwa, na kila mtu alirudi kwa familia yake na kwa urithi wake. Hakuna familia iliyopaswa kuwa na ufukara wa kudumu. Kila familia ilipaswa kustahiwa na kuheshimiwa. Hata mtu aliyefuja mali yake hangeweza kupoteza urithi wake kabisa kwa sababu ya wazao wake. Kwa kweli, nchi yote ilikuwa ya Yehova, na Waisraeli wenyewe walikuwa wageni na wahamiaji machoni pa Yehova. (Law 25:23, 24) Ikiwa taifa hilo lingetii sheria zake, basi kama Mungu alivyosema, ‘Hakuna yeyote kati yao angepaswa kuwa maskini.’​—Law 25:8-10, 13; Kum 15:4, 5.

Kwa sababu ya sheria hiyo ya Mwadhimisho wa Miaka 50, hakuna ardhi yoyote ambayo ingeuzwa milele. Mungu alisema kwamba ikiwa mtu angeuza ardhi yoyote ya urithi, bei ya ardhi hiyo ingekadiriwa kulingana idadi ya miaka iliyobaki kabla ya Mwadhimisho wa Miaka 50. Sheria hiyohiyo ilifuatwa ardhi ya urithi iliponunuliwa tena na mmiliki wake. Kwa hiyo, kilichouzwa ni matumizi ya ardhi hiyo na mazao yake kwa miaka iliyobaki kabla ya mwaka wa Mwadhimisho wa Miaka 50. (Law 25:15, 16, 23-28) Sheria hiyo ilihusu nyumba zilizokuwa katika vijiji ambavyo havikuzingirwa na ukuta, ambazo zilihesabiwa kama mashamba; lakini nyumba zilizokuwa katika majiji yaliyozingirwa hazikuwa kati ya mali iliyorudishwa wakati wa Mwadhimisho wa Miaka 50. Hata hivyo, sheria hiyo haikuhusu nyumba za Walawi, kwa kuwa walimiliki tu nyumba na malisho yaliyozingira majiji ya Walawi. Nyumba zao zilirudishwa wakati wa Mwadhimisho wa Miaka 50; malisho ya majiji ya Walawi hayakupaswa kuuzwa.​—Law 25:29-34.

Mtu anaweza kuthamini zaidi uandalizi huo mzuri wa Mwadhimisho wa Miaka 50 anapofikiria, si faida alizopata Mwisraeli mmoja-mmoja, bali pia taifa lote. Mpango huo wa Mwadhimisho wa Miaka 50 ulipofuatwa ifaavyo, taifa hilo lilirudia hali yake mwaka huo na kuwa taifa lililoongozwa ifaavyo kitheokrasi kama Mungu alivyokusudia na alivyoanzisha mwanzoni. Serikali ilikuwa na msingi mzuri. Sikuzote uchumi wa taifa ungekuwa imara, na taifa halingekuwa na deni. (Kum 15:6) Mwadhimisho wa Miaka 50 uliweka kiwango cha bei ya ardhi na pia uliwazuia watu kuwa na madeni makubwa, jambo linalofanya ionekane kana kwamba kuna ufanisi nchini lakini linalosababisha mfumuko wa bei, vitu kupoteza thamani, na kudorora kwa biashara.

Walipotii sheria ya Mwadhimisho wa Miaka 50, taifa lao lililindwa dhidi ya hali mbaya tunayoona leo katika nchi nyingi ambazo zina makundi mawili tu ya watu, matajiri kupindukia na maskini hohehahe. Faida walizopata watu binafsi ziliimarisha taifa hilo, kwa maana hakuna aliyekandamizwa sana na hali mbaya ya kiuchumi, na kila mtu angeweza kutumia kipaji chake na uwezo wake kuboresha masilahi ya taifa. Ikiwa Waisraeli wangetii, Yehova angebariki mazao yao na kuwaelimisha, nao wangefurahia serikali bora kabisa na ufanisi ambao unaweza kuletwa tu na utawala wa Yehova.​—Isa 33:22.

Watu walisomewa Sheria katika miaka ya Sabato, hasa wakati wa Sherehe ya Vibanda, au ya Kukusanya. (Kum 31:10-12) Kwa hiyo wangemkaribia Yehova zaidi na kuendelea kuwa huru. Yehova aliwaonya Waisraeli kwamba wangepatwa na msiba ikiwa hawangetii na ikiwa wangeendelea kupuuza sheria zake (zilizotia ndani sheria za mwaka wa Sabato na Mwadhimisho wa Miaka 50).​—Law 26:27-45.

Tukihesabu kuanzia mwaka ambao Waisraeli waliingia katika Nchi ya Ahadi, Mwadhimisho wa kwanza wa Miaka 50 ulianza mwezi wa Tishri 1424 K.W.K. (Law 25:2-4, 8-10) Tangu walipoingia katika Nchi ya Ahadi mwaka wa 1473 K.W.K. mpaka Yerusalemu lilipoanguka mwaka wa 607 K.W.K., Waisraeli walipaswa kusherehekea Miadhimisho 17 ya Miaka 50. Lakini kama historia inavyoonyesha inasikitisha kwamba hawakumthamini Yehova akiwa Mfalme wao. Hatimaye walivunja amri zake, kutia ndani sheria za Sabato, na hivyo wakapoteza baraka alizokuwa amewaahidi. Kutotii kwao kulimletea Yehova suto mbele ya mataifa ya ulimwengu na kuwazuia kuona ubora wa serikali yake ya kitheokrasi.​—2 Nya 36:20, 21.

Maana ya Mfano. Mpango wa Mwadhimisho wa Miaka 50 umerejelewa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Yesu Kristo alisema kwamba alikuja ‘kuwatangazia mateka uhuru.’ (Lu 4:16-18) Baadaye alisema hivi kuhusu kuweka huru kutoka katika utumwa wa dhambi: “Mwana akiwaweka ninyi huru, kwa kweli mtakuwa huru.” (Yoh 8:36) Kwa sababu Wakristo watiwa-mafuta walitangazwa kuwa waadilifu ili wapate uzima, nao walizaliwa wakiwa wana wa Mungu kuanzia Pentekoste ya 33 W.K., mtume Paulo aliandika hivi: “Sheria ya roho ambayo hutokeza uzima katika muungano na Kristo Yesu imewaweka ninyi huru kutoka katika sheria ya dhambi na kifo.” (Ro 8:2) Wakati wa Utawala wa Kristo wa Miaka Elfu Moja, wengine pia, kama andiko la Waroma 8:19-21 linavyosema, ‘watawekwa huru kutoka katika utumwa wa uharibifu’ na, baada ya kudumisha ushikamanifu wao kwa Yehova chini ya jaribu, ‘watakuwa na uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu.’ Watawekwa huru kutoka katika dhambi waliyorithi na pia kifo kinachosababishwa na dhambi hiyo. Waabudu wa kweli wataimiliki dunia tena ili waitunze kulingana na kusudi la kwanza kabisa la Yehova kwa ajili ya wanadamu.​—Ufu 21:4; Mwa 1:28; Isa 65:21-25.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki