RUTHU
Mwanamke Mmoabu aliyeolewa na Maloni. Maloni na mama yake, Naomi, na kaka yake Kilioni, waliishi Moabu. Maloni alimwoa Ruthu baada ya baba yake Elimeleki kufa. Njaa kali ilikuwa imewafanya wahame kutoka kwenye mji wao wa Bethlehemu ya Yuda. Kilioni, shemeji ya Ruthu alikuwa amemwoa mwanamke Mmoabu aliyeitwa Orpa. Baada ya muda, ndugu hao wawili walikufa na kuwaacha wajane wawili bila watoto. Naomi alipopata habari kwamba Yehova ameanza tena kuwaonyesha kibali Waisraeli, alirudi Yuda pamoja na binti wakwe zake.—Ru 1:1-7; 4:9, 10.
Upendo Wake Mshikamanifu. Ingawa mwishowe Orpa alirudi kwa watu wake baada ya Naomi kumwomba afanye hivyo, Ruthu alishikamana na mama mkwe wake. Upendo wake mwingi kumwelekea Naomi na tamaa yake ya kutoka moyoni ya kumtumikia Yehova pamoja na watu wake ulimsaidia Ruthu kuacha wazazi wake na nchi aliyozaliwa, akiwa na tumaini dogo sana la kupata ulinzi ambao ndoa huleta. (Ru 1:8-17; 2:11) Upendo wake kwa mama mkwe wake ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba baadaye watu walisema kwamba Naomi alikuwa amepata binti bora kuliko wana saba.—Ru 4:15.
Walipofika Bethlehemu mwanzoni mwa mavuno ya shayiri, kwa niaba yake na Naomi, Ruthu alienda kutafuta chakula kwenye mashamba. Kwa tukio alifika kwenye shamba la Boazi, mtu wa ukoo wa Elimeleki, kisha akaomba ruhusu ya kuokota masalio kutoka kwa msimamizi wa wavunaji. Bidii yake ya kuokota masalio ilikuwa ya pekee sana kwa kuwa msimamizi alimtajia Boazi jambo hilo.—Ru 1:22–2:7.
Ruthu alipoonyeshwa fadhili na Boazi, alionyesha uthamini mkubwa na kwa unyenyekevu akasema kwamba yeye ni mdogo kuliko vijakazi wa Boazi. Wakati wa mlo Boazi alimpa nafaka nyingi zilizokaangwa hivi kwamba akabakiza kwa ajili ya Naomi. (Ru 2:8-14, 18) Ingawa Boazi alifanya mipango ili iwe rahisi kwa Ruthu kuokota masalio, Ruthu hakuacha kazi mapema badala yake aliendelea mpaka jioni, “alipoyapura, alipata karibu efa moja [lita 22; vibaba 20] ya shayiri.” Boazi alimwomba Ruthu aendelee kuokota masalio katika shamba lake, naye aliendelea kwa kipindi chote kilichosalia cha mavuno ya shayiri, na mavuno ya ngano pia.—Ru 2:15-23.
Boazi Aombwa Awe Mkombozi. Kwa kuwa Naomi alitamani kumpa Ruthu “mahali pa kupumzika,” Naomi alimwagiza Ruthu amwombe Boazi amkomboe. Kwa hiyo, Ruthu alienda kwenye uwanja wa kupuria wa Boazi. Baada ya Boazi kulala, Ruthu alikuja kimyakimya, akafunua miguu yake, na kulala miguuni pake. Katikati ya usiku, Boazi alianza kutetemeka na akaamka. Kwa kuwa hakumtambua gizani, akauliza “Wewe ni nani?” Ruthu akajibu: “Mimi ni Ruthu, kijakazi wako. Nifunike mimi kijakazi wako kwa vazi lako, kwa maana wewe ni mkombozi.”—Ru 3:1-9.
Jambo ambalo Ruthu alifanya kwa kufuata maagizo ya Naomi, yalipatana na desturi zilizofuatwa na wanawake waliotaka kupata haki ya kufunga ndoa ya ndugu mkwe. Kwenye kitabu Lange’s Commentary on the Holy Scripture, Paulus Cassel anasema hivi kuhusu Ruthu 3:9: “Bila shaka njia hii ya kuomba haki iliyohitaji uangalifu mkubwa, ilifunua tabia ya kale yenye adili na isiyohusisha mambo mengi. Uhakika wa mwanamke huyo unategemea heshima ya mwanamume anayehusika. Hata hivyo, njia iliyotumiwa haikuwa rahisi. Kwa sababu ikiwa jambo hilo lingejulikana mapema, heshima ya aliyefanya ombi hilo ingeharibika na jambo hilo halingekuwa siri tena. Lakini hatua hiyo ilipochukuliwa, ombi lililotolewa halingeweza kukataliwa bila kumwaibisha ama mwanamke au mwanamume aliyehusika. Hivyo, tunaweza kuwa na hakika kwamba Naomi alimtuma binti mkwe wake akiwa na uhakika kabisa kwamba atafanikiwa. Pamoja na changamoto nyingine zote, kulikuwa na changamoto nyingine ya pekee katika kisa hiki kwamba: Boazi, kama Ruthu mwenyewe anavyosema, alikuwa kwa kweli, mkombozi, lakini si mkombozi mwenye haki ya kwanza. Pia, jibu la Boazi linadokeza kwamba hilo lilikuwa jambo lililotazamiwa. Boazi alikuwa peke yake kwenye uwanja wa kupuria na alishtuka sana alipoamka kutoka usingizini na kumwona Ruthu. Hilo linafunua kwamba hakuwa amefanya mapatano yoyote na Naomi. Lakini wazo la kwamba angehusika ikiwa Ruthu angedai haki ya kufunga ndoa ya ndugu mkwe kutoka kwa mtu wa ukoo wake halikuwa jambo lililomshangaza sana. Hata iwe matokeo yangekuwa nini, bado Ruthu angehitaji kutumia uhuru wake wa kuchagua kwa kufuata utaratibu huo.—Imetafsiriwa na kuhaririwa na P. Schaff, 1976, uku. 42.
Boazi alimwona Ruthu kuwa mwenye maadili mazuri kwa sababu alisema hivi: “Yehova na akubariki, binti yangu. Wakati huu, umetenda kwa upendo mshikamanifu zaidi kuliko mwanzoni, kwa kuwa hukuwafuata wale vijana, matajiri au maskini.” Bila ubinafsi wowote Ruthu alimchagua Boazi, mwanamume mwenye umri mkubwa zaidi, kwa sababu alikuwa mkombozi, ili aendeleze jina la mume wake aliyekufa na jina la mama mkwe wake. Lingekuwa jambo la kawaida kwa mwanamke kijana kama Ruthu kuchagua mwanamume mchanga zaidi, hivyo Boazi aliona jambo hilo kuwa ishara ya upendo wake mshikamanifu kuliko hata alipochagua kushikamana na mama mkwe wake aliyezeeka.—Ru 3:10.
Hapana shaka sauti ya Ruthu ilifunua kwamba alikuwa na wasiwasi, kwa kuwa bila kukawia Boazi alimhakikishia hivi: “Sasa binti yangu, usiogope. Nitakufanyia kila jambo utakalosema, kwa maana kila mtu jijini anajua kwamba wewe ni mwanamke bora.” Ilikuwa usiku sana, basi Boazi akamwagiza Ruthu aendelee kulala. Hata hivyo, wote wawili waliamka kungali giza, labda ili kuepuka kuanzisha uvumi ambao ungeleta sifa mbaya juu ya mmoja wao. Pia, Boazi alimpa Ruthu vipimo sita vya shayiri. Huenda hilo lilionyesha kwamba, kama tu ambavyo pumziko lilifuata baada ya kufanya kazi kwa siku sita, pumziko la Ruthu lilikuwa linakaribia, kwa kuwa Boazi angehakikisha kwamba Ruthu amepata “mahali pa kupumzika.”—Ru 3:1 maelezo ya chini, 11-15, 17, 18.
Alipofika nyumbani, huenda Naomi hakumtambua mwanamke aliyekuwa gizani na aliyetaka kukaribishwa ndani, hivyo aliuliza hivi: “Wewe ni nani?” Au huenda swali hilo lilihusu uhusiano mpya ambao Ruthu alikuwa nao pamoja na mtu aliyemkomboa.—Ru 3:16.
Baadaye, mtu wa ukoo wa karibu alipokataa kufunga ndoa ya ndugu mkwe, Boazi alifanya hivyo bila kukawia. Hivyo, Ruthu akawa mama ya Obedi mwana wa Boazi, na bibi ya Mfalme Daudi na pia Yesu Kristo.—Ru 4:1-21; Mt 1:5, 16.