Yehova Atoa “Thawabu Kamili”
“[Yehova] na akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na [Yehova], Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake.” Rut. 2:12.
1-3. (a) Mazungumzo kati ya Naomi na Ruthu yanaonyesha nini juu ya kupashana habari katika jamaa inayopendana? (b) Ni mshangao gani uliotokea wakati Ruthu alipomwambia Naomi habari za kazi yake ya kuokota katika siku hiyo, na kwa hiyo ni uongozi wa nani unaoonekana?
“NA UPEWE thawabu kamili na [Yehova].” Ndivyo Mzee Boazi alivyokuwa amemwambia Ruthu Mmoabi. Hivyo ndivyo alivyokuwa amemtakia kwa moyo wote mwanamke huyu kijana ambaye alikuwa ametafuta ulinzi chini ya mabawa ya Mungu wa Israeli. (Rut. 2:12) Je! ingekuwa kama alivyotakiwa? Kama ndivyo, kwa njia gani? Tutaona.
2 Katika jamaa yenye upendo, wazee wanapendezwa na utendaji wa vijana. Wote wanakaribisha nafasi za kushiriki mawazo na kueleza utendaji wa siku. Nyumba alimokaa Naomi na Ruthu katika Bethlehemu haikuwa tofauti. Walishiriki katika mazungumzo yenye kupendeza saa za jioni. Sikiliza!
3 “Je! umeokota wapi leo? umefanya kazi wapi?” Kiasi kizuri cha nafaka na chakula ambacho Ruthu ameleta nyumbani kimefanya Naomi aulize hivyo. Kwa wazi, mtu fulani amemfikiria Mmoabi huyu kwa njia ya pekee. “Na abarikiwe yeye aliyekufahamu,” asema mwanamke huyo mzee. Lakini kila mmoja wao atapata jambo la kushangaza lenye kutia moyo. “Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo, jina lake aitwa Boazi,” ajibu Ruthu. Ni vyema namna gani! Bila shaka uongozi wa Yehova unaonekana wazi. “Na abarikiwe huyo na [Yehova], ambaye hakuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwao waliokufa,” asema Naomi kwa kupaza sauti. “Mtu huyu ni wa mbari yetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu [“mkombozi,” NW].”-Rut. 2:19, 20.
4. Ungemwelezaje “mkombozi” katika Israeli wa kale?
4 Jinsi roho zao zainuliwa! Wanawake hawa wanajua kwamba mkombozi (Kiebrania, go·ʼelʹ) ni mtu wa jamaa ya karibu (ndugu au mwanamume mwingine yo yote wa jamaa) aliye na haki ya kukomboa au kumnunua tena mtu, mali au urithi wa mtu wa jamaa ya karibu. Kwa mfano, anaweza kununua sehemu ya shamba ya urithi kabla ya kuuzwa kwa watu wengine wa nje na kwa njia hiyo iendelee kuwa katika jamaa hiyo. Ebu fiikiria! Kwa majaliwa Ruthu ameingia katika shamba la Boazi na yeye ni mkombozi, mtu wa jamaa ya Elimeleki.
5. Tofauti na alivyokuwa Dina binti Yakobo. Ruthu anatoa mfano gani juu ya kushirikiana na wengine?
5 Tena, Boazi anataka Ruthu aendelee kufuatana na wasichana wake wafanya kazi mpaka mavuno yote yamalizike. Bila shaka, Naomi anakubali, akisema: “Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, wala watu wasikukute katika konde linginelo lote.” Kwa hiyo Mmoabi huyo ataendelea kuokota mavuno katika shamba la Boazi kwa muda wa miezi miwili au mitatu, mpaka mavuno ya shayiri na ya ngano yamalizike. Tofauti na alivyokuwa Dina binti ya Yakobo, aliyefuatana na wasichana wa Kanaani akajiletea msiba yeye mwenyewe na kuiletea jamaa yake taabu, Ruthu anaendelea kukaa na mkewe, na wakati uo huo akiangalia mashirika yake. Mfano mwema sana!—Rut. 2:22, 23; Mwa. 34:1-31; 1 Kor. 15:33.
UNYENYEKEVU WATENDA KAZI
6. Naomi anaonyeshaje kwamba anataka Ruthu ajifurahishe mambo mazuri?
6 Majuma yapita na mavuno yakaribia kumalizika. Naomi amwuliza Ruthu hivi: “Je! mwanangu, si vizuri nikutafutie raha [“mahali pa kupumzika,” NW] , ili upate mema?” (Rut. 3:1) Mjane huyu mzee hajaribu kumweka kijana huyu Mmoabi akae naye kwa uchoyo, bali anataka Ruthu apate pumziko, faraja, kutulia kwa moyo na usalama unaoweza kupatikana katika nyumba ya mume mwema na mwenye upendo. Lakini Naomi pia anahangaikia kuendelezwa kwa jina la mumewe Elimeleki katika Israeli. (Kum. 25:7) Kupatana na jambo hili, anaeleza mpango wa kitendo cha pekee, naye mkwewe mnyenyekevu anafurahia kukubaliana nao. Kwa hiyo Ruthu anaoga, na kujipaka mafuta, na kuvaa mavazi yake, na kutoka aende katika kazi kuu aliyotumwa afanye.
7. Katika kupepeta shayiri, Boazi anafuata mpango gani?
7 Kwa wakati huo, Boazi—mtu mwenye mali, lakini pia mwenye kufanya kazi kwa nguvu—amekuwa akitumia vizuri upepo wa jioni akipepeta shayiri katika sakafu ya kupuria nafaka. Kupura kumezitoa nafaka katika maganda yake, nayo majani yake makavu yamekatwakatwa sehemu ndogo-ndogo. Sasa, katika kupepeta, hivi vyote vinatupwa juu hewani katika upande unakotoka upepo kwa kutumia kiuma au jembe la kupepetea. Upepo unapeperusha makapi, na kupeleka majani makavu upande mmoja, na kuziacha nafaka zianguke sakafuni ya kupuria nafaka. Huu ni wakati wenye furaha, na kwa hiyo kazi hizi gumu zinafuatwa na chakula kizuri. Boazi ala na kunywa na moyo wake “umekunjuka,” ingawaje haionekani kwamba amekula na kunywa kupita kiasi. (Zab. 104:15) Halafu alala “penye mwisho wa chungu ya nafaka,” na mara baada ya hapo analala usingizi mzito nje chini ya mbingu zenye nyota zenye kung’aa—Rut. 3:1-7.
8. Ni kitendo gani anachochukua Ruthu juu ya Boazi sakafuni ya kupuria nafaka, na je! Kusudi lake ni la uasherati?
8 Kunakuwa kimya mpaka umbo lenye kivuli lakaribia polepole kwa kimya, bila kuonekana. Ni mwanamke, ambaye anamfunua Boazi mwenye usingizi miguuni pake na kulala hapo akiwa bado anavaa mavazi yake yote. Usiku wa manane anaanza kutetemeka, ainama mbele, na kushtuka kwa kumwona mwanamke amelala, kwa wazi kwa kukingama, miguuni pake! Kwa kushindwa kumtambua gizani, anauliza: “Ama! ni nani wewe?” Anasikia jibu: “Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako.” Lakini anaongeza kwa haraka: “Uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu [“mkombozi,” NW].” (Law. 25:25) Ingawa Boazi anashangaa sana, yeye hakuona haya wala hakukasirika. Wala huyu Mmoabi hako hapo kwa kusudi la uasherati. Kwa njia hii ya tendo hili la mfano na kwa maneno yake, yeye ametimiza maagizo ya Naomi kwa unyenyekevu. Ruthu amemfanya Myahudi huyu ajue daraka lake la kuwa mkombozi, mtu wa jamaa ya karibu wa mumewe marehemu Maloni na babaye aliyekufa Elimeleki. Naomi alikuwa na hakika kwamba mpango huu utatimia, na bila shaka kijana huyu mwanamke alikuwa na hakika kwamba Boazi angemtendea kwa heshima. (Rut. 3:4, 7-9) Lakini yeye Boazi atafanya nini?
9. (a) Jinsi gani Ruthu ameonyesha fadhili za upendo katika kile Boazi anachokiita “mwanzo” na “mwisho”? (b) Je! Ruthu ni “mwanamke mwema” kwa sababu ya mali, mtindo wa nywele na mavazi yenye bei, au namna gani?
9 Boazi ambarikia na kumsifu Mmoabi huyu mnyenyekevu na mshikamanifu, akisema: “Mwanangu, ubarikiwe na [Yehova]; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo, kwa vile usivyowafuata vijana, kama ni maskini kama ni matajiri.” Mwanzoni, Ruthu alimwonyesha Naomi upendo msikamanifu. Na sasa badala ya kutafuta urafiki na vijana wenye umri wa kuoa, mwanamke huyu Mmoabi ana nia ya kuolewa na mwanamume mzee zaidi, ili afanyize jina kwa mumewe marehemu Maloni, na mkwewe, mjane mzee wa Elimeleki. Lakini Boazi anaonaje juu ya jambo hili? Kwa kumpa moyo, anasema: “Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.” Ruthu hakutangaza sifa zake, na bila shaka si mali, mtindo wa nywele na mavazi yenye thamani yanayowafanya wengine wamsifu. Badala yake, kumcha Yehova, kazi zake nzuri, roho yake tulivu, na ya upole, upendo wake mshikamanifu, bidii yake—vitendo na sifa kama hizi zimewafanya watu wamwone kuwa “mwanamke mwema.” Je! kuna mwanamke anayemwogopa Mungu ye yote aliye hai ambaye hangependa kuwa na sifa nzuri kama hiyo?—Rut. 3:10, 11; linganisha Mithali 31:28-31; 1 Timotheo 2:9, 10; 1 Petro 3:3, 4.
10. Kwa sababu gani Ruthu hatakuwa mke wa Boazi mara hiyo?
10 Je! Boazi atamchukua Ruthu mara moja awe mkewe? Hapana, kwa sababu kuna mwanamume wa jamaa ya Elimeleki na Maloni aliye karibu zaidi. “Lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa [“mkombozi,” NW] ,” asema Boazi kwa kiapo, “[kama Yehova] aishivyo.” Boazi ataangalia jambo hilo asubuhi.—Rut. 3:13.
11. Ni kitu gani, kinachomfanya Boazi ampe Ruthu vipimo sita vya shayiri?
11 Kwa kuwa ni usiku, Boazi amwambia Ruthu akae mpaka mapema asubuhi. Lakini hakukufanyika uasherati wo wote, na wanaamka kukiwa bado kuna giza, kwa Wazi ili kuzuia uvumi mbaya usio na msingi. Kabla Mmoabi huyo kuondoka, Boazi alijaza vazi lake kwa vipimo sita vya shayiri, labda akionyesha kwamba, kama vile siku sita za kazi zinavyofuatwa na siku ya mapumziko, hivyo ndivyo siku ya mapumziko kwa huyo mwanamke kijana ilivyokuwa inakaribia, kwa kuwa atachukua daraka la kuona kwamba mwanamke huyo amepata “mahali pa kupumzika,” nyumba na mume. (Rut. 1:9; 3:1, NW) ‘Bila shaka, Boazi mkarimu hataki Ruthu amrudie mkwewe akiwa mikono mitupu.
12. Kwa sababu gani Naomi anauliza: “Wewe ni nani, binti yangu?”
12 Hatimaye yule Mmoabi afika nyumbani, naye Naomi amwuliza: “Je! mwanangu, imekuwaje? [“Wewe ni nani, binti yangu?”, NW] ” Labda hamtambui yule anayetaka afunguliwe gizani, lakini ulizo hili huenda likahusiana (patana) na kitambulisho kipya cha Ruthu kuhusiana (kupatana) na mkombozi wake. Baada ya kuambiwa yaliyotukia usiku wa jana, Naomi ana tumaini kamili kwamba Boazi atafanya kulingana na alivyosema na atafanya hivyo upesi sana. “Basi, mwanangu, tulia; hata utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili,” amsihi mwanamke huyo kijana, akiongeza katika hekima yake ya kike na ufahamu wa hali ya kibinadamu hivi: “Kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.”—Rut. 3:12-18.
13. Tunaweza kufaidikaje kwa kuchunguza imani ya Naomi na Ruthu?
13 Wajane hao wawili wanapongojea katika makao yao hayo ya kimaskini, tunaweza kuchunguza imani yao kwa faida. Je! sisi tunawatumaini waamini wenzetu kama Naomi? Je! tunamtegemea Yehova wakati wa taabu, tukiwa na uhakika kwamba mipango yake ni bora zaidi kama Ruthu? (Zab. 37:3-5; 138:8) Ebu mfikirie Ruthu. Yeye hata hamjui mwanamume huyu wa jamaa aliye na haki ya kwanza katika jambo hili; yeye hajui lo lote juu ya tabia zake, hata hivyo yeye ana nia ya kukubaliana na sheria ya Yehova juu ya kuolewa na ndugu ya mume marehemu. Ni lazima awe na hakika kwamba Mungu atafanya mambo yote yawe sawa. Kwa kulinganisha, je! sisi wenyewe tunakuwa na hakika kwamba Yehova “anafanya kazi zote zishirikiane pamoja kwa faida ya wale wanaompenda Mungu”?—Rom. 8:28, NW; 1 Pet. 5:6, 7.
BOAZI ATENDA KULINGANA NA UAMUZI WAKE
14, 15. (a) Ni nani mkombozi yule aliye jamaa wa Elimeleki aliye karibu kuliko Boazi? (b) Kwa wazi, afanye nini, na kwa hiyo ni jambo gani linalohitajiwa kufanywa, ama na jamaa yule aliye wa karibu zaidi au na Boazi?
14 Mwangaza wa siku mpya waangaza Bethlehemu. Watu wanatembea barabarani zake, wanabiashara wanaonyesha bidhaa zao, watu vikundi vikundi wanaongea uwanjani mbele ya lango la mji nao wakulima wanaondoka kwenda kazini katika mashamba yao yanayouzunguka mji. Naye Boazi anakaa hapa langoni pa mji. Macho yake yanachunguza nyuso za watu wanaopita. Kwa ghafula, anaita kwa sauti: “Haya! wewe [“Fulani,” NW] karibu, uketi hapa.” (Rut. 4:1) Basi, mwanamume huyu asiyetajwa jina lake ndiye mkombozi aliye wa jamaa ya karibu zaidi ya Elimeleki kuliko Boazi. Huenda ikawa yeye alikuwa ndugu ya kimwili wa marehemu Elimeleki.
15 Langoni pa mji ndipo shughuli (kazi) zote za kibiashara zinapoandikishwa na ndipo wazee wanakaa na kuamua kesi. Kwa hiyo, kwa kuwa Boazi alikuwa karibu kuwakilisha Naomi na Ruthu katika jambo hili la kukomboa na kufanya ndoa na mke wa ndugu marehemu, yeye anakusanya wazee 10 wa mji wa Bethlehemu papo hapo langoni. (Kum. 16:18; 22:15; 25:7, 8) Halafu Boazi amwambia mkombozi aliye Karibu zaidi: “Naomi, . . . anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu [au, jamaa] yetu, Elimeleki,” kwa wazi ni kwa sababu ya hali yake ya umaskini. (Rut. 4:3) Ikiwa Mwisraeli maskini analazimika kuuza shamba la jamaa, mtu wa jamaa aliye karibu (au mkombozi) ndiye aliyekuwa na haki ya kuikomboa kwa kulipa bei inayolingana na hesabu ya miaka inayobaki mpaka kufikia wakati wa yubile, wakati ambapo mali hiyo ya urithi ingerudishiwa mwenyewe. (Law. 25:23-25) Badala ya kujaribu kumpita jamaa aliye karibu zaidi na kuinunua shamba hiyo kwa siri, mheshimiwa Boazi kwa kufaa anajulisha mambo hayo hadharani. Ikiwa jamaa huyo wa karibu zaidi ataikomboa, vema; ikiwa sivyo Boazi atafanya hivyo.
16, 17. Ikiwa mtu huyo wa jamaa asiyetajwa jina anataka kununua shamba hilo kutoka kwa Naomi, ni lazima afanye jambo gani jingine? Amefanya nini juu ya jambo hilo?
16 “Nitaikomboa mimi,” asema jamaa huyu aliye karibu zaidi. Kwa wazi anafurahia kulipata shamba hilo kwa njia hiyo aongeze mashamba yake. Lakini atashtushwa, kwa sababu Boazi anaendelea kusema: “Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu [Maloni mwana wa Elimeleki], ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake.” (Rut. 4:4, 5) Ikiwa mtu huyu wa jamaa anataka shamba hilo, ana wajibu wa kumwoa Ruthu amzalie jamaa yake mtoto—mwana ambaye atarithi shamba hilo.
17 Sasa, hilo ni jambo tofauti kabisa. “Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafasi yangu, nisije nikaharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa.” (Rut. 4:6) Jinsi mtu huyu wa jamaa ‘angeharibu urithi wake mwenyewe’ yeye hasemi. Lakini angetumia fedha kwa ajili ya shamba hilo, na kwa kadiri hiyo angepunguza thamani (bei) ya mali yake. Halafu tena mwana wa Ruthu, wala si wana wo wote ambao mtu huyu wa jamaa ya karibu zaidi anaweza kuwa anao, ndiye angerithi shamba hilo. Fulani mchoyo hataki jambo lo lote kama hilo! Kwa hiyo, ‘ujichukulie wewe mwenyewe, Boazi.’
18, 19. Jamaa huyu wa karibu zaidi anakana haki yake ya kukomboa kwa kitendo gani katika habari hii, na kwa hiyo Boazi anafanya nini?
18 Kwa hiyo, mtu huyo wa jamaa ya karibu asiyetajwa jina lake afanya kulingana na desturi inayofuatwa kuhusu (kupatana) na haki ya kukomboa na kubadilishana. Anavua kimojawapo viatu vyake na kumpa Boazi. Kwa kufanya hivyo mbele ya mashahidi, yeye anakana haki yake ya kukomboa katika jambo hili. Bila shaka mwenendo wake wa choyo ndiyo sababu hatajwi kwa jina lake. Sasa Boazi ana haki ya kukomboa.—Rut. 4:7, 8; Kum. 25:7-10.
19 Bila kukawia, Boazi ananunua kutoka kwa Naomi vitu vyote vilivyokuwa vya Elimeleki na wanawe Kilioni na Maloni. Pia, anamnunua Ruthu ‘awe mke wake, makusudi apate kumwinulia marehemu [Maloni] jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake.’ Ndiyo, jina la Maloni, na kwa hiyo jina la babaye Elimeleki, litakumbukwa na watu pamoja na wazee wakusanyikapo langoni pa mji wa Bethlehemu wakati ujao. “Ninyi ni mashahidi,” asema Boazi. Katika kushuhudia, watu wote na wazee wanapaza sauti na kusema: “Sisi tu mashahidi.”—Rut. 4:9-11.
YEHOVA AMTOLEA RUTHU “THAWABU KAMILI”
20. Mashahidi hawa wanatamani Yehova ampe nina mke anayekuja katika nyumba ya Boazi na ni nani wanayesifu kwa sababu ya mwana ambaye angezaliwa kupitia kwa Ruthu?
20 Ni jambo la kupendeza kusikia mashahidi hawa wakiendelea kusema hivi: “[Yehova] na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli [kwa kuwa wana wao walikuwa wengi sana]. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu. Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi [yenye watu wengi sana], ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa [Yehova] katika mwanamke huyu.” (Rut. 4:11, 12) Ndiyo, mashahidi hawa tayari wanamsifu Yehova kwa sababu ya mwana huyo ambaye angezaliwa kupitia kwa Ruthu, yule Mmoabi mshikamanifu.
21, 22. Ni kwa sababu gani wanawake jirani wanasema: “Naomi amezaliwa mwana”?
21 Ndipo Boazi anapomtwaa Ruthu akawa mke wake na kufanya ngono naye, Yehova amjalia kuchukua mimba, na kuzaa mtoto wa kiume. Kunakuwa na furaha namna gani! Wanawake wa Bethlehemu wanamwambia Naomi mwenye furaha: “Na ahimidiwe [Yehova], asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu [au, mkombozi]; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli. Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto [wa asili wa kiume] saba, ndiye aliyemzaa.” Naomi mwenye furaha amchukua mtoto huyu kifuani pake na kuwa mlezi, au mtunzaji wake—Rut. 4:13-16.
22 “Naomi amezaliwa mwana,” wasema wanawake jirani. Wanamwona mtoto huyo kama mwana wa Elimeleki na mjane wake. Na kwa sababu gani isiwe hivyo? Ruthu alikuwa mke wa Boazi badala ya Naomi aliyekuwa mzee, kulingana na sheria ya kumwoa mke wa ndugu marehemu. Boazi na Ruthu wamefanya utumishi kwa Yehova, na ni jambo la kuangaliwa kwamba wanawake jirani wanamwita mtoto huyo Obedi, maana yake “mtumishi” au “anayetumikia.” Mtoto huyo ndiye aliye na haki ya kuwa mrithi katika nyumba ya Kiyahudi ya Elimeleki.—Rut. 4:17.
23. Boazi ametumiwaje katika baraka aliyomtakia Ruthu?
23 Miezi fulani imepita tangu Boazi alipomwambia Ruthu: “[Yehova] na akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na [Yehova].” (Rut. 2:12) Sasa, kwa kumzaa Obedi, Boazi ametumiwa katika baraka aliyomtakia mwanamke huyu kijana Mmoabi. Siku moja, Obedi, wa ukoo wa Yuda kupitia kwa Peresi, Hesroni, Ramu, Aminadabu, Nashoni, Salmoni na Boazi, atapata mwana aitwaye Yese, ambaye atakuwa baba ya Daudi, mfalme wa pili wa Israeli.—Rut. 4:18-22.
24. (a) Tamasha ambayo tumekwisha kuchunguza inatoa ushuhuda wa uongozi wa Mungu juu ya jambo gani? (b) Hivyo basi, “thawabu kamili” aliyopewa Ruthu na Yehova ilikuwa nini?
24 Katika tamasha hii ya kweli ya watu walioishi tunapata ushuhuda wa uongozi wa Mungu katika kuchagua watu mmoja mmoja katika kutunza nasaba iliyo ya maana zaidi, ile inayoongoza kwenye Masihi, Yesu Kristo. Ni kweli kwamba, wanawake Waisraeli walioolewa na wanaume wa kabila la Yuda walikuwa na nafasi ya kushiriki katika nasaba ya kidunia ya Masihi. (Mwa. 49:10) Walakini, ya kwamba mwanamke Mmoabi alipendelewa hivyo inaonyesha kanuni ya kwamba “[inategemea] si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye yaani, Mungu.” (Rum. 9:16) Ruthu alikuwa amemchagua Yehova awe Mungu wake, na kwa rehema nyingi yeye alimpa “thawabu kamili” katika kumruhusu mwanamke huyu mnyenyekevu awe kiungo katika nasaba ya Masihi.—Mt. 1:3-6; Luka 3:23, 31-33.
25. Kuchunguza kwetu “thawabu kamili” ambayo Ruthu alipewa na Mungu kunapaswa kutufanye tuoneje?
25 Bila shaka, hiyo “thawabu kamili” aliyopewa Ruthu mshikamanifu na Mungu inapaswa iwasukume watu wenye kufikiri wamkaribie yeye wakiwa na imani kamili, wakiwa na tumaini kabisa kwamba Yehova yuko na ya kwamba yeye “huwapa thawabu wale wamtafutao.” (Ebr. 11:6) Ndiyo, kitabu cha Ruthu kinamwonyesha Yehova kuwa Mungu wa upendo ambaye hutenda kwa faida ya wale waliojitoa kwake. Zaidi ya hayo, kinashuhudia kwamba kusudi la Mungu halishindwi hata kidogo. Hivyo, tunaweza na tunapaswa kuwa na roho kama ile aliyoionyesha Daudi, aliyesema: “[Tutashangilia] wokovu wako, kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. [Yehova] akutimizie matakwa yako yote. Sasa najua kuwa [Yehova] amwokoa masihi wake; atamjibu toka mbingu zake takatifu, kwa matendo makuu ya wokovu ya mkono wake wa kuume.”—Zab. 20:5, 6. —Kutoka The Watchtower Feb. 15,1978
[Picha katika ukurasa wa 13]
“Ama! ni nani wewe?” auliza Boazi. “Ni mimi, Ruthu, mjaka wako”