Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w78 10/15 kur. 20-24
  • ‘Mdogo Akawa Elfu’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Mdogo Akawa Elfu’
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ZIARA YA KWANZA KATIKA AFRIKA
  • NJIA ZA KUFUNDISHIA
  • KURUDI KATIKA VISIWA VYA CARIBBEAN
  • Walimwita “Bible” Brown
    2014 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
  • Urithi Mkubwa wa Kiroho Ulinisaidia Kusitawi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2019
  • ‘Upendo Haupungui Wakati Wowote’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Sehemu ya 2—Kuwa Mashahidi Hadi Sehemu ya Mbali Zaidi Sana ya Dunia
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
w78 10/15 kur. 20-24

‘Mdogo Akawa Elfu’

Imesimuliwa na W. R. Brown

KUJITAWALA kulikuwa kunakaribia katika Nigeria Koloni ya Uingereza katika masika ya mwaka wa 1960. Katika maandalio ya tukio hilo Dakt. Nnamdi Azikiwe gavana mkuu aliiambia Baraza yake ya Mawaziri: “Sasa viongozi wote wa kidini wamekwisha alikwa, namna gani juu ya kiongozi au mwenye kuwakilisha Mashahidi wa Yehova?” Wengine wa Baraza ya mawaziri kutia na viongozi fulani wa kidini walipinga wakisema kwamba Mashahidi wa Yehova wanajiepusha na siasa zote na kwa hiyo hawakusaidia serikali. Kusikia hayo Dakt. Azikiwe, niliyemjua kwa miaka mingi, alijibu: “Kama dini zote zingekuwa kama Mashahidi wa Yehova, tusingekuwa na mauaji, ukosefu wa utii kwa watoto, maabusu wafungwa na bomu za atomiki. Milango haingekuwa ikifungwa usiku na mchana.” Mawaziri wote wa Baraza hiyo walinyamaza kimya. Ndipo gavana mkuu alipomalizia akisema: “Mwalikeni Bw. Brown awakilishe Mashahidi wa Yehova.”

Hilo linaeleza sababu ya simu niliyoipokea nikiwa Trinidad karibu na mwisho wa mwaka 1959, ikitualika mimi na mke wangu tutembelee nchi ya Nigeria kwa mara nyingine, gharama zote zikiwa zimelipiwa. Tulikubali mwaliko huo kwa furaha. Septemba iliyofuata, baada ya kutua kidogo katika New York na London, tulifika katika uwanja wa ndege wa Ikeja huko Nigeria, ambapo afisa mmoja alitusalimu. “Gari hilo jipya ni lenu,” akasema, “kuwapeleka po pote mtakapo katika Nigeria mpaka mtakapoondoka nchini humu. Mtu huyu ndiye dereva wenu.” Tulikwenda mpaka makao ya Gavana, ambapo Dakt. Azikiwe alitulaki. Alikuwa amepanga ili sisi tutumie chumba chao cha kulala wakati wa ziara yetu.

Siku chache baadaye wakuu wenye vyeo vya juu na wake zao walikuja kwenye chakula cha mchana. Miongoni mwao alikuwako mjumbe wa Malkia, Maulana Perth, na aliyekuwa gavana wa Jamaica na Nigeria hapo zamani, Bw. Mheshimiwa Arthur Richards. Dakt. Azikiwe alituita kwenye meza ya chakula ambapo sote tuliketishwa isipokuwa mimi na mke wangu. “Nimemjua Bw. na Bi. Brown kwa muda wa zaidi ya miaka thelathini,” akasema Dakt. Azikiwe, “na wameongeza sana hali ya kiroho ya watu wetu wa Nigeria, kwa hiyo, Bw. Brown keti katika mahali pa heshima zaidi mezani, nawe Bi. Brown keti mahali pale pengine upande mwingine wa meza.”

Bila mashaka gavana mkuu wa Nigeria alionyesha kuthamini sana kazi yetu sisi Mashahidi wa Yehova. Lakini naweza kukumbuka wakati kazi yetu ilipokuwa haijulikani, si Nigeria peke yake, bali pia Afrika yote ya Magharibi. Hiyo ndiyo sababu Hakimu Rutherford msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society alikuwa amenialika pamoja na jamaa yangu ndogo kutoka katika visiwa vya Carribean upande mwingine wa Bahari ya Atlantic mpaka pwani ya magharibi ya Afrika. Nilifurahi sana kukubali mgawo huo.

ZIARA YA KWANZA KATIKA AFRIKA

Mimi, mke wangu na mtoto wangu tulifika katika Freetown, Sierra Leone, Aprili 1923. Zamani hizo hatukuwa wageni wa mkuu ye yote wa serikali. Kwa kweli hata hatukujua ni wapi tungeishi. Nilimwuliza mwenyeji mmoja, “Je! kuna hoteli humu?” akanijibu, “Kuna mbili. Moja inaangaliwa na Mzungu, na nyingine inaangaliwa na mwanamke mwenyeji. Je! unaiona nyumba ile yenye orofa tatu iliyoko pale? Nenda hapo na utapatiwa mahali pa kukaa.” Tulipewa chumba cha kukaa, safi na chenye baridi ya kiasi.

Kwa kutumia magazeti ya huko na vikaratasi nilitangazia watu mfululizo wa hotuba katika Jumba la Wilberforce Memorial. Kichwa cha kwanza kilikuwa “Roho Walioko Kifungoni​—Ni Nani? Kwa Nini Wako Humo? Yesu Aliwahubirije?” Mji huo ulioamshwa ulitaka kujua mtu huyu anayeitwa Brown alitoka wapi na ni nini anachokusudia kusema. Jumba hilo kubwa lilijaa sana, na mamia mengi alirudishwa. Viongozi wa dini wapatao sita wakivalia nguo zao za ukasisi walijiunga na watu katika kushangilia wakati jambo kuu baada ya jingine lilipokuwa likitajwa na kuelezwa vizuri. Makutano walienda zao wakiwa wametosheka na maelezo yaliyotolewa, unaweza kuwazia furaha yangu. Kichwa cha hotuba ya Jumapili iliyofuata kiliwafanya wafikiri na kusema. “Je! umesikia ya karibuni?” wakasema. “Unaweza kwenda kaburini na kurudi!”

Jumapili hiyo umati mwingine wa wasikilizaji ulikuja ukasikiliza hotuba: “Kwenda kaburini na kurudi​—Ni Nani Walioko Huko?” Tena wasikilizaji walishangilia sababu nyingi za Biblia na matokeo yake yakawa kwamba wenye vyeo katika dini waliokuja kusikiliza hotuba hiyo waliacha dini zao na kujiunga na tengenezo la Yehova. Viongozi wa dini waliona lililokuwa likitendeka wakaanza kunishambulia kupitia kwa magazeti.

Shambulio la magazeti liliposhindwa, walijipatia jengo kubwa liitwalo Kanisa la Buxton, na wakijifananisha na wapiganaji na wanyama katika michezo ya kale ya kirumi, walitoa mfululizo wa hotuba sita kila jioni. Yule wakili waliomweka kama mwenyekiti wao mwishowe aliwaambia kwamba wamekwisha shindwa kunyamazisha “Ufuasi wa Russel,” kama vile walivyouita. Katika gazeti la kila siku niliwaita washindane nami. Katika mahojiano sita hadharani kwa muda wa saa mbili kila jioni juu ya habari mbalimbali. Walikataa wakamkemea mhariri wa gazeti hilo kwa kuandika mwito wangu wa kushindana nao bila kuwauliza kwanza. Baada ya hapo kazi ya kutoa ushuhuda katika Freetown ilikuwa nyepesi.

Niliendelea kuhubiri zaidi na kutoa hotuba baada ya hapo naye Yehova akatupa ongezeko kundi la Freetown likaendelea kupanuka. Nilitembelea Bathurst, Gambia, katika mwaka wa 1927 na nikatoa ushuhuda katika Liberia katika Jumba la Mawakili nikiangusha vitabu vingi vya kujifunza Biblia. Vilevile, nilipata pendeleo la kufika Ghana na Nigeria, nikiwa na gari langu lenye vikuza sauti. Viongozi wa dini katika Nigeria walifadhaishwa na ushuhuda wangu nilioutoa kwa uhodari wakaanza kuukomesha.

Wakati huo watu wote hawakuheshimu sana kile walichokiita “dini ya wazungu.” Ilifaa sana nikahutubu katika jumba la Glover Memorial juu ya kushindwa kwa dini za Jumuiya ya Wakristo. Kwa hiyo nilitangaza hotuba hiyo katika magazeti matatu makubwa ya humo nchini. Mhariri Mkatoliki alituma maandishi yangu kwa Dakt. Moses Da Rocha, aliyeandika barua ichapwe pamoja na matangazo yangu. Alisihi serikali ya Nigeria ikataze mikutano yangu au itume polisi ihifadhi amani. Aliwaambia viongozi wa kidini mbalimbali katika mji wa Lagos watume mawakili wao walio na uwezo kabisa kwenye mikutano yangu na kuharibu kabisa “mafundisho ya uzushi” wangu. Polisi na mawakili wengi wa makanisa walifika.

Wakati wa kufunua wazi uongo wa Jumuiya ya Wakristo wasikilizaji walikuwa wakikatiza-katiza hotuba kwa kushangilia. Wakati wa maulizo ulipofika, mwana mmoja wa kiongozi wa dini ya Kianglikana aliuliza maulizo mawili, ambayo yalijibiwa akajaribu la tatu, lakini nikasema: “Tafadhali keti uwape wengine nafasi waulize.” Maulizo mengine yaliulizwa yakajibiwa na wasikilizaji wakatosheka. Nilifunga mkutano nikawatolea kitabu kilichofungwa kwa jalada ya karatasi kiitwacho Deliverance kwa bei nafuu. Vitabu tulivyokuwa tumevileta kwenye jumba vikiwa katika vibweta vilikwisha na hata wakaja nyumbani kwangu jioni hiyo wapate vingine zaidi. Tulipohesabu tuliona kwamba walikuwa wamechukua vitabu 3,900! Walienda kotekote wakiwaangushia jirani zao vitabu hivyo. Ilikuwa siku yenye furaha katika utumishi wa umisionari.

NJIA ZA KUFUNDISHIA

Nilipokuwa nikitoa hotuba nilikuwa nikitumia vipande vya picha, hiyo ilinisaidia kuonyesha kila Andiko katika kiwambo cha nguo na kulieleza. Watu walipata ufahamu mwingi wa Maandiko kisha wakaandika barua nyingi kwa Sosaiti wakitaka Biblia. Hivyo ndivyo nilivyoanza kuitwa “Bible Brown,” jina la kupewa ambalo linajulikana sana katika pwani ya Afrika magharibi.

Nilipokuwa nikiingia kijiji nikiwa na gari langu lenye vikuza sauti nilikuwa nikimwendea chifu (mkuu) wa mahali hapo kumwalika kwenye hotuba itakayotolewa katika uwanja wake. Halikuwa jambo lisilo la kawaida kwa chifu huyo kutuma mtu katika kijiji atangaze hotuba itakayotolewa akiwa na kengele. Watu wa chifu walikuwa wakitandaza mkeka mkubwa kwa ajili yake na kuweka kiti chake cha kuketia. Alikuwa akiketi huku mtu mwingine akimshikia mwavuli juu yake mara nyingine kukiwa na mtu mwingine anayepeperusha manyoya makubwa ya mbuni kumpasha baridi. Maelfu mengi waliweza kuhudhuria na kuitikia kwa shauku mambo ya Biblia.

Katika nyakati mbalimbali nilikuwa nikisafiri kutoka Freetown kwenda Ghana, ambako nilikuwa nikitoa ushuhuda, nikatoa hotuba, na kuonyesha sinema ya sosaiti ‘Photo Drama of Creation.’ Katika Accra nilijipatia jumba la maonyesho lililokuwa kubwa zaidi katika mji huo kwa ajili ya hotuba yangu “Mataifa yote Yanaelekea kwenye Har–​Magedoni​—Mamilioni Walio Hai Sasa Hawatakufa Hata.” Mamia mengi walilazimika kusimama nje ili wasikilize, nayo magazeti yaliandika habari nzuri sana. Walakini “Baraza ya Wakristo” katika Ghana ilipinga hotuba yangu iliyosema wazi na kama matokeo serikali ikatangaza kwamba mimi ni mhamiaji asiyetakiwa. Miaka miwili ilipita naye gavana mpya akachukua mamlaka. Ndugu walitoa lalamiko wakiuliza niruhusiwe kutembelea Ghana. Lilitiwa sahihi na watu elfu nyingi, likatumwa kwa wakuu. Ruhusa ilitolewa! Ebu wazia furaha niliyokuwa nayo kuwaona tena watoto wangu katika Bwana na kuweza kuhudhuria kusanyiko katika Ghana.—3 Yohana 4.

Kwa miaka ishirini na mitano (25) ambayo nilikaa kama mtumishi wa tawi katika Afrika ya Magharibi, sikujisikia nimetulia nikiketi katika kiti afisini kwa wakati mrefu wo wote. Niliweza kupanga wakati wangu ili niweze kutoka nje na gari langu lenye vikuza sauti nitoe habari njema kwa kusema na kugawa vitabu. Barua alizoniandikia Ndugu Rutherford zilinifariji na kunitia nguvu katika miaka hiyo.

Katika mwaka wa 1930 tulianza kuishi katika Nigeria. Makundi kumi na manne yalianzishwa kuanzia mwaka 1931 mpaka 1938, na kufikia mwaka 1947 hesabu iliongezeka kufika 165. Likiwa eneo jipya nililokuwa nikiweka msingi, nililazimika kutumikia kama mtumishi (mwangalizi-msimamizi) wa kundi, mtumishi (mwangalizi) wa mzunguko, mtumishi (mwangalizi) wa wilaya ingawa kazi hizo zilikuwa na majina tofauti siku hizo. Mara mbili kila mwaka tulikuwa na makusanyiko katika sehemu tano ama sita hivi nami nilihudhuria hayo yote, nyakati nyingine nikiendesha gari langu maili 400 (kilometres 640) ili nifike katika kusanyiko lililokuwa linafuata. Hudhurio lilitofautiana kuanzia watu 65 mpaka zaidi ya watu 2,400. Katika miaka ya shida ya Vita vya Pili vya Ulimwengu ndugu hawakulegea. Afisi ya Tawi katika Afrika Magharibi ilitafsiri vitabu na vijitabu vingi kwa lugha za kienyeji.

Katika mwaka wa 1947 Sosaiti iliweza kututumia wamisionari kumi waliohitimu katika shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower. Watatu wao walipata mgawo katika Sierra Leone, wawili katika Liberia, wawili katika Ghana na watatu katika Nigeria. Wakati huo nilikuwa nilikaribia umri wa miaka sabini na nilikuwa na furaha sana kwamba Yehova alitoa wengine wenye moyo wa kujitoa wachukue kazi hiyo. Miezi michache baada ya wamisionari kuchukua mzigo wa kazi za afisi ya tawi, msimamizi wa Sosaiti Ndugu Knorr, alifika huko akiwa pamoja na katibu wake, Ndugu Henschel. Kukutana huko kulikuwa kwenye furaha sana.

KURUDI KATIKA VISIWA VYA CARIBBEAN

Mimi na mke wangu tulikaa katika Afrika ya magharibi mpaka mwaka 1950 kisha tukapanga kurudi katika Visiwa vya Caribbean. Mmoja wa wanabunge aliyekuwa vilevile mhariri wa gazeti moja mashuhuri (lenye kujulikana sana) alifikiria kwamba kuondoka kwetu ni jambo linalostahili kuandikwa. Aliandika makala katika gazeti la Daily Times iliyokuwa na kichwa: “BIBLE BROWN ASEMA TUTAONANA TENA SIYO KWA HERI.” Mhariri huyo alieleza habari juu ya kuishi kwangu katika Afrika ya Magharibi miaka ishirini na saba (27) kama mwalimu wa Biblia aliyepatwa na ubishi mwingi akaeleza: “Leo Bible Brown amefanyiza jamii ya watu na yeye ni rafiki wa wote, vijana kwa wazee, Mwingereza, Mwafrika na Mlebanoni, hata na wale ambao hawakukubaliana naye na waliochukia propaganda (maenezi) zake za kidini. . . Lagos utamkosa mtu aliyejulikana sana ‘Bible’ Brown, na rafiki wote wanamtakia yeye na Bi. Brown bahati njema nyumbani kwao huko Visiwa vya Caribbean.” Sana sana barua ya kuniaga kutoka kwa ndugu wa Nigeria. Ilikuwa yenye kuhuzunisha sana. Ilisema kwa sehemu: “Ndiyo, ‘mtu mmoja amekuwa elfu’ si maneno matupu, lakini mambo ya hakika yasiyoweza kukanushwa yanaonyesha kwamba ulipofika kwanza katika Afrika ya Magharibi hakukuwa hata mtu mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Lakini ulipoendelea kuhubiri, kulipata kuwa mmoja kutoka hapo kufika saba katika mwaka 1928. Bila kuachia hapo, ongezeko liliruka kutoka saba mpaka kufanyizwa kwa makundi. Kuanzishwa kwa afisi ya tawi kulitokea na leo kuna zaidi ya elfu kumi wakijibu kwa jina lenye kusifika, Mashahidi wa Yehova katika Pwani ya Afrika Magharibi . . . kwa machozi tunasema kwa heri kwako wewe na kwa jamaa yako.”

Tukiwa njiani kurudi Trinidad tulikuwa na pendeleo la kuhudhuria kusanyiko la mataifa yote katika mwaka wa 1950 huko Yankee Stadium katika New York. Tukiwa tumeburudika, ndipo tulipoendelea mpaka Trinidad, na baadaye tukaelekea Jamaica, ambapo sasa nafanya kazi katika utumishi wa wakati wote. Walakini kwa sababu ya uzee na afya mbaya, siwezi kufikia kiwango cha saa za painia. Kama tu ningeweza: Naupenda sana upainia. Ni mojawapo ya mapendeleo makubwa sana ambayo viumbe vya kibinadamu vyaweza kupewa, kuwa balozi wa Yehova!

Kulingana na kitabu Yearbook of Jehovah’s Witnesses cha mwaka 1962 kunao Mashahidi 35,729 (1978, 104,973) katika Nigeria, 8,662 (22,508, mwaka 1978) katika Ghana na mamia wengine katika sehemu zilizo karibu. Baada ya kutumiwa na Bwana kupanda mbegu na kuona jinsi Yehova alivyozifanya zikue nakumbuka maneno ya Paulo katika Warumi 15:17-21. Namna ilivyo furaha kuona wanaume na wanawake wakizitii habari njema za ufalme wa Mungu. Nikitazama nyuma na kuthamini maisha ya ajabu yaliyotumiwa katika utumishi wa Yehova miaka hamsini na mitatu nikiwa [mtumishi] painia, ninatoa shukrani kwa Yehova kwa kuwa nilisikia kweli kutoka kwa yule Mwalimu wa Watchtower aliyekuwa akisema kando ya barabara huko Panama. Tulikuwa tukipata dhahabu kama mshahara katika Mfereji [wa Panama] katika siku hizo, lakini kweli ilikuwa ya maana kwangu kuliko fedha. Kwa kuhudhuria mafunzo ya Biblia nilijifunza kusudi la Mungu ni nini kwa wanadamu. Nikiazimia kuwaambia wengine nilikodi majumba nikitoa hotuba za Biblia. Gazeti la Watch Tower lilipoomba makolpota, niliuliza niwe mmoja wao na sijasikitika kwa kufanya hivyo.

Katika mwaka wa 1920 mimi na mke wangu tulioana, lakini kulikuwa na kazi ya kufanywa. Siku mbili tu baada ya kufunga ndoa tulitoka Trinidad kwenda Montserrat tukiwa na sinema Photo-Drama of Creation. Tulitoa ushuhuda katika Dominica, Barbados na Grenada, kisha tukarudi Trinidad. Ilikuwa fungate (kipindi cha baada ya arusi) yenye furaha katika utumishi wa Yehova.

Katika mwaka wa 1922 Nilimwandikia msimamizi wa Sosaiti, Ndugu Rutherford, barua, nikimjulisha kwamba kwa msaada wa Yehova nilikuwa nimetoa ushuhuda katika vingi vya visiwa vya Caribbean na nikafanya wanafunzi wengi. Je! niwarudie tena? Si siku nyingi zilizopita jibu hili likaja: ‘Nenda Sierra Leone, Afrika ya Magharibi, ukiwa na mkeo na mtoto.’ Lo! unaweza kuwazia furaha yangu, kwenda kwa watu ambao hawajasikia habari njema!

Bado furaha yanijaa moyoni mwangu ninapowaona watu wengi zaidi na zaidi wenye nia njema wakijiunga na tengenezo la Yehova Mungu pande zote mbili za Bahari ya Atlantic. Ni wangapi bado watakaofanya hivyo kabla ya kazi kufungwa, sijui. Lakini ninajua kwamba Baba yetu wa kimbinguni ametimiza ahadi hii yake aliyoitoa kupitia kwa Isaya: “Mdogo atakuwa elfu, na Mnyonge atakuwa taifa hodari; Mimi, [Yehova] nitahimiza hayo wakati wake.”—Isa. 60:22.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki