Furaha ya Kibinadamu Chini ya Serikali ya Kimungu
Makala hii ni ya kutumia kwa mafunzo ya kitabu ya kundi
1, 2. Ni nini mojawapo ya sababu kubwa ambazo ni za lazima ili mwanadamu ajifurahishe uzima duniani?
INGEKUWA vizuri sana kuishi katika afya katika mazingira yenye mfano wa bustani. Yakiwapo maziwa safi na vijito, chakula kizuri na hewa safi, maisha yangekuwa yenye kufurahisha kweli kweli. Kwa kuongeza, kama watu wote wangeshirikiana katika mwendo mmoja, kutumia machumo ya dunia kwa ajili ya faida ya wanadamu, kazi ingekuwa ya kupendeza. Dunia ingekuwa paradiso kweli kweli.
2 Bila shaka, ingehitaji zaidi ya mazingira tu yenye kupendeza na watu wenye ushirikiano kuleta hali hiyo yenye kutamanika. Ingehitaji serikali safi, isiyo na upotovu. Kwa maana kwa upesi inakubaliwa kwamba “wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; bali mwovu atawalapo, watu huugua.” (Mit. 29:2) Serikali zilizofanywa na wanadamu zimeshindwa kuleta hali zinazotakiwa. Je! hiyo maana yake kwamba serikali kama hiyo yenye kutamanika haiwezi kuwapo?
3, 4. Mungu anakusudia nini kwa dunia, naye atafanya nini ili awapatie wote furaha?
3 Muumba anatuambia, katika Biblia, kwamba yeye anakusudia serikali yenye haki kwa ajili ya dunia. Yeye ndiye “Mungu mwenye furaha” na, akiwa Muumba wa mwanadamu, yeye anaijua namna ya serikali wanayohitaji watu ili wawe wenye furaha. (1 Tim. 1:11, NW) Kupitia kwa nabii wake Ezekieli amefunua namna ya serikali hiyo.
4 Kama Mwenyewe wa dunia, Yehova ameitoa sayari hii kwa mwanadamu kama makao yake. Kama Mtawala Mwenye Enzi Yote, yeye atawaweka watu mmoja mmoja duniani kama atakavyochagua, si kwa ajili ya uradhi wake mwenyewe tu, lakini kwa ajili ya furaha kuu zaidi ya wote wanaopaswa.—Kut. 19:5; Zab. 115:16.
MFANO
5. Ni mfano gani ambao Yehova alitoa kwa habari ya ugawaji wa dunia katikati ya wakaaji wake?
5 Kama mfano wa hili, Yehova alimpa nabii Ezekieli njozi ambamo Yeye alionyesha mahali pa kila moja la makabila kumi na mawili ya Israeli, mipaka yake ikiwa imeonyeshwa. Katika ramani inayofuata utaona kwamba kulikuwako kipande cha nchi cha usimamizi, kilichoandikwa “The Chieftain” (“Mkuu”) pamoja na sehemu saba kaskazini mwa kipande na kulingana nacho. Upande wa kusini ndiko ilikokuwa migawo ya makabila mengine matano ya Israeli. Vipande vya eneo vilitokea Bahari ya Kati kuelekea masharikini kwenye Mto wa Yordani au kuelekea Bahari ya Chumvi.—Eze. 47:15-20.
6. Katika njozi ya Ezekieli, mahali patakatifu au hekalu lilikuwa wapi?
6 Kabila la Lawi halikuwa na urithi uliotolewa kwa sababu lilitumikia penye patakatifu pa Yehova, palipokuwa katika kipande cha nchi cha usimamizi, ndani ya sehemu yenye dhiraa (mikono) 25,000 (karibu futi 42,500 [maili 8]) za eneo. (Dhiraa iliyotumiwa kupima ilikuwa “dhiraa na shubiri” [karibu inchi 20.4].) Sehemu hii ya eneo, inayoitwa “matoleo mtakayotoa,” ilikuwa karibu ya ujirani wa Mlima Moria.—Eze. 43:13; 48:8, 9.
7. (a) “Matoleo” ya nchi yaligawanywaje, na ni nani waliokaa katika kipande cha kaskazini? (b) Ni sehemu gani waliyogawiwa makuhani?
7 “Matoleo” haya ya nchi, nayo, yalipaswa yagawanywe vipande vitatu vya nchi, kila kimoja kikiwa na urefu wa dhiraa 25,000. Vipande vya kaskazini na katikati vilikuwa vyenye upana wa dhiraa 10,000; cha kusini, upana wa dhiraa 5,000. Kipande cha kaskazini walipewa Walawi wasio wa kikuhani. (Eze. 48:13, 14) Sehemu ya katikati yenye dhiraa 10,000 ya “matoleo” ilikuwa na patakatifu pa Yehova nayo iliitwa ‘matoleo matakatifu kwa makuhani’ na “kitu kitakatifu sana, karibu na mpaka wa Walawi.”—Eze. 48:10-12.
8. Kipande cha nchi kilichokuwa kusini kabisa kilikuwa cha matumizi gani?
8 Kipande kilichokuwa kusini kabisa cha nchi, chenye upana wa dhiraa 5,000 (maili 1.61), ndicho kilichokuwa na “mji” katikati yake, wenye dhiraa 5,000 za eneo. Ukuta uliouzunguka mji ulikuwa wenye dhiraa 4,500 kwa upande mmoja, pamoja na dhiraa 250 pande zote kama uwanja wa malisho. (Eze. 48:15-17) Katika kila upande wa mji (mashariki na magharibi) lilikuwako eneo lenye urefu wa dhiraa 10,000 na upana wa dhiraa 5,000. Nchi hii iliyo wazi ilipaswa ilimwe izae chakula kwa wote waliokuwa wanafanya kazi katika mji. Hawa walikuwa jamii ya wafanya kazi wa kabila zilizochanganyika, watu kutoka makabila yote kumi na mawili yasiyo ya Kilawi.—Eze. 48:18, 19.
MAWAKILI WAONEKANAO WA SERIKALI YA KIMBINGUNI
9. Ni nani aliyekuwa “mkuu,” na ni nini iliyokuwa milki yake?
9 Kichwa kionekanacho cha hii serikali ya njozi kilikuwa “mkuu.” Eneo lake lililotolewa lilikuwa kubwa sana, likiwa na nchi ya “matoleo” yenye dhiraa 25,000 za eneo za nchi kila upande. Kipande hiki, chenye upana wa dhiraa 25,000, kilienea sehemu yote mpaka kwenye Bahari ya Kati katika magharibi ya “matoleo” na kwenye Mto wa Yordani na Bahari ya Chumvi katika mashariki.—Eze. 47:18, 20.
10. (a) Ebu onyesha kwamba ule “mji” haukuwa mfano wa mji wa kimbinguni Yerusalemu Mpya. (b) Ule “mji” ulikuwa mfano wa nini?
10 Inastahili kuangaliwa kwamba katika njozi ya Ezekieli mji haukuwa na hekalu, ijapokuwa hekalu lilikuwa karibu katika “matoleo” ya pekee ya nchi. Makuhani na Walawi hawakukaa wala kufanya kazi katika mji huu. Kwa hiyo, katika utimizo wa njozi chini ya utawala wa Masihi wa miaka 1,000, mji wa njozi usingeufananisha mji wa kimbinguni, Yerusalemu Mpya, uliofanyizwa na kundi la Kristo la Waisraeli wa kiroho, Bibi-arusi wake. (Ufu. 20:3, 4, 6; 21:1, 2, 9-21) Kwa maana wao ni makuhani, “ukuhani wa kifalme,” majina yao yakiandikwa mbinguni. (1 Pet. 2:9; Ebr. 12:23) Kwa hiyo, “mji” unafananisha, sio serikali ya kimbinguni ya Yesu Kristo na wafalme wake na makuhani washirika 144,000, bali, kikao cha kidunia cha usimamizi juu ya mambo ya wanadamu waliokombolewa.
11. Onyesha kwamba yule “mkuu” aliyemo katika njozi si mfano wa Masihi.
11 Kwa hiyo “mkuu” katika njozi si umbo la mfano la Yesu Kristo. Mkuu alitumikia katika sehemu ‘iliyo najisi,’ si katika hekalu, lakini Yesu Kristo ndiye Kuhani Mkuu, anayetumikia katika eneo la kimbinguni la hekalu la kiroho la Yehova. (Ebr. 3:1; 8:1) Kweli, Yehova alimwita Masihi “mkuu” katika sura iliyotangulia mapema ya unabii wa Ezekieli. Lakini humo Mungu anamsema mkuu huyo kama “mtumishi wangu, Daudi,” hali mtajo huo haufanywi kwa mkuu katika njozi hii ya “mji.” Daudi alikuwa ndiye mfalme wa Israeli ambaye kutoka kwa ukoo wake Masihi alikuja, kwa habari ya ukoo wake wa kimwili. (Eze. 34:24; 37:25; Matendo 2:29-36) Yesu Kristo ndiye, kama Masihi aliyetabiriwa, Mfalme wa kimbinguni na vile vile Kuhani Mkuu.
12. Basi yule “mkuu” ni mfano wa nani?
12 Basi, “mkuu” katika njozi ya hekalu anafananisha nani? Kama vile neno “mtumishi” lilivyokuwa na maana ya jumla mara nyingi, kama Yehova alipoliita taifa la Israeli “mtumishi” wake, ndivyo na “mkuu” lilivyo na maana ya jumla. Linasimamia wale ambao Masihi wa kimbinguni Yesu anawaweka kama mawakili wake waonekanao katika “nchi mpya,” chini ya uongozi wa “mbingu mpya.”—Isa. 43:10; Ufu. 21:1, 2.
13-15. (a) Kwa uongozi wa roho ya Mungu, mtunga zaburi anasimuliaje jamii ya “mkuu”? (b) Nabii Isaya anaonyeshaje matokeo ya utawala wa jamii ya “mkuu”?
13 Mtunga Zaburi aliandika kwa unabii akisimulia Mfalme Yesu Kristo na kuelekeza kwenye watoto wake wa kidunia: “Badala ya baba zako [wa kidunia] watakuwapo watoto wako, utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.” (Zab. 45:16) Kristo atahakikisha kwamba hawa na wengine, wakiwa wamekuwa “watoto” wake kwa sababu ya kupata uzima kupitia kwake, watasimamia mambo ya wanadamu kwa haki na watawatunza katika usalama kama “wakuu” wenye haki duniani, kwa maana huu ndio uhakikisho katika Isaya sura ya 32 katika maneno haya mazuri:
14 “Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu. Na [kila mmoja] atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu.
15 “Ndipo hukumu itakaa katika jangwa, na haki itakaa katika shamba lizaalo sana, Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima. Na watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu.”—Isa. 32:1, 2, 16-18.
16. Maneno ya Kristo kwa mitume wake katika Mathayo 19:28 na Luka 22:29, 30 yatatimizwaje wakati huo?
16 Yehova aliwafanyia watu wake hivi kwa kadiri ndogo alipowarudisha kutoka uhamishoni Babeli wakaujenge Yerusalemu upya na hekalu lake. Ni zaidi namna gani atakavyowafanyia hivi watu wa dunia yote wakati wa utawala wa Kristo wa miaka 1,000! Ndipo maneno ya Kristo kwa mitume wake yatakapokuwa kweli, ya kwamba wataketi pamoja naye ‘wakiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli,’ yaani, wanadamu wote waliokombolewa, kupitia kwa mawakili wenye haki na fahari waonekanao duniani.—Mt. 19:28; Luka 22:29, 30.
JINA LA MJI LINA MAANA
17. (a) Ni nani watakaofanya kazi pamoja na jamii ya “mkuu”? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na masimulizi ya njozini ya milango iliyo katika ukuta wa mji?
17 Ndipo wenye kujitolea kutoka sehemu zote za dunia na kutoka safu zote za wanadamu waliokombolewa watakapoingia kushirikiana kwa bidii na jamii ya “mkuu.” Hii itakuwa penye “mji,” unaosimamia kikao rasmi kionekanacho cha jamii ya “mkuu” cha kuyasimamia mambo ya wanadamu wote. Njozi ya Ezekieli ilionyesha malango matatu katika kila mmojawapo wa kuta nne za mji, yakiwa wazi kwa makabila yote kumi na mawili ya Israeli. (Eze. 48:30-34) Usimamizi wa mji utafananisha Yerusalemu Mpya wa kimbinguni sawasawa, ulio na milango kumi na miwili iliyoandikwa majina ya “kabila kumi na mbili za Waisraeli.” (Ufu. 21:12) Kwa hiyo kupatikana na uangalizi wenye upendo wa Kristo na ukuhani wake mdogo vile vile vitaonyeshwa na usimamizi wenye fahari duniani. Kutakuwako njia iliyo huru na wazi kwa wote watakao kupokea msaada juu ya jambo la lazima.
18. Jina la ule mji linatupa sisi ahadi gani?
18 Unabii wa Ezekieli unamalizia ukitoa jina la mji huu: “Kuuzunguka [mzingo wa mji] ni mianzi kumi na nane elfu; na jina la mji huo tangu siku hiyo litakuwa hili, [Yehova] yupo hapa.” (Eze. 48:35) Ni sawa na vile Ufunuo 21:3 unavyoahidi: “Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.” Yehova mwenyewe ataonyesha kuwapo kwake kwa kimungu wazi kwa kuuelekeza uangalizi wake wenye upendo na mwema kwenye “mji.” Tunda la roho yake litakuwa jingi humo kwa utukufu wake, yaani, “upendo, furaha, amani, uvumilivu, fadhili, wema, imani, upole, kujiweza.”—Gal. 5:22, 23, NW.
19. Ni faida gani zitakazowajia wanadamu kupitia kwa utawala wa jamii ya “mkuu” chini ya uongozi wa “mbingu mpya”?
19 Roho ya Yehova ikiwa inatenda kupitia kwa hao “wakuu,” twaweza basi kuwa na uhakika wa serikali yenye haki itakayokuwa na utukufu wa Mungu, uadilifu, haki, na furaha ya watu moyoni. Kutoka kwa Yesu Kristo Kuhani Mkuu na ukuhani wake mdogo katika mbingu yatakuja matumizi ya ubora wa dhabihu ya Kristo yenye kulipia dhambi, pamoja na faida zake zote. Chini ya uongozi wa “mbingu mpya” kabisa, usimamizi uonekanao wenye mfano wa mji utasaidia katika kuinuliwa kwa wanadamu wote watiifu kwenye ukamilifu wa moyo, akili na mwili katika Paradiso ya dunia iliyoimarishwa tena. Ufunuo 21:4 unaendelea kusema: “Naye [Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
TUMAINI LA KWELI LA KUSHIKA SASA
20. (a) Ni vita gani vinavyofanyika sasa katika kila mtu anayetaka kutenda yaliyo mema? (b) Wanyofu wa moyo watawezaje kufikia ushindi kamili katika kupigana na mabaya?
20 Wakati huu, chini ya maongozi ya hii taratibu ya mambo, na kwa sababu ya dhambi tuliyoirithi kutoka kwa babu yetu Adamu, ni pigano la sikuzote kwa hata Mkristo wa kweli kuyashinda maelekeo mabaya, yenye kuharibu ya mwili usio mkamilifu. (Rum. 7:19, 24, 25) Wanadamu wako hoi wakiwa peke yao, nayo maongozi ya Shetani, “mungu wa hii taratibu ya mambo,” na kukosekana kwa uangalizi kwa upande wa serikali za dunia kwa hali njema ya watu, vimewaacha wao katika hali yenye kutia huruma. (2 Kor. 4:4, NW) Lakini chini ya “mbingu mpya na nchi mpya” yenye haki, kwa usimamizi wa wakuu wenye kumcha Mungu duniani, unabii utatimizwa: “Dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa [Yehova], kama maji yaifunikavyo bahari.” (Hab. 2:14; 2 Pet. 3:13) Wakija kumjua Yehova Mungu na fadhili zake zenye upendo zisizopitika, hekima yake, uadilifu wake na mipango yake kwa ajili ya furaha ya wanadamu, watamtukuza yeye na kuziiga njia zake. Ndipo, kama vile mtunga Zaburi alivyoimba kwa unabii: “Fadhili na kweli zimekutana, haki na amani zimebusiana. Kweli imechipuka katika nchi, haki imechungulia kutoka mbinguni. Naam, [Yehova] atatoa kilicho chema, na nchi yetu itatoa mazao yake.”—Zab. 85:10-12.
21. Tukiwa tofauti na mazoea ya taratibu hii ya mambo, imetupasa tufanye nini, na wakati gani?
21 Ikiwa wewe u mtu anayeyataka mambo haya mema, bila shaka waona kwamba hayafanywi katika hii taratibu iliyopo ya mambo. Huenda ukasumbuliwa na kufadhaishwa na mambo unayoyaona yakiendelea. (Eze. 9:4) Ikiwa ndivyo, onyesha kupenda kwako haki sasa. Mungu anaweka mbele yako nafasi ya ukombozi, sawa na alivyomfanyia Lutu mwenye haki katikati ya mji mpotovu wa Sodoma. (2 Pet. 2:7-9) Usiketi kwa kinaya na kungoja, kwa maana Yehova atauharibu ulimwengu huu mpotovu na wote wanaofungamana nao. (2 Pet. 3:7-9; 1 Pet. 4:17-19) Uchukue hatua za kujifunza mapenzi ya Mungu sasa na kuyafanya njia yako ya maisha.
—Kutoka Kitabu “The Nations Shall Know that I Am Jehovah”—How?
[Diagram/Map katika ukurasa wa 32]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
HOLY CONTRIBUTION and the TWELVE TRIBES
ENTERING INTO HAMATH
DAN
ASHER
NAPHTALI
Sea of Galilee
MANASSEH
EPHRAIM
REUBEN
JUDAH
Jordan River
THE CHIEFTAIN
Holy Contribution
En-eglaim
BENJAMIN
En-gedi
SIMEON
Salt Sea
ISSACHAR
ZEBULUN
Tamar
GAD
Meribath-kadesh
T.V. of Egypt
SCALE OF MILES
0——5——10——20——30
[Diagram]
Enlargement of Holy Contribution
A
B
C
a b c
l d
D k E e D
j f
m i h g
“A” indicates Levites’ portion; B, Sanctuary of Jehovah; C, Priests’ portion; D, City’s productive land; E, City: Jehovah Himself Is There (Jehovah-shammah).
Gates: a, of Reuben; b, of Judah; c, of Levi; d, of Joseph; e, of Benjamin; f, of Dan; g, of Simeon; h, of Issachar; i, of Zebulun; j, of Gad; k, of Asher; l, of Naphtali.
Pasture ground: m.