Je! Imekupasa Kunywa Vileo?
Mambo ya hakika ambayo vijana wanataka kujua
VIJANA wengi zaidi na zaidi wanaelekeana na ulizo hili leo. Ni mambo gani ya hakika yatakayokusaidia sana ujue namna ya kuwa na maoni yenye busara ya shauri hili, kwa ajili ya faida yako mwenyewe ya milele?
Vileo ni vya namna mbalimbali. Vingine havina nguvu nyingi za kulevya, kama vile beer (pombe). Vingine ni vyenye nguvu za kadiri, kama zilivyo namna mbalimbali za divai inayotumiwa wakati wa chakula. Halafu kuna ile iitwayo “mvinyo” iliyo na nguvu nyingi za kulevya, kama vile brandy (ifanyizwayo kwa zabibu), whiskey (kileo kifanyizwacho kwa nafaka), gin (kileo cheupe kama maji), vodka (kileo cha nguvu cha Urusi), tequila cha Latin-America au ouzo cha Kigiriki.
Hali za nchi na desturi ni za namna mbalimbali vile vile. Katika nchi nyingine—Ufaransa, Italia, Spania, Ugiriki, Chile na nchi nyingine—divai inatumiwa kama kinywaji cha kawaida mezani inapokula jamaa. Huenda hii ikawa ni kwa sababu ya ugumu wa kupata maji mazuri au huenda ikawa ni kwa sababu ya desturi tu. Lakini hata katika nchi hizi hali ya matumizi ya vileo itatofautiana katika jamaa mbalimbali.
Si hivyo tu, bali matokeo ya kutumia vileo vile vile yanatofautiana katika nchi mbalimbali, katika jamaa mbalimbali, na kwa watu mbalimbali. Yakupasa ukumbuke hivi ili ukuze maoni yenye busara juu ya vileo hivyo.
Basi je!, kwa kuwa zipo namna hizi mbalimbali, kuna kanuni yo yote iliyo imara na inayopatana kukuongoza katika shauri hili? Ndiyo, Biblia inaitoa kwa ajili yetu. Mashauri yake yaliyoongozwa na roho ya Mungu yanatoa maoni yaliyosawazika sana juu ya matumizi ya vileo.
MAONI YALIYOSAWAZIKA YA BIBLIA
Biblia yaonyesha kwamba tangu nyakati za kale divai ilikuwa kinywaji cha kawaida kilichonywewa pamoja na vyakula, ikitumiwa na watu kama vile Mfalme-Kuhani Melkizedeki, na Ibrahimu, Isaka na wengine wengi. (Mwa. 14:18, 19; 27:25; 1 Sam. 16:20; Mhu. 9:7) Yesu alifanyiza divai kwa ajili ya karamu ya arusi, naye mtume Paulo alimshauri kijana Timotheo ‘kutumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.’—1 Tim. 5:23; Yohana 2:1-10.
Kwa kufaa Biblia inapanga divai kati ya mipango ya Mungu na baraka kwa ajili ya furaha ya mwanadamu mwenye kufa. (Kum. 11:13, 14; Zab. 104:15; Yoeli 2:19) Vile vile yaonyesha kwamba watu wa Mungu walitumia vileo vya namna nyingine.—Kum. 14:26.
Je! maana yake ni kwamba hakuna haja ya uangalifu kwa upande wako juu ya kunywa vileo? Hata kidogo. Kwa maana Biblia kwa upande mwingine yatoa maoni mengine zaidi. Viko vitu vingi maishani visivyo vibaya vyenyewe lakini viwezavyo kuleta matokeo mazito vikitumiwa vibaya au mapema mno. Mungu alimpa mwanadamu nguvu za uzazi, lakini zapaswa hizi zitumiwe katika ndoa yenye kuheshimika peke yake nayo matumizi yazo yaweza kuleta madaraka mazito ya kuangalia jamaa. Moto, mvuke (stimu), umeme na vyombo mbalimbali vyaweza kuwa vyenye manufaa sana kwa wanaume na wanawake katika kazi yao, lakini, vikitumiwa bila ya uangalifu unaostahili, vyaweza vile vile kudhuru sana. Angalia sasa matokeo yenyewe ya pombe kali sana katika mwili wa mwanadamu.
Tofauti na vitu vingine, pombe kali sana haihitaji kuyeyushwa. Inaanza kuvutwa katika damu mara inapoingia tumboni, ijapokuwa hili linatukia zaidi sana katika chango. Inapelekwa upesi ubongoni, kwenye ini na sehemu nyingine za mwili. Kwa kuwa pombe kali sana ina joto, sasa mwili unaanza kuigeuza kuwa namna ya mchanganyiko wa vitu mbalimbali ambao kwao unafanyiza joto. Ini ndilo linalofanya kazi nyingi zaidi katika hili. Mapafu na figo yanapunguza kazi kwa kuwa yanaondoa kadiri fulani ya ile pombe kali sana kwa kupumua na kwa mikojo.
Iingiapo damuni, pombe kali sana ina matokeo gani juu ya mtu? Ikinywewa kwa kadiri yo yote, haizichochei chembe za mwili, bali inazipunguza nguvu. Ikinywewa kwa kadiri ndogo, matokeo yanakuwa utulivu na burudisho. Ikinywewa kwa wingi, matokeo iliyo nayo ya kuzipunguza nguvu za ubongo au kuzikomesha yanawafanya watu wengine kuwa walimi, wenye kutenda kupita kiasi na hata wenye jeuri.
Katika mkazo zaidi wa fikira, ubongo unadhoofishwa zaidi sana, neva za uti wa mgongo zinapatwa, na ndipo mtu mwenyewe anapoanza kuona ugumu katika kusawazisha miendo yake. Ndiyo sababu anaona ugumu wa kutembea, akiona vizuri sana na kuzungumza sana, anachanganyika na kuburugika katika mawazo yake. (Linganisha Zaburi 107:27.) Ugumu unazidishwa na matokeo ya ajabu yanayoletwa na pombe kali sana katika kumfanya mtu adhani akili yake inafanya kazi kweli kweli kwa njia bora isivyo kawaida. Kwa hiyo, kwa kawaida yeye ndiye anayekuwa wa mwisho kugundua kwamba amekunywa kupita kiasi. Na mara afikiapo hatua ya kulewa hatalevuka mpaka muda umekwisha kupita.
Biblia inatupa sisi mfano unaofaa sana juu ya hatari na maumivu yanayofuatana na kunywa vileo kupita kiasi. Katika Mithali 23:29-35, twasoma: “Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu? Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; waendao kutafuta divai iliyochanganyika. . . . Macho yako yataona mambo mageni; na moyo wako utatoa yaliyopotoka. Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari [ukiwa na wasiwasi na hoi kama mtu anayekufa maji]; au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti [ambapo kutoka hapo kuyumbayumba kwa merikebu kunaonekana zaidi sana, ikiwa ni vyepesi kuanguka]. Utasema, Wamenichapa wala sikuumia; wamenipiga wala sina habari [kwa maana mlevi hajui yanayotukia naye mara nyingi hajui majeraha yaliyompata mpaka amekwisha kulevuka].”
UGUMU UNAOONGEZEKA KWA VIJANA
Lakini je! vijana wamo katika hatari yo yote ya kulewa au hata kuwa wanywaji wa pombe? Ndiyo, wamo katika hatari hiyo. Gazeti la Newsweek la Machi 5, 1973, laonyesha maelekeo yanayoongezeka kati ya vijana wasiofikia umri wa 20 ya kutumia pombe, mara nyingi mahali pa dawa za kulevya. Na wengi wanakunywa kufikia hatua ya kulewa.
Kwa mfano, katika kitongoji kimoja cha Boston, mmoja kati ya kila wanafunzi watatu wa darasa la nane aliripotiwa kuwa analewa walau mara moja. Katika California ya kusini, kijana mmoja kati ya kila vijana 20 ni “mnywaji aliyekolea,” na, kulingana na National Council on Alcoholics (Baraza ya Kitaifa ichunguzayo matumizi ya vileo), umri wa vijana wachanga zaidi watumiao vileo katika taifa umeshuka kutoka miaka 14 kuwa 12. Kwa muda mrefu Ufaransa imeona ugumu mkubwa wa unywaji wa pombe kati ya watoto, wengine wao wakionyesha dalili za ugonjwa wa ini wakiwa wachanga sana. Katika Hungary (nchi mojawapo ya zilizo na hesabu kubwa ya watu wajiuao wenyewe), mahospitali yamekuwa yakitibu maelfu ya watoto kila mwaka kwa sababu ya ulevi.
Kwa sababu gani vijana wanapatwa na ugumu huu? Mara nyingi mtu fulani katika jamaa yao ni mnywaji wa kupindukia. Mara nyingi, ni kwa sababu wanaanza kunywa kwa shauri la vijana wengine. Nyakati nyingine mvulana mdogo anakazwa na wengine wa rika lake ‘kujionyesha ni mwanamume’ kwa kunywa sana kinywaji fulani cha nguvu, au msichana mdogo anaonyeshwa yuko nyuma kwa kijamii asipokunywa.
Je! kwa kweli kunywa kileo kunahakikisha lo lote juu ya namna ulivyo? Kwa wazi sivyo, kwa maana hata wanyama wanaweza kuvutwa kukinywa. Kwa kweli, watu wanaokukaza unywe wanataka nini? Je! wao wanajaribu kukufaidi wewe? Au, kuliko hivyo, wanajaribu tu kukuweka wewe katika kundi lao, pengine ‘kufurahia’ kukuona ukipotewa na fahamu na kutenda, si kama mwanamume mzima au mwanamke, bali kama kitoto kidogo kisichoweza kutembea, kuzungumza wala kuona vizuri na kinachofanya na kusema mambo ya kipumbavu?
Angalia ambavyo mkuu mmoja, Dr. Giorgio Lolli, anavyotajwa kama akisema juu ya watumiao vileo: “Mtu atumiaye vileo anaacha kuwa mtu mzima na kuwa kitoto, kwa kimwili na kwa akili. Nguvu zake za kuwaza na maoni ya kimwili vinakuwa visivyofahamika waziwazi. Kama vile kitoto, anakuwa hoi naye anahitaji kuangaliwa kama kitoto.” Zaidi ya hayo, watu wanaojaribu kufanya ufisadi huenda vile vile wakamtia mtu moyo anywe kusudi kwamba kujiweza kwake (awe ni mwanamume au mwanamke) kudhoofike.
Kwa hakika kushindwa na wo wote wa mikazo hii kungeonyesha—si kwamba mtu anazo nguvu ama ni mtu mzima—lakini kwamba mtu ni dhaifu naye hana ujasiri wa adili. Ni kwa sababu nzuri kwamba Mithali 20:1 inaonya kuwa divai yaweza kuwa ‘mfanya dhihaka, kileo huleta ugomvi; na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima.’ Si lazima ulewe ili ujue namna kusivyopendeza—kama vile isivyo lazima kuvunja mguu ili ujue namna kufanya hivyo kulivyo kwenye maumivu.
Siyo hatari ya kuwa “mlevi aliyekolea” tu inayohitaji uangalifu. Kulewa mara moja tu kwa kupindukia kwaweza kuleta madhara ya sikuzote: ajali mbaya sana ya motokaa, yawezekana kupoteza uhai, mguu au mkono—wako mwenyewe au ule wa mtu fulani asiye na hatia; au tendo la ufisadi litakaloweka doa katika maisha yako yote na liwezalo kuleta maumivu makali; au pengine mwenendo wa jeuri utakaoujutia kwa muda mrefu. Sababu gani ujihatirishe bure?
Uwezekano wa matokeo hayo yenye msiba u wazi kutokana na uhakika wa kwamba, kati ya watu 50,000 wanaokufa kila mwaka katika barabara za United States, zaidi ya nusu za vifo hivyo vinasababishwa na ajali za ulevi. Nayo ripoti ya Times la New York la Julai 18, 1972, yasema kwamba “zaidi ya kiasi cha 80 kwa 100 cha uuaji na matendo ya jeuri yanafanywa na walevi.”
KULIFIKIRIA SHAURI HILI KWA HEKIMA
Unapolifikiria shauri hili, kumbuka kwamba vileo si mojawapo la mambo yaliyo ya lazima kama ilivyo hewa, chakula na maji. Waweza kuendelea kuishi bila ya kuwa navyo, na watu wengi wanapendelea kuwa hivyo. Vile vile, kumbuka kwamba mtu atakaye kuwa na ukubali wa Yehova Mungu, Mpaji wa Uzima, lazima amtumikie yeye kwa ‘moyo wake wote, nafsi, akili na nguvu.’ (Luka 10:27, NW) Si kwamba tu matumizi mabaya ya pombe kali sana yanaweza kumwondolea mtu utimamu wa akili na wepesi wa macho na nguvu za kimwili, lakini vile vile yanaugeuza moyo wa mtu, yakitokeza usitawi wa nia mbaya.—Isa. 28:7, 8; 1 The. 5:6-8; Hos. 4:11.
Kweli, Biblia inazungumza kwa kuyapendelea matumizi ya kiasi ya vinywaji hivyo kama vile divai. Lakini namna gani mtu akivitazamia vileo hivyo kama njia ya kuiepuka hali ya maisha au uchovu kwa kupata furaha ya juujuu na maono ya kufanyizwa tu ya urafiki? Au kama dawa ya utu ya ‘kutilia nguvu neva za mtu’ kusudi aondoe woga au hofu? Huenda hata akaona kwamba dawa yenyewe ni mbaya zaidi kuliko maumivu yenyewe. Fedha ina faida gani ikiwa ni ya bandia? Nayo maono ya furaha au ujasiri yana faida gani ikiwa ni ya kufanyizwa tu?
Ripoti yenye kufundisha ya National Institute of Mental Health (iliyochapwa na U.S. Department of Health, Education and Welfare) yaonyesha kwamba hatari za matumizi mabaya ya pombe kali sana hazikuelekea sana kuwapo ambapo hali zifuatazo zilikuwapo:
(1) Ambapo kunywa kwa mtu vileo kulikuwa katika jamaa iliyo imara au kikundi cha kidini na ambapo kwa kawaida vinywaji vilikuwa havina nguvu nyingi (kama vile divai zinazonywewa wakati wa chakula au beer) na vilivyonywewa nyakati za vyakula kwa kawaida kama sehemu tu ya chakula. (2) Ambapo matumizi ya vinywaji hivyo yalionwa si kama wema wala dhambi, ambapo unywaji haukuonwa kama wonyesho wa utu mzima ama wa mtu kuwa “mwanamume halisi.” (3) Ambapo hakuna aliyelazimishwa kunywa na ambapo kukataa kinywaji hakukuonwa kama dharau kama vile kukataa kipande cha mkate kusivyoonwa kama dharau. (4) Ambapo kunywa kwa kupindukia kulikatazwa kwa nguvu, kukionwa kama kusiko ‘kwa utaratibu’ wala kwa mzaha wala kitu cha kuvumiliwa. Na, pengine, lililo la maana zaidi, (5) ambapo mapatano yalikuwapo juu ya yaliyo haki na yasiyo haki juu ya matumizi ya vinywaji hivyo, wazazi wakiweka mfano mwema wa kiasi.
Bila shaka, kiongozi kilicho bora na salama zaidi ni Neno la Mungu. Kama tulivyoona, linatoa mifano ya matumizi yafaayo ya vileo na maonyo juu ya kuvitumia vibaya. Linawaonya vijana ‘kuwa watiifu kwa wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.’ (Efe. 6:1) Yaheshimu maamuzi ya wazazi wako, ambayo msingi wayo ni Neno la Mungu, juu ya kama imekupasa kunywa vileo au sivyo au ni katika hali gani uwezapo kufanya hivyo. Wewe u mwenye hekima ukiepuka kuvinywa wakati ambapo wale wote wanaovinywa ni vijana wanaofanya hivyo wazazi au jamaa wasipokuwapo kuwapa uongozi.—Mit. 1:7-9; 6:20-22; 22:15.
Zaidi ya yote, kwa ajili ya furaha yenu ya sikuzote, ‘ulapo, au unywapo, au utendapo neno lo lote, fanya yote kwa utukufu wa Mungu.’—1 Kor. 10:31.