Wakati Ibada Inapowekwa Juu ya Hekalu la Kidunia
Makala hii ni ya kutumia kwa mafunzo ya kitabu ya kundi
1, 2. Je! mahekalu ya dini za ulimwengu yamewaleta watu pamoja katika umoja? Kwa sababu gani?
YAKO maelfu ya mahekalu na makanisa makuu katika ulimwengu mzima. Mengi yayo yamejengwa vizuri na kupambwa sana, mara nyingi kwa dhahabu na vito vyenye thamani.
2 Je! mahekalu haya yamewaleta watu wa dunia karibu karibu zaidi katika ibada ya kweli yenye umoja, pamoja na upendo kwa mtu na mwenzake? Sivyo; badala yake, yameweka vizuizi vinavyoelekea kutoshindika. Huenda, tukaona mungu katika mahekalu hayo au sanamu wanayopigia magoti wafuasi, lakini je! twaweza kumwona Mungu wa kweli, kusudi wote waweze kumwabudu yeye “katika roho na kweli,” katika umoja na upendo kwa mtu na mwenzake? Mtunga zaburi alisema hivi: “Miungu yote ya watu si kitu,” naye mtume Paulo akasema: “Vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu.”—Yohana 4:24; Zab. 96:5; 1 Kor. 10:20.
3. Je! hekalu la kidunia lililoifananisha ibada ya Mungu wa kweli lilikuwa na sanamu ya Mungu ndani yake? Kwa sababu gani?
3 Lakini wakati mmoja kulikuwako hekalu lililoifananisha ibada ya Mungu wa kweli duniani. Haikutia ndani sanamu ya Mungu wake, kwa maana Mungu huyu ndiye Muumba, na juu yake imeandikwa hivi: “Mtamlinganisha Mungu na nani? au mtamfananisha na mfano wa namna gani?” (Isa. 40:18, 25) Kwa kweli, Mungu huyu aliwakataza waabudu wake wasifanyize cho chote cha kumfananisha yeye. Isingewezekana kufanya hivyo, kwa maana, kama vile mjumbe wake Musa alivyowatangazia Israeli: “Hamkuona umbo la namna yo yote siku ile [Yehova] aliyosema nanyi kutoka kati ya moto.” Kujifanyia kwao “sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote,” kungekuwa ‘kujiharibu.’ (Kum. 4:15, 16) Zaidi ya hayo, wakati wa kumzindulia Mungu huyu hekalu, mjenzi wake alisema hivi: “Lakini Mungu je! atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!”—1 Fal. 8:27.
4. Hili lilikuwa hekalu gani, ambamo ibada kwa Mungu wa kweli iliendeshewa?
4 Hili lilikuwa ndilo hekalu la Yehova, lililokamilishwa na Mfalme Sulemani Yerusalemu katika mwaka wa 1027 B.C.E., na kuharibiwa na Wababeli mwaka wa 607 B.C.E. Waisraeli walipokwisha kurudi wakarudishe ibada safi mwaka wa 537 B.C.E., hekalu lilijengwa upya katika eneo lile lile. Jengo hilo, nalo, lilijengwa upya na kupanuliwa na Herode Mkuu. Lakini, kwa kweli na kwa ajili ya makusudi yanayofaa, miaka yote kulikuwako hekalu moja tu, lenye kazi na kusudi lile lile.
HEMA MFANO WA MAMBO YA KIMBINGUNI
5, 6. “Hekalu” la kweli la asili lilikuwa nini, na kwa sababu gani kulichunguza ni kwa maana kwetu leo?
5 Mapema hata kabla ya hekalu la Mfalme Sulemani, Musa alikuwa amesimamisha hema (mara nyingine iliyosemwa kama “hekalu”) katika jangwa kwa kuamriwa na Mungu na kulingana na mfano aliopewa na Mungu. (1 Sam. 1:9; 3:3; Kut. 25:40; 39:43) Kati ya mahekalu yote aliyoyakubali Yehova hili ndilo jengo lililokuwa halina mambo mengi, lakini lilikuwa na mambo yote ya lazima. Mahekalu yaliyolifuata yalikuwa majengo yaliyopanuliwa na kutengenezwa zaidi tu nayo yalikuwa ya kudumu, na hali hema iliweza kuhamishwa.
6 Kwa sababu gani hema hii, iliyojengwa karibu miaka 3,500 iliyopita katika jangwa la Sinai, ina maana kwetu? Kwa sababu sehemu kubwa ya kitabu au barua fulani ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo imeandikwa juu yake. Kusudi la kwanza la hema hiyo lilikuwa la kinabii. Mwandikaji wa barua hiyo anaonyesha hili anaposema kwamba makuhani waliotumikia katika hema hiyo na mahekalu ya baadaye walikuwa ‘wakitumikia mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana [Mungu] asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima.’—Ebr. 8:5.
7. Kwa sababu gani Mungu ametupa sisi mfano wa mambo mengine ya kimbinguni?
7 Kila mtu aliye Mkristo anataka ajue mambo mengi ya kimbinguni kama iwezekanavyo, walau mambo yale yanayohusiana sana na kuishi kwetu kwa njia impendezayo Yehova. Mwanadamu hawezi akaelewa jambo vizuri sana asipokuwa ameliona au akapatwa nalo, au asipokuwa ana kitu cha kulilinganisha nacho. Kwa mfano, mtu katika nchi isiyostaarabika ambaye hajapata kuona jengo refu sana la kisasa linalofika juu sana angani (“skyscraper”), akiambiwa kwamba mengine yayo ni yenye urefu wa orofa 40, aweza akauliza, ‘Je! ni refu kama mti ule?’ Ukimwambia, ‘Ee! ni refu mara nne kuliko huo,’ anaanza kuelewa unavyomaanisha, naye aweza kuwaza akilini mwake urefu wa jengo hilo. Kwa hiyo Mungu ametupa sisi kwa huruma mfano wa kidunia uonekanao unaotupa mawazo fulani juu ya mambo ya kimbinguni, hasa kanuni na matakwa ya ibada ya kweli.
8. Je! tunafanya uchunguzi huu kusudi tujifunze namna hema ilivyokuwa tu?
8 Kwa hiyo, itatufaidi kuuangalia mwundo wa hema na vitu vilivyokuwamo ndani yake, kwa maana hilo ndilo lililokuwa kusudi la Mungu kuijenga. Ndipo tunapoweza kuelewa zaidi anayotazamia kutoka kwetu katika ibada leo. Kama vile Mwana wa Mungu mwenyewe alivyomwambia mwanamke Msamaria: “Saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”—Yohana 4:23.
9. Ni kwa njia gani hema ilivyokuwa mahali pakuu kwa Waisraeli?
9 Hema hii au “hekalu” ndipo palipokuwa mahali pakuu pa ibada ya kweli kwa taifa la Israeli. Kwa kweli, hema ndiyo iliyokuwa mahali pakuu penyewe pa kambi ya Waisraeli ya watu kati ya milioni mbili na tatu. Walawi, waangalizi wa jengo hilo, walipiga hema umbali wa kadiri kuizunguka, kisha, mbali zaidi, makabila kumi na mawili, matatu matatu pande zote nne. Mahali ilipokuwa hema paliweza kuonekana kwa vyepesi kwa kuwa palikuwa na wingu juu ya chumba cha Patakatifu Sana. Wingu hili lilionekana kama moto usiku, na kwa hiyo lilionekana kwa wote, po pote walipopiga hema. Watu walipofikiria ibada, waliifikiria hema, kwa maana humu ndimo dhabihu zote zilimotolewa na ndimo makuhani walimofanyia utumishi wao. Hata maulizo ya maana yaliyohusu taifa yalijibiwa humu na Mungu kupitia kwa kuhani mkuu kwa kura takatifu, Urimu na Thumimu.
10. Ni kwa njia gani Mungu alivyokaa hemani?
10 Kama yalivyokuwa majengo yenye kudumu zaidi yaliyochukua mahali pake, hema ilikuwa “patakatifu.” Mungu mwenyewe hakukaa katika hema hii, wala yeye hakuwa na sanamu yake mwenyewe humo. Alikaa humo kwa roho tu. Hii ilionyeshwa na nuru ya mwujiza juu ya Sanduku la Agano katika chumba cha Patakatifu Sana. Lakini na tuuangalie mwundo wote zaidi.
MWUNDO WA HEMA
11. Simulia ua.
11 Sehemu ya nchi iliyotengwa iwe eneo la hema ilikuwa dhiraa 100 urefu wake (karibu futi 146) na dhiraa 50 (karibu futi 73) upana wake. Eneo hili liliitwa “ua.” Katika ukingo huu kiambaza cha kitani kilisimamishwa, chenye urefu wa dhiraa tano (karibu futi 7 1/4) kwenda juu, kikitegemezwa na nguzo za shaba nyekundu. Katikati ya upande wa mbele (wa mashariki) wa eneo hilo lilikuwapo lango lililofanyizwa kwa kisitiri kilichosokotwa chenye rangi nzuri cha dhiraa 20 (karibu futi 29) urefu wake.—Kut. 27:9-19.
12. (a) Ni vitu gani vilivyokuwa ndani ya ua? (b) Simulia mwundo wa hema.
12 Mtu alipokuwa akiingia langoni angeweza kuiona madhabahu ya shaba nyekundu kwanza ya sadaka ya kuteketezwa, ambayo dhabihu za namna mbalimbali ziliwekwa juu yake. (Kut. 27:1-8) Nyuma yake lilikuwapo birika la shaba nyekundu lenye maji ya kunawia makuhani. (Kut. 30:17-21) Halafu, nyuma kidogo katika ua, ndipo hema yenyewe ilipokuwa. Jengo hili lenye pembe nne lilikuwa dhiraa 30 (karibu futi 44) urefu wake, dhiraa kumi (karibu futi 14 1/2) upana wake na dhiraa kumi urefu wa kwenda juu. Lilifanyizwa kwa mbao 48 zilizofunikwa kwa dhahabu, kila ubao ukiwa wenye maboriti matatu, juu, chini na katikati. Ukumbini mlikuwa na nguzo tano zilizofunikwa kwa dhahabu, na katikati ya Patakatifu, au chumba kilicho kikubwa zaidi, na Patakatifu Sana mlikuwa na nguzo nne zilizofunikwa kwa dhahabu. Mbao zote na nguzo zilisimamishwa juu ya matako ya fedha ngumu, isipokuwa zile nguzo tano za mbele, zilizokuwa na matako ya shaba nyekundu.—Kut. 26:15-33, 37.
13. Jengo la hema lilifunikwa au likahifadhiwaje?
13 Hema ilifunikwa kwa mapazia ya kitani nzuri, iliyotiwa mapambo kwa rangi nzuri ikiwa na michoro ya makerubi. Hawa wangeweza kuonekana kutoka ndani ya hema katika mianya iliyokuwa katika mbao. Pazia zuri lililo laini la singa za mbuzi lilikuwa juu ya kifuniko cha kitani na juu yake mapazia mengine mawili ya kuhifadhi, moja la ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu na kifuniko cha nje cha ngozi za pomboo, haya yakifanyiza paa.—Kut. 26:1-14.
14. Simulia visitiri viwili na mahali vilipokuwa katika “hema.”
14 Kisitiri kilichokuwa mbele kilikuwa cha kitani iliyotiwa mapambo mazuri, lakini hakikuwa na makerubi. (Kut. 26:36) Kisitiri kilichokuwa katikati ya vyumba vya Patakatifu Sana kilitiwa mapambo ya makerubi.—Kut. 26:31-33.
15. (a) Vipimo vya vyumba viwili vya hema vilikuwa nini? (b) Ni “vyombo” gani vilivyokuwa ndani ya chumba cha Patakatifu?
15 Chumba cha ndani zaidi, Patakatifu Sana, kilikuwa chenye mapana na marefu yanayolingana ya dhiraa kumi. Chumba cha mbele au cha mashariki, Patakatifu, kilizidi urefu wa hiki maradufu. Ndani ya Patakatifu, upande wa kaskazini, ilikuwako meza iliyofunikwa kwa dhahabu ya mikate ya wonyesho, juu yake pakiwa na mikate kumi na miwili, mmoja kwa kila kabila, pia ubani. (Law. 24:5-7) Upande wa kusini kilikuwako kinara cha taa cha dhahabu ngumu (si mshumaa). Mbele ya pazia kuelekea kwenye Patakatifu Sana ilikuwako madhabahu ya uvumba, iliyofunikwa kwa dhahabu.—Kut. 25:23-36; 26:35; 30:1-6.
16. Ni nini vilivyokuwa ndani ya chumba cha Patakatifu Sana?
16 Sanduku la Agano lilikuwa ndani ya Patakatifu Sana, likiwa limefunikwa kwa dhahabu pamoja na “kiti cha rehema” cha dhahabu ngumu, juu yake wakiwapo makerubi wawili wa dhahabu. Juu ya kiti na katikati ya makerubi lilikuwapo wingu la mwujiza la nuru, likionyesha kwamba Mungu alikuwa pamoja na watu wake hekaluni, si yeye mwenyewe, bali kwa roho. Roho takatifu yake ilikuwa ikitenda humo kwa kuitoa nuru hii.—Kut. 25:10-22; Law. 16:2.
SIKU YA UPATANISHO
17. (a) Siku ya Upatanisho ilikuwa wakati gani? (b) Mingine ya mipango ya pekee ya siku hiyo ilikuwa nini?
17 Watu walileta dhabihu zao kwenye hema hii wakati wote wa mwaka. Lakini siku ya kumi ya mwezi wa kumi na saba wa kalenda ya Kiebrania ndiyo iliyokuwa siku ya kutazamisha ya mwaka. Ilikuwa ndiyo Siku ya Upatanisho. (Law. 16:29-31; 23:27) Siku hii lango la kuelekea kwenye ua lilifunguliwa kusudi watu waweze kuona yaliyotukia uani, lakini watu wo wote wasiopewa utumishi wa hekaluni wasingeweza kuingia. Kisitiri cha hema kilichokuwa nyuma ya zile nguzo tano za ukumbini kilibaki pale pale wakati wote, hivi kwamba hakuna mtu aliyeweza kuona yaliyotukia ndani ya hema isipokuwa makuhani waliotumikia humo. Walakini, ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia hemani wakati mambo ya upatanisho yalipokuwa yakiendeshwa. (Law. 16:17) Hakuna mtu aliyeingia katika Patakatifu Sana wakati wo wote isipokuwa kuhani mkuu, aliyeingia katika chumba hicho siku hii moja tu ya mwaka.—Ebr. 9:7.
18. Ni wanyama gani hasa waliotumiwa Siku ya Upatanisho?
18 Mbali na sadaka za kuteketezwa zilizo za lazima, Siku ya Upatanisho dhabihu kuu zilikuwa ng’ombe mume mchanga asiye na kasoro, na mbuzi, aliyeitwa ‘mbuzi kwa ajili ya Yehova.’ Mbuzi mwingine aliletwa ndani pia, ambaye juu yake kuhani mkuu aliziungama dhambi za watu, naye mbuzi huyo alielekezwa jangwani, akafie huko.—Law. 16:3-10.
19. Simulia kuingia kwa mara ya kwanza na ya pili kwa kuhani mkuu katika Patakatifu Sana Siku ya Upatanisho.
19 Yule ng’ombe mume alisimamishwa upande wa kaskazini wa madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kisha alichinjwa. (Linganisha Mambo ya Walawi 1:11.) Kuhani mkuu aliingia kwanza katika Patakatifu Sana akiwa na chetezo chepesi chenye makaa yaliyotolewa madhabahuni. (Law. 16:12, 13) Baada ya kufukizia uvumba katika Patakatifu Sana aliingia ndani tena, wakati huu akiwa na kadiri fulani ya damu ya yule ng’ombe mume, ambayo aliinyunyiza nchini mbele ya Sanduku la Agano na kulielekea pamoja na kiti cha rehema chake. Damu hii ilikuwa ombi la rehema ya Mungu kwa ajili ya kipatanisho cha dhambi za kuhani mkuu na “nyumba yake,” iliyotia na kabila lote la Lawi.—Law. 16:11, 14.
20. Kuingia kwa mara ya tatu kwa kuhani mkuu kulikuwaje, nayo mafuta na mizoga ya sadaka za dhambi yalifanyiwa nini siku hiyo?
20 Mara ya tatu aliingia katika Patakatifu Sana akiwa na damu ya ‘mbuzi kwa ajili ya Yehova,’ iliyonyunyizwa mbele ya Sanduku kwa ajili ya dhambi za watu. Kadiri fulani ya damu ya ng’ombe mume na ya yule mbuzi iliwekwa juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya pembe zake. Mafuta ya wanyama hawa yaliteketezwa juu ya madhabahu, nayo mizoga ilichukuliwa nje ya kambi na kuteketezwa, ngozi na kila kitu.—Law. 16:25, 27.
21. Waisraeli walipata faida gani kutokana na dhabihu za Siku ya Upatanisho?
21 Kwa njia hii watu waliridhika kwa kujua kwamba walikuwa wakiyafanya aliyoyaamuru Mungu, yaliyompendeza yeye, na kwamba dhambi zao zilisukumiwa mbali mpaka mwaka mwingine. Mtume Paulo anatoa maelezo juu ya mpango wa dhabihu wa Torati: “Damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili.”—Ebr. 9:13.
22, 23. Kwa sababu gani dhabihu zilizotolewa huko nyuma Siku ya Upatanisho hazikuwa nzuri kama dhabihu ya Kristo?
22 Lakini ilikuwa lazima Waisraeli waishike Siku ya Upatanisho kila mwaka, na vipindi fulani watoe dhabihu zilizotajwa wazi kwa ajili ya dhambi fulani za mtu mmoja mmoja. Kama vile mtume alivyoendelea kusema: “Si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa [roho ya] milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”—Ebr. 9:14.
23 Torati, pamoja na hema na hekalu lake, ilikuwa tu na “kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo,” kwa maana “mwili ni wa Kristo.”—Ebr. 10:1; Kol. 2:17.
24. Waisraeli wa kale walishindwa kujua nini ambacho sisi tumejulishwa leo?
24 Waebrania hawakupata kuwaza kwamba siku moja wangekuwa na Kuhani Mkuu ambaye angetoa uhai wake mwenyewe wa kibinadamu kama dhabihu na ambaye angeingia, si katika Patakatifu Sana pa ile hema au hekalu la kidunia, bali mbinguni penyewe, mbele za Mungu katika hekalu lake kuu la kiroho. Hekalu hilo la kiroho na namna ambavyo linatumikia kama mahali pakuu pa ibada ya kweli leo litazungumzwa katika makala ifuatayo ya mfululizo huu katika Mnara wa Mlinzi.—Ebr. 9:24.
—Kutoka Kitabu God’s Kingdom of a Thousand Years Has Approached.
Mchorokatika ukurasa wa 429]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
1. Sanduku
2. Pazia
3. Patakatifu Zaidi
4. Madhabahu ya Uvumba
5. Meza
6. Kinara cha Taa
7. Kiwambo
8. Patakatifu
9. Birika
10. Madhabahu ya Sadaka ya Kuteketezwa
11. Ua
12. Lango
13. Mashariki
14. Kaskazini
15. Magharihi
16. Kusini