Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w74 9/15 kur. 415-420
  • Zawadi Inayotoka kwa Yehova Mwenyewe

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zawadi Inayotoka kwa Yehova Mwenyewe
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MAARIFA YA KWELI
  • NIA IFAAYO NI YA MAANA
  • USIIPUZE ZAWADI
  • Kwa Nini Sisi Twahitaji Maarifa Sahihi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Je! Wewe Hutafuta Hazina Zilizofichika?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Wanadamu Wahitaji Ujuzi Juu ya Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Kupata Ujuzi Sasa na Milele
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
w74 9/15 kur. 415-420

Zawadi Inayotoka kwa Yehova Mwenyewe

“Kila zawadi njema na kila upaji mkamilifu hutoka juu, kwa maana hushuka kwa Baba wa mianga ya mbinguni.”​—Yak. 1:17, NW.

1. Watu wengi wanalionaje shauri la kufuata kanuni za Biblia?

HUENDA umesikia watu wakisema hivi: “Hakuna faida ya kuwa mwema au kufuata kanuni za Biblia.” Wakitegemeza dai hili huenda wakasema: “Haya, ebu tazama karibu yako. Ni nani aliye na mali nyingi za ulimwengu huu? Ni wale walio Wakristo wenye kufuata kanuni za Biblia au wale wafanyayo yanayowapendeza? Kwa kawaida, ni nani awezaye kuwa na nyumba kubwa zaidi na fedha nyingi zaidi katika benki, motakaa za bei ghali zaidi na mali nyingine za kimwili zilizo ghali? Je! ni Mkristo mwaminifu, mnyofu, mwenye bidii anayeishi kulingana na kanuni za Biblia, au ni mtu mdanganyifu, mwenye kupunja, mwenye kusema uongo, bila ya kujali yumo katika siasa, biashara au dini?” Huenda hata wakafikia hatua ya kusema kwamba Biblia inaliunga mkono shauri hili na kusoma maneno ya Yesu aliposema kwamba Mungu “huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (Mt. 5:45) Huenda wakasema hii yaonyesha kwamba Mungu hapendelei watu, bila ya kujali ni wema au wabaya. Kwa hiyo kuna faida gani kuwa wema, wanyofu na waaminifu? Sababu gani kuishi kulingana na kanuni za Biblia?

2. Ni zawadi gani Mungu aliyowapa watu wake, nayo ni yenye thamani gani?

2 Lingekuwa kosa kukata maneno kwamba Mungu anawabariki waovu kwa njia ambayo anawabariki wale walio na nia ya haki. Usidanganywe na ye yote ufikiri kwamba una vitu vichache au utakuwa na vichache kwa sababu tu ya kufuata Neno la Mungu. Mkristo wa kweli anabarikiwa zaidi naye ni tajiri zaidi sana kuliko wengine wote. Ni kweli kwamba huenda usiwe na eka nyingi za nchi, fedha nyingi, motakaa nzuri, au nyumba kubwa, lakini Wakristo wana zawadi ambayo Mungu ameiweka akibani kwa ajili ya watu wake na ‘akawaficha’ wengine. Uwezo wote na utajiri wa hii taratibu mbovu ya mambo hauwezi kuipata zawadi hii aliyoiweka Mungu akibani kwa ajili ya watu wake. Uwezo wote wa mtawala mwenye kutumia nguvu hauwezi kuipata. Nguvu za mfalme au rais haziwezi kuipata. Dhahabu yote na fedha ya matajiri haiwezi kuinunua. Zawadi hii ambayo Mungu amewapa watu wake ni yenye thamani kuu kuliko dhahabu na fedha. Hiyo ndiyo nini? Ni maarifa ya kweli ya Neno la Mungu na kusudi!​—Mhu. 2:26; Mt. 11:25; Mit. 8:10, 11.

3. Ni kwa njia gani maarifa ya Yehova yalivyo makuu kuliko elimu ya kilimwengu?

3 Maarifa fulani juu ya uhai na juu ya mazingira yetu ni ya lazima ili kuishi siku baada ya siku. Huenda watu wengine wakatumia miaka mingi wakijipatia maarifa wanayodhani yatasaidia kufanya maisha zao zenye kufurahisha na kufaidi zaidi. Wengine wanachunguza maarifa wanayotumaini yatawapa afya bora na maisha marefu zaidi, ambazo ndizo tamaa za kawaida za wanadamu wote. Linganisha faida za maarifa haya na ambavyo maarifa ya Mungu wa kweli yatafanya. “Uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” (Yohana 17:3) Kuishi milele​—ni faida kama nini inayotokana na kuipata zawadi hii ya Mungu mwenyewe, maarifa ya kweli juu yake na Mwanawe. Je! kuna elimu ya kilimwengu ya kadiri yo yote iwezayo kumpatia mwenyeji wake uzima wa milele? Si ajabu kwamba Sulemani alisema hivi: “Ukiutafuta kama fedha, na kuutafutia kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha [Yehova], na kupata kumjua Mungu.” (Mit. 2:4, 5) Wanadamu wanatumia wakati mwingi, wanatia bidii nyingi na kuvumilia taabu wapate mambo ya asili. Je! mtu asiyathamini zaidi sana maarifa ya Mungu?

4. Mkristo anafaidikaje kutokana na tumaini na ahadi za Biblia?

4 Ebu fikiri ingekuwa na maana gani kwako kujua kwa hakika kwamba ungeweza kuishi milele papa hapa duniani chini ya hali za paradiso. Kujua kwamba kwa kweli wakati huo unakuja, tena karibuni, wakati ambapo wanadamu wataishi katika usalama, wakati ambapo vizuizi vya kitaifa na vya kikabila vitaondolewa na wakati ambapo uhusiano wa viumbe na mazingira yavyo wa dunia hii utasawazika kunaleta amani ya akili kweli kweli. Ni tofauti sana na watu wa siku zetu wasio na haya maarifa ya kweli ambao Biblia inasema juu yao hivi: “Watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu.” (Luka 21:26) Tofauti yake, wale waliojipatia zawadi ya Mungu mwenyewe ni watulivu na wenye matumaini namna gani. Ni kama vile alivyoandika nabii Malaki: “Nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.”​—Mal. 3:18.

5. (a) Je! maarifa ya kweli yaweza kurithiwa? (b) Huenda kweli ya Biblia ikavihusuje vifungo vyetu vya jamaa, na imetupasa tulioneje hili?

5 Zawadi hii ya maarifa haipitishwi kwa kizazi kimoja hata kwa kingine bila ya jitihada yo yote, kutoka kwa baba hata kwa mwana au kutoka kwa mama hata kwa binti, kama zinavyopitishwa tabia za kimwili. Hata inaelekea kwamba washiriki wengine wa jamaa huenda wakaipokea zawadi hii inayotoka kwa Yehova mwenyewe na wengine wasipokee, bila kujali kama ni baba au mama, mwana au binti. Huenda wale wasio na zawadi ya maarifa ya kweli hata wakawa adui zetu, wajapokuwa wa jamaa ile ile. Yesu alikuwa akifikiria hili aliposema: “Adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.” (Mt. 10:34-37) Je! mtu ambaye labda amekataliwa na jamaa yake anapata hasara kwa njia hii? Sivyo, kwa maana zaidi ya kuipata zawadi ya kimungu ya maarifa yenyewe, mtu anapata pia “ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto” wa kiroho mara mia. (Marko 10:29, 30) Furaha tunayoweza kupata katika kumtumikia Yehova kwa kushirikiana na jamaa hawa wa kiroho inapita hasara yo yote.

MAARIFA YA KWELI

6. (a) Mapenzi ya Yehova kwa wanadamu ni nini? (b) Mtu ‘anapataje kujua yaliyo kweli’?

6 Watu wengi wameisoma Biblia na wana maarifa kadiri fulani juu ya Muumba wao. Walakini, inapendeza kuangalia kwamba mapenzi ya Mungu ni kwamba “watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.” (1 Tim. 2:4) Inampasa mtu ajue kwamba mengi zaidi kuliko maarifa yasiyofahamika vizuri yanahitajiwa. Hili lilikuwa mojawapo la matatizo waliyokuwa nayo watu wa Kiyahudi wa siku za mtume Paulo. Aliwataja kama “wenye msingi wa maarifa na wa kweli.” (Rum. 2:20, NW) Kama mtu anayejenga nyumba angeacha baada ya kumaliza msingi, jitihada yake isingefaa sana. Inapaswa nyumba ikamilike itumike ilivyokusudiwa. Ikiwa mtu anajifunza sehemu fulani za Biblia “zinazopendeza” tu, maarifa yake yatakuwa “msingi” tu usiofaa sana. Inampasa mtu afahamu kwamba “Andiko lote liliongozwa na roho ya Mungu na ni lenye faida” ikiwa mtu ‘atapata kujua yaliyo kweli.’​—2 Tim. 3:16, NW.

7. Je! moyo mweupe watosha kumpendeza Mungu? Eleza.

7 Kwa kweli, ufahamu usiokamilika wa Neno la Mungu waweza kuwa hatari. Bila ya ufahamu uliokamilika tungeweza kupotezwa kwa vyepesi tudhani kwamba twamtumikia Mungu huku tukifanya jambo linalotofautiana kabisa na mapenzi yake. Yesu aliwaonya wafuasi wake juu ya watu hao: “Saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.” (Yohana 16:2) Huenda wakawa walikuwa wenye moyo mweupe kwa kuwaua wafuasi wa Kristo, lakini walikosea. Paulo anatuambia tatizo lao lilikuwa nini: “Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.” (Rum. 10:2) Wale wanaodhani wanamtumikia Mungu kwa bidii inawapasa ‘waendelee kujijaribu kama wamo katika imani, waendelee kujithibitisha walivyo.’​—2 Kor. 13:5, NW.

NIA IFAAYO NI YA MAANA

8. (a) Ni nini msingi wa maarifa ya kweli? (b) Maana yake nini kumcha Yehova?

8 Kwa kuwa maarifa ya Mungu wa kweli ni yenye faida sana nayo yapatikana kwa vyepesi, kwa sababu gani wanadamu wachache sana ndio walio nayo? Mara nyingi sababu ni kwamba wana nia isiyofaa juu ya Yehova na Neno lake. Kwa mfano, jambo moja la lazima lilitajwa na Sulemani, mmojawapo wa watu wenye hekima zaidi waliopata kuishi: “Kumcha [Yehova] ni chanzo cha maarifa.” (Mit. 1:7) Hii haina maana ya kwamba mtu atamwogopa Mungu kama ambavyo angeogopa adui anayejaribu kumdhuru. Badala yake, kwa kumheshimu Mungu na kwa kushukuru kwa yote aliyoyafanya na atakayoyafanya, mtu asingetaka amkatishe tamaa kamwe au aghadhibikiwe naye. Mtu yule yule mwenye hekima aliyetajwa juu baadaye alisema hivi: “Kumcha [Yehova] ni kuchukia uovu.” (Mit. 8:13) Kwa hiyo, ili mtu aweze kusema kwa kweli kwamba anao uchaji huu wa Kimungu, lazima auhakikishe kwa kuchukia maovu. Huenda ikampasa kufanya mabadiliko makubwa maishani mwake ajipatanishe na kanuni ya haki ambayo Mungu ameweka. Uchaji, heshima na hofu ifaayo ya Yehova vinaweka msingi wa maarifa ya Mungu wa kweli na ulimwengu wake wote.

9. Inatupasa tutambue mambo gani juu ya Kristo Yesu?

9 Kitu kingine ni cha lazima katika kuipata zawadi ya maarifa ya kweli juu ya Mungu, nacho hicho ndicho heshima ifaayo kwa Mwana wa Mungu, Kristo Yesu. Mbali na kuwa mkombozi wa wanadamu wote, yeye ana cheo cha kiserikali katika ulimwengu wote kipitwacho na kile cha Baba yake tu, Yehova Mungu. Kulingana na mambo yalivyo kweli yeye aliweza kusema hivi: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” (Mt. 28:18) Amekabidhiwa hukumu yote. Ufufuo unatukia kwa amri yake naye ndiye mwenye uwezo wa kuponya wanadamu wote na matokeo ya dhambi yenye kufisha. Kwa kweli, madhara yote yaliyoletwa na uasi wa Shetani katika bustani ya Edeni yataondolewa kupitia kwa Yesu Kristo. Si ajabu kwamba mtume Paulo alisema hivi juu ya Yesu: “Ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.” (Kol. 2:3) Lazima cheo chake katika kusudi la Mungu kitambuliwe ikiwa tutaipata zawadi ya Mungu ya maarifa.​—Mt. 20:28; Yohana 5:22-27; 6:39, 40; Ebr. 7:23-25; 1 Yohana 3:8.

10. Kwa sababu gani wengine hawaielewi kweli wanapoyasoma Maandiko, na imetupasa tuwe na hali gani ya akili?

10 Mtu hawezi kusoma Biblia akiwa na mawazo ya zamani akatumaini kupata yale Yehova anayotaka tuelewe kutokana nayo. Ikiwa mtu amejiacha aongozwe na fundisho la kipagani la kutokufa kwa nafsi ya kibinadamu huenda akasoma na kuyapita maneno haya moja kwa moja, “Nafsi inayofanya dhambi​—hiyo yenyewe ndiyo itakufa,” hata asielewe nayo. (Eze. 18:4, 20, NW) Huenda akaendelea kuamini kwamba nafsi haiwezi kufa. Na hali mtu uyu huyu aweza kupotoa maneno au mafungu ya maneno penginepo katika Biblia akijaribu kuhakikisha imani yake. Ni namna gani wale walio na uelekevu wa akili walivyo tofauti, kwa maana wanaacha yale wanayojifunza katika Neno la Mungu yatengeneze kuwaza kwao na njia ya maisha! Wanajisikia kama alivyojisikia mtunga zaburi: “Ee [Yehova], unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.”​—Zab. 25:4; 2 Kor. 4:4.

11. Ni kwa njia gani nia mbaya inavyoweza kuhusu kujifunza kwetu Neno la Mungu?

11 Zaidi ya kuwa na uelekevu wa akili inampasa mtu awe na nia inayofaa katika kujifunza Neno la Mungu. Wayahudi fulani wa siku za Yesu walikuwa wenye bidii nyingi ya kujifunza na hali Yesu aliwaambia hivi: “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake.” Hakuna ubaya wa kutamani uzima wa milele. Ni tumaini linalofaa, lakini ikiwa kuupata ndilo kusudi lake tu katika ‘kuyachunguza maandiko,’ basi hatutayapata maarifa yanayoongoza kwenye uzima wa milele. Baada tu ya maneno ya juu Yesu aliionyesha nia ifaayo waliyoikosa watu hao wa Kiyahudi: “Nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu.” (Yohana 5:39, 42) Inatupasa tumpende Mungu ili tuipokee zawadi hii ya kipekee ya maarifa ya kweli.

12. (a) Yesu alikuwa na maana gani aliposema ‘tuwe kama vitoto’? (b) Ili tupate maarifa, ni hatari gani inayopaswa kuepukwa?

12 Kitu kingine cha lazima ili kuipokea zawadi hii isiyolinganika thamani kutoka kwa Mungu kinatajwa katika zaburi: “Wenye upole atawaongoza katika hukumu, wenye upole atawafundisha njia yake.” (Zab. 25:9) Kwa hiyo, mtu mwenye majivuno na kiburi hawezi kutazamia kuyapata maarifa haya mpaka abadili nia yake. Imetupasa ‘tuwe kama vitoto,’ tukiwa na uelekevu wa akili na mioyo yenye kufundishika, ili tuelewe Neno la Mungu. (Mt. 18:3) Hii yatusaidia kufahamu sababu kwa nini watu wengi waliofanya uchunguzi mwingi wa Biblia huenda hata sasa wasielewe mambo ya msingi kama vile kusudi la Mungu kwa dunia. Huenda wakazijua lugha za kwanza za Biblia za Kiebrania, Kiaramu na Kigiriki, lakini mara nyingi wameacha maarifa yao ‘yawatutumue kwa kiburi.’ Ni kama vile Yesu alivyosema: “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.” (Mt. 11:25) Maoni yafaayo juu ya maarifa yo yote ambayo huenda tukawa nayo yanasemwa na Paulo akiongozwa na roho ya Mungu: “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.” (1 Kor. 8:2) Unyenyekevu na kutegemea msaada wa Mungu kupitia kwa roho yake ni vya lazima ili kupata maarifa ya kweli ya Biblia.​—1 Kor. 8:1; Yak. 1:5.

USIIPUZE ZAWADI

13. Je! zawadi itokayo kwa Yehova inakuja bila jitihada kwa upande wetu?

13 Ijapokuwa ni kweli kwamba maarifa ni “zawadi” kutoka kwa Mungu, hayapatikani au kudumishwa bila jitihada kubwa ya mtu mwenyewe. Kwa mfano, huenda mwanamuziki akasemekana kuwa mwenye kipawa cha kupiga kinanda cha nyuzi (piano). Anapokipiga, inaonekana kana kwamba hakihitaji jitihada kukipiga. Huenda akawa na maelekeo fulani ya asili yanayoufaa uwezo wake wa muziki, hata hivyo haitupasi kukata maneno kwamba uwezo wake wa kupiga ulikuja bila jitihada au kwamba anakidumisha kipawa hiki bila mazoezi. Ndivyo na kupata kwetu maarifa ya Neno la Mungu na kuyadumisha. Huenda ukaona wengine ni wenye ujuzi katika matumizi yao ya Biblia. Hata lizuke ulizo gani, wanaelekea kuwa na jibu la Maandiko. Wanafanya ionekane kana kwamba ni vyepesi sana kutoa majibu. Lakini usikate maneno kwamba wao walipata maarifa yao bila jitihada. Bila ya kujali sisi ni akina nani, kuongeza maarifa ya kweli ya Biblia kunahitaji kujifunza kwa makini, na mara tuyapatapo inatupasa tuendelee kujifunza tuyadumishe. Hii inatukumbusha maneno ya mtume Paulo kwa Timotheo juu ya “karama,” mgawo wake wa utumishi katika kundi la Kikristo: “Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako.”​—1 Tim. 4:14.

14. Mtu anasitawishaje mbegu ya kweli, na kwa sababu gani?

14 Kutazama kwa Mkristo machezo katika televisheni, kusikiliza vipindi vya radio vinavyoshughulika na matatizo ya kinyumbani, au kusoma vitabu vya hadithi zilizobunika ili ayaendeleze maarifa yake juu ya kusudi la Muumba kungekuwa sawa na mkulima kutumia mashine ya kukatia majani akuze mihindi yake. Hicho ni chombo kisichofaa. Badala ya kufaa ingeharibu zaidi. Biblia ndicho chombo kilichotolewa na Yehova Mungu, na kupitia kwa tengenezo lake lionekanalo ametoa misaada mingi ya kusitawishia mbegu ya kweli. Haja yetu ya kusitawisha na kuendeleza maarifa yetu ya kweli inapatana na ambavyo Paulo aliwaandikia Waebrania: “Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.” (Ebr. 6:1-3) Kwa kuwa ni kusudi la Mungu dunia ijazwe na wanaume na wanawake wenye maarifa kamili chini ya Ufalme, basi ni vema sasa Wakristo wafanye maendeleo katika maarifa yanayowafaa watumishi wa Yehova.​—Isa. 11:9.

15. Ni mtego gani unaopaswa uepukwe, na kwa sababu gani?

15 Lisingekuwa jambo la hekima kwa Mkristo kuzoea kusikiliza maenezi ya dini za uongo katika radio au televisheni, wala kuacha vitabu vya namna hiyo viletwe nyumbani kwake kwa kawaida, akidhani kwamba hii itamtayarisha akanushe mafundisho yasiyopatana na Maandiko. Wala isingefaa kufanya upekuzi usiofaa wa maandishi ya Biblia, akidhani kwamba hii ingemsaidia azungumze kwa njia ya busara na wale wasioiamini Biblia. Ili mtu aweze kusema vizuri, hajifunzi sarufi (grammar) mbaya bali, anajifunza kanuni za sarufi nzuri. Mtu akijua sarufi nzuri, makosa yataonekana wazi. Vivyo hivyo, mtu akijifunza kweli kutoka kwa Neno la Mungu, mambo ya uongo yataonekana wazi. Mtu aliye na maarifa ya kweli ya Neno la Mungu hatatatizwa katika kukanusha maoni ya uongo ya kidini. Lakini kuna hatari ya kujaza akili na mafundisho ya kidini yasiyopatana na Neno la Mungu. Mtume Paulo anatuonya katika habari hii anaposema hivi: “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”​—Kol. 2:8; 1 Kor. 10:12.

16. Zaidi ya funzo la mtu mwenyewe, ni nini zaidi kilicho cha lazima katika kupata maarifa ya kweli?

16 Ijapokuwa Biblia inatia moyo kujifunza kwa mtu mwenyewe kama njia ya kupatia maarifa ya kweli, vile vile inasema hivi: “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; hushindana na kila shauri jema.” (Mit. 18:1) Kwa hiyo imetupasa tuutafute ushirika wa wengine wenye hamu ya kuyajua mapenzi ya Mungu kwa njia ya kweli kama sisi. Si kwamba tu hii itakusaidia uongeze maarifa yako, bali pia itakutia moyo uendelee kujifunza na kuyatumia mambo unayojifunza. Kwa sababu ya haja hii ya kutiwa moyo, Neno la Mungu linashauri: “Tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”​—Ebr. 10:24, 25.

17. Nia inayofaa itatusaidiaje kupata maarifa ya Mungu?

17 Kwa habari ya kutwaa maarifa, watu wengi wangeweza kuonyesha kwa vyepesi kukosa kwao elimu ya kutosha, kutokuwa na kumbukumbu zuri na kutoweza kusoma. Hata hivyo, ukweli ungali kwamba Yehova ni “Mungu wa maarifa,” na imewapasa wanadamu wajitahidi kuonyesha mfano wake. (1 Sam. 2:3) Ikiwa hatujui kusoma wala kuandika twaweza kujifunza kufanya hivyo. Ikiwa hatujui maana ya maneno fulani twaweza kuyatazama katika kamusi. Ni kama vile kitabu cha Mithali kinavyosema: “Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.” (Mit. 15:19) Mvivu wa akili anaviona vizuizi tu, lakini njia inaonekana laini kwa “wenye unyofu.” Nia inayofaa itatusaidia sana tupate maarifa ya kweli.​—Kol. 3:10.

18. Bila ya kujali hali zetu zilivyo, nia yetu imepaswa kuwa nini juu ya zawadi inayotoka kwa Mungu mwenyewe?

18 Maarifa ya kweli juu ya makusudi ya Mungu kama yalivyofunuliwa katika Neno lake Takatifu Biblia ni zawadi nzuri ajabu kutoka kwa Baba mwenye upendo wa kimbinguni. Ikiwa wewe hujafaidika bado kutokana na msaada huu wa ukarimu kutoka kwa Muumba wetu, sababu gani usiwatafute wale unaojua ni wenye zawadi hii katika mtaa wako. Utawapata penye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova. Au, ikiwa wewe ni mmojawapo wa wale walioyapokea maarifa yaongozayo kwenye uzima wa milele karibuni au pengine miaka mingi iliyopita, yatumie uliyo nayo na kuyasitawisha. Kumbuka, pia, kwamba yale ambayo huenda hunayo kwa njia ya kimwili ukilinganishwa na wale wanaopuza Neno la Mungu, yeye ameyalipia kwa kukufaidi wewe na zawadi inayotoka kwake mwenyewe ya maarifa yenye kutoa uzima.​—Mit. 2:6.

[Picha katika ukurasa wa 415]

Fikiri ingekuwa na maana gani kujua kwa hakika kwamba ungeweza kuishi milele duniani chini ya hali za paradiso

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki