Tulidhani Taratibu Ingeweza Kubadilishwa
Mamilioni ya vijana wameona kwamba badiliko lahitajiwa. Pengine wewe wakubaliana nao au hukubaliani nao, lakini utasaidika ukijua sababu gani wana maoni hayo. Haya ni masimulizi yanayohusu jinsi kijana mmoja na mkewe walivyojaribu kubadili mambo, kisha wakajua njia ya pekee ya kuyabadili.
TULISHANGAA sana sisi watu zaidi ya 10,000 tuliokusanyika katika uwanja uitwao Chicago’s Grant Park alasiri ya Jumatano. Bunduki zilikuwa juu ya majengo yaliyokuwa karibu zikiwa zimeelekezwa tulikokuwa. Askari walinzi walikuwa kando kando ya barabara wakiwa na bunduki zenye visu virefu. Mapolisi wenye kofia za chuma walikuwa kila mahali. Kwa sababu gani? Kulikuwa na nini?
Ilikuwa Agosti 1968. Kilomita karibu sita na nusu kutoka uwanjani, kusanyiko la taifa la kidemokrasi lilikuwa likiendelea. Kusanyiko hilo ndilo lililokuwa limetuleta Chicago. Tulitumaini kwamba tukiwapo kwa wingi maamuzi mazuri yangefanywa katika kusanyiko hilo. Hasa tulitaka vita ya Vietnam ikomeshwe.
Lakini kwa sababu gani kukawa na bunduki zenye kumimina risasi kama maji, nyingine zenye visu virefu na mapolisi wenye kofia za chuma?
Kumbuka, ilikuwa Agosti 1968. Amerika ilizidi kujitia katika vita; Vietnam ya Kaskazini ilikuwa ingali inaangushiwa makombora. Viongozi wengi wa kisiasa walipendelea vita iongezeke. Walitaka mambo yaamuliwe kwa kupigana, na wengine hata waliwachukua wenye kutetea amani kuwa wenye hatia ya kufitini serikali.
Lakini sisi tuliona kwamba haikuwa lazima kutumia nguvu hivyo. Sisi tuliokuwa uwanjani hatukuwa na silaha. Wengi wetu tuliona kwamba viongozi wa Amerika walikuwa wameshauriwa vibaya. Sasa tulipanga kufanya maandamano yasiyo na fujo mpaka uwanjani. Lakini nililofanyiwa siku hiyo pamoja na mpenzi wangu Jeanne lilibadili mawazo yetu yote, likabadili sana maisha yetu.
Najua kwamba huenda watu wengine wakasema: “Lilikuwa shauri lenu kuandamana Chicago. Mlistahili kuona mlichokiona.”
Hata hivyo, wakati huo Jeanne nami tulidhani tulikuwa tukitenda mambo yanayofaa. Lakini, sasa twaweza kuona kwamba hiyo siyo njia inayofaa kubadili mambo, na twasikitika kwa sababu ya mambo tuliyofanya. Lakini kwa sababu gani maelfu ya vijana, naam, makumi ya maelfu ya vijana, walijikaza sana walete mabadiliko miaka hiyo? Nadhani maono yangu mwenyewe yatakusaidia ufahamu.
NILIKUWA NA MATUMAINI MAZURI JUU YA WAKATI UJAO
Mimi nilizaliwa na wazazi weupe wasio matajiri wala maskini, katika Minneapolis, Minnesota, mwaka 1947. Mwaka 1952 tulihamia Hawaii, ambako baba alipata ufanisi kwa kufanya mikataba ya kazi. Sisi tuliishi katika nyumba iliyokuwa karibu na bahari kuu, tukawa na vitu vyote vya kimwili tulivyohitaji. Amerika ilielekea kuwa nchi ambako mtu angeweza kupata cho chote alichotaka; tulikuwa na matumaini mazuri juu ya wakati ujao.
Maishani nilikuwa na mambo ya kunifurahisha—kuchezea kikoa chetu cha mpira nikiwa msaidizi wa mkingaji mkuu karibu na lango letu, kupiga mbio, kuogelea katika maji ya bahari kuu ya Pacific katika ua wa nyumba yetu, na kusimamia mambo ya shule. Baada ya muda mfupi nilipanga kuingia chuo kikuu katika bara.
KUONA MAGUMU MAKALI
Septemba 1965, nilijiandikisha katika Williams College katika Massachusetts. Ingawa nilikuwa na wakati mwingi wa kusoma na kutafakari, jambo fulani lilianza kunisumbua. Nilipokuwa Hawaii nilizoea kuona watu wa mataifa mbalimbali wakitendewa sawasawa, lakini mambo yalikuwa tofauti bara.
Wakati wa likizo la masika mwaka 1966 nilipanda ndege nikaenda Chicago kutembelea ndugu yangu mkubwa, aliyekuwa msimamizi wa University of Chicago Hospitals. Tuliposafiri kwa gari kupitia mitaa michafu ya Kusini ya Chicago, nilishangazwa sana na mambo niliyoona. “Watu wanawezaje kuishi hivi?” nilijiuliza. Lililonihuzunisha zaidi ni kwamba kwa ujumla watu hao walikuwa weusi.
Nilitaka kujua maoni ya weusi, kwa hiyo nikaanza kusoma vitabu walivyoviandika, pamoja na vile vilivyohusu maisha yao mmoja mmoja. Niliposoma habari ya udhalimu waliotendwa—kuuzwa kama watumwa, kutendwa kama kwamba walikuwa watu wanyonge, kuzuiwa wasiingie katika mikahawa, kuuawa kwa sababu ya makosa madogo tu—machozi yalinitoka. Nilikasirika, nikaanza kufikiria nitakavyoleta hali bora.
Nilianza kutazama mambo mengine pia yaliyohusu mataifa mbalimbali, kama vita ya Vietnam. Nilisoma magazeti nikaona Waamerika wakiwadharau sana Wavietnam nikashangaa kama tungaliwaangushia makombora hivyo kama wangalikuwa weupe. Nilisikia pia habari za jinsi faida kubwa za pesa zilivyopatikana kwa kutengeneza vifaa vya vita. Nikashangaa: Ni kweli kwamba watu wenye kutaka faida ya pesa, wenye nia ya kuua watu bila kujali, ndio wanaofanya vita iongezeke? Nilianza kufikiria hilo nilipopata habari kwamba wenye kugombea urais walitegemea pesa za watengenezaji hao ili waendeleze shughuli zao za uchaguzi.
Rais Johnson aligombea uchaguzi mwaka 1964 akaahidi kuleta amani Vietnam. Lakini baadaye, kila mwezi ulipopita vita iliongezeka kinyume cha vile alivyokuwa ameambia watu. Ili kudanganya watu, magazeti na radio zilisema kwamba wasimamizi walikuwa wakijitahidi sana. Kwa hiyo, je’. unaweza kuona sababu gani vijana wengi hatukutaka tena kutumaini viongozi wetu?
Lakini sasa kwa kuwa vita ilikuwa imeongezeka, wanachuo walianza kuingizwa jeshini. Ikanilazimu kufanya uamuzi mgumu.
JE! NIKUBALI KUINGIA JESHINI?
Miezi mingi nilijitahidi sana kuamua maulizo haya: Je! nitaiunga vita mkono? Nitachukua silaha nikaue Wavietnam?
Mwishowe nikaamua kwamba siwezi kufanya hivyo. Mimi niliona ilikuwa vibaya kufanya hivyo. Najua kwamba huenda watu wengine wakabisha wakisema: “Wapi, uliogopa tu kuingia jeshini. Nchi yako ikuambiapo ufanye jambo, kulingana na sheria inafaa utii.”
Wakati huo nililifikiria sana jambo hilo. Nilijua kwamba katika kesi zilizofanywa Nuremberg, Wajeremani na vilevile Adolf Eichmann wa nyakati za karibuni, walijaribu kujitafutia udhuru wa uhalifu waliotenda kwa kusema kwamba walikuwa wakitii maagizo ya wakuu tu. Hata hivyo, walionekana na hatia wakauawa! Walihesabiwa hatia ya matendo yao, ingawa nchi yao ndiyo iliyowaagiza watende maovu hayo.
Kulingana na maoni yangu watu wa United States walikuwa katika hali kama hiyo. Habari zenye kuhuzunisha sana zilizochapwa katika magazeti ya Amerika juu ya jinsi wanaume, wanawake na watoto walivyoteketezwa kwa moto zilinionyesha kwamba matendo hayo yalikuwa sawa na yaliyofanywa katika kambi za mateso za Ujeremani kumaliza watu katika majoko ya moto. Wazo hilo lilihakikishwa wakati Premier Ky wa Vietnam, kiongozi ambaye vikosi vya United States vilielekea kumwacha atawale, alipotangaza kwamba shujaa wa pekee ambaye yeye alipendelea ni Adolf Hitler.
JITIHADA ZA KUIBADILI TARATIBU
Sikuamua kutoingia jeshini nikiwa na kusudi la kuepa kazi hiyo. Bali, niliipenda sana nchi yangu, kwa hiyo nikaanza kufikiria jinsi ambavyo ningeweza kuiletea hali bora. Niliona kwamba nikiwa mtaalamu wa tabia za jamii ya watu ningeweza kusaidia kutatua matatizo makubwa ya Amerika ya kubagua mataifa, na hata matatizo kati ya mataifa yote. Kwa hiyo mwaka 1967 nilihamia University of Hawaii nianze mwaka wa kwanza wa kujifunza utaalamu huo.
Nilipokuwa shuleni niliona taarifa fulani katika ubao wa matangazo. Ilikaribisha wenye kupinga vita ya Vietnam wahudhurie mkutano wa chama cha wanafunzi cha kutetea umoja wa watu wote (Students for a Democratic Society). Karibu na wakati huo nikamjua Jeanne, mwanafunzi mwenzangu, naye akajiunga nami katika jitihada za kupinga vita.
Sasa hata habari zilikuwa zikionyesha wazi kwamba wakuu walikuwa wakitoa taarifa za uongo juu ya vita. Kwa hiyo, mwanzoni mwa 1968, kura zilipopigwa kuonyesha maoni ya watu juu ya vita, wengi waliipinga tukaanza kuona uwezekano wa kufaulu katika jitihada za kuibadili taratibu. Uwezekano huo ulielekea kuwa hakika wakati Rais Johnson alipotangaza siku ya Machi 31, 1968 kwamba asingegombea uchaguzi tena. Ilionekana kwamba hakutaka cheo hicho tena kwa sababu watu walichukizwa naye.
Siku chache baadaye msimamizi wa chama chetu cha wanafunzi alitoa hotuba yenye kusisimua, akapinga vita kwa kuchoma kipande chake cha kuingia jeshini, huku kamera za televisheni zikimpiga picha. Nilijiunga na wanafunzi wale wengine tukafanya vivyo hivyo—lakini sasa siwezi kufanya hivyo. Jioni hiyo matukio hayo yalitiwa katika habari za televisheni, na asubuhi yake yakaandikwa magazetini.
Mwezi Aprili, wanafunzi wenye kupinga vita katika mji wa New York walisimamia majengo ya Columbia University kwa nguvu, kisha wakafunga shule hiyo. Katika University of Hawaii, wanafunzi walikusanyika karibu kila siku wapinge vita. Halafu mwezi Mei, wakati Mtaalamu Oliver Lee alipoondolewa kazini na Chuo kwa sababu ya kupinga sana vita, wanafunzi walisimamia chuo kwa nguvu kwa muda wa siku kadha.
Jeanne nami tulikuwa kati ya mamia ya wanafunzi waliokaa katika Bachman Hall, tukidai Lee arudishwe. Mwishowe mapolisi walituondoa huku kamera za televisheni zikipiga picha. Tulikamatwa lakini tukafunguliwa asubuhi yake kwa kuwekewa dhamana.
Siku chache baadaye wanafunzi walitawanyika kwenda likizoni. Sasa tungefanyaje? Mwaka huo wa uchaguzi Waamerika wote walitazamia Kusanyiko la Kidemokrasi katika Chicago. Je! tungeweza kuleta badiliko, tufanye viongozi wakomeshe vita? Tulidhani tungeweza, tukaamua kujaribu.
“MAUAJI YA MICHIGAN AVENUE”
Yaliyotukia Jumatano ya Kusanyiko la Kidemokrasi yameitwa tangu wakati huo “Mauaji ya Michigan Avenue.” Mamilioni ya watu yaliona mauaji hayo katika televisheni. Serikali ilipochunguza matukio hayo iliyaita “ghasia za mapolisi.” Uchunguzi ulionyesha kwamba mapolisi walitenda jeuri “mara nyingi juu ya watu wasiovunja sheria yo yote, wasioasi agizo lo lote, wasiofanya tisho lo lote.” Nasi twaweza kuhakikisha hilo, ingawa waandamanaji wengine walichokoza mapolisi kwa kuwatukana.
Tulipojaribu kuanza maandamano baada ya kusikiliza hotuba katika uwanja Grant Park, mapolisi walitushambulia. Tulitupiwa sumu ya kutoa machozi tukasambaa. Askari wenye bunduki zenye visu virefu walikuwa kila mahali, wakiwa wamezuia watu madarajani katika sehemu kuu ya mji. Mwishowe tulipata daraja lisilochungwa sana tukaponyoka.
Tuliongezeka sana wakati wanafunzi zaidi walipofaulu kupanda madarajani na kujiunga nasi katika Michigan Avenue (mojawapo barabara za mji). Tulipokuwa tukidhani kwamba tutafaulu katika maandamano yetu, mapolisi na askari walitukatiza, wakaanza kutushambulia kwa sumu ya kutoa machozi na virungu. Waliokuwa karibu nao walikanyagwa-kanyagwa, damu ikawatoka-toka katika vichwa vyao vilivyopondwa-pondwa kwa rungu. Magari yaliyofungiliwa seng’enge upande wa mbele yalianza kuingilia makundi ya watu kama plau za kulima mashamba. Miili ya watu ilisagwa pamoja. Nilimshika Jeanne mkono nikajitahidi sana kumvuta kwenye usalama.
Mwishowe Jeanne, dada yake nami tuliponyoka katikati ya mapolisi tukakimbia tukawa mbali na matata. Ilikuwa saa 3 ya usiku nasi tuliona njaa, kwa hiyo tukala mkahawani. Njia ya pekee tuliyojua ya kurudi nyumbani ni kupanda gari-moshi karibu na Michigan Avenue.
KILICHOTUCHOSHA
Tulikuwa tunakaribia kituo cha garimoshi wakati kikosi cha mapolisi kilipoingilia pembeni mbio-mbio. Nikasema, “Twataka kupanda gari.” Walitutolea ukali wakatushika kwa nguvu, wakaanza kumpiga dada ya Jeanne kwa rungu alipojiponyosha. Tukatupwa katika behewa la mpunga. Katika kituo cha polisi, zaidi ya wanafunzi 100 tulifungiwa usiku kucha katika chumba kinachoitwa “tangi.”
Asubuhi yake nikapelekwa mbele ya hakimu. Lakini hakunipa nafasi ya kujitetea; hata hakuinua kope zake za macho anitazame! Dhamiri yangu haikuniruhusu kamwe nikubali kuwa mwenye hatia, kwa hiyo nikaamua kuhakikisha mashtaka yalikuwa ya uongo.
Basi Jeanne akarudi shuleni Hawaii, nami nikarudi Massachusetts kufanya masomo ya juu zaidi. Miezi iliyofuata nilisafiri-safiri kwa ndege kwenda Chicago mahakmani. Lakini, kila mara polisi aliyepaswa kutokeza mashtaka hakuonekana, kwa hiyo hakimu akawa akiahirisha kesi mpaka mwezi utakaofuata. Baada ya kutumia pesa nyingi sana, wakili wangu alisema ilikuwa kazi bure, kwamba wangeendelea kuiahirisha-ahirisha hata nishindwe kufika mahakmani, halafu waseme nina hatia.
Mambo hayo yalinionyesha kwamba taratibu isingeweza kubadilishwa. Niliacha kujaribu kuibadili, filosofia yangu ikawa ‘kula, kunywa na kufurahi.’ Mimi nilihudhuria shule nipate kuhitimu tu. Jeanne alitoka Hawaii, tukaishi pamoja na kutumia sana dawa za kulevya. Lakini maisha hayo ya anasa hayakutufurahisha.
TUMAINI LINGEWEZA KUPATIKANA?
Tulidhani tulikuwa tukionyesha twapinga unafiki na udhalimu wa serikali kwa mavazi tuliyovaa, sura zetu na mienendo yetu. Lakini je! dawa za kulevya, ngono za ovyo na mambo mengine katika maisha yetu yalileta hali bora? Nilianza kushangaa. Vijana wengi waliiona ndoa kuwa jambo la kizamani, lakini niliona kwamba kufanya-fanya ngono na watu mbalimbali hakukuwaletea furaha halisi. Sikutaka Jeanne nami tukose furaha, kwa hiyo kiangazi cha 1969 tukaoana.
Ingawa niliona kwamba ilikuwa kazi bure kujitahidi kuibadili taratibu, bado nilitaka kusaidia watu, kwa hiyo nikaamua kuwa mwalimu. Kwa kuwa nilitaka kwenda mahali ambako watoto walihitaji msaada hasa, nilianza kufundisha darasa la tatu katika mtaa mmoja wa weusi Kaskazini ya Philadelphia.
Nilipochunguza kumbukumbu za hospitali za wanafunzi wengi, niliona kwamba wengi walikuwa hawapati chakula cha kutosha na hawakuwa na uzito wa kutosha. Wengi waliishi katika vijumba vichafu ajabu, vilivyosongamana watu. Nikapata kujua kwamba wengine walikuwa wamekwisha fanya uasherati. Wachache walitumiwa na wazazi wao kuwauzia dawa za kulevya. Wengi hawakuweza kuongeza 2 + 3 wala kutambua herufi za alfabeti. Nilishangaa sana kuona hali mbaya hizo; nilidhani hakukuwa na tumaini! Nilivurugika akili kuona kwamba sikusaidia sana baada ya kujitahidi sana. Tungepata wapi shughuli yenye matokeo mazuri, yenye kufurahisha?
Tulichunguza sana mambo ya unajimu, imani za mafumbo na dini za Mashariki tusipate cho chote cha kutufurahisha. Ndipo niliposoma kitabu The Population Bomb cha Mtaalamu Paul Ehrlich wa Stanford University. Ehrlich alipotembelea Philadelphia, tulihudhuria hotuba yake. Alisema kwamba ilikuwa kuchelewa mno, kwamba wanadamu wangepatwa na mabaya yasiyo na kifani kwa sababu ya kuharibu mazingira na kuongoza vibaya mambo ya dunia. Lakini nikawaza labda mazingira yangetengenezwa kuwe na tumaini.
Tulipokumbuka jinsi tulivyovurugika akili baada ya kufanya maandamano ya kupinga vita, tulisita-sita tulipokaribishwa tuhudhurie mkutano wa kutengeneza mazingira katika Temple University, lakini mwisho tukakubali. Tulipoingia chumba kilichojawa na moshi wa sigareti na kusikia mazungumzo juu ya kumaliza uchafu wa hewa, tulijua shughuli hiyo ilikuwa ya bure tu. Hata hivyo, nilianza kusoma vitabu vingi juu ya mazingira na kujiandikisha katika mpango wa masomo ya mazingira, nipate daraja la juu. Nilisadiki kwamba taratibu ya viwanda ingekwisha, nikaanza kujitayarisha jinsi nitakavyoishi baada ya hapo.
Baba alikuwa na maelfu ya eka ya mimea ya kangaga (nyasi ndefu) katika kisiwa cha Hawaii. Tulianza kupanga kuanza huko mtaa wenye kujitegemea kabisa, usioharibu mazingira yake. Bila mchezo tulikuwa tukitafuta njia mpya za maisha, maana tulisadiki kwamba taratibu ingeangamia. Lakini, majibu tuliyokuwa tukitafuta yalitoka mahali ambapo hatukutazamia hata kidogo.
TUMAINI HALISI LA BADILIKO LENYE MANUFAA
Shule ilipofungwa ili kwenda likizoni ndugu yangu mdogo David alitoka Hawaii nasi watatu tukafunga safari fupi ya kupiga hema vichakani. David, aliyekuwa akifikiria kuwa mwalimu wa dini, alikuja na Biblia, na kila usiku tukaota moto huku akitusomea sura alizochagua. Tulishangaa kuona kwamba Biblia inapendeza sana tuliposikiliza masimulizi kuhusu Yusufu na nduguze na Daudi na Goliathi. Tena tuliposoma kitabu cha Mhubiri, maneno aliyokata humo kuhusu ubatili wa maisha katika taratibu hii ya mambo yalionekana kuwa ya kweli.
Kiangazi hicho Jeanne nami tulikuwa na wakati mwingi. Kazi ya pekee tuliyokuwa nayo ni kujaribu kupanda chakula cha kutosha katika kishamba chetu katika Philadelphia, chenye marefu na mapana ya futi 13. Kwa hiyo tulichukua Authorized Version ya Biblia tukaanza kusomeana kwa sauti kubwa. Kwanza, tulisoma masimulizi ya Injili na Matendo ya Mitume. Tuliposikiliza malawama makali ambayo Yesu alifanyia viongozi wa dini wa siku zake (Mathayo sura ya 23), moja kwa moja tuliwafikiria viongozi wa dini wa kisasa. Wao ndio waliokuwa wametufanya tusipendezwe na dini kwa sababu ya unafiki wao. Mfano mmoja ni wakati walipounga sana mkono vita ya Vietnam, wakati watu wote walipoipendelea, tena wakaipinga baada ya watu wale wengine kuacha kuiunga mkono.
Vilevile, tulisoma unabii mbalimbali wa Isaya, ukatupendeza sana. Nilipoyaona maneno, “nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” nilimwambia Jeanne, “Jama, Isaya huyu alikuwa mpinga vita. Hata alitaka kutengeneza mazingira; alitaka kutumia vifaa vya vita katika ukulima.”—Isa. 2:4.
Halafu tukayaona maneno yaliyotangulia hayo, “itakuwa katika siku za mwisho,” tukashangaa kama maneno hayo yalihusu siku zetu kwa njia fulani. Tulipoendelea kusoma, tuliona kwamba Isaya alikuwa akisema habari ya Yuda na Yerusalemu ya kale, lakini bado tuliona hali hizo zililingana na za karne ya 20. Kadiri tulivyozidi kusoma ndivyo tulivyozidi kusadiki kwamba unabii huo ulihusu kwa njia fulani taratibu yetu ya ulimwengu.
Ikiwa ndivyo, ilimaanisha taratibu potovu ya leo itaharibiwa, kama unabii mmoja ulivyoendelea kutabiri: “Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.”—Isa. 24:5, 6.
Je! tungeweza kuamini unabii huo? Tuliamini kwamba kuna Mungu Mwenye Nguvu Zote. Nasi tulistaajabishwa sana na viumbe vyake na kawaida za maumbile duniani. Tulistaajabishwa na vile mbegu ndogo sana tulizopanda udongoni zilivyozaa vyakula mbalimbali baada ya muda mfupi tu. Je! Muumba anayefanyiza miujiza hiyo aweza kuwa ndiye Mungu aliyempa Isaya ujumbe huo ulioelekea kulingana sana na siku zetu?
Tulianza kufikiri hivyo. Lakini, ikiwa taratibu hii ingeharibiwa kama Biblia ilivyoonyesha, je! kungekuwa na nyingine nzuri? Tulitaka kujua. Ili kutusaidia katika uchunguzi wetu tulinunua tafsiri ya kisasa ya Kiingereza, The Jerusalem Bible, na nyakati nyingine tukaisoma pamoja mchana kutwa.
MUNGU MWENYE UTU NA KUSUDI
Katika kurasa nyingi Jerusalem Bible hiyo ilitumia jina “Yahweh” badala ya majina “Bwana” na “Mungu.” Nikakumbuka kwamba nilipokuwa chuo kikuu nilisoma masomo ya dini nikaona kwamba Yahweh (au Yehova, kama linavyojulikana na watu wengi) ndilo neno la Kiingereza linalolingana na jina la Mungu linalopatikana katika hati za Biblia za lugha ya asili. Tuliposoma jina la Mungu mara nyingi tulianza kupendezwa. Tukaanza kumwona Mungu kuwa mtu halisi, mtu mwenye kusudi ambaye tungeweza kuongea naye. Lakini tukashangaa, Yahweh huyu ni mtu wa aina gani?
Tulizidi kumthamini Yahweh tulipoendelea kusoma habari za makusudi yake. Tulikumbuka sana sehemu ambazo Biblia yatabiri uharibifu wa taratibu potovu hii, kwa maana zilipatana na vile tulivyoamini. Lakini sasa tukaanza kuona kwamba inasema pia habari za taratibu mpya. Tuliposoma unabii kama ule unaopatikana katika sehemu ya mwisho ya Isaya sura ya 65 tuliona kwamba huenda wakati ujao ukawa bora. Unasema hivi:
“Naumba mbingu mpya na dunia mpya . . . Watajenga nyumba na kuzikaa, wapande mashamba ya mizabibu na kula matunda yake. . . . Hawatajitaabisha bure wala kuzaa watoto na kujiletea uharibifu, kwa maana watakuwa taifa lililobarikiwa na Yahweh, pamoja na watoto wao. Muda mrefu kabla hawajaita nitawajibu; kabla hawajaacha kusema nitakuwa nimekwisha sikia. Mbwa-mwitu na mwanakondoo watakula pamoja, simba ale majani kama ng’ombe . . . Hawatafanya madhara yo yote, hawatadhuru mlima wangu wote mtakatifu, asema Yahweh.”—Isa. 65:17-25, JB.
Je! Yahweh huyu kweli angeweza kuumba taratibu mpya yenye maisha mazuri hivyo? Ikiwa ndiye aliyeumba ulimwengu wote huu ulio mzuri sana, tuliona labda angeweza kutimiza ahadi zake. Lakini tulishangaa: Je! Yahweh ataokoa watu wo wote katika uharibifu wa ulimwengu unaokuja na kuwaingiza katika taratibu mpya? Ikiwa ndivyo, watu hao ni akina nani?
Kati ya makanisa tuliyoyajua, hakuna moja lililoelekea kuwa litaokolewa na Mungu. Kama tulivyoona, wanasiasa na wafanya biashara wapotovu walikuwa hasa ndio washiriki wa makanisa hayo, tena waliheshimiwa. Tena washiriki wa makanisa hayo ndio waliokuwa wakifanya vita katika mashariki ya kusini ya Asia. Kadiri tulivyozidi kusoma Biblia, ndivyo makanisa yalivyozidi kulaumiwa na kitabu kile kile walichodai kufuata.
Nikawa nitaanza kufundisha tena baada ya siku chache na kujaribu kujipatia daraja la juu nikimaliza masomo katika chuo kikuu. Vilevile, tulikuwa tumeanza kuvunjika moyo tusisome Biblia, maana hatukuwa na mtu wa kujibu maulizo mengi tuliyokuwa nayo. Wakati mmoja tulipokuwa tumekata tamaa tukafanya jambo tusilopata kulifanya. Jeanne nami tuliinama vichwa nikamtolea Yahweh sala kwa sauti kubwa, nikamwomba atuonyeshe tutakalofanya.
TWAJIFUNZA JINSI BADILIKO LITAKAVYOKUJA
Baada ya kusali, tuliwasha bangi tuanze kuivuta. Lakini muda si muda mlango ukagongwa. Je! ni mapolisi? Jeanne alikimbia-kimbia hapa na hapa akificha dawa za kulevya na kunyunyizia hewa manukato, nami nikatoka nje na kuufunga mlango.
Nilimwona mwanamke mweusi akasema ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alianza kunieleza mambo yale yale tuliyokuwa tumemaliza kuyaomba. Akanitolea kitabu Kweli Iongozayo kwenye Uzima wa Milele, nikakichukua. Nikauliza: “Naweza kuja wapi nijionee mwenyewe jinsi Mashahidi wa Yehova walivyo?” Akatukaribisha kwenye mkutano wao katika Jumba la Ufalme, akatupa pia nakala za magazeti Mnara wa Mlinzi na Amkeni!
Ilikuwa Jumamosi adhuhuri, naye Jeanne alikuwa ameketi katika chumba kimoja kusoma Mnara wa Mlinzi na Amkeni!, nami nikaanza kusoma kitabu kile katika chumba kingine. Muda si muda tukaanza kuelezana-elezana tuliyokuwa tukisoma: “Jama, ebu sikia!” “Salaa-la!” Karibu na usiku wa manane nikakimaliza kitabu hicho. Miezi miwili iliyotangulia nilikuwa nimesoma Biblia yote, na sasa nikaanza kufahamu jinsi sehemu zake mbalimbali zilivyohusiana.
Tangu ujana wangu nilisali jinsi Yesu alivyowafundisha wanafunzi wake: “Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.” (Mt. 6:9, 10) Nilikuwa nimedhani kwamba ufalme wa Mungu ni amani ambayo mtu anakuwa nayo akilini na moyoni. Kumbe sivyo! Lo! sasa niliona kwamba ufalme wa Mungu ni serikali halisi! Hicho ndicho chombo ambacho Mungu atatumia kufutilia mbali taratibu potovu hii!
Nilifahamu jambo hilo waziwazi niliporudia Danieli 2:44, inayosema hivi: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele . . . Utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” Hivyo, nikajua kwamba jitihada nilizofanya zamani niibadili taratibu kwa kufanya maandamano zilikuwa za bure tu, tena zilikuwa kinyume cha yanayosemwa na Biblia katika Warumi 13:l-7. Sasa nikaona kwamba Wakristo wa kweli hawajiingizi katika siasa, wanamngojea Mungu mwenyewe aibadili taratibu kwa kuiharibu.
Vilevile nikaanza kufahamu kwamba serikali ya Mungu itakapokwisha haribu taratibu hii ya ulimwengu, Yeye atahakikisha kusudi lake la kwanza la kufanya dunia iwe paradiso limetimizwa, kama unavyoonyesha unabii mbalimbali tuliokuwa tumesoma. Lakini sasa nikajifunza jambo zuri sana nililokuwa sijaliona—kwamba Mungu ataruhusu watu waishi milele katika paradiso hiyo ya dunia! Maandiko kama lifuatalo yalinivuta sana: “Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.”—Zab. 37:29.
Lakini, nikaanza kuona kwamba jawabu la kuleta mambo hayo ni UFALME WA MUNGU. Naam, Mungu anajali, tena ana serikali halisi atakayotumia kutimiza makusudi yake. Katika kitabu Kweli, sura inayosema “Kwa Nini Mungu Ameruhusu Uovu Mpaka Siku Yetu ya Leo?” ndiyo iliyonisaidia kufahamu sababu gani anaonekana kama kwamba amekawia kuchukua hatua. Ikanieleza wazi jinsi masuala ya maana yanayohusu hata makao ya kiroho yalivyopaswa kujibiwa kabla hajaiharibu taratibu potovu hii.
Lakini je! yote hayo yalikuwa mafundisho ya kukisia tu? Je! kulikuwa na uhakikisho uonekanao kwamba serikali ya Mungu iko? Nilitaka kujua mambo hayo.
KITU TULICHOKUWA TUMEKITAFUTA
Kesho yake, Septemba 6, 1970, Jeanne nami tulikwenda kwenye Jumba la Ufalme, tukafika baada ya mkutano kuanza. Watu wote walikuwa wamenyolewa vizuri, tena walikuwa wenye furaha nyingi. Hata watoto wadogo walitoa maelezo, wakasoma kwa ufasaha vifungu vya Biblia. Kwa kuwa nilijua shule hazikufundisha sana watoto, niliona kwamba wazazi wao bila shaka waliwasaidia sana. Nikashangazwa na vile watu hao walivyoijua Biblia. Lakini jambo lililonipendeza zaidi lilitukia mkutano ulipokwisha.
Zaidi ya watu mia moja, tangu mtoto mpaka mzee, walikuja wakatusalimu kwa urafiki tusiopata kuuona. Tulishangaa sana kwa sababu mimi nilikuwa na nywele ndefu na ndevu, naye Jeanne alikuwa amevaa mavazi ya kihipi. Vilevile, karibu kila mtu alikuwa mweusi, maana huo ulikuwa mtaa wa weusi. Katika shule niliyofundisha, weusi hawakushirikiana nami kwa muda mrefu. Walitilia weupe mashaka, lakini sivyo ilivyokuwa katika Jumba la Ufalme.
Tulikaribishwa turudi Alhamisi tuhudhurie Shule ya Kitheokrasi. Tulipofika, watu wote walitutendea kama kwamba tulikuwa rafiki zao kwa muda mrefu. Tulipendezwa sana kwa vile kusudi la mikutano hiyo lilikuwa kupata ufahamu zaidi juu ya Biblia. Tuliona pia kwamba watu hawa walitumia mambo waliyojifunza kubadili maisha zao. Ndipo tulipokaribishwa tukale, naye mume mwenye nyumba akatutia moyo tujifunze Biblia kila juma bila malipo, tukakubali.
Baada ya juma chache Jeanne nami tulijua kwamba tumekipata kitu tulichokuwa tumetafuta. Watu hawa walipendana kikweli, nao walikuwa wakijitayarisha kupata uzima katika taratibu mpya wakiwa na tumaini hakika. Kila upande wa maisha zao uliongozwa na sheria za Mungu katika Biblia, kwa hiyo walikuwa raia halisi za serikali ya Mungu. Tulipoendelea kujifunza, utimizo wa unabii wa Biblia ulitusadikisha kwamba tunaishi karibu na mwisho wa kizazi kitakachoiona serikali ya Mungu ikiiponda taratibu nzima ya mambo iliyo mbovu.—Mt. 24:3-14.
Tuliona kwamba watu wote wanapaswa kusikia upesi habari hizo za maana juu ya ufalme wa Mungu, kwa hiyo tukaomba turuhusiwe kushiriki na Mashahidi kueleza watu habari hizo. Tulikuwa tumeacha kutumia dawa za kulevya, na muda mfupi baadaye tukabadili hali ya sura zetu na mitindo ya mavazi. Januari mwaka 1971, tulibatizwa na Mashahidi wa Yehova kuonyesha tulikuwa tumejiweka wakf tumtumikie Yehova Mungu. Nikaacha kazi yangu ya ualimu, nikatafuta kazi nyingine, kisha Jeanne nami tukaingia katika kazi ya kuhubiri wakati wote. Tumepata thawabu nyingi.
Baada ya kupokea mazoezi ya umisionari katika Watchtower Bible School of Gilead mjini New York, tumekwenda Afrika kuzihubiri habari njema za ufalme wa Mungu. Ni jambo zuri sana kuonyesha watu katika Neno la Mungu, Biblia, kwamba umaskini, vita, chuki zisizo na msingi na udhalimu wa taratibu hii utakwisha karibuni, kisha kuwe na hali zenye haki chini ya utawala wa serikali ya Ufalme wa Mungu!—2 Pet. 3:13.
[Blabu katika ukurasa wa 388]
“Niliposoma habari ya udhalimu . . . machozi yalinitoka.”
[Blabu katika ukurasa wa 389]
“Hata habari zilikuwa zikionyesha wazi kwamba wakuu walikuwa wakitoa taarifa za uongo juu ya vita.”
[Blabu katika ukurasa wa 389]
“Mapolisi na askari walitukatiza, wakaanza kutushambulia kwa hewa ya kutoa machozi na virungu.”
[Blabu katika ukurasa wa 390]
“Vijana wengi waliiona ndoa kuwa jambo la kizamani.”
[Blabu katika ukurasa wa 391]
‘Viongozi wa dini walipinga vita baada ya watu wale wengine kuacha kuiunga mkono.’
[Blabu katika ukurasa wa 391]
“Kadiri tulivyozidi kusoma Biblia, ndivyo makanisa yalivyozidi kulaumiwa na kitabu kile kile walichodai kufuata.”
[Blabu katika ukurasa wa 393]
“Watu hawa walipendana kikweli.”
[Picha katika ukurasa wa 392]
Jeanne nami tukawa tukiangalia majibu ambayo tulikuwa tumetafuta