Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w76 11/1 kur. 491-496
  • Vile Unyenyekevu Unavyoweza Kukulinda

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vile Unyenyekevu Unavyoweza Kukulinda
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • NIA YA MITUME
  • LAZIMA TUJIFUNZE SOMO
  • SOMO LAKAZIWA​—⁠SABABU GANI?
  • Yesu Aliweka Kielelezo Cha Unyenyekevu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • “Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”
    ‘Njoo Uwe Mfuasi Wangu’
  • Sitawisha Unyenyekevu wa Kweli
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Unyenyekevu
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
w76 11/1 kur. 491-496

Vile Unyenyekevu Unavyoweza Kukulinda

“Jifungeni wenyewe unyenyekevu wa akili kuelekea mtu na mwenzake, . . . Iweni timamu akilini, kesheni.”​—1 Pet. 5:5-8, NW.

1. Wanadamu wengi wana maelekeo gani, na yanaweza kuwa na matokeo gani?

JE! UMEONA maelekeo ya wanadamu ya kujiona kuwa wa maana kupita kiasi? Wengi wana maelekeo ya kudai sana mambo, na kutaka wengine wawaangalie sana kwa sababu ya sura yao, usemi wao au mtindo wa maisha. Nia yao ya kutaka makuu, ya kujitumainia kupita kiasi huenda mwishowe ikawaletea aibu mbaya sana, kama vile mithali ya kale ya Biblia isemavyo: “Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna.”​—⁠Mit. 18:12.

2, 3. (a) Yesu aliona nini alipohudhuria karamu? (b) Yesu alifundishaje somo la unyenyekevu wakati huo?

2 Wakati mmoja Yesu Kristo alipokubali ukaribishaji wa Farisayo aende karamuni, aliona kwamba wageni walikuwa na nia hiyo ya moyoni ya kujitukuza. Biblia yasema: ‘Aliona jinsi walivyochagua viti vya mbele.’ (Luka 14:1, 7) Kwa hiyo Yesu alitumia wakati huo kufundisha somo la unyenyekevu. Aliwapa wageni mfano ufuatao:

3 “Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”​—⁠Luka 14:8-11.

4, 5. (a) Unyenyekevu unaweza kukulinda na nini? (b) Yesu alitoa mfano gani kwa watu waliojitumainia kuwa wenye haki?

4 Yesu alionyesha vile unyenyekevu unavyoweza kulinda mtu kwa maneno mepesi na yenye kueleweka sana. (Mit. 16:18) Lakini hauwezi kukusaidia usiaibike mbele ya wanadamu tu, bali pia utakuokoa na hukumu kali ya Mungu, ambaye aelezwa hivi: “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” (Yak. 4:6; Luka 20:45-47) Yesu alionyesha vile Mungu anavyowaona wenye kujikuza, wenye kujiona kuwa wakubwa, wakati mwingine alipokuwa akisema na “watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.” (Luka 18:9) Aliwapa watu hao mfano juu ya Farisayo na mtoza kodi akaeleza:

5 “Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”​—⁠Luka 18:9-14.

6. (a) Yesu aliona nia gani mara kwa mara? (b) Hiyo yatokeza maulizo gani?

6 Tusomapo Biblia, ni ajabu kuona vile Yesu alivyokutana mara nyingi na watu waliodhani walikuwa wakuu kuliko wengine, na vile alivyowaonya mara nyingi juu ya hatari ya nia yao ya kujidhania kuwa bora kuliko wengine. Tena alifanya hivyo akisema na makundi ya watu na mitume wake Yerusalemu siku chache tu kabla ya kuuawa kwake. Alisema: “Msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. . . . Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.” (Mt. 23:1-12) Lakini ni kwa faida ya nani hasa Yesu alitia mkazo tena juu ya uhitaji wa unyenyekevu? Alikuwa akijaribu kusaidia na kulinda nani hasa?

NIA YA MITUME

7. Kwa sababu gani si ajabu kwamba watu wana maelekeo ya kuwa wenye kiburi na wenye kutafuta ukubwa?

7 Ni jambo la maana kuangalia kwamba, kwa sababu ya kutokamilika tulikorithi, wanadamu wana maelekeo ya kuwa wachoyo na kujifikiria zaidi kuliko inavyowapasa. (Zab. 51:5; Rum. 12:3) Tena, ulimwengu hujaribu kukuza ndani yetu maoni ya kwamba jamaa yetu, kabila au taifa letu ni bora kuliko la wengine. Hututia moyo pia tujaribu kujitanguliza, kushinda wengine, bila kujali njia tunazotumia. Kwa hiyo si ajabu kwamba watu wana maelekeo ya kutafuta cheo na fahari. Oh, huenda watu wakakana jambo hilo, “Mimi sitaki ukubwa,” huenda wakasema. Lakini matendo yao yaonyesha nini? Je! Petro kwa mfano, au Yakobo, Yohana, au ye yote wa mitume wengine, walionyesha wazi tamaa ya kuwa na ukubwa? Basi, ni nini lililotukia siku moja wakati walipokuwa wakirudi nyumbani Kapernaumu wakiwa na Yesu?

8, 9. (a) Mitume wa Yesu walianza mabishano gani walipokuwa katika njia ya kwenda Kapernaumu? (b) Wakati huo Yesu alifundishaje mitume wake kwamba walikuwa na nia mbaya?

8 Hivi ndivyo Marko alivyoandika yaliyotukia: “Hata [Yesu] alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa.” Luka pia aliandika tukio hilo, lakini kwa wazi yeye wala Marko hakuwako. (Marko 9:33-37; Luka 9:46-48) Walakini, mtume Mathayo alikuwako, na bila shaka aliaibika maana alishiriki katika mabishano hayo. Ingawa Mathayo hataji mabishano yenyewe, anasimulia vile Yesu alivyowafundisha wakali huo somo la unyenyekevu, akieleza:

9 “Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.” (Mt. 18:2-4) Lo! ni njia nzuri namna gani ya kukazia juu ya wanafunzi wake ubora wa unyenyekevu! Kwa asili watoto wadogo hutegemea wazee wao na kuwaona kuwa wakubwa zaidi yao. Mitume walipaswa kugeuka wawe hivyo. Je! waligeuka? Je! nia yao ilibadilika?

10. Baadaye, Yakobo na Yohana walimwomba Yesu nini, mitume wengine kumi walionaje?

10 Muda mfupi baada ya hapo mitume walifuatana na Yesu Yerusalemu wakaadhimishe juma ya mwisho yenye matukio mengi ya maisha yake. Walipokuwa wakielekea kwenye mji huo, Marko aandika yaliyotukia: “Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.” Pengine ombi hilo lakukumbusha juu ya wageni waliokaribishwa karamuni wakajichagulia viti vilivyo bora. “Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.” Mitume wengine hawakukubali jaribio hili la kichinichini la Yakobo na Yohana la kujitafutia cheo kikubwa zaidi katika serikali ya Kristo.​—⁠Marko 10:35-41.

11. (a) Mitume walikuwa na maoni gani mabaya? (b) Yesu alijaribuje kunyosha kuwaza kwao?

11 Yakobo na Yohana, na vilevile mitume wengine, walikuwa na maoni mabaya ya kilimwengu. Pengine walikumbuka wakati wafalme wa Kiisraeli wa ukoo wa Daudi walipotawala mamia ya miaka huko nyuma. Pengine walidhani kwamba mfalme wa Kimasihi Yesu Kristo pia angekuwa na serikali ya kidunia yenye watu wenye vyeo na madaraja makubwa. Pengine wao walikuwa na tamaa kuu za kutumikia katika vyeo vikubwa hivyo. Kwa vyo vyote, wao hawakuwa wamejifunza somo la unyenyekevu. Kwa hiyo Yesu alijaribu kunyosha kuwaza kwao, akiwaambia: “Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumwa wa wote.”​—⁠Marko 10:42-44; Mt. 20:20-28.

12. Yesu alikuwa akimaanisha nani hasa alipowasihi watu wajinyenyekeze wasiitwe ‘kiongozi’?

12 Kwa sababu ya kuwaza huko kwa mitume wa Yesu, twaweza kuwa na hakika kwamba alikuwa akiwamaanisha wao hasa wakati alipowaambia watu Yerusalemu siku chache baadaye kwamba yawapasa kuwa wanyenyekevu, wasijiinue kama ‘waalimu’ wala “viongozi.” (Mt. 23:8-12) Kwa sababu ya kubishana-bishana kwa mitume, pengine Yesu aliamua kukazia hata zaidi uhitaji wao wa unyenyekevu. Alipata nafasi siku mbili baadaye wakati wale kumi na wawili walipokusanyika katika chumba orofani Yerusalemu waadhimishe sikukuu yao ya mwisho ya Kupitwa wakiwa pamoja.

13. (a) Katika nchi za Mashariki, mkaribishaji alionyeshaje wageni wake ukarimu kama desturi? (b) Kwa hiyo, hiyo iliwapa mitume nafasi gani walipokusanyika waadhimishe sikukuu yao ya mwisho ya Kupitwa wakiwa pamoja?

13 Kwa kuwa mitume hawakuwa wageni, bali waliruhusiwa tu watumie chumba hicho, hakukuwa na watumishi wa kuosha miguu yao. Katika nchi za Mashariki, ambako kwa kawaida watu walivaa ndara (sandals) au walitembea miguu mitupu, lilikuwa tendo la ukarimu mkaribishaji akiagiza miguu ya wageni ioshwe walipoingia nyumbani mwake. Kwa kawaida kazi hiyo alipewa mtumishi wa cheo cha chini zaidi katika nyumba. Hivyo, mwanamke kijana Abigaili alionyesha unyenyekevu wa kweli wakati alipowaambia hivi watumishi wa Daudi: “Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu.” (1 Sam. 25:41; Luka 7:44; 1 Tim. 5:10) Kwa hiyo, mitume walikuwa na nafasi nzuri ya kutoa kwa unyenyekevu utumishi huo uliohitajiwa, lakini yaelekea roho ya mashindano ilikuwa yenye nguvu sana mioyoni mwao hata mmoja wao hakujitolea. Kwa hiyo, wakaendelea kula chakula, kinyume cha desturi, wakiwa hawajaosha miguu.

14, 15. (a) Ni utumishi gani wa maana ambao Yesu alifanyia mitume wake? (b) Kwa kufanya hivyo Yesu alikuwa akikazia somo gani, lakini ni nini linaloonyesha kama wakati huo mitume walisikia?

14 Mtume Yohana aliandika lililotukia halafu: Yesu “aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. . . . Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.”​—⁠Yohana 13:1-14.

15 Lo! ilikuwa njia nzuri namna gani ya kufundisha mitume wake unyenyekevu! Ungedhani sasa walisikia. Alikuwa akiwafundisha nia ya akili​—⁠ya unyenyekevu, nia ambayo ingewafanya wajitolee kufanya kazi zile ndogo kabisa kwa ajili ya wengine. Lakini ikawaje? Jioni ilipozidi kusonga, Luka aeleza: “Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa.” (Luka 22:24) Wazia hilo! Baada ya Yesu kujitahidi sana hivyo awafundishe unyenyekevu, bado hawakuondoa akilini wazo la daraja, na la kuwa na vyeo vikubwa zaidi kuliko wengine. Malezi yao yote, yakiongozwa na Mafarisayo na Masadukayo wenye kiburi, kwa wazi yalikuwa yamewafanya wawe na nia iliyopotoka sana hata hawakuweza kufahamu kwamba wote walikuwa ndugu, wenye kulingana cheo.

16. (a) Bila shaka ni maelezo gani ya Yesu yaliyotokeza mabishano? (b) Yesu aliendeleaje kusaidia mitume wake kwa saburi?

16 Bila shaka mitajo ya Yesu juu ya ufalme wa Mungu usiku huo ndiyo ilifanya mabishano haya yatokee juu ya aliyeelekea kuwa mkubwa zaidi ya wote. (Luka 22:16-18) Ni ushuhuda wa ajabu sana wa saburi na ustahimilivu ambao Yesu alikuwa nao maana hakukasirikia mitume wake na kuwakaripia vikali kwa sababu ya tamaa yao ya kichoyo ya cheo kikubwa zaidi, na ya kuwa na vyeo vya umashuhuri pamoja naye katika utukufu wake wa Ufalme. Badala yake, aliwaambia tena kwa saburi, bila shaka sauti yake ikiwa ya kusihi: “Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.”​—⁠Luka 22:25-27.

LAZIMA TUJIFUNZE SOMO

17, 18. (a) Kwa sababu gani ilikuwa lazima mitume wajifunze unyenyekevu? (b) Nia ya kujitumainia kupita kiasi ya mitume usiku huo ilitokeza nini?

17 Ilikuwa lazima wajifunze somo hilo la unyenyekevu. Maisha zao zenyewe zilikuwa hatarini, vilevile maisha za kundi la Kikristo. Namna gani? Basi, angalia nia yao ilitokeza nini usiku huo. Yesu aliwaonya hivi: “Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu.” Lakini mitume wakapinga kwamba isingekuwa hivyo. Walijiona walikuwa tayari kwa tukio lo lote, kwa hiyo kila mmoja akasema: ‘Hata ikiwa tutakufa, hatutakukana kamwe.’ Na katika jibu kali la Petro, twaona wazi mashindano yaliyokuwa kati yao: “Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.”​—⁠Mt. 26:31-35.

18 Basi, twakumbuka ilikuwaje. Mitume wote walimwacha Bwana wao kwa njia ya kusikitisha sana. Wao walikuwa hawategi sikio, walikuwa hawasikilizi maagizo yake ya kurudia-rudia. Na mwishowe walikimbia wakiogopa, wakamwacha Yesu aelekeane na kundi la watu wenye ghasia lililokuja kumkamata. Naye Petro alikana mara tatu kwamba hata hamjui Bwana wake! Kwa kweli Petro alikuwa amesema: ‘Wengine wote huenda wakawa na udhaifu mbalimbali katika imani yao, lakini mimi​—⁠mimi sitakuacha kamwe, Bwana.’ Lakini kujitumainia kwake kupita kiasi, nia yake ya kujiona yeye ni mwaminifu kuliko wao ilimletea Petro msiba mkubwa sana. Ni lazima sana tujifunze unyenyekevu! Mitume walijifunza mwishowe?

19, 20. (a) Kuna ushuhuda gani kwamba mitume walijifunza unyenyekevu? (b) Kwa wazi, kundi la kwanza la Kikristo lilisimamiwaje, na hii yaonyesha nini juu ya nia ya mitume?

19 Ndiyo. Saburi ya upendo ya Yesu ilithawabishwa sana. Ushuhuda wa hilo ni namna walivyoandika kwa unyofu mafundisho ya Yesu juu ya unyenyekevu. Tunaweza kuwazia walivyoona vibaya walipokumbuka vile walivyokuwa wametenda. Hata hivyo, walitaka wengine wafaidike kutokana na makosa yao na hasa mafundisho mema aliyowapa Yesu. Ushuhuda zaidi kuonyesha walijifunza sana somo hilo ni mashauri waliyotoa wenyewe wakitia wengine moyo wawe na unyenyekevu. Kwa mfano, mtume Petro aliandika baadaye hivi: “Mwe na nia moja . . . wanyenyekevu.”​—1 Pet. 3:8.

20 Ushuhuda mwingine bado kwamba mwishowe walijifunza unyenyekevu wapatikana katika kitabu cha Biblia cha Matendo. Kwa kukisoma twaweza kuona vile mitume walivyofanya kazi pamoja na kwa umoja walijenge kundi la Kikristo. Hakuna ye yote kati yao aliyejitakia makuu wala fahari, wala ye yote hakutenda kama kwamba ndiye mkuu kati yao, akijaribu kufanya maneno yake yawe sheria. Badala ya kuwa hivyo, kwa wazi baraza ya wanaume, kutia hata na wazee wengine wasio mitume, waliamua mambo ya maana yenye kuhusu kundi la Kikristo. Mwanafunzi Yakobo, ndugu mzazi mmoja na Yesu, ambaye hakuwa mtume, aelekea kuwa ndiye alisimamia uamuzi ulipofanywa kuhusu kutahiriwa. (Matendo 15:6-29; 12:1, 2) Hiyo yadokeza kwamba pengine wazee-wasimamizi walipokezana zamu, mmoja akitenda kama mwenyekiti pindi fulani na mwingine wakati mwingine. Roho ya unyenyekevu wa kweli ilisitawi kati ya mitume.

SOMO LAKAZIWA​—⁠SABABU GANI?

21. Mtume Petro alikaziaje ubora wa unyenyekevu?

21 Miaka mingi baadaye, mtume Petro aliona uhitaji wa kukazia ubora wa unyenyekevu, akafanya hivyo katika ya kwanza ya barua zake zilizoongozwa na Mungu zilizomo katika orodha ya vitabu vya kweli vya Biblia. Katika sura ya nne ataja mateso ambayo Wakristo wanaweza kutazamia kwa sababu ya kuwa waaminifu kwa Mungu, kisha asema: “Kwa hiyo, mimi nawatia moyo wanaume wazee miongoni mwenu hivi . . . Lichungeni kundi la Mungu lililo katika uangalizi wenu, si kwa kulazimishwa, bali kwa moyo wa kupenda . . . wala si kupiga ubwana juu ya wale ambao ni urithi wa Mungu, bali kuwa mifano kwa kundi. . . . Lakini ninyi nyote jifungeni wenyewe unyenyekevu wa akili kuelekea mtu na mwenzake, kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu fadhili zisizostahilika. Jinyenyekezeni, basi . . . Iweni timamu akilini, kesheni. Adui yenu, Ibilisi, hutembea-tembea kama simba anayenguruma, akitafuta kumeza mtu.”​—1 Pet. 5:1-8, NW.

22. Kwa sababu gani Petro alitumia maneno “kwa hiyo” akianza kutia wazee moyo, baada ya kutaja mateso ya Wakristo?

22 Kwa sababu gani Petro alisema, “Kwa hiyo, mimi nawatia moyo wanaume wazee miongoni mwenu hivi,” baada ya kutaja mateso ya Wakristo? Ni kwa sababu wazee wakikosa kuwa na unyenyekevu, nia hiyo itaongeza mateso na mizigo inayotatiza ndugu za Kikristo. Lakini nia ya unyenyekevu ya wazee inaburudisha, inafanya iwe vyepesi zaidi ndugu waonyeshe uvumilivu. (Isa. 32:1, 2) Kwa hiyo Petro anaonya wazee kwa upole ‘wasipige ubwana juu ya wale ambao ni urithi wa Mungu, bali wawe mifano kwa kundi.’

23. (a) Ni maelezo gani ya Yesu huenda yakawa yalimwongoza Petro kushauri wazee wasipige ubwana juu ya kundi? (b) Yawapasa wazee wajifunge sifa gani, na kwa matokeo gani?

23 Kwa wazi Petro alikumbuka maelezo ya Yesu juu ya watawala wa kilimwengu ambao “huwatumikisha,” na ambao “huwatawala,” na akakumbuka kwamba alisema: “Lakini haitakuwa hivyo kwenu.” (Marko 10:42-44; Luka 22:25-27) Wazee wa Kikristo hawapaswi kuwa kama Mafarisayo wenye kiburi walioagiza wengine mambo ya kufanya, lakini wao wenyewe hawakutaka kuinua kidole kimoja wayafanye mambo hayo. (Mt. 23:3, 4) Bali, yawapasa waweke mfano; wao wenyewe wapaswa kuwa na nia ya kufanya jambo lo lote wanaloagiza wengine wafanye. Pamoja na Wakristo wengine wote, yawapasa ‘wajifunge wenyewe unyenyekevu wa akili.’ Kulingana na maana ya neno la Kigiriki enkombóomai, lililotafsiriwa katika 1 Petro 5:5 “jifungeni wenyewe,” yawapasa ‘wajifungilie wenyewe kama kwa mafundo’ unyenyekevu huu. Wakifanya hivyo, hawatajiona kamwe kuwa wakubwa kutostahili kufanya kazi za chini chini, kama kusafisha Jumba la Ufalme, au kushiriki katika sehemu zote za utendaji wa kuhubiri wa kundi la Kikristo.

24. Ni kwa njia gani huenda wazee wakapiga ubwana juu ya kundi?

24 Tena, wale wanaojifunga wenyewe unyenyekevu hawatajichukulia starehe za pekee wala mapendeleo ya pekee, kama kwamba wanastahili mambo bora zaidi kuliko wengine. Kwa mfano, katika makusanyiko ya Kikristo, je! wazee wasingekuwa wakipiga ubwana juu ya ndugu zao wakijitafutia vyakula bora na migawo bora ya kazi, huku wakiwapa ndugu zao kazi zile za chini chini? Au je! wangekuwa wakiweka mfano kwa kundi wakijipeleka mbele ya mstari wa cafeteria na kupakuliwa vyakula vyao kabla ya wale ambao wamekuwa wakingojea kwa muda mrefu zaidi? Ni kweli, huenda nyakati nyingine wakawa na migawo ya kazi za haraka, na huenda hapo ikawa lazima wajipeleke mbele ya mstari wa cafeteria au wale wakati tofauti au mahali tofauti na wengine. Hata hivyo hayo ni mambo ya kufikiria kwa uzito. Kwa sababu gani?

25. (a) Je! wale wenye uwezo wa pekee au mapendeleo ya pekee ya utumishi ni wakuu zaidi? (b) Kwa hiyo ni lazima Wakristo watii shauri gani?

25 Kwanza, wakati mtu anapopokea mamlaka, hasa wakati huo huenda akawa na maelekeo ya kudhani yeye ni bora, ni mtu mwenye kustahili zaidi kuliko wengine. Lakini ndivyo? Huenda akawa ana uwezo mbalimbali unaomstahilisha kuwa mzee wa Kikristo na kusimamia kazi fulani ya kusanyiko, lakini uwezo huo haumfanyi mkuu kuliko wengine. (1 Tim. 3:1-7) Yehova Mungu hamhesabu mzee huyo, wala mwanadamu mwingine ye yote mwenye uwezo wa pekee, kuwa mkuu zaidi kuliko ndugu zake. Kwa hiyo, ni lazima kama nini mtu huyo awe akitii shauri la Mungu kuonyesha “unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake”! (Flp. 2:3) Hali hiyo ya akili itamlinda Mkristo na msiba mkuu unaoweza kutokana na kiburi.​—⁠Mit. 16:18; 18:12.

26. Ukosefu wa unyenyekevu kwa upande wa wazee unawezaje kuhatirisha kundi?

26 Vilevile, nia hiyo ya unyenyekevu ya mzee wa Kikristo italinda kundi. “Kondoo” wanaweza kukwazika vyepesi na kuondoka katika kundi la Kikristo wazee wakijichukulia mapendeleo ya pekee, wakitafuta fahari au umashuhuri, au wakionyesha kwa njia nyingine roho ya majivuno, ya kiburi. Neno la Mungu lasihi: “Katika kuonyeshana heshima wekeni mfano.” (Rum. 12:10, NW) Lakini kundi likiona wazee, wanaopaswa kuwa mifano, wakijiheshimu na mambo bora na kupiga ubwana kupita kiasi, kwa majivuno, kundi litakuwaje? Litaumia. Mateso wanayovumilia kwa sababu ya kuwa Wakristo yataongezeka, na hiyo yaweza kuleta msiba.

27. Wazee wanawezaje kuwa timamu akilini na kumzuia Ibilisi asiwameze wao na kundi?

27 Ni ajabu basi kwamba mtume Petro alionya hivi: “Iweni timamu akilini, kesheni. Adui yenu, Ibilisi, hutembea-tembea kama simba anayenguruma, akitafuta kumeza mtu”? Mzee wa Kikristo akisitawisha roho ya majivuno, ya kiburi, huenda akafungulia Ibilisi njia ya kummeza, na vilevile ya kumeza washiriki wa kundi. Kwa hiyo wazee, jaribuni kuepuka hata kuonekana kama kwamba mnajikuza au kujiona kuwa wakuu zaidi. Jifungeni wenyewe unyenyekevu. Iweni wenye kuambilika, wafadhili, wanana na wenye huruma, kama wakati mama mwenye kunyonyesha anapotunza watoto wake mwenyewe. (Efe. 4:32; 1 The. 2:7, 8) Sikuzote utegemeeni mfano na mafundisho ya Yesu Kristo, mfanye yote mwezavyo mmwige yeye.​—⁠Flp. 2:5-8.

28. Kuna tumaini gani zuri la wakati ujao, nasi twapata wapi mfano mdogo wake?

28 Ebu wazia itakuwa vizuri namna gani watu wote walio hai watakapoonyesha unyenyekevu wa akili na kuhesabu wengine kuwa bora kuliko wao. Lo! kutakuwa na burudisho na amani namna gani! Hata sasa, ndani ya kundi la Kikristo, tunapokea mfano mdogo wa baraka hii ya kushirikiana na wanaume, wanawake na watoto wanyenyekevu wasiojifikiria wenyewe tu. Je! hatutiwi moyo basi tujifunge wenyewe unyenyekevu? Unaweza kutulinda tusimezwe na Ibilisi, na kutusaidia tuiokoke ‘dhiki kubwa’ tuishi milele katika taratibu mpya ya Mungu yenye haki inayokaribia sana.​—⁠Zab. 133:1-3; Ufu. 7:9-14​—⁠Kutoka The Watchtower, June 15, 1976.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki