Maswali Kutoka kwa Wasomaji
● Je! maiti za Wakristo zapaswa kuhifadhiwa zisioze kwa sababu maiti ya Yakobo ilihifadhiwa?
Hakuna ushuhuda wa kuonyesha kwamba kuhifadhiwa kwa maiti ya Yakobo kulipaswa kuwa kielelezo cha kufuatwa na waabudu wa kweli. Bali, inaelekea kwamba ilihifadhiwa kwa sababu ya kusadiki kwamba Mungu angetimiza ahadi ya kuupa uzao wa Ibrahimu nchi.
Yakobo alipofia Misri mwanawe Yusufu aliagiza madaktari wa Misri wahifadhi maiti yake. (Mwa. 50:2, 3) Wamisri wa kale walikuwa na desturi ya kuhifadhi maiti kwa kutia dawa. Ni wazi kwamba walifanya hivyo kwa sababu waliamini ilikuwa lazima maiti ihifadhiwe ili nafsi ya mtu iweze kuungana nayo tena mwishowe. Bila shaka, Yakobo wala Yusufu hakukubali fundisho la kipagani la kutokufa kwa nafsi. Wote wawili walikuwa na ufahamu sahihi kwamba wafu walio katika mpango wa Mungu huenda Sheol, kaburi la kawaida la wanadamu, naye Mungu atawafufua humo katika wakati wake. (Mwa. 37:35; 42:38; Ebr. 11:21, 39, 40) Basi, kwa sababu gani Yusufu aliagiza maiti ya Yakobo ihifadhiwe?
Yehova Mungu alikuwa ameagana na Ibrahimu kuwapa wazao wake nchi ya Kanaani, Nchi ya Ahadi. (Mwa. 15:16-21) Hata kabla uzao huo haujairithi nchi hiyo, Ibrahimu na Isaka walikuwa wamekwisha zikwa humo katika pango la jamaa. Lakini Yakobo alipokaribia kufa, yeye na jamaa yake walikuwa wakiishi Misri. Je! alikuwa ameacha kuiamini ahadi ya Mungu, akakata shauri kwamba Waebrania wangekaa Misri daima? Sivyo hata kidogo. Alimwagiza Yusufu aahidi kumzika pamoja na baba zake Kanaani. Hivyo Yakobo alionyesha alisadiki kwamba Mungu angewapa wazao wa Ibrahimu nchi hiyo.—Mwa. 49:29-33.
Ili kutimiza alivyoombwa na Yakobo, ilikuwa lazima Yusufu apeleke maiti yake nchi ya Kanaani. Lakini maiti hiyo ingalioza kabla safari yake ndefu ya wakati wa joto haijaisha, kama isingalihifadhiwa. Lakini, kwa kutumia njia za ufundi za kuhifadhi maiti zilizotumiwa Misri, Yusufu angeweza kuhifadhi maiti ya baba yake Yakobo mpaka azikwe katika nchi ambayo wazao wake wangerithi.—Mwa. 50:2, 3, 7-14.
Karibu miaka 55 baadaye Yusufu mwenyewe aliagiza mifupa yake pia isafirishwe wakati ambao Mungu angeondoa Waisraeli Misri mwishowe. Hivyo Yusufu alionyesha kwamba hata yeye alisadiki Mungu angetimiza ahadi Yake ya kuupa uzao wa Ibrahimu nchi. Kwa hiyo, maiti ya Yusufu pia ilihifadhiwa Misri, halafu wakati wa kutoka mabaki yake yakatolewa katika nchi hiyo.—Mwa. 50:25, 26; Yos. 24:32; Ebr. 11:22.
Ingawa katika vizazi vilivyofuata Waebrania waliliona kuwa jambo la maana kuzika watu, hakuna ushuhuda wa kuonyesha kwamba walihifadhi maiti za watu wao waliokufa. (1 Fal. 2:31; 2 Fal. 13:21; Zab. 79:1-3; Yer. 16:4) Badala ya kutumia njia za Wamisri za kuhifadhi maiti kwa kuitia katika dawa muda wa juma nyingi,a Waebrania walizika watu wao mara baada ya kufa, hata siku ile ile.—Kum. 21:23; Mwa. 50:2, 3.
Ndivyo Yesu alivyofanyiwa. Alizikwa siku aliyokufa. Maiti yake ilifanyiwa nini kabla ya kuzikwa? Twasoma hivi: “Wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.” (Yohana 19:40) Na ingawa wanafunzi fulani walienda kaburini kwake baada ya sabato ili kupaka sehemu za nje za maiti yake manukato zaidi, ni wazi kwamba hawakujaribu kuhifadhi maiti yake kwa kuitia muda mrefu katika dawa kama ilivyofanywa Misri. Inaweza kuonekana katika habari ya Lazaro kwamba Yesu hakuzikwa kwa kuhifadhiwa maiti yake. Ingawa inaelekea kwamba maiti ya Lazaro ilishughulikiwa kwa njia ya kawaida, jamaa yao ilitazamia kwamba siku ya nne baada ya kufa kwake maiti yake ingekuwa imekwisha oza na kunuka.—Yohana 11:39.
Inaelekea kwamba kwa kawaida Wakristo wa kwanza walifuata desturi za Kiyahudi za kuzika. Walizika wafu upesi bila kutumia njia za kuhifadhi maiti zenye gharama nyingi. (Matendo 5:5-10; 9:37) Kwa hiyo hakuna linaloonyesha kwamba wazao wa Yakobo au Wakristo wa kwanza walitegemea kuhifadhiwa kwa maiti ya Yakobo au ya Yusufu kama kielelezo walichopaswa kufuata.
Leo katika sehemu nyingi za dunia wafu hawahifadhiwi. Lakini huenda nyakati nyingine maiti ikatakiwa ihifadhiwe, kwa mfano ikiwa haitazikwa kwa muda wa siku fulani, au ikiwa itapelekwa mbali. Kwa kawaida katika United States wafanya kazi katika nyumba za maiti hutia maiti dawa hata kama itazikwa moja kwa moja au itachomwa. Lakini, ikiwa sheria haitaki jambo hilo lifanywe, jamaa ya marehemu yaweza kuagiza maiti isitiwe dawa ili kuepuka gharama za bure au kwa sababu nyinginezo za kibinafsi.
Kwa hiyo, hakuna sababu ya kudhani kwamba Yakobo na Yusufu walipohifadhiwa Wakristo waliwekewa kielelezo ambacho lazima wafuate. Lakini inastahili iangaliwe kwamba Mungu hakuonyesha katika Neno lake kwamba alichukizwa walipohifadhiwa. Kwa hiyo Wakristo hawana sababu ya kudhani ni kinyume cha Maandiko kuhifadhi maiti hali zikitokea zinazohitaji ihifadhiwe.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa muda wa juma nyingi Wamisri walikuwa wakitumia dawa za pekee na kuloweka maiti katika natron (magadi) ili isioze kwa muda wa miaka mingi, hata karne nyingi.