Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 4/15 kur. 171-172
  • Kujiweza—Kunalinda Mtu na Msiba

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kujiweza—Kunalinda Mtu na Msiba
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Habari Zinazolingana
  • Kujidhibiti —Kwa Nini Ni Kwa Maana Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Kusitawisha Tunda La Kujidhibiti
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Iweni Wenye Kujidhibiti Ili Mshinde Tuzo!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Jazeni Kwenye Ujuzi Wenu Kujidhibiti
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 4/15 kur. 171-172

Kujiweza​—Kunalinda Mtu na Msiba

MWANAMUME na mwanamke walikuwa pamoja. Mwanamume alikuwa akifanya kazi siku chache akimtengenezea mwanamke nyumba yake. Wote wawili walikuwa washiriki wa kundi la Kikristo. Mwanamke alihuzunishwa na ndoa yake. Alianza kumweleza mwanamume huyo huzuni na matatizo yake. Mwanamume alimhurumia, kisha alipokuwa akiendelea kujaribu kumshauri na kumfariji mwanamke huyo, alizungusha mkono wake mabegani pake. Urafiki ukaongezeka, na muda si muda wakajikuta wakifanya uzinzi.

Watu hao wawili hawakuwa wamepanga kutenda dhambi hiyo. Mpaka wakati huo wote wawili walikuwa wameishi maisha ya adili na walikuwa wakitembea kulingana na njia iwapasayo Wakristo. Je! walifanya hivyo kwa sababu ya kutolipenda Neno la Mungu au kutokuwa na kanuni bora za adili? Sivyo hasa. Walishindwa KUJIWEZA.

Kujiweza ni mojawapo la matunda ya roho ya Mungu. Kujiweza kwa Mkristo hakurithiwi bali kunaongozwa na kumjua Mungu na Neno lake. Ndiyo sababu mtume Petro anaonya kwa upole kwamba, ‘Ongezeeni maarifa yenu kujiweza.’​—2 Pet. 1:5, 6. NW.

Yale matunda tisa ya roho yanapopangwa, upendo ndio unaokuwa wa kwanza, kabla ya kujiweza. (Gal. 5:22, 23, NW) Bila shaka, kama Mkristo angalikuwa na upendo nyakati zote, angalikuwa na kujiweza nyakati zote. Lakini kwa sababu watu wote, hata Wakristo, wana makosa, kujiweza ni sehemu ya utu wa Kikristo inayohitajiwa kufikiriwa nyakati zote.

Kukosa kujiweza kunaweza kuongoza mtu kwenye msiba. Huenda mtu akawa ana furaha, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani na upole. Huenda akawa amezoea sifa hizo wakati wote. Lakini, akiacha kujiweza, huenda akapoteza sifa nyingine zote hizi pia kwa muda. Wakati huo huenda akajiharibia sana maisha yake mwenyewe na ya wengine.

Kwa hiyo Wakristo wanaagizwa wajiweze. Ama sivyo wanaweza kuingia mtegoni. Dhambi inatenda kazi katika mwili wa kila mtu, hivi kwamba ‘lile alipendalo, halitendi; bali lile alichukialo ndilo analolitenda.’ (Rum. 7:15) Kwa sababu ya hali hiyo yenye kuhuzunisha, mtume Paulo alisema: “Nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”​—1 Kor. 9:27.

Ndiyo sababu Yesu alitia ndani ya sala aliyofundisha wanafunzi wake ombi hili: “Usitutie majaribuni.” (Mt. 6:13) Mungu hajaribu mtu ye yote ili afanye mabaya. Yeye ajua kwamba Mkristo akifanya jambo baya, ni mara chache sana anapolifanya bila kujua ubaya wa jambo lenyewe. Kwa kawaida mtu anajua analofanya linamchukiza Mungu. Anaposhawishwa atende dhambi, ataelekea kufikiri, Mungu ataonaje? Litakuwa na matokeo gani juu ya uhusiano wangu na Mungu? na kundi la Kikristo? Litahusuje jamaa yangu? Tendo langu litaleta suto juu ya jina la Mungu na la Kristo? juu yangu mwenyewe kama Mkristo? juu ya kundi? Ama atatii mawazo hayo yake yenye kumwonya au atayapuza na kuingia katika dhambi bila kujali.

Kwa hiyo, wakati Mkristo anaposali, “Usitutie majaribuni,” anamwomba Mungu amkumbuke wakati wa majaribu na amkumbushe maonyo makali ya Biblia​—⁠kumzuia asifanye mambo mabaya. Yeye huwa akimwomba Mungu amrudishie fahamu zake na kumzuia asifanye ubaya akianza kudhoofika. Mungu hatamzuia kwa nguvu na hivyo amharibie uhuru wake wa hiari, lakini Yehova anapoimarisha akili ya mtu huyo na mawazo yanayofaa yanayotokana na hekima ya kimungu, ‘hufanya na mlango wa kutokea, ili aweze kustahimili.’​—1 Kor. 10:13.

Mkristo akishindwa kumtegemea Mungu akiwa na ombi hilo moyoni mwake, kanuni hii itatumika kwake: “Kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi.” Mtu huyo atashawishwa kufikia kiasi ambacho atakosa kujali na kuingia moja kwa moja katika dhambi ‘kama vile ng’ombe aendavyo machinjoni.’ (Mit. 7:22) Hivyo hasa ndivyo Ibilisi atakavyo. (1 Pet. 5:8) Lakini Mungu atatetea Mkristo anayesali anapokuwa katika mkazo, na kumpa uwezo wa kujiweza.

Wakati mmoja Mungu alimwokoa Daudi na msiba mkuu kwa kumrudishia kujiweza. Mungu alimtumia mwanadamu, mwanamke, kumwomba Daudi aache mwendo wake wa haraka haraka. Mwanamke huyo alikuwa Abigaili. Daudi na watu wake, waliochukuliwa na Mfalme Sauli mwovu kuwa maharamia, walikuwa wamelinda wachungaji na mifugo ya mume wa Abigaili, Nabali tajiri. Wakati Daudi alipopeleka wajumbe wakaombe chakula, Nabali aliwatukana kwa kelele nyingi. Kwa sababu ya uovu na upumbavu wa Nabali, Daudi alikasirika sana akaanza kwenda akaimalize jamaa ya Nabali, lakini Abigaili akamlaki akamwomba amwachie Yehova jambo hilo badala ya kujilipiza.

Daudi aliona msiba ambamo hasira yake ilikaribia kumwingiza, akajibu: “Na ahimidiwe [Yehova], Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki; na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu.”​—1 Sam. 25:2-35.

Fikiria msiba ambao Daudi angalijiletea kama Mungu asingalimsaidia arudiwe na kujiweza alipokuwa akifanya haraka akaue watu wa jamaa ya Nabali! Na katika nyakati hizi zenye upotovu kujiweza ni kwa lazima pia kwa Mkristo. Kwa kawaida vijana wanaojaribu kuishi kulingana na kanuni za Kikristo huwa wakishirikiana na wale wenye mazoea mabaya kila siku. Watu hao wasiojiweza wanakaza sana vijana Wakristo kuwashawishi watumie dawa za kulevya au wafanye uasherati, wawe waasi, waharibu mali za watu ovyo tu au wafanye jeuri. Naam, vijana au wazee Wakristo wakiacha kujiweza wanaweza kufanya jambo litakaloharibu maisha yao na kuumiza sana wengine. Kwa dakika moja wanaweza kuharibu sifa yao ya Kikristo na kutia kovu katika dhamiri zao.

Kama vile katika habari ya matunda mengine ya roho, lazima kujiweza kusitawishwe kwa kujifunza Neno la Mungu na kuishi kupatana na amri zake. Kujiweza kunaendeleza kiasi na kuongeza sifa nyingine za Kikristo. Kwa kutumia “tamaa ya mwili na tamaa ya macho na kujionyesha kwa mtu mali yake,” ulimwengu huu unavuta “utu wa kale unaofanana na namna ya mwenendo [wetu] wa zamani na unaoharibika kulingana na tamaa [za utu wa kale] za udanganyifu.” (1 Yohana 2:16; Efe. 4:22, NW) Kwa hiyo Wakristo wa kweli wanajua ubora mkuu wa kusitawisha sifa yenye kulinda sana​—kujiweza.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki