Kujidhibiti —Kwa Nini Ni Kwa Maana Sana?
“Mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi [kujidhibiti, NW].”—2 PETRO 1:5, 6.
1. Ni onyesho lipi la ajabu la kujidhibiti kimwili lililotukia katika karne ya 19?
BILA shaka yoyote, mojawapo la maonyesho yenye kushangaza sana ya kujidhibiti (kujiweza) kimwili lilitolewa na Charles Blondin katika nusu ya mwisho ya karne ya 19. Kulingana na ripoti moja, yeye alivuka Maporomoko ya Maji ya Niagara mara kadhaa, kwanza katika 1859, kwenye kamba iliyonyoshwa kwa kukazwa urefu wa meta 340 na meta 50 juu ya maji. Baada ya hiyo, alifanya hivyo kila wakati akionyesha uwezo wake tofauti: akiwa amefungwa kitambaa machoni, akiwa katika gunia, akisukuma wilibaro (kigari-kisukumwa), akiwa kwenye milonjo, na akiwa amebeba mwanamume mgongoni pake. Katika hali nyingine, alipinduka juujuu hewani akiwa kwenye milonjo kwenye kamba iliyonyoshwa meta 52 juu ya ardhi. Kudumisha usawaziko wa jinsi hiyo kulitaka kujidhibiti kwingi kwa kimwili. Kwa jitihada zake, Blondin alipewa thawabu ya umashuhuri na utajiri pia.
2. Kuna namna zipi nyingine za utendaji zinazohitaji kujidhibiti kimwili?
2 Ingawa ni wachache waweza hata kukaribia kujaribu kuiga maonyesho hayo, umaana wa kujidhibiti kimwili katika kufanya kazi za ustadi au katika michezo uko wazi kwa sisi sote. Kwa mfano, mwanamuziki mmoja akieleza ustadi wa Vladimir Horowitz mpiga piano mashuhuri aliyekufa, alisema hivi: “Jambo lililonisisimua zaidi lilikuwa ile hisia ya kuwa na udhibiti kamili . . . hisia ya kutumia nishati isiyosadikika.” Ripoti nyingine kuhusu Horowitz ilisema juu ya “miongo minane ya kurusha-rusha vidole kwa kasi sana vikiwa katika udhibiti kamili.”
3. (a) Namna ya udhibiti unaohitaji mengi sana ni gani, nayo inafasiliwaje? (b) Ni nini maana ya neno la Kigiriki linalofasiriwa “kujidhibiti” katika Biblia?
3 Jitihada nyingi inatakiwa ili kusitawisha stadi za jinsi hiyo. Hata hivyo, la maana na lenye kuhitaji mwito wa ushindani hata zaidi ni kujidhibiti. Kumefasiliwa kuwa “kujizuia kunakoonyeshwa juu ya misisimuko ya ghafula, hisia za moyoni, au tamaa za mtu mwenyewe.” Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno linalotafsiriwa “kujidhibiti” kwenye 2 Petro 1:6 na kwingineko, limefasiliwa kuwa “wema wa mtu ambaye ana udhibiti juu ya tamaa na uchu wake mbalimbali, hasa hamu zake za nyege.” Kujidhibiti kwa mtu mmoja mmoja hata kumeitwa “kipeo cha kufaulu kwa kibinadamu.”
Sababu Kujidhibiti Ni kwa Maana Sana
4. Ukosefu wa kujidhibiti umechuma uzao upi mbaya?
4 Ukosefu wa Kujidhibiti umechuma mavuno yaliyoje! Matatizo mengi ulimwenguni leo yamesababishwa hasa na ukosefu wa kujidhibiti. Kwa kweli, tunaishi katika “siku za mwisho,” wakati ambapo ‘nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo zipo hapa.’ Mara nyingi watu ni ‘wasiojidhibiti’ kwa sababu ya pupa, namna moja ya hiyo ikiwa ni “wapenda raha kuliko kuwa wapenda Mungu.” (2 Timotheo 3:1-5, NW) Ukweli huo wenye kuleta fikira nzito umekaziwa kwetu kwa kuondolewa katika ushirika wa kundi la Kikristo kwa watu 40,000 wenye kukosa katika mwaka wa utumishi uliopita, sana sana kwa sababu ya mwenendo mbaya sana. Kwa hao ni lazima tuongeze wale wengi waliopewa karipio, hasa kwa sababu ya ukosefu wa maadili katika ngono lakini wote kwa sababu ya kukosa kuzoea kujidhibiti. Lenye kuleta fikira nzito pia ni uhakika wa kwamba wengine waliokuwa wazee kwa muda mrefu walipoteza mapendeleo yao yote wakiwa waangalizi kwa sababu hiyo hiyo.
5. Umaana wa kujidhibiti waweza kutolewa mfano wa nini?
5 Umaana wa kujidhibiti waweza kutolewa mfano wa gari. Lina magurudumu manne yanayoliwezesha lisonge, injini yenye nguvu iwezayo kuyazungusha magurudumu hayo kasi, na breki ziwezazo kuyasimamisha. Hata hivyo, msiba waweza kutokea ikiwa hakuna dereva wa kuamua mahali magurudumu hayo yaendapo, mwendo yanavyozunguka, na wakati yasimamapo, kwa kudhibiti usukani, kiongeza-mwendo, na breki.
6. (a) Ni kanuni gani ya kupima upendo inayoweza kutumiwa kwa kufaa kuhusu kujidhibiti? (b) Ni lazima tukumbuke shauri lipi zaidi?
6 Ingekuwa vigumu kukazia kupita kiasi umaana wa kujidhibiti. Lile alilosema mtume Paulo kwenye 1 Wakorintho 13:1-3 kuhusu umaana wa upendo laweza kusemwa pia kuhusu kujidhibiti. Haidhuru ni jinsi gani sisi huenda tukawa wasemaji bora wa hotuba za watu wote, haidhuru ni kiasi gani cha maarifa na imani huenda tukapata kupitia mazoea mazuri ya kujifunza, haidhuru ni kazi zipi huenda ikawa tunafanya ili kuwafaidi wengine, tusipozoea kujidhibiti, yote hayo ni ya bure. Twapaswa kukumbuka maneno haya ya Paulo: “Je! hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia [hujidhibiti, NW] katika yote.” (1 Wakorintho 9:24, 25) Linalotusaidia kuzoea kujidhibiti katika yote ni onyo la Paulo katika 1 Wakorintho 10:12: “Anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”
Mifano ya Kuonya
7. (a) Ukosefu wa kujidhibiti uliongozaje jamii ya kibinadamu katika mwendo wa kudhoofika? (b) Maandiko yanatupa mifano gani mingine ya mapema ya ukosefu wa kujidhibiti?
7 Kwa kuruhusu vitendo vyake viongozwe na hisia za moyoni badala ya kuongozwa na usababu wa kiakili, Adamu alishindwa kuzoea kujidhibiti. Tokeo likawa kwamba, “dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti.” (Warumi 5:12) Uuaji wa kwanza ulikuwa pia kwa sababu ya kutojidhibiti, kwa kuwa Yehova Mungu alikuwa amemwonya Kaini hivi: ‘Kwa nini una ghadhabu na kwa nini uso wako ukakunjamana? Dhambi inakuotea mlangoni, na je! utaishinda?’ Kwa sababu Kaini hakuishinda dhambi, alimwua ndugu yake Habili. (Mwanzo 4:6-12) Mke wa Loti alishindwa pia kuzoea kujidhibiti. Yeye hakuweza kukinza kile kishawishi cha kuangalia nyuma. Ukosefu wake wa kujidhibiti ulimgharimu nini? Uhai wake mwenyewe!—Mwanzo 19:17, 26.
8. Mambo yaliyoonwa na wanaume gani wa kale watatu huandaa maonyo kwetu kuhusu uhitaji wa kujidhibiti?
8 Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, alipoteza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa sababu ya kutojidhibiti. Alikitia kitanda cha baba yake unajisi kwa kufanya ngono na mmoja wa masuria wa Yakobo. (Mwanzo 35:22; 49:3, 4; 1 Mambo ya Nyakati 5:1) Kwa sababu Musa alipoteza udhibiti wa hasira yake kwa vile Waisraeli walivyomjaribu kwa kunung’unika, kulalamika, na kuasi, alinyimwa lile pendeleo lenye kutamaniwa sana la kuingia Bara Lililoahidiwa. (Hesabu 20:1-13; Kumbukumbu la Torati 32:50-52) Hata Mfalme mwaminifu Daudi, ‘mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu,’ alipatwa na matatizo makubwa kwa sababu ya ukosefu wake wa kujidhibiti wakati mmoja. (1 Samweli 13:14; 2 Samweli 12:7-14) Mifano yote ya jinsi hiyo hutuandalia maonyo yanayofaa ambayo tunahitaji ili kuzoea kujidhibiti.
Lile Tupaswalo Kudhibiti
9. Ni baadhi gani ya maandiko yanayokazia umaana wa kujidhibiti?
9 Kwanza, kujidhibiti kunatia ndani mawazo na hisia-moyo zetu. Hizo hurejezewa mara nyingi katika Maandiko kuwa utumizi wa ufananisho wa maneno kama vile “moyo” na “figo.” Lile ambalo tunaruhusu akili zetu zifikirie sana ama linatusaidia ama linatuzuia katika jitihada yetu kumpendeza Yehova. Kujidhibiti kunahitajiwa ikiwa tutatii shauri la Kimaandiko lipatikanalo kwenye Wafilipi 4:8, kuendelea kufikiria mambo yaliyo ya kweli, safi, na yenye sifa njema. Mtunga zaburi Daudi alionyesha maoni kama hayo katika sala, akisema hivi: “Na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee BWANA [Yehova, NW], Mwamba wangu, na mwokozi wangu.” (Zaburi 19:14) Amri ya kumi—kutotamani chochote kilicho cha mwanadamu mwenzako—ilitaka mtu adhibiti mawazo yake. (Kutoka 20:17) Yesu alikazia uzito wa kudhibiti mawazo na hisia zetu za moyoni aliposema hivi: “Kila mtu atazamaye [anayeendelea kutazama, NW] mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”—Mathayo 5:28.
10. Ni maandiko gani ya Biblia yanayokazia umaana wa kudhibiti usemi wetu?
10 Kujidhibiti kunatia ndani pia maneno yetu, usemi wetu. Maandiko yanayotushauri tudhibiti ndimi zetu ni mengi kweli kweli. Kwa mfano: “Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, kwa hiyo maneno yako na yawe machache.” (Mhubiri 5:2) “Katika wi-ngi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.” (Mithali 10:19) “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji . . . Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” Na Paulo aendelea kututolea shauri tuondolee mbali na sisi maongezi ya kipumbavu na mzaha wa maneno machafu.—Waefeso 4:29, 31; 5:3, 4.
11. Yakobo anashugulikaje na tatizo la kudhibiti ulimi?
11 Yakobo, ndugu-nusu wa Yesu, alaani vikali usemi usiotiwa lijamu na kuonyesha jinsi ilivyo vigumu kudhibiti ulimi. Asema hivi: “Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo [kuendelea kutukia hivyo, NW].”—Yakobo 3:5-10.
12, 13. Ni baadhi gani ya maandiko yanayoonyesha umaana wa kudhibiti vitendo na mwenendo wetu?
12 Bila shaka, kujidhibiti kunatia ndani vitendo vyetu. Hali moja ambayo katika hiyo kujidhibiti kwingi kunahitajiwa inahusu uhusiano wetu pamoja na watu wa jinsia tofauti. Wakristo wanaamuriwa hivi: “Kimbieni ukosefu wa maadili katika ngono.” (1 Wakorintho 6:18, New International Version) Waume wanahimizwa waweke mipaka ya upendezi wao wa ngono uwe kwa wake zao wenyewe, wakiambiwa kwa sehemu: “Unywe maji ya birika lako mwenyewe, na maji yenye kububujika katika kisima chako.” (Mithali 5:15-20) Tunaambiwa wazi kwamba “waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” (Waebrania 13:4) Kujidhibiti kunahitajiwa hasa na wale ambao wangesitawisha zawadi ya useja.—Mathayo 19:11, 12; 1 Wakorintho 7:37.
13 Yesu alitoa muhtasari wa habari hiyo yote kuhusu vitendo vyetu kuelekea wanadamu wenzetu alipotoa ile inayoitwa kwa ujumla “Kanuni ya Kidhahabu,” akisema hivi: “Yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.” (Mathayo 7:12) Kwa kweli, kujidhibiti kunatakiwa ili tusiache mielekeo yetu ya ubinafsi au mikazo ya nje au vishawishi vitusababishe tutendee wengine tofauti na njia ambayo tungependa watutendee.
14. Ni shauri gani ambalo neno la Mungu linatoa kuhusu chakula na kinywaji?
14 Kisha kuna habari ile ya kujidhibiti kuhusu chakula na kinywaji. Neno la Mungu lashauri kwa hekima hivi: “Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; miongoni mwao walao nyama kwa pupa.” (Mithali 23:20) Kuhusu siku yetu hasa, Yesu alionya hivi: “Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo.” (Luka 21:34, 35) Naam, kujidhibiti kunatia ndani mawazo yetu na hisia zetu, na pia maneno yetu na vitendo vyetu.
Sababu Kujidhibiti Ni Mwito wa Ushindani Sana
15. Maandiko yanaonyeshaje uhalisi wa upinzani wa Shetani kuelekea kuzoea kujidhibiti kwa Wakristo?
15 Kujidhibiti si rahisi kwa sababu, kama Wakristo wote wajuavyo, tuna kani tatu zenye nguvu zilizopangwa dhidi ya kuzoea kwetu kujidhibiti. Kwanza, kuna Shetani na roho waovu wake. Maandiko yanaonyesha bila shaka yoyote kwamba wao ni halisi. Hivyo, twasoma kwamba “Shetani alimwingia” Yuda kabla tu ya yeye kwenda nje kumsaliti Yesu. (Yohana 13:27) Mtume Petro alimwuliza Anania hivi: ‘Kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kuambia uongo roho takatifu?” (Matendo 5:3) Kwa kufaa sana, Petro alionya pia hivi: “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”—1 Petro 5:8.
16. Ni kwa nini ni lazima Wakristo waonyeshe kujidhibiti kwa mambo ya ulimwengu huu?
16 Katika jitihada zao za kuzoea kujidhibiti, ni lazima Wakristo washindane pia na ulimwengu huu ulio “katika uwezo wa yule mwovu,” Shetani Ibilisi. Kuhusu hilo, mtume Yohana aliandika hivi: “Msiipende dunia [ulimwengu, NW], wala mambo yaliyomo katika dunia [ulimwengu, NW]. Mtu akiipenda dunia [ulimwengu, NW], kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani [ulimwenguni, NW], yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia [ulimwengu, NW]. Na dunia [ulimwengu, NW] inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” Tusipojidhibiti na kukinza kwa uthabiti mwelekeo wowote wa kuupenda ulimwengu, tutashindwa na uvutano wao, kama alivyofanya Dema aliyekuwa mfanya kazi mwenzi wa Paulo wakati mmoja.—1 Yohana 2:15-17, UV; 5:19, NW; 2 Timotheo 4:10, UV.
17. Tunazaliwa na tatizo lipi linalohusu kujidhibiti?
17 Tukiwa Wakristo, tunahitaji kujidhibiti pia ikiwa tutashindana kwa mafanikio na udhaifu na upungufu wetu wenyewe wa kimnofu tuliourithi. Hatuwezi kuepuka ule uhakika wa kwamba “mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake.” (Mwanzo 8:21) Kama Mfalme Daudi, ‘tuliumbwa katika hali ya uovu; mama zetu walituchukua mimba hatiani.’ (Zaburi 51:5) Mtoto aliyetoka tu kuzaliwa hajui lolote kuhusu kujidhibiti. Anapotaka kitu fulani, anaendelea kulia tu mpaka anapokipata. Ripoti moja juu ya kuzoeza mtoto yataarifu hivi: ‘Watoto husababu katika njia tofauti kabisa na njia ambayo watu wazima husababu. Watoto hufikiria yao wenyewe tu na mara nyingi hawaitikii sihi yenye kusadikisha na yenye kupatana na akili sana kwa sababu hawawezi “kujitia katika hali za wengine.”’ Kwa kweli, “ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto.” Hata hivyo, Kwa kutumia “fimbo ya adhabu,” yeye hujifunza pole kwa pole kwamba kuna kanuni ambazo ni lazima atii na kwamba ni lazima ubinafsi uzuiwe.—Mithali 22:15.
18. (a) Kulingana na Yesu, ni mielekeo gani inayokaa katika moyo wa ufananisho? (b) Ni maneno gani ya Paulo yanayoonyesha kufahamu kwake tatizo la kuzoea kujidhibiti?
18 Naam, mielekeo yetu ya ubinafsi tuliyozaliwa nayo hutokeza mwito wa ushindani kwetu tunapohitaji kuzoea kujidhibiti. Mielekeo hiyo hukaa katika moyo wa ufananisho, ambao Yesu alisema hivi juu yao: “Moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano.” (Mathayo 15:19) Ndiyo sababu Paulo aliandika hivi: “Lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.” (Warumi 7:19, 20) Hata hivyo, hiyo haikuwa hali yenye kukosa tumaini, kwani Paulo aandika hivi pia: “Nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” Kuutesa mwili wake kulitaka kuzoea kujidhibiti.—1 Wakorintho 9:27.
19. Kwa nini Paulo angeweza kusema kwa kufaa kwamba aliutesa mwili wake?
19 Paulo angeweza kusema kwa kufaa kwamba alikuwa ameutesa mwili wake, kwa sababu kuzoea kujidhibiti kunatatanishwa na mambo mengi ya kimwili, kama vile msongo wa damu, mishipa dhaifu ya fahamu (neva) iliyo rahisi kuamshwa hasira, ukosefu wa usingizi, maumivu ya kichwa, chakula kutosagwa tumboni, na kadhalika. Katika makala inayofuata, tutazungumzia sifa na misaada itakayotusaidia kuzoea kujidhibiti.
Je! Unakumbuka?
◻ Kwa nini kujidhibiti ni kwa maana?
◻ Ni baadhi gani ya mifano ya wale waliopatwa na hasara kwa sababu ya ukosefu wa kujidhibiti?
◻ Ni lazima sisi tuzoee kujidhibiti katika sehemu zipi?
◻ Ni maadui gani watatu wanaofanya iwe vigumu kwetu kuzoea kujidhibiti?
[Picha of Charles Blondin katika ukurasa wa 8]
[Hisani]
Historical Pictures Service
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wakristo wanahitaji kuzoea kujidhibiti kuhusu chakula na kinywaji
[Picha katika ukurasa wa 11]
Kujidhibiti kutatusaidia tuepuke porojo zenye kudhuru