Urafiki wa Kweli Una Nguvu
IBADA ya kweli ina matokeo mazuri juu ya nia ya mtu. Inamchochea kwa ndani ahurumie watu wengine. Mara nyingi humfanya awe mwenye urafiki anaposema na kushughulika na watu asiowajua. Nyakati nyingine urafiki huo umekuwa na matokeo mazuri juu ya wenye kupinga vikali ujumbe wa Biblia.
Hivyo ndivyo ilivyotukia katika kisiwa cha kusini ya Ugiriki. Mwanamume mmoja alikuwa akijifunza Biblia na mmoja wa Mashahidi wa Yehova, lakini mkewe alimpinga vikali sana. Mwadhimisho wa Chakula cha Bwana cha Jioni ulikuwa ukikaribia naye mwanamume huyo akaamua kuhudhuria. Mkewe alipoona mumewe akijitayarisha kwenda, akamwuliza anakwenda wapi. Mumewe akamwambia, “Sikiliza, leo Mashahidi wa Yehova wanaadhimisha mwadhimisho wa maana zaidi sana ulioanzishwa na Yesu, yaani, Ukumbusho wa kifo chake. Mimi nitahudhuria. Nitafurahi sana hata wewe ukihudhuria.” Mkewe akakasirika sana akaanza kulaani Mashahidi na kumtukana mumewe.
Mwishowe mwanamume huyo akaanza kwenda peke yake. Alipokuwa akiondoka, mkewe akapaza sauti kwa ghafula: “Ngoja! Hata mimi ninakuja.” Mwanamume huyo alishangazwa na aliyosikia. Machozi yakamtoka. Wote wawili wakahudhuria mkutano huo na mkewe akasikiliza kwa unyamavu. Mwishoni mwa hotuba, Shahidi mwanamke akasema na mke huyo kwa urafiki mwingi na kupanga kumtembelea nyumbani kwake. Funzo la Biblia likaanzwa.
Mwezi ule ule wa kwanza mwanamke huyo akamwambia Shahidi hivi: “Sasa mimi pia ni shahidi wa Yehova, dada yako. Sijamwambia bado mume wangu. Sasa nitakueleza jambo nililotaka kufanya. Siku ambayo mume wangu alinieleza habari za Ukumbusho, nilikuwa nimeficha kisu chini ya mto wangu na nilikuwa nikitazamia nafasi ya kumwua. Nilipokuwa nimekaza nia nifanye hivyo, yeye alinikaribisha twende mkutanoni. Mwishowe nikaamua kwenda, halafu tukifika niite polisi waje kukamata kila mtu. Wewe ndiwe umefanya niijue kweli. Nayo kweli ndiyo imefanya mume wangu awe hai mpaka sasa nami nikawa huru bila kuwa gerezani.”
Lo! urafiki wa Shahidi huyo ulikuwa na nguvu namna gani!