Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 5/1 kur. 18-19
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Habari Zinazolingana
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Ni Nini Kinachofanya Maisha Yawe Yenye Kusudi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Ni Urithi Gani Unaopaswa Kuwaachia Watoto Wako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Kitabu Cha Biblia Namba 21—Mhubiri
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 5/1 kur. 18-19

Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?

Unaweza Kutimiza Nini Ukilinganishwa na Mfalme?

Mfalme Sulemani alifanya uchunguzi wa uangalifu wa mambo ya wanadamu. Alikuwa na wakati, mali na ufahamu wa kumsaidia afanye uchunguzi wake kwa ukamilifu. Ndiyo sababu mtu anaweza kufaidika sana akijifunza matokeo ya uchunguzi wa Sulemani kama vile yalivyoandikwa katika kitabu cha Mhubiri.

Akionyesha namna ilivyo kazi bure kwa wengine kujaribu kufanya uchunguzi kama huo, mwenye hekima aliandika hivi: “Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa.” (Mhu. 2:12) Ndiyo, mtu wa kawaida tu akiwa na mali chache zaidi na nafasi chache zaidi kuliko zile za mfalme anaweza kufanya nini? Akijaribu kufanya yale aliyofanya Sulemani angefanya machache tu ya yale yale yaliyofanywa na watu wengine. Hakuna jambo jipya ambalo angejifunza juu a yale yanayofanya maisha yawe yenye kuridhisha kweli kweli.

Hivyo, basi, Sulemani alithibitisha jambo gani? Anaendelea kusema hivi: “Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza.” (Mhu. 2:13) Bila shaka mfu mwenye hekima ni bora kuliko mtu asiye nayo. Hekima inasaidia mtu ashindane na magumu ya maisha na kumwezesha kutumia nguvu na uwezo wake katika njia bora zaidi kuliko vile angefanya ikiwa angekuwa na ufahamu mdogo tu. Mengi zaidi yaweza kutimizwa nuruni kuliko yanayoweza kutimizwa gizani.

“Macho yake mwenye hekima,” akaandika Sulemani, “yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani;” (Mhu. 2:14) Mwenye hekima hufungua macho yake. Yamo “kichwani” mwake katika maana ya kwamba yanatumikia uwezo wa akili zake. Kwa hiyo yeye hutimiza jambo wala hapotezi wakati akifanya majaribio ya bure ya kufikia mradi fulani. Walakini, mpumbavu yuko gizani; amefunga macho yake nayo hayamsaidii hata kidogo kuona mwendo unaofaa kuchukuliwa.

Hata hivyo, ubora wa hekima kinyume cha upumbavu haumaanishi kwamba hekima ya kibinadamu inaweza kuleta furaha ya kweli pamoja na uradhi wenye kudumu. Hivyo ndivyo Sulemani anavyokubali katika maneno yanayofuata: “Ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja liwapatalo wote sawasawa. Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili. Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu”? (Mhu. 2:​14-16) Kwa habari ya mauti, hakuna faida ya kuwa na hekima ya ulimwengu. Kazi zote za mtu pamoja na utendaji wake zinafanywa kuwa bure. Mwishowe mfu aliyekufa, bila kujali namna alivyokuwa na hekima, anasahauliwa na walio hai.

Lakini je! si jambo lenye faida mtu kuachia watoto wake urithi kwa sababu ya kutumia mali zake kwa hekima? Hilo pia ni jambo ambalo hakuna mtu anayeweza kuwa na hakika nalo. Sulemani anasema hivi: “Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo. Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata. Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili. Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni [msiba mkuu].”​—⁠Mhu. 2:​17-21.

Kwa kweli hakuna njia yo yote ya kujulia yatakayoupata urithi ambao huenda mtu akaacha nyuma. Wale wanaoupokea urithi huo, huenda wasiuthamini kwa sababu hawakuufanyia kazi na kwa hiyo wanautapanya upesi baada ya hapo. Hivyo, basi, kazi yote ngumu iliyofanywa kujipatia mali hizo ingekuwa na faida gani? Iliyo mbaya hata zaidi ni hali ya mtu ambaye alifanya kazi ngumu akajitaabisha na kupatwa na magumu hata hakupata usingizi mzuri kwa sababu ya wasiwasi mwingi na masumbufu. Sulemani anaandika hivi: “Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua? Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili.”​—⁠Mhu. 2:​22, 23.

Kwa sababu ya hali hii, wewe unaweza kufanya nini? Sulemani anajibu hivi: “Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake. Hayo nayo naliona ya kwamba hutoka mkononi mwa Mungu. Kwa maana ni nani awezaye kula au kujiburudisha kuliko mimi?” (Mhu. 2:​24, 25) Mtu anapaswa kufurahia matunda ya kazi yake wakati wa maisha yake. Bila shaka ni jambo la kawaida kwa wazazi vilevile kufikiria watoto wao. Mtume Mkristo Paulo aliandika: “Haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto.” (2 Kor. 12:14) Hata hivyo, hii haina maana kwamba wazazi wangeweka mali akiba kwa ajili ya watoto wao hata wajinyime mambo ya lazima ya maisha au kufanya maisha yao kuwa yenye shida. Wazazi wanapaswa kukumbuka kwamba, hata watoto wao wawe wenye hekima au wema namna gani, bado mali zaweza kupotezwa, kuibwa, kutumiwa vibaya au kuharibiwa. Kwa hiyo inafaa zaidi mtu afurahie mambo mema katika njia inayofaa wakati mtu anapoweza kufanya hivyo, mahali pa kupita kiasi katika kulundika mali kwa ajili ya watoto bila kupata faida yo yote ya kweli kutokana na mali hiyo wakati wa maisha yake mwenyewe.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki