Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 11/1 kur. 501-502
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mali Bila Furaha
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Ni Nini Kinachofanya Maisha Yawe Yenye Kusudi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 11/1 kur. 501-502

Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?

Mali Bila Furaha

Wakati Mfalme Sulemani mwenye hekima alipokuwa akichunguza mambo ya kibinadamu, aliziona hali zinazozuia watu kabisa wasifurahie mali zao.

Aliandika yafuatayo juu ya hali moja: “Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito; mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu cho chote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani; walakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya.”​—Mhu. 6:1, 2.

Mwenyezi anaruhusu kila mtu atumie uwezo aliompa ajipatie mali na heshima au utukufu kati ya wenzake. Katika maana hiyo Sulemani angeweza kusema kwamba Mungu ‘anampa’ mtu mali na utukufu. Lakini, linalosikitisha ni kwamba, huenda mtu akawa na mali nyingi sana lakini hali zikamzuia asizifurahie.

Huenda akawa na chakula chenye ladha nzuri lakini asikifurahie kwa sababu matumbo yake si mazuri. Mfano mzuri ni kisa cha Nebukadreza. Alipata cheo cha kuwa mtawala wa ulimwengu katika Babeli. Halafu Yehova Mungu alimshusha kwa sababu ya kiburi chake, akamtia wazimu. Nebukadreza hakupendezwa tena na anasa alizokuwa nazo katika jumba lake la kifalme, hata chakula kizuri na divai bora haikumpendeza. Alijidhania kuwa mnyama-mwitu, akaliacha jumba lake lenye anasa na kuishi kwa kutafuna majani kama ng’ombe. ‘Wageni’ ndio waliofaidika kutokana na mali za Nebukadreza alipokuwa haishi katika anasa za jumba lake la kifalme. Kweli Nebukadreza alipatwa na “ugonjwa mbaya” muda wa miaka saba.​—Dan. 4:28-37.

Halafu, Sulemani alionyesha kwamba kuwa na maisha marefu na jamaa kubwa siyo mambo ya pekee yanayompa mtu maisha yenye kumtosheleza. Anaendelea kusema hivi: “Mtu akizaa watoto mia, akaishi miaka mingi, nazo siku za maisha yake ni nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko [kwa sababu labda anataka kwenda kaburini, kama Ayubu alipokuwa matesoni (Ayubu 3:11-22) ], mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo; yaani, hiyo [mimba iliyochukuliwa kisha mtoto akazaliwa kabla ya wakati wake] huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza; tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule, naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! wote hawaendi mahali pamoja?”​—Mhu. 6:3-6.

Kuna faida gani ya kuwa na maisha marefu na watoto wengi ikiwa mtu hawezi kufurahia maisha hata kidogo? Watu wote wanakwenda mahali pamoja wanapokufa, hata wakiwa matajiri au maskini, vijana au wazee, napo mahali hapo ndipo kaburini. Mtu asiyefurahia maisha akiendelea kuishi muda mrefu kuliko anayekufa akiwa kijana, anapatwa na matatizo zaidi tu. Kitoto kinachozaliwa kabla ya wakati wake, kinachozaliwa kikiwa kimekufa, kiko afadhali kuliko mtu huyo kwa sababu hakitalazimika kuvumilia magumu yote yanayotokana na maisha yasiyo ya maana, yenye mvurugo mwingi.

Sulemani anaendelea kuandika hivi: “Kazi yote ya binadamu ni kwa kinywa chake, walakini hata hivyo nafsi yake hashibi. Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele yao walio hai? Heri kuona kwa macho, kuliko kutangatanga kwa tamaa. Hayo nayo ni ubatili, na kujilisha upepo.”​—Mhu. 6:7-9.

Watu wanafanya kazi kwa bidii ili kujipatia mahitaji ya maisha; wanafanyia kazi “kinywa” chao. Lakini mara nyingi hawatosheki. Mtu mwenye hekima asiyetosheka aweza kujaribu kunyamazisha tamaa zinazomsumbua, lakini mpumbavu anaziachilia zimtawale, hazizuii. Inaonekana hilo ndilo jambo lililomfanya Sulemani aulize hivi: “Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele yao walio hai?” Kwa sababu mwenye hekima na mpumbavu pia wana tamaa zinazowasumbua, mwenye hekima hapati faida kuliko mpumbavu. Vivyo hivyo, huenda maskini akawa anajua kuficha tamaa zinazomsumbua anapokuwa mbele ya wengine, lakini hata hivyo haziondoi. Zinaendelea kumsumbua. Hata yeye si bora kuliko mpumbavu. Basi jambo la hekima ni kutosheka, kufurahia vitu ulivyo navyo, unavyoweza kuona kwa macho yako, badala ya kutamani kitu kingine, kuacha tamaa hiyo ikumalizie amani.

Jambo jingine linaloweza kufanya mtu asitosheke ni kutojua kwamba mambo mengi hayawezi kubadilishwa. Sulemani alisema: “Na awe kitu cho chote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe.” (Mhu. 6:10) Huenda mtu akapata mali nyingi na cheo. Lakini hapati jina tofauti na lile alilopewa mtu wa kwanza, yaani mwanadamu wa duniani, ‘a·dhamʹ, ambalo ni jina la Kiebrania lililotolewa katika asili inayomaanisha “-ekundu.” Naam, bado anaendelea kuwa mtu wa duniani, mtu mwenye kufa. Kwa hiyo hawezi kupiga bei ili kuishi milele. Mtunga zaburi alitaja wazo hilo akasema: “Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake, (maana fidia ya nafsi zao ina gharama, wala hana budi kuiacha hata milele;) ili aishi sikuzote asilione kaburi.”​—Zab. 49:7-9.

Tena, maisha ni yenye mashaka mengi sana katika taratibu hii. Wakati na hali zinawapata wote, halafu mashaka yanazidi kuongezeka. Ndiyo sababu Sulemani aliuliza maulizo haya: “Kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini? Kwa maana ni nani ajuaye yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua?”​—Mhu. 6:11, 12.

Kwa sababu kifo kinamaliza jitihada zote za mtu, anapokea faida gani kutokana na mali au cheo anachopata? Ni nani awezaye kutaja mradi wa kilimwengu unaostahili kufuatwa hasa​—mali, cheo au mamlaka? Mara nyingi watu wanadhani kwamba kitu kinapendeza, halafu wakiisha kipokea wanakata tamaa, hata wanaona uchungu mwingi. Wanaudhika zaidi kwa sababu maisha ni mafupi sana, ‘yanapita kama kivuli.’ Hakuna njia ya kupata tena wakati wa kufuata upya mradi mwingine. Tena, kwa kuwa hakuna njia ya kujua litakalotukia baada ya mtu kufa, hata kutafutia watoto na wajukuu mali kwa kuachilia mambo ya kiroho hakumletei mtu furaha.

Maneno ya mwenye hekima yanaonyesha sana kwamba inampasa mtu atosheke, afurahie maisha! Badala ya kuongeza tamaa za mali, mtu mwenye hekima kweli kweli atakaza fikira juu ya kuendelea kuwa na uhusiano mwema na Mungu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki