Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 10/1 kur. 439-440
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ubatili wa Kutafuta Sana Mali
  • Je, Mali Zaweza Kukufanya Uwe Mwenye Furaha?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • ‘Tukiwa Hatuna Kitu Lakini Tukiwa na Vitu Vyote’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Sababu “Kupenda Fedha” Kunaangamiza Watu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Mwenye Hekima Alikuwa na Maana Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 10/1 kur. 439-440

Mwenye Hekima Alikuwa na Maana gani?

Ubatili wa Kutafuta Sana Mali

Mfalme Sulemani mwenye hekima aliona kwamba kukusanya sana mali hakufanyi mtu atosheke. Aliandika hivi: “Apendaye fedha hatashiba fedha, wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili. Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka; na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?”​—Mhu. 5:10, 11.

Mwenye vingi hatosheki bali anataka zaidi. Mali zake zikiongezeka, anahitaji kuandika vibarua na watumishi zaidi watunze vitu vyote, tena anawalipa. Lakini tajiri hawezi kufaidika na utajiri wake wote kwa sababu ni mwingi. Kwa mfano, aweza kuvaa vazi moja moja tu na kula na kunywa chakula na kinywaji cha kiasi tu. Kwa hiyo, thawabu anayopata mwishowe ni kutazama utajiri aliokusanya na kujivuna kwamba ni mali yake. Ikiwa ni mwenye pupa, huenda akachukia kuandika watumishi na vibarua, maana hataki kuwalipa kutokana na mali zake.

Tena, huenda tajiri akawa na wasiwasi mwingi juu ya mali zake. Mtu asiye na mali nyingi sana hana wasiwasi, lakini huenda tajiri akakosa kulala usingizi mzuri akiona wasiwasi juu ya mali zake. Sulemani alisema: “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.”​—Mhu. 5:12.

Kwa sababu ya mashaka ya maisha, huenda mwenye kuzidi kukusanya mali akajikuta ameingia katika umaskini wakati asipojiweza. Sulemani alitaja hilo alipoandika hivi: “Kuna balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima; na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake.”​—Mhu. 5:13, 14.

Ebu fikiria msiba mkubwa unaoelezwa hapa. Mtu anafanya kazi kwa bidii na kupata utajiri. Lakini, badala ya kufurahia kazi yake, analundika mali zake tu. Afanyapo hivyo anajiumiza, maana hafurahii mambo ya kawaida ambayo angeweza kufurahia. Tena, anakuwa na wasiwasi wa kutunza mali zake na kuziongeza. Halafu mkasa unapotokea, kama kuharibikiwa na biashara, anapoteza mali zote. Kwa hiyo, ingawa alikuwa na utajiri, hakuufurahia, naye anapopata mwana wa kumrithi mwishowe, mwana hakuti urithi wo wote.

Ndipo Sulemani anapoonyesha jambo jingine linalobatilisha ukusanyaji wa mali. Tunasoma hivi: “Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake. Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo?” (Mhu. 5:15, 16) Naam, wakati wa kufa mtu atakuwa amefanya kazi ya bure akijikusanyia pesa. Mwenye kulundika mali anapoanza kufa, hawi na furaha inayotokana na kugawia wenzake.

Bahili anapata hasara nyingi sana kwa sababu ya pupa nyingi ya pesa. Sulemani anaendelea kusema hivi: “Siku zake zote hula gizani, mwenye fadhaa nyingi, mwenye ugonjwa na uchungu.” (Mhu. 5:17) Mtu wa namna hiyo hana furaha. Ni mtu wa huzuni siku zote. Anapokula anakuwa na kinyongo kwa sababu chakula anachokula kinamlazimisha atumie kiasi fulani cha utajiri wake. Anakuwa mgonjwa fikira, na huenda afya yake ikaharibika kwa sababu hiyo. Anapokuwa mgonjwa, anakuwa na wasiwasi kwa sababu analazimika kupumzika asiweze kufanya kazi zake. Anaona wasiwasi juu ya kitu cho chote kinachoweza kumzuia asipate utajiri zaidi.

Kwa kweli, maisha hayo ya kutafuta mali tu ni ya bure. Ndiyo sababu Sulemani anapendekeza tufurahishwe na kazi zetu, akisema: “Tazama, mimi niliyoyaona kuwa ndiyo mema na ya kufaa, ni mtu kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua, siku zote za maisha yake alizopewa na Mungu; maana hilo ndilo fungu lake.”​—Mhu. 5:18.

Sulemani anaeleza matokeo mema ya jambo hilo na kusema: “Tena, kwa habari za kila mwanadamu, ambaye Mungu amempa mali na ukwasi, akamwezesha kula katika hizo, na kuipokea sehemu yake, na kuifurahia amali yake; hiyo ndiyo karama ya Mungu. Kwa kuwa mtu hatazikumbuka mno siku za maisha yake; kwa sababu Mungu humtakabali katika furaha ya moyo wake.”​—Mhu. 5:19, 20.

Mtu anayejua kwamba ufanisi alio nao ni zawadi kutoka kwa Mungu hatalundika mali, bali atazitumia kufurahisha wenzake. Mtu wa namna hiyo ana maoni ya kiasi juu ya mali zake, kwa sababu anakubali kuongozwa na hekima ya kimungu. Kwa hiyo, anajifurahisha na mali zake. Yehova Mungu amemwezesha kufurahia vyakula na vinywaji kwa maana anampa hekima ya kutumia vizuri mali. Vilevile mtu huyo hawi na wasiwasi bure akiogopa ufupi wa maisha na mashaka yake. Yeye anapata furaha nyingi kwa kutimiza mambo yenye faida maishani, hivi kwamba hafikirii mambo yenye kumvunja moyo. Moyo wake ni wenye furaha.

Hakika njia ya hekima ni kujitahidi kufurahia maisha. Kufanya hivyo kunazuia mtu asikate tamaa kama watu wanaojishughulisha wakitafuta mali tu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki