Wewe Wauthaminije Uhai Wako?
MWENDESHAJI motokaa katika Brooklyn, New York, aanza kurudisha motokaa yake nyuma aipange katika nafasi tupu ya kuegeshea motokaa. Motokaa nyingine inatokea nyuma, na kwa haraka inaingia katika ile nafasi. Kwa hasira mwendeshaji motokaa wa kwanza anaendea motokaa ile nyingine amkemee mwendeshaji. Kwa ghafula mwendeshaji wa pili anamchoma kwa kisu.
Katika duka jirani la vyakula watu wawili wanaanza kuteta. Wanatoka nje barabarani, na mmoja anampiga yule mwingine na kumwua.
Twaweza kusoma matukio kama hayo karibu kila siku. Watu wengi katika wakati huu wenye shida ni wakali sana, kwamba hasira ikitokea ama neno baya, yaweza kuanzisha vita yenye kuua mtu. Kwa kiasi kikubwa, jeuri na maasi zinafanya watu wengi sana wafe. Uhai kwa kweli unaendelea kuwa kitu ovyo katika macho ya watu wengi zaidi.
Je! wewe wauonaje uhai? Unauthamini? Kama ndivyo, ziko hatua unazoweza kuchukua sasa kuulinda uhai wako. Liko jambo lo lote litakaloleta ulinzi, ama, angaa uwezekano mkubwa zaidi wa usalama?
Ndiyo, liko. Lakini unahitaji bidii ili kujua la kufanya, na uangalifu wa kawaida katika kulifanya. Kutuliza hali yako ya moyo ni mojawapo ya sifa za maana sana unazopaswa kujitahidi kupata. “Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga,” inasema mithali ya kweli. Kutuliza ulimi nyakati unazokasirishwa kunaweza kuokoa uhai wako na wa wale wengine, kama mithali nyingine ielezavyo: “Upole wa ulimi ni mti wa uzima.” (Tafsiri ya New World [Kiingereza]) Kujiweza kunaweza kuzuia masikitiko makubwa, na wakati mwingine kunawezesha mtu aishi badala ya kufa. “Jawabu la upole hugeuza hasira, bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.” (Mit. 14:17; 15:1, 4; 16:32) Lakini si rahisi kuupata uwezo wa kutuliza roho.
Unawezaje kudumisha kujiweza ili uweze kuwa na utulivu nyakati za hatari? Kwa kuonyesha kujiweza kwa usemi wako wakati unapokuwa na jamaa yako, wakati uko kazini, ama wakati mambo hayakuwa vile wewe ungetaka. Kwa hakika, huwezi ukajiepusha kabisa na kukasirika. Bali ukifuata shauri: “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka,” utapata kujiweza zaidi, pamoja na furaha, katika maisha ya jamaa na katika uhusiano wako na wengine.—Efe. 4:26.
Walakini, bila kujali afanyavyo, mtu anayeishi katika ulimwengu wenye choyo hawezi kulinda uhai wake katika mambo yote. Lakini yuko Mmoja ambaye huthamini sana uhai kuliko tuuthaminivyo, kwa vile anajua uzima unavyoweza kufurahisha chini ya hali nzuri. Huyo ni Muumba wa wanadamu. Yeye huahidi kuondoa mauti na maombolezo katika dunia hii. (Ufu. 21:3, 4) Na sasa, anatoa hekima ifaayo kwa wale wanaotaka uzima na amani. Ukiwa na hekima hii unaweza kupata mwenendo ulio salama zaidi sasa, pamoja na “ahadi ya uzima wa sasa na ya ule utakaokuwapo baadaye.”—1 Tim. 4:8.
Basi yako mambo mawili yanayokusaidia kupata ulinzi katika taratibu ya sasa na hasa uzima katika dunia iliyosafishwa ambayo itakuja. La kwanza ni bidii yako, kwa kuiepuka roho ya ulimwengu huu, ambapo kufikiri kwingi, usemi na matendo yanaharibika na ni hatari. Jingine ni sala na kusoma Biblia, ili usaidike kupata msaada wa roho ya Mungu kwa kufanya kama Biblia ishaurivyo: “Mfanywe wapya katika roho ya nia zenu.” Pia inasema: ‘Vueni kabisa utu wa kale pamoja na matendo yake, mkavae utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.’—Efe. 4:23.; Kol. 3:9, 10.
Unaweza kufanya hili ukifanya bidii ya kujifunza kanuni zilizo katika Neno la Mungu na kuzitumia. Ni rahisi, zimeelezwa waziwazi na zaeleweka kwa wepesi. Tunaambiwa: “Hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.”—Mhu. 7:12.
Hekima kutoka kwa Mungu yaweza kweli kusaidia mtu apate maisha marefu zaidi, kama mtume Petro alivyoandika: “Atakaye kupenda maisha, na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila . . . kwa kuwa macho ya [Yehova] huwaelekea wenye haki, na masikio yake husikiliza maombi yao.” (1 Pet. 3:10-12) Kuwa na uhusiano wa karibu na Mungu ni kwa maana sana, maana kunamlinda mtu kiroho, na mara kwa mara humtoa kwenye msiba. Jinsi gani?
Kwa mfano, fikiria yale Yesu alisema kuhusu wanafunzi wake: “Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” (Yohana 17:16) Wale wanaochukua msimamo huu wa hekima hujiepusha na fitina za kisiasa na mashindano ya ulimwengu huu. Mara kwa mara hilo huokoa maisha zao. Kwa mfano, katika Ireland Mashahidi wa Yehova hawaungani na fitina yo yote ya kidini wala ya kisiasa ya wenye kung’ang’ania utawala. Shahidi alikuwa akiendesha motokaa barabarani akasimamishwa na wanaume watatu waliovaa vifuniko vya uso. Aliwaambia yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, lakini walimlazimisha atoke katika motokaa yake. Kwa kawaida hii ingemaanisha kwamba alikuwa karibu kupigwa risasi. Hata hivyo, watu hao walipopekua motokaa yake wakahakikisha wenyewe kwamba kweli alikuwa Shahidi, walimwambia aendelee mbele, wakimtakia mema.
Jambo la maana kupita yote, mwishoni mwa taratibu hii ya mambo iliyoharibika, Mungu atawathawabisha wale wapendao njia zake za haki kwa kuwaokoa wangali hai, wapate uzima katika dunia iliyosafishwa. Hili lilihakikishwa katika njozi aliyopewa Yohana. Hapo aliona “mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha.” Wakati ulizo lilipozuka juu ya waliofananishwa na mkutano huu, jibu lilitolewa: “Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu [itakayomaliza taratibu hii ya mambo].” (Ufu. 7:9, 14) Ebu wazia ukiona kuondolewa kwa taratibu hii yenye kuhatirisha maisha na kuishi ujifurahishe taratibu itoayo uzima ambamo watu wataweza kubadilisha nyutu zao chini ya uangalizi wa Mungu, waishi kwa amani na umoja! Kweli ikiwa wauthamini uhai wako, inafaa ujitahidi kuupata mradi huo.