Maswali kutoka kwa Wasomaji
● Mimi nilidhani kwamba nyakati zote Ukumbusho unafanywa jioni yenye mwezi mpevu (kamili). Lakini mwaka 1977 Ukumbusho ulifanywa Aprili 3, nayo kalenda yangu ikaonyesha kwamba Aprili 4 ndiyo iliyokuwa siku ya mwezi mpevu. Kwa sababu gani kukawa na tofauti hiyo?
Kwa kawaida mwadhimisho wa Chakula cha Bwana cha Jioni unalingana na wakati wa kutokea mwezi mpevu, lakini si nyakati zote. Kwa mfano, huenda mambo hayo mawili yakapitana kwa siku moja ikitegemea mahali unapoishi na kalenda inayotumiwa.
Ili ufahamu sababu, unahitaji kuifahamu njia ya msingi inayotumiwa na Baraza Inayoongoza ya Mashahidi wa Yehova kuamua tarehe ya mwadhimisho wa kila mwaka wa Ukumbusho.
Siku ya 14 ya mwezi Nisani wa Kiyahudi, yaani, tarehe ya Sikukuu ya Kupitwa, ndipo Yesu alipoagiza wafuasi wake wawe wakikumbuka kifo chake. (Luka 22:14-20) Imefaa kwamba tarehe ya mwadhimisho wa Ukumbusho inaamuliwa kama vile Wayahudi huko nyuma walivyoiamua tarehe ya Sikukuu ya Kupitwa. Mwezi wa Nisani ulianza wakati walipoweza kuuona mwezi mwandamo (mpya) kwa mara ya kwanza katika kipindi cha masika kinachokaribiana zaidi na wakati mchana na usiku zinapolingana urefu. Sikukuu ya Kupitwa ilitokea siku kumi na nne baada ya hapo.—Isa. 66:23; Kut. 12:2, 6.
Sasa Mashahidi wa Yehova wanafuata kielelezo hicho cha kale kuamua tarehe ya Ukumbusho. Tafadhali fahamu kwamba jambo la kwanza linalohitaji kuamuliwa ni wakati mwezi mwandamo (mpya) utakapoonekana Yerusalemu, katika wakati unaokaribiana zaidi na siku ya masika ambayo mchana na usiku zinalingana urefu (karibu na Machi 21). Huo sio wakati unaoonyeshwa katika kalenda au katika orodha yenye kutayarishwa na wachunguzi wa elimu ya nyota. Kwa sababu gani? Kwa sababu kipande cha kwanza chembamba cha mwezi mwandamo kinakuja kuonekana kati ya saa kumi na nane na 30 baada ya wakati wa kuwako mwezi mwandamo unaoonyeshwa na wachunguzi wa elimu ya nyota.
Na tuchukue mwaka 1977 kama mfano. Ili Baraza Inayoongoza ya Mashahidi wa Yehova iamue jambo hilo miezi mingi kabla halijakuwako kwa kusudi la kueleza makundi duniani pote, ilihesabu ikajua wakati mwezi mwandamo ungeonekana Yerusalemu. Kulingana na habari za wachunguzi wa nyota, mwezi mwandamo ulitukia saa 20:33 (2:33 jioni) Machi 19, 1977, kulingana na saa za Yerusalemu. Lakini, mwezi huo mwandamo haukuweza kuonekana wakati huo wala usingeweza kuonekana mpaka saa nyingi zipite. Lakini je! kipande chembamba cha kwanza cha mwezi huo mwandamo kingeweza kuonekana jioni iliyofuata karibu na machweo (kushuka kwa jua)? Kwa sababu ya mambo mbalimbali, haikuelekea kwamba mwezi ungeweza kuonekana katika anga lenye mwangaza magharibi ya Yerusalemu karibu na wakati wa machweo ya Machi 20, 1977. Basi, Baraza Inayoongoza iliona kwamba Machi 21, 1977 ndipo kwa uhakika mwezi mwandamo ungeweza kuonekana Yerusalemu karibu na machweo. Kwa hiyo Nisani 14 ingeanza wakati wa machweo ya Aprili 3. Siku hiyo ndipo Mashahidi wa Yehova walipoadhimisha Chakula cha Bwana cha Jioni. Lakini mwezi mpevu ulitokea tarehe gani?
Orodha za wachunguzi wa elimu ya nyota zinaonyesha mwezi mpevu ulitokea Aprili 4 saa 04:09 (10:09 alfajiri na mapema), kulingana na saa za Greenwich (Uingereza) ambazo ndizo zinazoamua saa za ulimwengu wote. Lakini ikiwa unaishi katika eneo tofauti, saa yako ingeonyesha wakati tofauti dakika iyo hiyo. Kwa mfano, miji ya Stockholm (Sweden) na Rome (Italia) imo katika eneo la kwanza lenye saa zinazokaribiana zaidi na za Greenwich, upande wa mashariki. Kwa hiyo, katika miji hiyo mwezi mpevu ulitokea Aprili 4 saa 05:09 (11:09 alfajiri na mapema). Lakini, New York (U.S.A.) na Lima (Peru) ni maeneo yaliyo mara tano mbali na saa za Greenwich upande wa magharibi, kwa hiyo katika maeneo hayo mwezi mpevu ulitokea saa 23:09 (5:09 usiku) Aprili 3, 1977. Kwa sababu ya maeneo mbalimbali kutofautiana saa, kalenda fulani za 1977 zilionyesha kwamba mwezi mpevu ulitokea Aprili 4 na nyingine zikasema ulitokea Aprili 3.
Kwa vyo vyote, jambo kuu unalopaswa kufahamu ni kwamba tarehe ya mwadhimisho wa Chakula cha Bwana cha Jioni inaamuliwa na mwezi mwandamo (au mpya, unaoonekana Yerusalemu), wala haiamuliwi na mwezi mpevu (kamili). Hata hivyo, Ukumbusho unafanyika siku kumi na nne baada ya mwezi mwandamo kuonekana. Basi ukumbusho unatukia nyakati zote karibu na wakati wa mwezi mpevu. Ni vizuri kujua habari hizi ili Mashahidi fulani wa Yehova wasipopashwa habari na Baraza Inayoongoza kwa sababu ya vizuizi fulani waweze kuijua tarehe ya Ukumbusho. Ikiwa hivyo, wakiadhimisha Ukumbusho katika jioni ya tarehe ambayo kalenda inaonyesha mwezi mpevu utatokea baada ya siku ya masika inayolingana urefu mchana na usiku, inaelekea kwamba watakuwa wameuadhimisha tarehe moja na ndugu zao wengine au katika wakati unaokaribiana sana.