Kaini na Mkewe
Alimpata wapi? Kutoka taifa jingine la kibinadamu? Walioana wakati gani? Je! Uhusiano wao ulikuwa zinaa?
WASOMAJI wote wa Biblia wanajua kwamba Kaini ndiye mwanadamu wa kwanza aliyezaliwa duniani. Yeye ndiye aliyekuwa mwana wa kwanza wa Adamu na Hawa, waliokuwa wameumbwa na Mungu moja kwa moja.—Mwa. 4:1.
Masimulizi ya Biblia yanaeleza habari za kuumbwa kwa Adamu na Hawa, na dhambi yao. (Mwa. 2:7, 21, 22; 3:1-6) Yanaeleza jinsi Mungu alivyowahukumia kifo na kuwafukuza katika bustani ya Edeni. (Mwa. 3:14-19) Lakini, Mungu alimwambia Hawa kwamba angezaa watoto.—Mwa. 3:16.
Habili ndiye mvulana wa pili kuzaliwa. (Mwa. 4:2) Maandiko yanaeleza habari chache sana katika masimulizi hayo ya kwanza, lakini habari hizo zinatosha kutueleza kiasi cha mambo tunayohitaji kujua. Yanatuambia kwamba wavulana wawili hao walikua wakawa watu wazima, kila mmoja akaanza kazi yake mwenyewe. Kaini alichagua kazi iliyoanza kabla ya kazi nyingine zote, yaani, ukulima, naye Habili akawa mchunga kondoo. Hiyo inaelekea kuonyesha kwamba miaka mingi ilikuwa imekwisha pita.
Kwa hiyo masimulizi yanaeleza habari hizi: “Ikawa hatimaye” wanaume wawili hao walileta matoleo mbele za Mungu ili wapate upendeleo wake. (Mwa. 4:3, 4) Tunaona pia kwamba wakati Sethi, mwana aliye wa tatu kwa kutajwa, alipozaliwa, Hawa mama yake alimchukua kama amekuwa badala ya Habili. (Mwa. 4:25) Adamu alikuwa na umri wa miaka 130 wakati Sethi alipozaliwa.
Hiyo inaonyesha kwamba labda Adamu alikuwa amekwisha kuwa na watoto wengine wengi wakati huo, kutia na mabinti. Biblia haitutatizi inapokosa kutoa majina ya mabinti wa Adamu, kwa maana haikuwa kawaida sana kutaja kuzaliwa kwa mabinti, tena walitajwa mara chache sana katika orodha za vizazi. Lakini Biblia inatuambia waziwazi katika masimulizi mafupi ya maisha ya Adamu kwamba ‘alizaa wana, waume na wake.’—Mwa. 5:4, 5.
Hakukuwa na mataifa mengine ya kibinadamu—hakukuwa na jamaa yo yote ya wanadamu kabla ya mwanadamu yule wa kwanza wala hakukuwa na wanadamu wengine wenye chanzo tofauti kama ambavyo watu wengine wamekisia wakijaribu kulijibu ulizo juu ya mahali mke wa Kaini alikotoka. Maneno ya Adamu na jina Hawa lenyewe linaonyesha isingeweza kuwa hivyo. Hiyo ni kwa sababu Biblia inasema haya juu ya wakati uliofuata baada ya Mungu kutoa hukumu: “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa [maana yake “-enye kuishi”]; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.”—Mwa. 3:20.
Basi, uamuzi usioepukika ni kwamba Kaini alioa mmoja wa dada zake.
WANADAMU WOTE WANA CHANZO KIMOJA
Wanafunzi wa Biblia wanakubali kwamba mambo ya hakika yanaonyesha ukweli wa maneno ya Biblia yaliyo katika Matendo 17:26, yanayosema kwamba “[Mungu] alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote.” Kitabu Commentary on the Holy Scripturesa (Ufafanuzi juu ya Maandiko Matakatifu) cha John Peter Lange, kinachozungumza hoja na maelezo yanayotolewa na wanafunzi wengi wanapoichunguza Biblia, kinasema haya katika ukurasa wa 191:
“Kwamba Maandiko hayasemi wala hayatasema kulikuwa na wanadamu kabla ya Adamu . . . au mataifa mbalimbali hapo kwanza, inaonyeshwa si na Mwanzo i. na ii. tu, bali pia na sababu zenye kupatana za Maandiko Matakatifu yote; kwa mfano, Mt. xix.4; Matendo xvii. 26; 1 Kor. xv.47. . . . Uhakika wa kwamba taifa la kibinadamu lilikuwa taifa moja hapo kwanza unalingana na fundisho linaloonyesha wanadamu wote kwa ujumla waliingia katika dhambi kupitia kwa Adamu, na kwamba wote pamoja walikombolewa kupitia kwa Kristo. . . . Wengi wa wachunguzi wakuu zaidi wa maumbile wamejitangaza kuwa wanapinga kwamba hapo mwanzo kulikuwa na mataifa mbalimbali ya kibinadamu . . . kwa maana mataifa mbalimbali yanapoweza kuchangamana na kuzaa watoto huo unakuwa uhakikisho mmoja wenye nguvu zaidi kuonyesha kwamba mataifa hayo yalikuwa kitu kimoja hapo kwanza. . . . Lile kisio [la kwamba vitu vilivyo hai (au wanadamu katika habari hii) vilifanyika au vilitokea katika maeneo vilikopatikana] [haliwezi] kukana kwamba makao ya asili ya wanadamu wa namna mbalimbali yalikuwa Asia.”
Maneno hayo yanayohusu umoja wa taifa la kibinadamu (kwamba wote ni taifa moja walioumbwa wakiwa jinsi moja, wala wao si makabila au mataifa yaliyoumbwa au kutokea katika maeneo mbalimbali) yanalingana na maneno haya ya Biblia: “Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti,” na, “kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.” Hata hivyo, Muumba amepanga chembe za uzazi zisizohesabika ziweze kuungana na kutokeza namna nyingi sana za wanadamu wenye kupendeza sana.—Rum. 5:12; 1 Kor. 15:22.
Kwa kuwa Adamu ndiye aliyekuwa baba ya wanadamu wote, Kristo anaweza kuitwa “Adamu wa mwisho,” kwa maana alikuwa mwanadamu mkamilifu duniani, naye sasa anaweza kuwa baba ya wazao wote wa Adamu wanaoiamini dhabihu yake. (1 Kor. 15:45) Kama wanaume na wanawake wangalikuwa na mababa mbalimbali, kifo cha mwanadamu mmoja, Yesu Kristo, kisingalitosha kuwa bei ya kuwanunua wote.—Kum. 19:21; Mt. 20:28.
Wasomaji fulani wa Biblia wamedhani kwamba Kaini alimpata mke wake katika nchi ya Nodi (utoro). Union Version ya mwaka 1952 inasema haya katika Mwanzo 4:16, 17: “Kaini akatoka mbele za uso wa BWANA, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni. Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko.”
Huenda mtu akadhani kutokana na andiko hilo kwamba Kaini alikwenda katika nchi ya Nodi (maana yake “Utoro”) halafu “akamjua” mkewe katika maana ya kwamba, alipofika huko, hiyo ndiyo iliyokuwa mara ya kwanza kuonana naye. Lakini Kaini alifika katika nchi hiyo akiwa pamoja na mkewe, kwa maana neno ‘kujua’ lilitumiwa kujua mtu mwilini, au kufanya ngono naye. Kwa hiyo, tafsiri za kisasa zinasema hivi: “Basi Kaini akaenda zake akatoka usoni pa Yehova na kuanza makao katika nchi ya Utoro kuelekea mashariki ya Edeni. Baadaye Kaini akawa na ngono pamoja na mke wake na yeye akawa mwenye mimba akazaa Henoko.” (New World Translation) Vivyo hivyo, hapo Tafsiri ya James Moffatt, An American Translation na Jerusalem Bible ya Katoliki zinatumia maneno, “Kaini akawa na ngono pamoja na mke wake.” Tafsiri New English Bible inasema: “Kaini akalala pamoja na mke wake.”
JE! NDOA YA KAINI ILIKUWA “ZINAA”?
Je! Mungu alikuwa akisaidia kuendeleza ile inayoitwa “zinaa” kwa kupanga watoto wa kwanza wa Adamu waoane—ndugu waoe dada zao? Hapana. Sababu ni kwamba, katika hali ya kwanza ya kukamilika kwa Adamu, watoto wake wangalizaliwa wakiwa wakamilifu. (Kum. 32:4) Baada ya watu wa jamaa moja kuoana, watoto wasingalipitishiwa udhaifu mbalimbali katika miili yao kama inavyokuwa leo wakati ambao taifa la kibinadamu limeharibika sana na kuna kasoro nyingi katika chembe za uzazi. Hata baada ya Adamu kutenda dhambi, wazao wake waliishi mpaka miaka 969 siku zilizotangulia Gharika.—Mwa. 5:27.
Kwa hiyo, muda mrefu ulipita ndipo kasoro za chembe za uzazi zikawa nyingi sana hata ikawa hatari sana watu wa jamaa moja kuoana. Hata Ibrahimu alioa dada wa baba mmoja naye karibu miaka 2,000 baada ya Adamu kuumbwa. (Mwa. 20:12) Mungu alikataza kusiwe na ndoa za watu wa jamaa moja kati ya Waisraeli baada ya kuwapa sheria ya Musa (karibu miaka 500 baadaye).—Law. 18:6-18.
Mungu alifanya mpango mzuri ajabu kwa kuwafanya wanadamu wawe taifa moja, wawe na chanzo kimoja. Wote wanaweza kupata faida zinazolingana kutokana na dhabihu ya upatanisho ya Yesu Kristo. (1 Tim. 2:5, 6) Wote wanaweza kumfikia Mungu kupitia kwa Huyo akiwa ndiye ‘Baba yao wa milele,’ tena wanaweza kuwa na uhusiano unaolingana wa kuwa “watoto wa Mungu.” (Isa. 9:6; Rum. 8:21) Chini ya utawala wa Kristo wanadamu watakuwa tena kitu kimoja. (Efe. 1:9,10) Vizuizi vyote au mipaka yote ya kitaifa, ya kikabila, ya kisiasa na ya kijamii itafutiliwa mbali kabisa, kisha kusudi ambalo Mungu alikuwa nalo pale pale mwanzoni litatimia.—1 Kor. 15:24, 28.
[Maelezo ya Chini]
a Chapa ya 1960, toleo la 1976, iliyochapwa na Zondervan Publishing House, Grand Rapids, Michigan.