Laodikia—Mji Wenye Utajiri Mwingi
KARIBU na Danizli katika kusini-magharibi mwa Uturiki kuna magofu ya mji wa kale wa Laodikia. Uliokuwa ukiitwa Dispoli kisha ukaitwa Roasi, kwa wazi mji huo ulisimamishwa kwa mara nyingine katika karne ya tatu K.W.K. na mtawala Antioko II wa nasaba ya Kiseleukia, aliyeupatia jina la mkewe Laodiki. Ukiwa kwenye makutano ya njia kuu za biashara katika bonde la mto Likasi lenye rutuba, Laodikia ulikuwa umesimamishwa mahali pazuri. Uliunganishwa kwa barabara na miji kama vile Efeso, Pergamo na Filadefia.
Mji huo ulikuwa na utajiri mwingi sana. Nayo idadi kubwa ya Wayahudi iliushiriki utajiri huo. Kinachoonyesha namna utajiri huo ulivyokuwa ni uhakika wa kwamba wakati Gavana (Liwali) Flako alipoamuru mchango wa kila mwaka uwe ukitolewa kwa ajili ya hekalu katika Yerusalemu, kiasi kilichopatikana kilikuwa zaidi ya ratili 20 (kilo 10) za dhahabu. Vilevile, wakati tetemeko la nchi wakati wa utawala wa Kaisari Nero lilipoleta uharibifu mkubwa humo mjini Laodikia, wakaaji wake waliweza kuujenga upya bila msaada wo wote kutoka Rumi.
Kazi za banki na viwanda ziliupa mji huo sehemu ya utajiri wake. Laodikia ulijulikana sana kwa sababu ya mavazi yenye kung’aa ya sufu nyeusi yaliyotengenezewa humo. Labda rangi ya asili ya namna fulani ya kondoo wa humo ilikuwa nyeusi. Au, labda Laodikia ulijulikana sana kwa sababu ya rangi nyeusi maalum (ya pekee) iliyotengenezewa humo.
Zaidi ya kuwa makao makuu ya kazi za banki na za viwanda, Laodikia ulikuwa makao ya shule ya utabibu (uganga). Kwa hiyo, kwa kuwa Laodikia ulikuwa katika mahali paitwapo Frigia, huenda ikawa kwamba dawa ya macho iitwayo “unga wa Frigia” ilitengenezewa mjini humo. Kwa hiyo si jambo la kushangaza kwamba ibada ya Esikulapo, mungu fulani wa utabibu (uganga), ilikuwa maarufu sana humo Laodikia.
Ijapokuwa ulikuwa na faida za kibiashara, Laodikia ulikuwa na tatizo la kupata maji yake. Mji huo haukuwa na chemchemi za maji ya moto zilizojulikana kwa sababu ya sifa zazo za kuponya, kama zile za Hierapoli uliokuwa karibu. Wala haukuwa na maji baridi yenye kuburudisha, kama yale ya Kolosai uliokuwa karibu. Maji yake yaliletwa Laodikia kwa mifereji kutoka kisima fulani cha maji kilichokuwa umbali mkubwa kuelekea upande wa kusini. Kwanza maji yaliletwa kwa mifereji, kisha yalipokaribia mji, yaliletwa kwa mawe ya miraba sita iliyolingana. Mawe haya yalikuwa na mashimo katikati toka upande mmoja mpaka mwingine kisha yalishikamanishwa pamoja kwa sementi (saruji). Kwa kuwa maji hayo yalisafirishwa kwa umbali mrefu, yaelekea kwamba yalipofika Laodikia yalikuwa na uvuguvugu.
KUNDI LA KIKRISTO KATIKA LAODIKIA
Wakati fulani kabla ya mwaka 61 W.K., kundi la Kikristo lilianzishwa huko Laodikia. Kundi hilo lilianzishwaje? Biblia haitoi habari ya waziwazi juu ya jambo hili. Hata hivyo, Mkristo wa Kolosai aitwaye Epafra alisaidia sana kuendeleza faida za kiroho huko. (Kol. 4:12, 13, 15) Vilevile, matokeo ya kazi ya Paulo kule Efeso huenda yakawa yalifika mpaka Laodikia.—Matendo 19:10.
Karibu na mwisho wa karne ya kwanza, Wakristo huko Laodikia waliingia katika hali mbaya sana ya kiroho. Yesu Kristo aliwapelekea ujumbe huu kupitia kwa mtume Yohana: “Nayajua matendo yako ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri; na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane; na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”—Ufu. 3:15-18.
Inafaa kuona kwamba kwa wazi Yesu Kristo alitumia hali za Laodikia ili kuonyesha kwa mfano kilichohitajiwa na kundi hilo. Bila shaka Wakristo huko waliushiriki utajiri wa mji na wakaaji wake wengine. Walakini, kiroho, kundi hilo lilikuwa maskini, kipofu na uchi, ijapokuwa lilifikiri vingine. Kwa hiyo, kilichohitajiwa na kundi hilo si dhahabu ya banki za Laodikia. Si mavazi ya sufu nyeusi yaliyotengenezewa humo. Si “unga wa Frigia” uliotengenezwa na matabibu (waganga). Wala si maji yenye moto yenye kutibu kutoka Hierapoli uliokuwa karibu, au maji yenye baridi ya Kolosai. Bali kundi la Laodikia lilihitaji kile kinachofanana na vitu hivyo katika maana ya kiroho.
Ili kutajirisha utu wao wa kiroho, washiriki wa kundi hilo walihitaji “dhahabu iliyosafishwa kwa moto” ya kiroho, kutia na imani yenye thamani kubwa zaidi ya dhahabu halisi. (1 Pet. 1:6, 7) Walihitaji “mavazi meupe,” yanayofananisha mwenendo na matendo ya Kikristo yasiyo na lawama. (Ufu. 16:15; 19:8) Kwa sababu ya upofu wao juu ya kweli ya Biblia na daraka lao la Kikristo, walihitaji “dawa ya macho.” Ulikuwa ni wakati wao wa kuonyesha msimamo wao kabisa juu ya utumishi wao mtakatifu. Kwa hiyo, huo ulikuwa wakati wao wa kuwa ama moto unaosisimua ama baridi inayoburudisha na kuacha uvuguvugu wao juu ya utendaji wa Kikristo.
Sisi leo tunaweza kufaidika kutokana na shauri zuri lililopewa Wakristo wa Laodikia. Kama Walaodikia walivyopaswa kujilinda wasivutwe na njia ya maisha ya kutafuta mali iliyowazunguka, lazima nasi tufanye vivyo hivyo. Kwa kuendeleza maoni ya kiroho yanayofaa, tunaweza kuepuka kuingia katika hali kama ile ya Wakristo wengine katika Laodikia wenye utajiri mwingi. Hivyo, maisha yetu yatakuwa yenye utajiri zaidi, kwa baraka yetu na kwa sifa ya Mungu.