Ukumbusho wa Kifo cha Kristo—Utaendelea kwa Muda Gani Zaidi?
UKUMBUSHO wa kifo cha Kristo utaendelea kwa muda fulani tu uliowekwa. Mtume Paulo aliwaandikia Wakristo wa karne ya kwanza hivi: “Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti [kifo] ya Bwana hata ajapo.” (1 Kor. 11:26) Kwa wazi, hili linamaanisha kwamba, Bwana Yesu Kristo ajapo, kule kutangazwa kwa kifo chake kwa njia ya kuadhimisha Chakula cha Bwana cha Jioni, au Kijio, kutakoma.—1 Kor. 11:20.
Katika wakati wa Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 33 Wakati wetu wa Kawaida, Bwana Yesu Kristo alianzisha “Chakula cha Bwana cha Jioni.” Akionyesha kusudi yacho, aliwaambia mitume wake waaminifu hivi: “Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Vilevile, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mkinywapo, kwa ukumbusho wangu.” (Luka 22:19; 1 Kor. 11:23-25) Kumwagwa kwa damu ya Kristo na kutolewa dhabihu kwa mwili wake mkamilifu wa kibinadamu kulimaliza kule kuwapo kwake kwa kinaganaga (moja kwa moja) kama mtu mwenye kuishi pamoja na wanafunzi wake wa kidunia, sana sana ilikuwa hivyo alipopaa kurudi mbinguni siku ya arobaini na mbili tokea wakati ule. Kwa hiyo, Chakula cha Bwana cha Jioni kingeadhimishwa kila mwaka katika siku ile ile ya kila mwaka (Nisani 14) kama kitu cha kuwakumbusha juu ya kifo cha Kristo kwa ajili yao. Kufanya hivi kungechochea kupendezwa kwao na jambo hilo.
Akikumbuka wakati ambao hangekuwapo na wakati ambao angerudi, Yesu aliwaambia wanafunzi wake hivi wakati alipokuwa akiuanzisha Ukumbusho: “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.”—Yohana 14:2, 3.
Ukumbusho wa kifo cha Yesu utaendelea kuadhimishwa, mpaka yeye atakapompokea wa mwisho wa wanafunzi hawa. Mwishowe, wakati wote watakapoungana pamoja naye mbinguni kusudi watumikie kama makuhani pamoja naye na kutawala kama wafalme naye, kuadhimisha Ukumbusho duniani kutakoma.
Utawala wa Kristo katika ile miaka 1,000 katika utukufu wa kimbinguni utakuwa wakati unaofaa kwa raia zake za kidunia kuadhimisha ufalme wake, si kifo chake cha dhabihu duniani. Utakuwa wakati wa wanadamu kufurahi, kushangilia pamoja naye kwa ajili ya zawadi yake ya kifalme. Wakati huo wanadamu watakuwa wakipokea zile faida kamili za mateso na kifo chake ambacho kwa lazima kingetangulia kutukuzwa kwake mbinguni.
Ni wangapi “watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, [na kutawala] pamoja naye hiyo miaka elfu”? Ni hesabu yenye kikomo, wanafunzi 144,000. (Ufu. 7:2-8; 14:1-3; 20:4-6) Wanafananishwa wakiwa wametiwa muhuri na ule “muhuri wa Mungu aliye hai.” Mtume Yohana anasema hivi:
“Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu. Wa kabila ya Yuda . . . Reubeni . . . Gadi . . . Asheri . . . Manase . . . Simeoni . . . Lawi . . . Isakari. . . Zabuloni . . . Yusufu . . . Benjamini.” Hawa walitiwa muhuri kwa roho takatifu ya Mungu. (2 Kor. 1:21, 22) Hesabu yao inathibitishwa na Ufunuo 14:1-5, ambalo linasema kwamba jina la Kristo na lile la Baba yake yameandikwa katika vipaji vya nyuso zao. Vilevile, wamesimama na Mwana-Kondoo aliyetukuzwa Yesu Kristo juu ya Mlima Sayuni, ule wa kimbinguni, wala si ule wa kidunia kule Mashariki ya Kati ambapo Yerusalemu wa kale ulikokuwa wakati mmoja.—Ebr. 12:22; Ufu. 3:12.
Katika Israeli wa kale wa kimwili, makuhani na walawi waliotumikia chini yao katika hekalu la Yehova walichukuliwa kutoka kwa kabila la Lawi peke yake. Hivi sivyo ilivyo kwa habari ya wale 144,000 ambao “watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo.” Kulingana na Ufunuo 7:4-8, ni 12,000 peke yao wanaochukuliwa kutoka kwa kabila la Lawi. Wale wengine 132,000 wanachukuliwa kutoka kwa yale makabila mengine 11 yaliyotajwa. Hili linathibitisha kwamba makabila yale 12 yanayotajwa hapo si yale yale 12 ya Israeli wa kimwili.—1 Kor. 10:18.
Yale “makabila” ambayo kutoka kwayo wote wale 144,000 wanachukuliwa na kutiwa muhuri ni Waisraeli wa kiroho. Wale wasiochaguliwa na kutiwa muhuri wanakataliwa. Jambo kama hilo lilitukia katika Israeli wa asili wa kale katika karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida. Ni “mabaki” tu ya Waisraeli wa asili wa kimwili waliochaguliwa ijapokuwa “wengi,” taifa zima ndio waliokuwa wameitwa na walikuwa na nafasi ya kufanyiza wale 144,000 makuhani na wafalme washirika wa Yesu Kristo mbinguni. Waliosalia wa taifa lisiloamini walikataliwa. Inasemekana kwamba, 1,100,000 yao walipata kifo cha jeuri wakati Yerusalemu ulipoharibiwa na Warumi katika mwaka 70 W.K. Vivyo hivyo leo, wale Waisraeli wa kiroho ambao hawatiwi muhuri kwa ule “muhuri wa Mungu aliye hai” hawapati ulinzi wake wakati upepo wa chamchela utokeapo wakati zile “pepo nne” ziwachiliwapo na wale malaika wanne kwa wakati wake Mungu uliowekwa ili zipate ‘kuidhuru nchi, bahari na miti?
Waisraeli wa kiroho waliokataliwa wasiotiwa muhuri ‘watadhuriwa’ hata waharibiwe. Hawatatoka katika ile “dhiki kuu” wakiwa hai kama vile “mkutano mkubwa,” ambao wanasemekana kuwa wanatoka katika kila kabila la kidunia, taifa, jamaa na lugha.—Ufu. 7:1-14.
CHAKULA CHA BWANA CHA JIONI CHAANZISHWA
Yesu Kristo alishirikisha chakula cha jioni cha ukumbusho na ufalme wa Mungu. Hili lilifaa kabisa, kwa kuwa kifo chake katika uaminifu kilikuwa, kwanza kabisa, ili atetee enzi kuu ya ulimwengu wote ya Yehova Mungu, “Mfalme wa milele.” (Ufu. 15:3) Kwa uaminifu wake mpaka kufa alikuwa akijionyesha mwenyewe kuwa anastahili kuwa Mrithi wa Milele wa Daudi ambaye Mungu alifanya agano la ufalme wa milele pamoja naye. (2 Sam. 7:1-29; 2 Nya. 13:5, 8; Luka 1:31-33; 22:29, 30) Uhakika huu unatokezwa wazi na masimulizi ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 33 W.K., kama yanavyosimuliwa na mwandikaji wa Injili Luka. Hapo twasoma hivi:
“Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila [Sikukuu hii ya Kupitwa] pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.”
“Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.”—Luka 22:14-20.a
Vile vikombe viwili vya divai alivyotumia Yesu, kulingana na hayo masimulizi yaliyo juu, vilikuwa vikombe viwili vya mwisho vya vikombe vya divai ambavyo kwa desturi vilinywewa na washiriki wote katika Sikukuu ya Kupitwa wakati wa karne ya kwanza W.K. Kwa hiyo kilikuwa kikombe cha 3 na 4. Kikombe cha 3 kilinywewa baada ya waadhimishaji kumla mwana-kondoo wa Kupitwa na mkate usiotiwa chachu. Kiliitwa “kikombe kile cha baraka” kwa sababu ya baraka zilizosemwa juu yacho. (1 Kor. 10:16) Yesu “alishukuru” Mungu kwa ajili ya kikombe kabla ya kukishiriki pamoja na mitume. Hivyo, Yesu aliongoza katika kuiadhimisha Sikukuu ya Kupitwa kulingana na desturi iliyokubaliwa ya wakati huo. Yeye hakuibadili au kuikatiza kwa kuanzisha kitu cho chote kipya katika kufuata mwadhimisho huu. Kwa njia hii aliifuata Torati akiwa Myahudi.
Hata hivyo, wakati chakula cha Sikukuu ya Kupitwa kilipokuwa kimekwisha liwa kulingana na torati ya Musa, Yesu, alikuwa yu huru kuanzisha kile chakula kipya cha jioni cha ukumbusho wa kifo chake kilichokuwa kinakaribia katika siku iyo hiyo ya Kupitwa. Mezani palikuwa pangali na mkate usiotiwa chachu na kikombe cha 4, ambacho baada ya kukinywea Zaburi 115 mpaka 118 za Hallel (“sifa”) ziliimbwa. Kwa hiyo kilikuwa “kikombe cha sifa.”—Tazama The Watch Tower ya Machi 15, 1921, kurasa 88, 89, chini ya kichwa kidogo “Kikombe cha Sifa”; pia, Critical and Exegetical Handbook to the Gospel of Matthew cha Meyer, Kurasa 45, 46, chini ya mstari 27; pia, The Jewish Encyclopoedia chini ya Siku-kuu ya Kupitwa, Seder na Arba Kosoth (Vikombe Vinne).
Mtume Mathayo alikuwa na Yesu usiku huo wa Sikukuu ya Kupitwa, naye anaanza masimulizi yake baada ya “Kikombe kile cha baraka” kunywewa:
“Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. Nao walipokwisha kuimba [Zaburi 115-118 za Hallel], wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.”—Mt. 26:26-30.
Wakati mitume waaminifu walipokinywea kikombe cha 4, au “Kikombe cha baada ya Kijio” (Ferrar Fenton), wao walikuwa, kulingana na maneno ya Yesu, wakinywa damu kwa njia ya mfano, damu ya Yesu. (Luka 22:20, FF) Ijapokuwa walikuwa Wayahudi waliokuwa katika agano la Torati ya Musa, wazo hilo halikuwachukiza. (Zab. 16:4) Yesu alikuwa amekwisha watayarisha kwa ajili ya hili kwa yale aliyokuwa amewaambia wakati fulani uliotangulia. Hii ilikuwa punde (muda mfupi) tu kabla ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 32 W.K., na siku iliyofuata baada ya kuulisha umati wa wasikilizaji kwa mwujiza kwa kuzidisha vipande vichache vya mkate na samaki wachache. (Yohana 6:4) Mtume Yohana atuambia hivi:
“Basi Yesu akajibu akawaambia: . . . Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.
“Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. . . . Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama. mababa walivyokula, wakafa, bali akilaye chakula hicho ataishi milele... “Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hilo ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? . . .
“Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.”
Lakini mtume Petro aliendelea kuandamana na Yesu na kusema: “Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki tena tumejua, ya kuwa ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”—Yohana 6:43-69.
Wakati huo Yesu hakuwa akisema na Waisraeli hao waliotahiriwa juu ya “uzima wa milele” wakiwa viumbe vya kibinadamu katika Paradiso ya kidunia chini ya ufalme wake wa mileani (miaka elfu).
Mahali yake, alikuwa akisema juu ya nafasi ile ile aliyokuwa akiweka mbele ya mtume Petro pamoja na mitume wenzake kupitia kwa “maneno ya uzima wa milele.” Ilikuwa nafasi ya kupata urithi wa uzima pamoja na Kristo mbinguni, “uzima ndani yenu.” (Yohana 6:53) Kwa kutawala naye mbinguni wangepitisha kwa wanadamu faida zenye kutoa uzima za dhabihu yake.b
Wayahudi hao walikuwa wamekuwa wakitaka “kumshika ili wamfanye mfalme” akae juu ya kiti cha enzi cha Daudi. Mahali pake, Yesu alichagua kufanywa mfalme mbinguni na Baba yake. (Yohana 6:15, 61, 62) Wayahudi hao walikuwa katika agano la Torati lililopatanishwa na Musa. Agano hilo la Torati lilikusudiwa kuwaongoza Wayahudi kwa Kristo na hivyo kuwapa nafasi ya kuwa “ufalme wa makuhani” pamoja naye.—Kut. 19:5, 6; Gal. 3:24, 25.
Hivyo basi, katika mazungumzo yaliyoandikwa katika Yohana 6:52-65, Yesu hakuwa akizungumza juu ya ulimwengu wa wanadamu kuwa ndio ungeinywa damu yake na kuula mwili wake, kwa njia ya mfano, wakati wa utawala wake wa miaka elfu. Alikuwa akizungumza juu ya waamini ambao angeleta katika agano jipya. (Yer. 31:31-34; Ufu. 20:4-6) Wao wangekuwa Waisraeli wa kiroho. Ndio sababu, wakati Yesu alipoanzisha “chakula cha Bwana cha jioni,” aliwaambia. mitume wake Waisraeli hivi: “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.” (Luka 22:20; 1 Kor. 11:20, 25) Au, kulingana na Mathayo 26:27: “Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” Wale mitume 11 waaminifu walioukubali mkate usiotiwa chachu na kikombe cha divai mikononi mwa Yesu usiku huo wa Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 33 W.K. waliingizwa katika hilo agano jipya katika siku ya Pentekoste, siku ya hamsini na mbili baada ya Sikukuu ya Kupitwa.
UKUMBUSHO NA UFALME
Agano la kale la Torati, na taraja lake la “ufalme wa makuhani,” lilikuwa ama kiongozi ili kuongoza mabaki wachache tu kwa Kristo, Wayahudi wengi wa Israeli wakiwa wamealikwa lakini waliochaguliwa wakiwa wachache. (Mt. 22:1-14; Rum. 9:27-30; 11:5) Lakini agano jipya linatokeza kile ambacho Petro aliita “mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu.”—1 Pet. 2:9.
Kwa sababu ya kweli hii, Yesu Kristo aweza kuwaleta katika agano la ufalme pamoja naye. (Luka 22:28-30; Ufu .20:4-6) Basi “Yerusalemu wa kimbinguni” aweza kufurahi zaidi ya “Yerusalemu” wa kidunia, ambaye alikuwa katika agano la Torati. Sababu gani hivyo? Kwa sababu “mwanamke” wa Mungu, “mama” wa kimbinguni, azaliaye ‘Mumewe’ watoto wa kiroho, anazaa washiriki wote warithi 144,000 wa Kristo na wala si mabaki wachache tu wenye taraja la kuwa warithi wa ufalme.—Gal. 4:21-31; Isa. 54:1.
Wana wa Mungu wa kiroho, Waisraeli wa kiroho walio katika agano jipya, ndio wanaopaswa kukila chakula cha Bwana cha jioni katika kukikumbuka kifo chake. Mtume Paulo anawafananisha hawa Waisraeli wa kiroho na anachoita “Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili.” Madhabahu halisi ambayo juu yake dhabihu zilitolewa kwa Mungu ilikuwa ikiitwa “meza ya [Yehova].” Wakati Waisraeli walipokula sehemu ya dhabihu, za ushirika zilizotolewa kwa Mungu walipata kuwa na ushirika pamoja Naye, kwa kuwa Yeye aliwakilishwa na madhabahu. (Mal. 1:7, 8) Vivyo hivyo, meza ambayo juu yake mkate usiotiwa chachu na ambayo kikombe cha divai kinawekwa kwa ajili ya chakula cha Bwana cha jioni inaweza kuitwa “meza ya [Yehova].” Waisraeli wa kiroho wanaoshiriki mifano hiyo ya Ukumbusho wanapata kuwa na ushirika pamoja na Yehova kwa njia hiyo. Wao wanakuwa washiriki pamoja Naye na vilevile wao kwa wao.—1 Kor. 10:18-21; 11:25.
Vivyo hivyo, basi, kwenye ukumbusho kile kikombe cha divai kinachofananisha ile “damu ya agano” chasemekana kuwa “kikombe cha[Yehova].” Wakati Waisraeli wa kiroho wanapokunywa sehemu ya kikombe hiki, wanakuwa washiriki pamoja na Yehova kwa njia ya damu ya Kristo inayohalalisha agano jipya. Kwa wonyesho huu Waisraeli wa kiroho wanaonyesha kwamba wanamwabudu Yehova akiwa Mungu wao na hawamwabudu shetani ye yote kama mungu. Yehova anaikubali damu ya Kristo kuwa ndiyo inayolifanya agano jipya kutenda kazi. Vivyo hivyo, wanywaji wa kikombe cha Ukumbusho wanaikubali damu ya Kristo kuwa ndiyo uhai alioutoa kuwa dhabihu kwa ajili yao ili Mungu apate kuwasamehe dhambi zao kupitia kwa agano hilo.
Ijapokuwa kile kikombe cha Ukumbusho kilifananisha kifo cha dhabihu ya Kristo kwa njia ya kuimwaga damu ya uhai wake, Yesu alimtolea Yehova shukrani kwa ajili yacho. Zaidi ya hayo, baada ya wanafunzi wa Yesu kunywea kikombe hiki cha divai, yeye pamoja nao waliimba Hallel (au “sifa”), iliyobakia, yaani, Zaburi 115 mpaka 118. (Mt. 26:27-30) Kwa hiyo, wanapouadhimisha Ukumbusho, walio katika agano jipya wanatolea kikombe hiki baraka. Ndicho “kikombe kile cha baraka” kwa sababu Yesu alikibariki. Twasoma hivi:
“Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.”—1 Kor. 10:16, 18.
WATAZAMAJI KATIKA UKUMBUSHO
Mabaki ya Waisraeli wa kiroho, ambao ni washiriki wa “mwili” wa kiroho wa Kristo, yangali duniani. Katika miaka ya karibuni wamealika wengine wahudhurie mwadhimisho wa Ukumbusho wa kila mwaka wawe mashahidi au watazamaji. Watu hawa wenye mfano wa kondoo na walio wakf walifananishwa na Yonadabu rafiki ya Mfalme Yehu wa Israeli. (2 Fal. 10:15-23; Yer. 35:1-16) Tangu mwaka wa 1935 W.K. Yesu Kristo Mchungaji Mwema ameleta “mkutano mkubwa” wa “Wayonadabu” wa kisasa ama “kondoo wengine” kwenye ushirika pamoja na mabaki waliozaliwa kwa roho wa “mwili” wake wa kiroho. Walakini kwanza, katika toleo la Watchtower (Mnara wa Mlinzi’) la Februari 15, 1938, twausoma mwaliko huu:
“. . . Baada ya saa 12 jioni Aprili 15 kila shirika la watiwa mafuta na likusanyike na kuadhimisha Ukumbusho, wenzi wao Wayonadabu wakiwapo vilevile. Mifano na iwe mkate usiotiwa chachu na divai iwe nyekundu kweli kweli.”—Ukurasa 50, chini ya “Ukumbusho.”
Hao “kondoo wengine” wasio wa “zizi” hili la “kundi dogo,” walihudhuria Ukumbusho wakiwa watazamaji, si washiriki. —Yohana 10:16; Luka 12:32.—Tazama The Watchtower Machi 1, 1938, ukurasa 75, mafungu 50-52.
Tangu wakati huo, “kondoo wengine,” ambao kwa sasa wameongezeka na kuwa “mkutano mkubwa,” wamekuwa wakihudhuria Ukumbusho wa kila mwaka wa kifo cha Kristo. Mbona isiwe hivyo? Ijapokuwa hawanywi kikombe kinachofananisha damu ya Kristo, wangali wanasemwa na ufunuo 7:14 kwamba “wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.” Pia Ufunuo 7:9, 10 unawaonyesha wakimhesabia Mungu na Mwana-Kondoo Yesu Kristo wokovu wao.
Basi, mwaka huu, Aprili 11, baada ya jua kutua, “kondoo wengine” wote walio wakf na kubatizwa na wakusanyike pamoja na mabaki ya “kundi dogo” kwa mwadhimisho wa chakula cha Bwana cha jioni wa 1979. Kadiri wakati unavyozidi kukaribia wa Bwana Yesu aliyetukuzwa kuchukua mabaki nyumbani kwa makao yao ya kimbinguni, “mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine” hautakuwa na muda mwingi zaidi wa kufanya hivyo tena.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa sababu hati nyingine zinaacha maneno yaliyo baada ya “mwili wangu” na kuendelea mpaka mwisho wa mstari wa 20, maneno hayo yameachwa katika The Bible in Living English (Byington), The New English Bible, na An American Translation, kwa wazi sababu ni kwamba masimulizi ya Mathayo na Marko yanasema kwamba Yesu alitumia kikombe tu katika wakati huu. The Holy Bible in Modern English ya Ferrar Fenton inatia maneno hayo katika vifungo viwili vya mraba kama kwamba maneno hayo yalikuwa ya uongo, ya kuongezwa.
b Tazama The Watchtower chini ya tarehe ya Januari 15, 1951, kurasa 55, 56, mafungu 22-25, chini ya kichwa kidogo “Kula na Kunywa kwa ajili ya Uzima ndani ya Mtu Mwenyewe.” Tazama pia toleo la Aprili 15, 1949, kurasa 119, 120, mafungu 23-28, chini ya “Zawadi ya Uzima ndani Yake.”
[Picha katika ukurasa wa 5]
“Mkate”—Luka 22:19 “Kikombe kile cha Baraka”—Luka 22:17 “Kikombe cha Sifa”—Luka 22:20