“Mfalme Mkuu” Amwadibu Mfalme Mwanadamu
NI NANI huyu “Mfalme mkuu”? Si mwingine ila Yehova, Mungu wa mbinguni. (Mt. 5:35) Naye mfalme mwanadamu anayeadibiwa ni nani? Mfalme Daudi. Kitabu cha Samweli wa Pili kinaeleza namna Mfalme mkuu anavyomwadibu Mfalme Daudi. Kitabu hiki kinaeleza mambo ya miaka 40 ya maisha ya Daudi, kuanzia na wakati kabila lake linapotaka kumtawaza kama mfalme mpaka karibu na wakati Daudi anapofanya mwanawe Sulemani atangazwe kuwa mfalme katika Israeli yote.
Habari ya utawala wa Daudi kama mfalme kwa kweli inaonyesha kwamba aliendelea kupokea adabu kutoka kwa Yehova Mungu wake. Lakini sikuzote Daudi aliipokea katika njia inayofaa, iwe adabu hiyo ilikuwa mafundisho, au adhabu kali kwa sababu ya makosa au dhambi alizozifanya.—Linganisha Waebrania 12:5, 11.
Kitabu cha Samweli wa Pili kinapoanza, tunamwona Daudi akiomboleza kwa sababu ya vifo vya Mfalme Sauli na rafiki yake mkubwa mshikamanifu Yonathani. Halafu, Daudi auliza achukue mwendo gani, naye Yehova amwambia aende katika mji wa Kiyahudi wa Hebroni. Kwa kutii Daudi anafanya hivyo, naye atiwa mafuta kuwa mfalme juu ya kabila la Yuda. Lakini, Abneri, mkuu wa jeshi la Israeli, afanya mwana wa Sauli Ishboshethi atangazwe kuwa mfalme juu ya makabila yote yaliyobaki ya Israeli. Hii inatokeza vita vya wao kwa wao, ambavyo vyaendelea kwa miaka fulani mpaka Abneri anapoasi na kujiunga na Daudi akileta utii wa makabila yote yaliyobaki ya Israeli pamoja naye. Baada ya kutawala juu ya Yuda miaka saba na nusu, sasa Daudi anatiwa mafuta awe mfalme juu ya makabila yote 12 ya Israeli. Daudi auteka Yerusalemu mara moja, ambao umekuwa ukikaliwa na Wayebusi, na kuufanya makao yake makuu.—2 Sam. 1:1—5:10.
Daudi anaendelea kumwuliza Yehova namna anavyopaswa kuendelea, na anaendelea kuwashinda Wafilisti vita baada ya vita. Anatamani sana sanduku takatifu la agano, ambalo ni mfano wa kuwapo kwa Mungu, liletwe katika Yerusalemu. Walakini kwa sababu hakufuata njia aliyoonyeshwa na Mungu, anaadibiwa; Mungu amwua mwanamume mmoja anayehusika kwa sababu ya kugusa sanduku isivyofaa. Baadaye, kwa furaha kuu, Daudi afanya sanduku liletwe sehemu inayobaki ya safari kufika Yerusalemu katika njia inayofaa, likichukuliwa kwa mabega ya makuhani Walawi. Kwa kuona kwamba haifai sanduku hilo liendelee kukaa katika hema wakati yeye anapokaa katika nyumba ya kifalme, Daudi atamani kulijengea hekalu. Lakini Yehova anamwambia kwamba kwa sababu yeye ni mtu wa vita na amemwaga damu nyingi sana, mwanawe atajenga hekalu hili. Hata hivyo, Yehova mwenyewe atamjengea Daudi nyumba, yaani, ukoo wa kifalme ambao utaendelea milele. Mungu ametimiza ahadi hii katika Mwanawe, Yesu Kristo, mzao wa Daudi.—2 Sam. 5:11—7:29; Luka 1:30-33.
Daudi aendelea kupiga vita na kuwashinda adui za Israeli. Walakini wakati mmoja wa masika, Daudi abaki nyumbani mahali pa kwenda vitani. Na kama matokeo, anafanya uzinzi na Bath-sheba, mke wa Uria, mmojawapo wa mashujaa (watu hodari) wake wakubwa. Achukua mimba, na bidii za Daudi za kuficha ubaya huo zinaposhindwa, anafanya mipango mumewe auawe vitani, halafu anamwoa.—2 Sam. 8:1—11:27.
Lakini, mwenendo huu unamkasirisha sana Yehova. Amtuma nabii wake Nathani amkemee Daudi, ambaye anakubali kosa lake na kutubu. Hata hivyo, Daudi ataabika sana kwa sababu ya dhambi yake. Hukumu ya kinabii inasema kwamba upanga hautaondoka katika nyumba yake. Kwanza, mwana aliyechukuliwa mimba kwa uzinzi anakufa. Halafu mmoja wa wana wa Daudi, Amnoni, anampenda Tamari dada baba mmoja naye, anamnajisi (chafua) halafu anamchukia sana. Ndugu mama mmoja naye Absalomu anatafuta wakati unaomfaa na kumwua Amnoni. Mwishowe anapatanishwa na baba yake, Daudi, halafu anaanza mpango wa kupata kibali ya watu wake wamwache Daudi. Absalomu afanya mpango wa mapinduzi, na kumfanya baba yake, pamoja na jamaa yake kubwa watoroke kutoka Yerusalemu. Kwa kweli Daudi anaadibiwa, na kuadhibiwa kwa sababu ya dhambi zake. Yehova anaongoza mambo hata majeshi ya Absalomu yanashindwa. Baada ya hapo yanafuata maandishi ya Daudi ya mashairi, ambayo vilevile mengi yake yanaonekana katika Zaburi ya 18.—2 Sam. 12:1—20:26; 22:1—23:7.
Kwa mara nyingine tena Daudi afanya kosa zito na kuadibiwa kwalo. Aagiza watu wahesabiwe, ingawa mkuu wa jeshi lake Yoabu anapinga jambo hilo. Mara tu baada ya kufanya hivyo dhamiri yake inaanza kumchoma. Lakini inakuwa kuchelewa mno. Anapoulizwa achague kati ya adhabu tatu, Daudi achagua pigo la tauni. Kwa kuona watu wake wakifa kama mainzi anasali hivi: “Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini?” Kwa kutoa sadaka Yehova anakomesha pigo hilo. Kitabu kinamalizika kwa tukio hilo.—2 Sam. 24:1-25.
Kwa kweli kitabu cha Samweli wa Pili kinatuonyesha namna Mfalme mkuu Yehova alivyomwadibu mtumishi wake Mfalme Daudi. Kwa kusifika, Daudi hakuasi au kulaumu mtu mwingine hata pindi moja, kama walivyofanya Adamu, Hawa na Mfalme Sauli. Moyo wa Daudi ulikuwa mwema, yeye alikubali kuadibiwa. Hatujasoma kamwe kwamba alirudia kosa lo lote. Utawala wake ulifanikiwa kwa kuwa alikuwa na kibali ya Mungu mpaka mwisho na alitumiwa naye afikishe mipaka ya Israeli mahali palipokusudiwa na Mungu. Bila shaka yeye alituwekea mfano wa namna itupasavyo kuitikia adabu bila kujali ni ya namna gani?—Ebr. 12:5-11.