Kitabu Cha Biblia Namba 10—2 Samueli
Waandikaji: Gadi na Nathani
Mahali Kilipoandikiwa: Israeli
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 1040 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 1077–c. (karibu) 1040 K.W.K.
1. Samweli wa Pili chaanzia kwenye hali gani ya msingi, na simulizi lacho linakuzwaje?
TAIFA la Israeli lilikuwa limekata tamaa kuhusiana na maafa ya Gilboa na mashambulizi yaliyofuata ya Wafilisti walioshinda. Viongozi wa Israeli na wanaume wao vijana walikuwa wamekufa. Ni katika kikao hicho kwamba ‘masihi wa Yehova’ mchanga, Daudi mwana wa Yese, aliingia kikamili katika mambo ya taifa. (2 Sam. 19:21) Ndivyo kinavyoanza kitabu cha Samweli wa Pili, ambacho kwa kufaa chaweza kuitwa kitabu cha Yehova na Daudi. Simulizi lacho limejawa na vitendo vya kusisimua vya kila aina. Twaanza na kushindwa kabisa hadi ushindi kamili, kutoka msononeko wa taifa lililogawanywa na mzozo hadi fanaka ya ufalme wenye umoja, kutoka nguvu za ujana hadi hekima ya umri mkubwa. Hili ni simulizi la kindani la maisha ya Daudi alipokuwa akijaribu kufuata Yehova kwa moyo wake wote.a Ni simulizi linalopasa kusababisha kila msomaji achunguze moyo wake ili aweze kutia nguvu uhusiano na msimamo wake mwenyewe na Muumba wake.
2. (a) Kitabu hicho kilikujaje kuitwa Samweli wa Pili? (b) Ni nani waliokuwa waandikaji, sifa zao zilikuwa zipi, nao walitafuta kuhifadhi maandishi gani pekee?
2 Kwa kweli, jina la Samweli hata halitajwi katika maandishi ya Samweli wa Pili, yaelekea kitabu kilipewa jina hilo kwa sababu kilikuwa kimekuwa hapo awali kunjo, au buku moja, pamoja na Samweli wa Kwanza. Manabii Nathani na Gadi, waliokamilisha uandikaji wa Samweli wa Kwanza, waliendelea kuandika kitabu chote cha Samweli wa Pili. (1 Nya. 29:29) Walistahili vya kutosha kwa kazi hii. Gadi alikuwa amekuwa na Daudi alipokuwa mkataliwa mwenye kuwindwa katika Israeli, na kuelekea mwisho wa utawala wa miaka 40 wa Daudi, alikuwa angali akishirikiana sana na mfalme huyo. Gadi ndiye aliyetumiwa kutangaza hasira ya Yehova juu ya Daudi kwa kuhesabu Israeli kwa njia isiyo ya hekima. (1 Sam. 22:5; 2 Sam. 24:1-25) Utendaji wa nabii Nathani, mshiriki wa karibu wa Daudi, ulikuwa wa wakati ule ule mmoja na wa Gadi na ulipita kipindi cha maisha yake. Lilikuwa pendeleo lake kujulisha agano la maana la Yehova pamoja na Daudi, agano kwa ajili ya ufalme wa milele. Ni yeye ambaye kwa moyo mkuu na akiwa chini ya upulizio wa Mungu alionyesha dhambi kubwa ya Daudi iliyohusu Bath-sheba na adhabu yayo. (2 Sam. 7:1-17; 12:1-15) Kwa hiyo Yehova alitumia Nathani, ambaye jina lake humaanisha “[Mungu] Ametoa,” na Gadi, ambaye jina lake humaanisha “Jaha Nzuri,” kuandika habari iliyopuliziwa na Mungu na yenye mafaa katika Samweli wa Pili. Wanahistoria hao wasiojitakia makuu hawakutafuta kuhifadhi kumbukumbu lao wenyewe, kwa kuwa hakuna habari yoyote inayotolewa juu ya nasaba au maisha yao ya kibinafsi. Wao walitafuta tu kuhifadhi maandishi yaliyopuliziwa na Mungu, kwa ajili ya mafaa ya waabudu wa Yehova wa wakati ujao.
3. Ni kipindi gani kinachohusishwa na Samweli wa Pili, na kuandikwa kwacho kulikamilishwa lini?
3 Samweli wa Pili chaanza usimulizi wa historia sahihi ya Biblia kufuatia kifo cha Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli, na kuuendeleza karibu na mwisho wa utawala wa Daudi wa miaka 40. Kwa hiyo, kipindi kinachohusika ni kuanzia 1077 K.W.K. hadi karibu 1040 K.W.K. Uhakika wa kwamba kitabu hicho hakiandiki kifo cha Daudi ni ushuhuda wenye nguvu kwamba kiliandikwa karibu 1040 K.W.K., au kabla tu ya kifo chake.
4. Ni kwa sababu gani lazima Samweli wa Pili kikubaliwe kuwa sehemu yenye kukubalika ya Biblia?
4 Kwa sababu zile zile zilizotolewa kuhusiana na Samweli wa Kwanza, kitabu cha Samweli wa Pili lazima kikubaliwe kuwa sehemu inayokubaliwa ya Biblia. Uasilia wacho hautiliki shaka. Usemaji ukweli wacho, bila kufunika hata dhambi na udhaifu mbalimbali wa Mfalme Daudi, ni ushuhuda wenye nguvu wa mambo ya hakika.
5. Ni nini sababu iliyo yenye nguvu zaidi ya kukubali Samweli wa Pili kuwa Andiko lililopuliziwa na Mungu?
5 Hata hivyo, ushuhuda wenye nguvu zaidi wa uasilia wa Samweli wa Pili wapatikana katika unabii mbalimbali uliotimizwa, hasa ule unaohusiana na agano la Ufalme pamoja na Daudi. Mungu alimwahidi Daudi hivi: “Nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.” (7:16) Hata ufalme wa Yuda ulipokuwa umefifia, Yeremia alitaja juu ya kuendelea kwa ahadi hiyo kwa nyumba ya Daudi kwa maneno haya: “Maana BWANA [Yehova, NW] asema hivi, Daudi hatakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli.” (Yer. 33:17) Unabii huo haukukosa kutimizwa, kwa maana Yehova baadaye alitokeza katika Yuda “Yesu Kristo, mwana wa Daudi,” kama ambavyo Biblia yathibitisha waziwazi.—Mt. 1:1.
YALIYOMO KATIKA SAMWELI WA PILI
6. Daudi atendaje asikiapo habari za kifo cha Sauli na cha Yonathani?
6 Matukio ya mapema ya utawala wa Daudi (1:1–4:12). Kufuatia kifo cha Sauli kule Mlima Gilboa, mtoro Mwamaleki kutoka piganoni afanya hima kwenda kwa Daudi kule Sikilagi akiwa na ripoti. Akitumaini kupata kibali cha Daudi, atunga hadithi kwamba ndiye mwenyewe aliyemwua Sauli. Badala ya kusifiwa, Mwamaleki apokea thawabu ya kifo tu, kwa maana amejihukumu mwenyewe kwa kushuhudia alipiga dharuba ‘masihi wa Yehova.’ (1:16) Mfalme mpya, Daudi, sasa atunga wimbo wa kuomboleza, “Ule Upinde,” (NW) ambao katika huo aomboleza kifo cha Sauli na Yonathani. Unafikia upeo mzuri katika usemi wao wenye kugusa moyo wa upendo wa Daudi wenye kufurika kwa ajili ya Yonathani: “Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, ulikuwa ukinipendeza sana; upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, kupita upendo wa wanawake. Jinsi mashujaa walivyoanguka, na silaha za vita zilivyoangamia!”—1:17, 18, 26, 27.
7. Ni matukio mengine gani yanayotia alama sehemu ya mapema ya utawala wa Daudi?
7 Kwa mwelekezo wa Yehova, Daudi na wanaume wake wahamisha watu wa nyumba zao hadi Hebroni katika eneo la Yuda. Hapa wazee wa kabila waja kumpaka Daudi mafuta kuwa mfalme wao katika 1077 K.W.K. Jemadari Yoabu awa mashuhuri zaidi miongoni mwa wanaounga mkono Daudi. Hata hivyo, akiwa mgombeaji wa ufalme juu ya taifa hilo, Ishboshethi, mwana mmoja wa Sauli, apakwa mafuta na Abneri, mkuu wa jeshi. Kuna mapigano ya pindi kwa pindi baina ya majeshi hayo mawili yenye kupingana, na Abneri aua ndugu mmoja wa Yoabu. Mwishowe, Abneri atorokea kambi ya Daudi. Apelekea Daudi, Mikali binti ya Sauli, ambaye Daudi alilipia mahari zamani. Hata hivyo, katika kulipa kisasi kwa ajili ya kuua ndugu yake, Yoabu apata sababu ya kumwua Abneri. Daudi asononeshwa sana na hilo, akikanusha daraka lolote. Upesi baada ya hapo Ishboshethi mwenyewe auawa “alipokuwa akipumzika adhuhuri.”—4:5.
8. Yehova afanikishaje utawala wa Daudi juu ya Israeli yote?
8 Daudi mfalme katika Yerusalemu (5:1–6:23). Ingawa tayari amekwisha tawala akiwa mfalme katika Yuda kwa miaka saba na miezi sita, sasa Daudi awa mtawala asiyepingwa, na wawakilishi wa makabila wampaka mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli yote. Hii ni mara yake ya tatu kupakwa mafuta (1070 K.W.K.). Mojawapo wa vitendo vya kwanza vya Daudi akiwa mtawala wa ufalme wote ni kuteka ngome ya Sayuni katika Yerusalemu kutoka kwa Wayebusi waliojichimbia mahandaki, akiwashtua kupitia mtaro uliochimbwa chini ya ardhi. Kisha Daudi afanya Yerusalemu kuwa jiji kuu lake. Yehova wa majeshi abariki Daudi, akimfanya kuwa mkuu zaidi na zaidi. Hata Hiramu, mfalme tajiri wa Tiro, apelekea Daudi mierezi yenye thamani na pia wafanya kazi wajenge nyumba kwa ajili ya Mfalme. Familia ya Daudi yaongezeka, na Yehova afanikisha utawala wake. Kuna mapambano mawili zaidi pamoja na Wafilisti wapenda vita. Katika la kwanza, Yehova apita katikati ya adui kwa ajili ya Daudi kule Baal-perasimu, akimpa ushindi. Katika lile la pili, Yehova afanya mwujiza mwingine kwa kufanyiza “sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi,” kuonyesha kwamba Yehova anatangulia Israeli akafagie majeshi ya Wafilisti. (5:24) Ni ushindi mwingine wenye kutokeza kwa ajili ya majeshi ya Yehova!
9. Eleza matukio yanayokamatana na kuleta Sanduku hadi Yerusalemu.
9 Akiambatana na wanaume 30,000, Daudi afunga safari ya kuleta sanduku la agano kutoka Baale-yuda (Kiriath-yearimu) hadi Yerusalemu. Likiwa linaletwa kwa muziki wa heko na kushangilia, mkokoteni ambao juu yao limepandishwa watetereka, naye Uza, anayetembea kando, anyoosha mkono aliimarishe Sanduku takatifu. “Ndipo hasira ya BWANA [Yehova, NW] ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake.” (6:7) Sanduku hilo laja kupumzika penye nyumba ya Obed-edomu, na miezi mitatu ifuatayo, Yehova abariki sana nyumba ya Obed-edomu. Baada ya miezi mitatu Daudi aja kuchukua Sanduku katika njia inayoifaa safari inayobaki. Kwa kelele ya shangwe, muziki, na kucheza dansi, Sanduku laletwa ndani ya mji mkuu wa Daudi. Daudi afungulia shangwe yake kubwa kwa kucheza dansi mbele ya Yehova, lakini mke wake Mikali apinga hilo. Daudi asisitiza: “Mimi nitacheza mbele za BWANA [Yehova, NW].” (6:21) Kama tokeo Mikali abaki bila mtoto hadi kifo chake.b
10. Kisha uangalifu wetu wavutwa kwenye agano na ahadi gani ya Yehova?
10 Agano la Mungu pamoja na Daudi (7:1-29). Sasa twaja kwenye mojawapo matukio ya maana zaidi katika maisha ya Daudi, ambalo lakamatana moja kwa moja na habari kuu ya Biblia, kutakaswa kwa jina la Yehova kupitia Ufalme chini ya Mbegu aliyeahidiwa. Tukio hilo latokana na tamaa ya Daudi ya kujenga nyumba kwa ajili ya sanduku la agano la Mungu. Yeye mwenyewe akiwa anaishi katika nyumba maridadi ya mierezi, adokezea Nathani tamaa yake ya kujenga nyumba kwa ajili ya sanduku la agano la Yehova. Kupitia Nathani, Yehova ahakikishia Daudi tena juu ya fadhili za upendo Zake kuelekea Israeli na afanya agano pamoja naye litakaloendelea kwa wakati wote. Hata hivyo, haitakuwa Daudi bali mbegu yake ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina la Yehova. Kuongezea hilo, Yehova afanya ahadi hii ya upendo: “Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.”—7:16.
11. Daudi aeleza shukrani kwa sala gani?
11 Kwa kuzidiwa na wema wa Yehova, kama ulivyoonyeshwa kupitia agano hilo la Ufalme, Daudi amimina shukrani zake kwa ajili ya fadhili zote za upendo za Mungu kwa maneno haya: “Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya? . . . Nawe, BWANA [Yehova, NW], umekuwa Mungu wao.” (7:23, 24) Kwa bidii asali kwa ajili ya utakaso wa jina la Yehova na kwa ajili ya nyumba ya Daudi iimarike thabiti mbele Zake.
12. Daudi apigana vita vipi, na ni fadhili gani anazoonyesha nyumba ya Sauli?
12 Daudi apanua utawala wa Israeli (8:1–10:19). Hata hivyo, Daudi haachwi atawale katika amani. Vita vingali vitapigwa. Daudi achukua hatua ya kupiga dharuba Wafilisti, Wamoabi, Wasoba, Washami, na Waedomi, akipanua mipaka ya Israeli hadi kwenye vipimo vilivyowekwa rasmi na Mungu. (2 Sam. 8:1-5, 13-15; Kum. 11:24) Kisha ageuza uangalifu wake kwa nyumba ya Sauli kusudi kwamba kwa ajili ya Yonathani, aonyeshe fadhili za upendo kwa yeyote aliyesalia. Siba, mtumishi wa Sauli, aelekeza fikira zake kwa mwana mmoja wa Yonathani, Mefiboshethi, ambaye ni kilema. Bila kukawia, Daudi ataka mali zote za Sauli apewe Mefiboshethi na kwamba ardhi yake ilimwe na Siba na watumishi wake wafanye matayarisho ya chakula kwa nyumba ya Mefiboshethi. Hata hivyo, Mefiboshethi mwenyewe atakula kwenye meza ya Daudi.
13. Ni kupitia kwa ushindi gani mbalimbali zaidi Yehova aonyesha kwamba yupo pamoja na Daudi?
13 Mfalme wa Amoni afapo, Daudi atuma wajumbe kwa Hanuni mwana wake pamoja na wonyesho wa fadhili za upendo. Hata hivyo, washauri wa Hanuni, washtaki Daudi amewatuma wapeleleze nchi, na kwa hiyo wawavunjia heshima na kuwarudisha wakiwa nusu-uchi. Kwa kukasirishwa na tendo hilo la kuaibisha, Daudi atuma Yoabu pamoja na jeshi lake akalipe kisasi. Akigawanya majeshi yake, akimbiza kirahisi Waamoni na Washami waliokuja kuwasaidia. Washami wakusanya tena majeshi yao, lakini washindwa tena na majeshi ya Yehova chini ya amri ya Daudi na wapata hasara ya wapanda-magari-farasi ya vita 700 na wapanda-farasi 40,000. Huu ni ushuhuda zaidi wa kibali na baraka ya Yehova juu ya Daudi.
14. Daudi atenda dhambi zipi kuhusiana na Bath-sheba?
14 Daudi amtenda Yehova dhambi (11:1–12:31). Masika yanayofuata kwa mara nyingine Daudi atuma Yoabu kuingia Amoni na kuzingira Raba, huku yeye mwenyewe akibaki Yerusalemu. Jioni moja akiwa juu ya dari yake, apata kumwona Bath-sheba mzuri, mke wake Uria Mhiti, akioga. Akimleta kwenye nyumba yake, afanya ngono naye, naye apata mimba. Daudi ajaribu kufunika hilo kwa kumrudisha Uria kutoka kwenye pigano kule Raba na kumwagiza aende kwenye nyumba yake akajiburudishe. Hata hivyo, Uria akataa kujipendeza mwenyewe kwa kufanya ngono pamoja na mke wake hali Sanduku na jeshi “wanakaa vibandani.” Kwa kufadhaika Daudi amtuma Uria arejee kwa Yoabu pamoja na barua yenye kusema: “Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe, akafe.” (11:11, 15) Kwa njia hiyo Uria afa. Baada ya kipindi cha kuomboleza cha Bath-sheba kwisha, bila kukawia Daudi ampeleka nyumbani mwake, ambamo awa mke wake, na mtoto wao, mwana, azaliwa.
15. Nathani atamkaje hukumu ya kiunabii juu ya Daudi?
15 Hilo ni baya machoni pa Yehova. Yeye atuma nabii Nathani kwa Daudi akiwa na ujumbe wa hukumu. Nathani amwambia Daudi juu ya mwanamume fulani tajiri na mwanamume fulani maskini. Yule mmoja alikuwa na kondoo wengi, lakini yule mwingine alikuwa na mwana-kondoo mmoja wa kike, aliyelelewa katika familia “akawa kwake kama binti.” Hata hivyo, ilipowadia kufanya karamu, mwanamume yule tajiri alichukua, si kondoo kutoka kwa makundi yake mwenyewe, bali mwana-kondoo wa kike wa yule mwanamume maskini. Akifoka kwa hasira kwa kusikia hilo, Daudi atamka hivi: “Aishivyo BWANA [Yehova, NW], mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa!” Nathani ajibu kwa maneno haya: “Wewe ndiwe mtu huyo!” (12:3, 5, 7) Kisha atangaza hukumu ya kiunabii kwamba wake wa Daudi watanajisiwa hadharani na mwanamume mwingine, kwamba nyumba yake itapigwa na vita vya kindani, na kwamba mtoto wake kupitia Bath-sheba atakufa.
16. (a) Ni maana zipi zinazoambatana na majina ya mwana wa pili wa Daudi kupitia Bath-sheba? (b) Tokeo la mwisho la shambulizi juu ya Raba ni nini?
16 Kwa majonzi na toba ya moyo mweupe, Daudi akiri hivi waziwazi: “Nimemfanyia BWANA [Yehova, NW] dhambi.” (12:13) Kwa kutimiza neno la Yehova, mzao wa muungano huo wa uzinzi afa baada ya maradhi ya siku saba. (Baadaye, Daudi apata mwana mwingine kupitia Bath-sheba; huyu wamwita Sulemani, jina ambalo latokana na shina linalomaanisha “amani.” Hata hivyo, Yehova atuma kupitia Nathani aitwe Yedidia pia, maana yake “Mpendwa wa Yah.”) Kufuatia tukio hilo lenye kutikisa nafsi yake, Daudi aitwa na Yoabu aende Raba, ambako shambulizi la mwisho latayarishwa. Akiisha kuteka chanzo cha maji ya jiji hilo, kwa heshima Yoabu amwachia mfalme heshima ya kuliteka jiji lenyewe.
17. Ni matata gani ya kindani yanayoanza kupata nyumba ya Daudi?
17 Magumu ya kinyumbani ya Daudi (13:1–18:33). Matata ya nyumba ya Daudi yaanza wakati Amnoni, mmojawapo wa wana wa Daudi, apenda kimahaba Tamari, dada ya ndugu-nusu yake Absalomu. Amnoni asingizia maradhi na kuuliza kwamba Tamari mrembo atumwe amtunze. Amnajisi kisha aja kumchukia mno, hata kwamba amfukuza bila heshima. Absalomu afanya mpango wa kulipa kisasi, akisubiri. Miaka miwili hivi baadaye, atayarisha karamu ambayo Amnoni na wana wengine wote wa mfalme wamealikwa. Moyo wa Amnoni uwapo mchangamfu kwa mvinyo, amrukia ghafula na auawa kwa amri ya Absalomu.
18. Absalomu arejeshwa kutoka uhamishoni kupitia udanganyifu gani?
18 Akihofu hasira ya mfalme, Absalomu atorokea Geshuri, ambako aishi katika hali ya kuwa nusu uhamishoni kwa miaka mitatu. Wakati ule ule, Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, atunga hila ya kuleta upatanisho baina ya Daudi na Absalomu. Apanga mwanamke mwenye hekima wa Tekoa amtokezee mfalme hali ya kujitungia kuhusu kulipa kisasi, kupelekwa uhamishoni, na adhabu. Mfalme apitishapo hukumu, mwanamke huyo afunua sababu ya kweli ya kuwapo kwake, kwa kuwa mwana wa mfalme mwenyewe Absalomu yuko uhamishoni katika Geshuri. Daudi atambua kwamba Yoabu amepanga hilo lakini atoa ruhusa mwana wake arejee Yerusalemu. Miaka miwili zaidi yapita kabla ya mfalme kukubali kuonana uso kwa uso na Absalomu.
19. Ni njama gani inayojitokeza wazi, na tokeo lawa nini kwa Daudi?
19 Ijapokuwa fadhili za upendo za Daudi, upesi Absalomu afanya njama ya kunyakua kiti cha enzi kutoka kwa baba yake. Absalomu ana sura nzuri sana miongoni mwa wanaume wote mashujaa wa Israeli, na hilo lazidisha kujitakia makuu na kiburi chake. Kila mwaka nywele zilizonyolewa kwenye kichwa chake chenye nywele nyingi zina uzito wa kilo 2.3 hivi. (2 Sam. 14:26, NW, kielezi-chini) Kwa mbinu mbalimbali za ujanja, Absalomu aanza kuiba mioyo ya wanaume wa Israeli. Mwishowe, njama yajitokeza wazi. Akiwa na ruhusa ya baba yake ya kwenda Hebroni, Absalomu atangaza kusudi lake la uasi na kuomba tegemezo la Israeli wote katika maasi hayo juu ya Daudi. Hesabu kubwa wamiminikapo upande wa mwana wake mwasi, Daudi atoroka Yerusalemu akiambatana na waungaji-mkono wachache wenye uaminifu-mshikamanifu, mfano wa Itai Mgiti, anayejulisha rasmi hivi: “Aishivyo BWANA [Yehova, NW], na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumwa wako!”—15:21.
20, 21. (a) Ni matukio gani yanayotokea wakati wa kutoroka kwa Daudi, na unabii wa Nathani watimizwaje? (b) Ahithofeli msaliti afikiaje mwisho wake?
20 Akiwa anatoroka kutoka Yerusalemu, Daudi apata kujua juu ya usaliti wa mmojawapo wa washauri wake wenye kutumainiwa zaidi, Ahithofeli. Asali hivi: “Ee BWANA [Yehova, NW], nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili!” (15:31) Sadoki na Abiathari, makuhani wenye uaminifu-mshikamanifu kwa Daudi, na Hushai Mwarki watumwa kurudi Yerusalemu wapeleleze na kuripoti juu ya utendaji wa Absalomu. Wakati ule ule, katika nyika, Daudi akutana na Siba, mtumishi wa Mefiboshethi, anayeripoti kwamba bwana yake sasa atazamia ufalme urudishwe kwa nyumba ya Sauli. Daudi aendeleapo na safari, Shimei, wa nyumba ya Sauli, amlaani na kumrushia mawe, lakini Daudi azuia wanaume wake wasilipe kisasi.
21 Kule Yerusalemu, baada ya kudokezewa na Ahithofeli, Absalomu mnyakuaji utawala afanya ngono na masuria wa baba yake “machoni pa Israeli wote.” Huo ni utimizo wa hukumu ya kiunabii ya Nathani. (16:22; 12:11) Pia, Ahithofeli amshauri Absalomu atwae jeshi la wanaume 12,000 na kumwinda Daudi katika nyika. Hata hivyo, Hushai, ambaye amefikia kutumainiwa na Absalomu, apendekeza mwendo tofauti. Na sawa na alivyokuwa amesali Daudi, shauri la Ahithofeli lavunjwa. Kama Yuda, Ahithofeli aliyevurugika aenda nyumbani na kujinyonga mwenyewe. Hushai aripoti mipango ya Absalomu kisiri-siri kwa Sadoki na Abiathari, ambao, nao wapokeza Daudi ujumbe huo katika nyika.
22. Ushindi wa Daudi wachanganyika na huzuni gani?
22 Hilo lawezesha Daudi avuke Yordani na kuchagua kituo cha pigano katika msitu kule Mahanaimu. Huko aweka majeshi yake na kuwaamuru watendee Absalomu kwa uanana. Waasi hao washindwa kabisa. Absalomu akiwa anatoroka juu ya nyumbu kupitia msitu wenye miti mingi, kichwa chake chakamatwa katika matawi ya chini ya mti mkubwa, na hapo aning’inia hewani. Akimkuta katika balaa hiyo, Yoabu amwua, kwa kupuuza kabisa amri ya mfalme. Huzuni kubwa ya Daudi asikiapo juu ya kifo cha mwana wake yaonyeshwa na ombolezo hili: “Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! mwanangu Absalomu! laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!”—18:33.
23. Ni mipango gani inayotia alama kurejea kwa Daudi akiwa mfalme?
23 Matukio ya kumalizia ya utawala wa Daudi (19:1–24:25). Daudi aendelea kuomboleza kwa uchungu hadi Yoabu amhimiza arudie cheo kilicho haki yake akiwa mfalme. Sasa amweka Amasa kuwa mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Arejeapo, akaribishwa na watu, kutia na Shimei, ambaye Daudi aponya maisha yake. Mefiboshethi pia aja kueleza kesi yake, na Daudi ampa urithi unaotoshana na wa Siba. Kwa mara nyingine, Israeli na Yuda wote waungana chini ya Daudi.
24. Ni matukio gani zaidi yanayotokea kuhusu kabila la Benyamini?
24 Hata hivyo, kungali na matata yanayokuja. Sheba, Mbenyamini, ajitangaza rasmi kuwa mfalme na akengeusha wengi kutoka kwa Daudi. Amasa, aliyeagizwa na Daudi akusanye wanaume akomeshe uasi huo, akutana na Yoabu na kuuawa kwa hila. Kisha Yoabu achukua mamlaka juu ya jeshi na kufuatia Sheba kwenye jiji la Abeli wa Bethmaaka na kuuzingira. Wakitii shauri la mwanamke mwenye hekima wa jiji hilo, wakaaji walo wamwua Sheba, na Yoabu aondoka. Kwa sababu Sauli alikuwa amewaua Wagibeoni na hatia ya damu ilikuwa haijalipizwa bado, kwawa na njaa kali ya miaka mitatu katika Israeli. Ili kuondoa hatia hiyo ya damu, wana saba wa nyumba ya Sauli wauawa. Baadaye, katika pigano pamoja na Wafilisti tena, uhai wa Daudi waponyolewa chupuchupu na Abishai mpwa wake. Wanaume wake waapa kwamba lazima asiende tena kwenye pigano pamoja nao “usije ukaizima taa ya Israeli!” (21:17) Ndipo watatu wa wanaume wake hodari wanapopiga dharuba kwa njia ya kutokeza majitu Wafilisti.
25. Ni nini yanayosemwa katika nyimbo za Daudi zinazofuata kuandikwa?
25 Kufikia hapa, mwandikaji akatiza simulizi hilo kwa wimbo wa Daudi kwa Yehova, unaolingana na Zaburi 18 na kueleza shukrani kwa ajili ya kukombolewa “mikononi mwa adui zake zote, na mkononi mwa Sauli.” Kwa shangwe ajulisha rasmi hivi: “BWANA [Yehova, NW] ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu. Ampa mfalme wake wokovu mkuu; amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake, hata milele.” (22:1, 2, 51) Ufuatao ni wimbo wa mwisho wa Daudi, ambao katika huo akiri hivi, “Roho ya BWANA [Yehova, NW] ilinena ndani yangu, na neno lake likawa ulimini mwangu.”—23:2.
26. Ni nini kinachoelezwa kuhusu wanaume hodari wa Daudi, naye aonyeshaje heshima kwa ajili ya damu yao ya uhai?
26 Tukirejea kwenye maandishi ya kihistoria, twapata orodha ya wanaume hodari wa Daudi, watatu wao wakiwa wenye kutokeza. Wao wahusika katika kisa kinachotukia wakati kituo cha Wafilisti kimesimamishwa katika Bethlehemu, mji wa nyumbani kwa Daudi. Daudi aeleza tamaa hii: “Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!” (23:15) Kwa sababu ya hilo, wanaume hao watatu hodari waingia kwa nguvu katika kambi hiyo ya Kifilisti, wateka maji kwenye kisima hicho, na kuyapeleka kwa Daudi. Lakini Daudi akataa kuyanywa. Badala yake, ayamwaga kwenye ardhi, akisema: “Hasha, BWANA [Yehova, NW], nisifanye hivi; je! si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao?” (23:17) Kwake maji hayo ni sawa na damu ya uhai ambayo wamehatirisha ili kuyateka. Kisha wanaume 30 hodari zaidi wa jeshi lake na matendo yao waorodheshwa.
27. Ni dhambi gani ya mwisho anayofanya Daudi? Tauni inayosababishwa yakomeshwaje?
27 Mwishowe, Daudi atenda dhambi kwa kuhesabu watu. Akisihi rehema za Yehova, apewa uchaguzi baina ya adhabu tatu: miaka saba ya njaa, miezi mitatu ya kushindwa kwa kijeshi, au siku tatu za tauni katika bara. Daudi ajibu: “Basi sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA [Yehova, NW]; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.” (24:14) Tauni hiyo ya taifa lote yaua watu 70,000, ikisimamishwa tu wakati Daudi, akitenda kulingana na maagizo ya Yehova kupitia Gadi, anunuapo sakafu ya kupepetea ya Arauna, ambapo atoa dhabihu za kuteketeza na dhabihu za shirika kwa Yehova.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
28. Ni maonyo gani yenye kutokeza yaliyomo katika Samweli wa Pili?
28 Kuna mengi yanayopatikana katika Samweli wa Pili ambayo ni yenye mafaa kwa msomaji wa kisasa! Karibu kila hisia-moyo ya kibinadamu inapatikana humo kwa uhalisi kamili wa maishani. Kwa hiyo, twaonywa kwa lugha yenye kutokeza juu ya matokeo yenye maafa ya kunia makuu na kulipa kisasi (3:27-30), juu ya kutamani isivyofaa mwenzi wa ndoa wa mwingine (11:2-4, 15-17; 12:9, 10), juu ya kitendo cha usaliti (15:12, 31; 17:23), juu ya upendo unaotegemea nyege tu (13:10-15, 28, 29), juu ya kuamua haraka-haraka (16:3, 4; 19:25-30), na juu ya kutoheshimu matendo ya ujitoaji ya mtu mwingine.—6:20-23.
29. Ni vielelezo gani bora vya mwenendo na matendo yanayofaa vinavyopatikana katika Samweli wa Pili?
29 Hata hivyo, mafaa yaliyo makuu zaidi katika Samweli wa Pili yapatikana katika ule upande chanya, kutii vielelezo vingi vyacho bora juu ya mwenendo na matendo yanayofaa. Daudi ni kiolezo katika ujitoaji wake kwa Mungu (7:22), unyenyekevu wake mbele za Mungu (7:18), kutukuza kwake jina la Yehova (7:23, 26), maoni yake yanayofaa chini ya hali zenye msiba (15:25), toba yake ya moyo mweupe ya dhambi (12:13), uaminifu wake kwa ahadi yake (9:1, 7), kuendelea kwake kuwa na usawaziko chini ya jaribu (16:11, 12), utegemeo wake wenye kudumu juu ya Yehova (5:12, 20), na heshima yake kubwa kwa ajili ya mipango ya Yehova na wale aliowaweka kwenye vyeo (1:11, 12). Si ajabu kwamba Daudi aliitwa ‘mtu aupendezaye moyo wake Yehova’!—1 Sam. 13:14.
30. Ni kanuni gani zinazotumiwa na kutolewa vielezi katika Samweli wa Pili?
30 Matumizi ya kanuni nyingi za Biblia yapatikana pia katika Samweli wa Pili. Miongoni mwazo ni kanuni za daraka la jumuiya (2 Sam. 3:29; 24:11-15), kwamba madhumuni mema hayabadili matakwa ya Mungu (6:6, 7), kwamba ukichwa katika mpango wa kitheokrasi wa Yehova wapasa kuheshimiwa (12:28), kwamba damu yapasa kuonwa kuwa takatifu (23:17), kwamba upatanisho wahitajiwa kwa ajili ya umwagaji wa damu (21:1-6, 9, 14), kwamba mwenye hekima aweza kuepusha wengi wasipatwe na maafa (2 Sam. 20:21, 22; Mhu. 9:15), na kwamba uaminifu-mshikamanifu kwa tengenezo la Yehova na wawakilishi walo lazima udumishwe “ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi.”—2 Sam. 15:18-22.
31. Samweli wa Pili chatoaje mimweko ya kimbele ya Ufalme wa Mungu, kama inavyothibitishwa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo?
31 La maana zaidi ya yote, Samweli wa Pili chaelekeza kwenye Ufalme wa Mungu na kutoa mimweko miangavu ya kimbele juu yao, ambao asimamisha mikononi mwa “mwana wa Daudi,” Yesu Kristo. (Mt. 1:1) Kiapo ambacho Yehova alitoa kwa Daudi kuhusu udumifu wa ufalme wake (2 Sam. 7:16) chatajwa kwenye Matendo 2:29-36 kwa kurejezea Yesu. Kwamba unabii, “Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu” (2 Sam. 7:14), ulielekeza hasa kwa Yesu yaonyeshwa na Waebrania 1:5. Hilo lilithibitishwa pia na sauti ya Yehova akinena kutoka mbinguni: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” (Mt. 3:17; 17:5) Mwishowe, agano la Ufalme pamoja na Daudi larejezewa na Gabrieli katika maneno yake kwa Mariamu kuhusu Yesu: “Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana [Yehova, NW] Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:32, 33) Jinsi ahadi ya Mbegu ya Ufalme inavyokuwa yenye kusisimua wakati kila hatua ya kusitawi kwayo inavyofunuka mbele ya macho yetu!
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 745-7.
b Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 373-4.