Wakati wa Kungojea kwa Uvumilivu
Katika karne ya nane K.W.K. hali yenye kusikitisha ilikuwako kati ya Waisraeli. Nabii Mika alitangaza hivi: “Ole wangu! maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa hari, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye akili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao inayashika mabaya wayatende kwa bidii; mtu aomba rushwa, [hakimu] yu tayari kuipokea; mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye akili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma.”—Mik. 7:1-4.
Kwa wazi Mika anajisema kama kwamba yeye ni taifa zima. Taifa hilo lilifanana na shamba la matunda au shamba la mizabibu ambalo toka hilo matunda yamekusanywa. Hakuna shada la zabibu linalobaki. Hakuna hata tini moja la mapema linalotamanika. Ulinganifu huo ulifaa kwa sababu ilikuwa vigumu kuona watu washikamanifu na wanyofu. Wengi walikuwa wakiwinda damu ya wanadamu wenzao. Kulikuwako mashindano makali sana. Hakukuwako kufikiria hali njema ya wengine. Upendo ulikosekana kabisa. Ili waendeleze makusudi yao wenyewe, watu walipanga kuwatega wenzao, wakiwawinda kana kwamba kwa wavu. Mikono yao ilitumiwa kabisa kutenda mabaya. Walijionyesha kuwa mafundi sana katika hilo, ‘walifanya vizuri.’
Jamii ya watu ilikuwa imeharibika sana katika mwenendo wake mwema. Wakuu au viongozi wa taifa hilo ‘waliomba rushwa,’ wakitafuta kwa pupa wapewe zawadi. Mahakimu walipokea mahongo nao wakapotosha haki ya hukumu. Matajiri na watu wa vyeo walisema walivyotaka, nao mahakimu wakakubaliana na tamaa zao. Katika njia hiyo, wakuu, mahakimu na watu wengine wenye vyeo walishirikiana pamoja katika mpango mbaya, ‘wakiufuma pamoja.’ Hata watu wema kati yao walikuwa kama mbigili unaochoma au kama boma la michongoma. Mbigili na boma lenye michongoma inaweza kupasua mavazi na kuchoma mwili wa mtu anayepita karibu yake kwa maumivu sana. Vivyo hivyo, watu wasiotii sheria waliokuwa katika wakati wa Mika walikuwa na hila, wenye kuchoma kama miiba na kuumiza. Kwa sababu ya hali hiyo yenye kusikitisha, Mika aliweza kuwaambia Waisraeli hivi: “Hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwako.” (Mik. 7:4) “Walinzi” hao walikuwa manabii. Basi, ‘siku hiyo ya walinzi’ inaweza kumaanisha wakati ambapo Yehova angewachukulia hatua waovu hao, kwa kutimiza yaliyokuwa yametangazwa na manabii. Kule kutekelezwa kwa hukumu ya Yehova ‘kungewafadhaisha’ au kuwatatiza waasi hao wa sheria.
Ufisadi huo ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba hakuna hata uhusiano wo wote wa jamaa uliounganisha watu katika vifungo vya upendo. Kwa hiyo, huyo nabii aliweza kuwaambia Waisraeli wenzake kwa maneno haya: “Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako [yaani, angalia usemayo] ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe.”—Mik. 7:5, 6.
Ebu fikiria, rafiki za mtu—mke wake, baba yake, mama yake na watoto wake hawangeweza kumwamini. Yeye angekuwa na adui katika nyumba yake mwenyewe.
Hali kama hiyo haingeweza kuendelea. Ilitaka Mungu wa haki ya hukumu, yaani, Yehova, achukue hatua. Kabla ya yeye kufanya hivyo, nia ya kungojea ingetakiwa. Nabii anaeleza hivi: “Lakini mimi, nitamtazamia [Yehova]; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia.”—Mik. 7:7.
Imetupasa sisi vilevile leo, tuwe na nia ya kumngojea Yehova Mungu kwa uvumilivu, achukue hatua juu ya udhalimu wote. Hukumu yake kali juu ya taratibu hii ya mambo itatekelezwa sawasawa na alivyowahukumu Waisraeli waasi, na hilo atafanya upesi sana!