Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 5/15 kur. 12-17
  • Mzabibu Unaotoa Divai Inayofurahisha Mungu na Mwanadamu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mzabibu Unaotoa Divai Inayofurahisha Mungu na Mwanadamu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UHITAJI WA “MZABIBU” MPYA
  • KUPANDA NA KULIMIA
  • Kuzaa Matunda Kunakomtukuza Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • ‘Utunze Mzabibu Huu’!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
  • Kuonea Shangwe Uhusiano wa Karibu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Kuzaa Matunda Kama Matawi na Kuwa Rafiki za Yesu
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 5/15 kur. 12-17

Mzabibu Unaotoa Divai Inayofurahisha Mungu na Mwanadamu

“Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.”​—Yoh. 15:8, Habari Njema kwa Watu Wote.

1. Mwanamume anayejulikana sana ambaye Yohana mwana wa Zebedayo alikuwa mwenzake alijilinganishaje na mmea?

KWETU sisi leo huenda ikaonekana kuwa ajabu mtu akijilinganisha na mzabibu. Walakini hivyo ndivyo alivyofanya mtu aliyepata kujulikana zaidi duniani. Katika usiku ule aliopata kunywa divai kwa mara ya mwisho akiwa pamoja na wenzake washikamanifu, aliyatamka maneno haya ya maana sana: “Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi.” Mmoja wa wenzake, Yohana mwana wa Zebedayo, aliyasikia maneno hayo yenye kuamsha fikira, akayakumbuka na kuyaandika kwa ajili yetu.​—Yoh. 15:1, 5, Habari Njema kwa Watu Wote.

2, 3. (a) Kulingana na mfano uliotolewa na Yothamu mwana wa Mwamuzi Gideoni, miti ya mfano iliiomba mimea gani iitawale bila kufaulu? (b) Uchaguzi wao wa mwisho ungekuwa na matokeo gani?

2 Mamia mengi ya miaka kabla ya hili mwanamume fulani katika nchi iyo hiyo alitoa mfano ambao katika huo alimlinganisha mwanamume fulani na mzabibu. Yeye, pia, maisha yake yalikuwa hatarini. Kama jambo la mwisho yeye alitoa mfano, akionyesha vile watu wanaojifanyia mfalme wangepatwa na msiba wa kitaifa kwa sababu ya kukosa kumchagua mtu anayefaa kuwa mfalme. Akiwalinganisha watu wake mwenyewe na miti, alifananisha namna hawa watafutaji wa mtawala walivyouomba mti mzeituni kwanza kisha wakauomba mti mtini, walakini miti hii yenye kuzaa matunda ilikataa.

3 “Kisha,” akaendelea kusema Yothamu, mwana peke yake aliyeokoka wa Mwamuzi Gideoni wa Israeli, “miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?” Baada ya kukataa huku kwa mara ya tatu, miti hiyo ya mfano ilijiona kuwa na wajibu wa kuomba mti wa miiba usiozaa uwe mfalme juu yao. (Amu. 9:3-14) Kwa sababu ya uchaguzi huu mbaya wa mtawala, Yothamu alionyesha kwamba hawatakunywa divai ya furaha kama ile ambayo ingetolewa na mzabibu wenye kuzaa.​—Amu. 9:15-20.

4. Muda mfupi kabla ya hapo Yesu alikuwa ameyatumia mazao ya mzabibu afananishe kitu gani, walakini, baadaye yeye aliyapaje maana yenye matumaini?

4 Kwa sababu hii, Yesu Kristo ambaye pia alikataliwa asiwe mfalme juu ya taifa la Israeli, hakuwa wa kwanza katika kufananisha mwanamume, yeye mwenyewe, na mzabibu. Alikuwa ndiyo amemaliza kuadhimisha ukumbusho wa kifo chake kilichokuwa kikikaribia, ambao katika huo alitumia divai iliyokuwa katika kikombe cha kawaida cha kunywea isimamie damu yake ambayo ingemwagwa alasiri iliyokuwa ikifuata. Walakini, ili aipe divai hiyo iliyokuwa mfano maana yenye matumaini, alisema hivi. “Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.” (Mt. 26:26-29) Sana sana divai mpya huchangamsha sana, nayo “divai” inayotumiwa ikiwa mpya katika ufalme wa Baba yake wa mbinguni bila shaka ingekuwa divai yenye kufurahisha.

5. Katika mfano wake wa mzabibu, ni kitu gani kinachoonyesha kama Yesu aliutumia umfananishe yeye peke yake au hapana?

5 Ukiwa usiku wa Sikukuu ya Kupitwa, divai ilikuwa nyingi, Wakinywa angawa vikombe vinne vya divai katika ushirika huu wa mwisho wa Yesu pamoja na wanafunzi wake katika mwaka 33 W.K. Ni jambo linalopatana na akili kwamba hii ilimwongoza atoe mfano mwingine mpya juu ya mzabibu. Walakini, katika mfano huu Yesu aliutumia mzabibu wote ufananishe zaidi yake mwenyewe. Ili aeleze waziwazi jambo hili, aliwaambia wanafunzi wake waaminifu hivi: “Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi.”​—Yoh. 15:5, Habari Njema kwa Watu Wote.

6. Kwa kuwa walikuwako mitume kumi na mmoja tu wakati huo, je! Yesu alimaanisha kwamba “mzabibu” huo ungekuwa na matawi kumi na moja tu, au sivyo, sana sana kwa sababu ya maneno yake katika Mathayo 21:43?

6 Kwa maneno hayo Yesu hakumaanisha kwamba “mzabibu” huu wa Kikristo ungekuwa na matawi kumi na moja tu, ili yalingane na mitume hao kumi na mmoja waaminifu waliokuwa wameketi mezani pamoja naye wakati huo. “Mzabibu” huo wa Kimasihi ungepata matawi mengi, mengi kutosha kufanyiza taifa zima jipya la Kikristo. Yesu alidokeza juu ya taifa hili jipya wakati alipowaambia wajumbe wa taifa lisiloamini la Kiyahudi hivi: “Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao [utapewa taifa] lingine lenye kuzaa matunda yake.”​—Mt. 21:43.

7. Ni taifa gani linalofananishwa na “mzabibu” katika Zaburi 80:​8-15, na ni kwa sababu gani Mungu alililiwa alifikirie?

7 Kufananisha taifa na mzabibu halikuwa jambo jipya. Baba ya mbinguni ya Yesu, Yehova, alitumia mmea huu kama mfano wa taifa. Kwa mfano, alimwongoza mwandikaji wa zaburi Asafu aseme na Yeye na kumwambia hivi: “[Wewe Yehova] ulileta mzabibu kutoka Misri [katika siku za Musa], ukawafukuza mataifa [kutoka Nchi ya Ahadi] ukaupanda. Ulitengeneza nafasi mbele yake, nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi. Milima ilifunikwa mbele kwa uvuli wake, . . . Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu. Na mche ule ulioupanda kwa mkono wako wa kuume.” (Zab. 80:8-15) Kwa kuwa Yerusalemu uliharibiwa katika mwaka 607 K.W.K. nazo Nyakati za Mataifa zikaanza wakati huo kwa mataifa ya kilimwengu kuitawala dunia, taifa la Israeli liliteswa sana na Mataifa hayo. Ndiyo sababu mwandikaji wa zaburi anamlilia Mungu awafikirie.

8. Yehova aliupanda ule “mzabibu” mpya wakati gani, naye Isaya 5:5-7 anaelezaje uhitaji wa hili?

8 Wakati Yehova alipomtia Yesu mafuta kwa roho takatifu baada ya kubatizwa katika Mto Yordani, “mzabibu” mpya ulipandwa. Kulikuwa na uhitaji mkubwa sana wa hili. Sababu gani? Zaidi ya miaka 700 kabla ya hapo nabii Isaya alikuwa ametabiri sababu yake. Yehova alimwongoza aseme hivi: “Na sasa, enyi, wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; . . . nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mibigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinye mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la [Yehova] wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kumpendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! alisikia kilio.”​—Isa. 5:3-7.

9. Baadaye katika siku za Yeremia, Yehova aliuliza ulizo gani juu ya “mzabibu” wake wa kitaifa?

9 Mambo katika Israeli hayakupata kuwa mazuri, bali, kama miaka 100 baadaye, Yehova aliwaambia Israeli hivi: “Zamani zilizopita mimi nalivunja nira yako [ya utumwa katika Misri] vipande vipande; nikavipasua vifungo vyako [vya kizuizi]. Lakini ulisema: ‘Mimi sitatumika,’ kwa maana juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi ulijilaza, ukifanya umalaya. Na kwa upande wangu, mimi nalikuwa nimekupanda ukiwa mzabibu mzuri sana mwekundu, wote ukiwa mbegu ya kweli. Sasa basi umegeukaje kwangu ukawa miche iliyoharibika ya mzabibu wa kigeni?”​—Yer. 2:20, 21 NW; Hos. 10:1, 2.

10. Kwa sababu shauri lingeondolewa katika Israeli, Kumbukumbu la Torati 32:​28-33 lilisema kwamba Israeli angekuwa “mzabibu” wa namna gani?

10 Ilikuwa kama vile Musa alivyotabiri huko nyuma katika mwaka 1473 K.W.K.: “Maana hawa ni taifa wasio shauri, wala fahamu hamna ndani yao. . . . Maana, mzabibu wao ni mzabibu wa Gomora nao ni mashamba ya Gomora; zabibu zao ni zabibu za uchungu, vichala vyao ni vichungu. Mvinyo yao ni sumu ya majoka, uchungu mkali wa nyoka.”​—Kum. 32:​28-33.

UHITAJI WA “MZABIBU” MPYA

11. Kulingana na mfano wa Yesu wa shamba la mizabibu, Masihi angetendwaje na wakulima katika wakati wa mavuno?

11 Wakati wa kuvuna “mzabibu” huu wa mfano wa kitaifa ulikuwa umekaribia wakati Yesu Mwana wa Mungu alipokuja akiwa ndiye mtiwa mafuta au Masihi, katika mwaka 29 W.K. Yeye akiwa wakili wa Mungu angevuna mazao gani kutoka katika “mzabibu” huu? Katika Nisani 11, 33 W.K., siku tatu kabla ya kumaliza huduma yake ya hadharani ya miaka mitatu na nusu, Yesu alitoa mfano akionyesha namna angepokewa. Akiuelekeza kwa makuhani wakuu na wazee katika hekalu kwa kutaja juu ya vipingamizi vyao juu ya utendaji wake na mafundisho yake, alisema hivi:

“Sikilizeni mfano mwingine, Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? . . .

“ . . . Hamkupata kusoma katika maandiko, jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa [Yehova] nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao [utapewa kwa taifa] lingine lenye kuzaa matunda yake. Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tiki-tiki.”​—Mt. 21:33-44.

12. Wakulima wa shamba la mizabibu la mfano la kitaifa walishindwa kutoa matunda ya namna gani, na kwa hiyo Mungu angehakikishaje kwamba angepata matunda ya namna inayofaa?

12 Wakulima hao Waisraeli wa “shamba la mizabibu” la kitaifa la Yehova walipaswa kumtolea Mwanawe Yesu Kristo matunda gani? Ilipaswa iwe imani katika Mwana akiwa Masihi wa kweli aliyeahidiwa na kumkubali kuwa Mwana wake Yeye aliyeupanda na aliye mwenyeji wa “shamba la mizabibu” la kitaifa la Israeli. Kama wangalimtolea Mwana wa Mungu matunda ya namna hiyo, matokeo yake yangekuwa kwamba wangaliingizwa katika ufalme wa kweli wa Kimashi wa Mungu. Kwa kuwa hawakutoa matunda yaliyopaswa kuuonyesha ufalme wa Mungu wa mfano katika Israeli, pendeleo la kuwa ufalme wa Mungu lingeondolewa kwao kama taifa. Kwa hiyo, taifa jingine la wakulima wa “shamba la mizabibu” lingeundwa. Taifa hili jipya lingetoa matunda yanayoufaa ufalme wa Mungu. Wakulima hao wangemtolea matunda aliyostahili Mpanzi na Mwenyeji wa Kimungu wa shamba hili ya mizabibu.

13. (a) Wakulima Wayahudi wa “shamba la mizabibu’’ walidhani wangeweza kufanyaje kwa kujitwalia urithi wa Mwana wa Mwenyeji? (b) Yesu alisema jambo gani lingelipata jiwe la kifalme lililokataliwa na waashi wa jengo?

13 Kwa Mungu, jambo la maana la kuamulia ni nani watakaojifurahisha mapendeleo ya ufalme wake wa Kimasihi ni “matunda.” Wakulima Wayahudi walidhani kwamba, kwa kukataa kutoa matunda yaliyotazamiwa na hata kwa kumwua Yesu “mrithi” wa ufalme wa Mungu, wangejitwalia urithi wake. Walidhani kwamba wangeendelea kuwa na utawala wa ufalme wa Mungu wa mfano, chini ya agano la torati ya Musa. (Yohana 11:47-53) Lakini sivyo, kulingana na vile tunavyoweza kuamua kutokana na mfano wa Yesu. (Mt. 21:41) Yesu alisema nini kwa habari ya Jiwe la kifalme lililokataliwa na waashi wa jengo la Mungu siku moja tu kabla yake kuingia Yerusalemu katika mwandamano akiwa amempanda mwana-punda? Lingefanywa kuwa jiwe kuu la pembeni katika jengo jipya la kifalme la Mungu, “ufalme wa Mungu” wa mbinguni.

14. Kwa sababu gani Yesu hakuliona kuwa jambo lisilo la maana kwake kutoa mfano wa mzabibu na matawi yake muda mfupi kabla ya kukamatwa kwake katika bustani ya Gethsemane?

14 Kwa habari ya “mzabibu wa kweli” ambao Yehova Mungu alikuwa amepanda na ambao alikuwa akilimia, Yesu alijua kwamba huo haungeweza kuuawa, ijapokuwa wakulima Wayahudi wa “mzabibu” wa mfano wa kitaifa waliruhusiwa wamwue baadaye katika Sikukuu ya Kupitwa. Kwa hiyo, ijapokuwa ilikuwa kabla tu ya kwenda katika bustani ya Gethsemane na kukamatwa, Yesu hakuliona kuwa jambo lisilo la maana kwake kuwapa wanafunzi wake mfano wa mzabibu na matawi yake.

15. Kulingana na Yohane 15:​1-5, ni nani mkulima wa “mzabibiu wa kweli,” naye huyafanyaje matawi kulingana na kama yanazaa matunda au hapana?

15 “Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika na nyinyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami nikiwa ndani yake, huyo huzaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya cho chote.”​—Yoh. 15:1-5, Habari Njema kwa Watu Wote.

KUPANDA NA KULIMIA

16, 17. (a) Yehova aliupanda huo “mzabibu wa kweli ‘ wakati gani, na kwa njia gani? (b) Yesu Kristo alikuwaje ndiye mkuu kuliko mzee wa ukoo Yakobo, nayo “matawi” yalitokezwa katika “mzabibu wa kweli” wakati gani?

16 Mkulima mkuu wa Mzabibu aliupanda mzabibu huu wenye kuzaa sana wakati gani? Ulikuwa mwaka 29 W.K., wakati Yesu aliyekuwa ndiyo amekwisha batizwa alipotiwa mafuta kwa roho Yake takatifu. (Isa. 61:​1, 2) Ndipo Yehova alipopanda shina la “mzabibu” wa mfano la ufalme wa Kimasihi. Tunakumbuka kwamba ufalme wa mfano wa Israeli ulitokana na mzee wa ukoo Yakobo aliyepewa jina Israeli. Alipata kuwa baba ya wana kumi na wawili, ambao katika hao yalitoka yale makabila kumi na mawili ya Israeli. (Matendo 7:8-14) Hivyo, Yesu Kristo alilingana na Yakobo.

17 Huyu Yakobo aliye Mkuu zaidi ndiye aliyekuwa shina la mzabibu. Aliwachagua mitume kumi na wawili waliotazamiwa kuwa “matawi” ya huu “mzabibu” wa kiroho. (Yohana 15:16; 6:70) Ndiyo sababu, katika usiku huo wa Sikukuu ya Kupitwa, aliwaita “matawi.” Walakini siku 51 baadaye, katika siku ya Pentekoste, mitume waaminifu kumi na wawili walitiwa mafuta kwa roho takatifu. Katika njia hiyo walipata kuwa misingi midogo kumi na miwili ya taifa jipya la Israeli wa kiroho. Juu yao umejengwa Yerusalemu Mpya wa mbinguni. (Ufu. 21:14; Efe. 2:20) Walakini, katika siku hiyo ya Pentekoste wengine wa kikundi hicho cha wanafunzi 120 walikuwa ndio wa kwanza kupokea roho takatifu na kuzungumza kwa lugha, na katika njia hiyo wao pia walifanywa kuwa “matawi” katika “mzabibu” huo wa kiroho, Yesu Kristo.

18. Ni nafasi gani ambayo Israeli wa asili hawakutumia kama ilivyoandikwa katika Kutoka 19:6, 7, naye Petro anayatumia maneno hayo ya kimungu juu ya nani?

18 Wakati huo, taifa hilo jipya la Israeli wa kiroho, likatokea. Israeli wa asili wakiwa kama taifa hawakutumia nafasi ambayo Yehova alikuwa ameweka mbele yao kupitia kwa mpatanishi Musa kama ilivyoandikwa katika Kutoka 19:6, 7. Kwa hiyo maneno ya tangazo hilo la kimungu yalitumiwa na mtume Petro juu ya washiriki wa taifa hilo jipya la Israeli wa kiroho. Wapi? Katika barua yake ya kwanza iliyoongozwa na Mungu, katika 1 Petro 2:9, 10, ambapo imeandikwa hivi: “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

19. Ni jambo gani lililotukia kwa taifa la Israeli wa kiroho, baada ya kutimizwa kwa maneno ya Isaya 5:5-7, na ni kwa sababu gani Yehova alilipa uangalizi ule ule aliokuwa amelipa “shamba la mizabibu” la, mfano la Israeli?

19 Kwa furaha, taifa la Kikristo la Israeli wa kiroho linaendelea kusitawi baada ya Yehova kutimiza maneno yake yenye kuonya juu ya “shamba la mizabibu” la mfano la Israeli wa asili, kama yalivyoandikwa katika Isaya 5:5-7. Akiwa ndiye Mlimiaji wa kile alichopanda, anayapa “matawi” ya “mzabibu wa kweli.” Yesu Kristo uangalizi unaohitajiwa, kama vile alivyoliangalia “shamba la mizabibu” la zamani la Israeli wa asili mpaka mwaka 33 W.K. Anafanya hivyo kusudi aweke kiasi fulani cha “matawi” safi, yenye kuzaa ambayo ni wanafunzi wa Yesu Kristo. Miche na miti iliyokufa haina sehemu kati ya matawi hayo yaliyo “safi.” Ndiyo sababu katika mfano wake, Yesu aliwaambia mitume wake waaminifu hivi: “Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni.”​—Yoh. 15:2, 3, Habari Njema kwa Watu Wote.

20. Yesu angeweza kuwatangaza wale mitume kumi na mmoja waaminifu kuwa “safi” kwa sababu ya kukubali nini, kulingana na habari iliyo katika Yohana 6:​67-69?

20 Yuda Iskariote, yule mtume msaliti hakuwapo wakati Yesu aliposema maneno hayo. Yesu alikuwa amekwisha mwachilia atoke katika ushirika wao baada ya chakula cha jioni cha Sikukuu ya Kupitwa. (Yohana 13:26-30) Wale mitume waaminifu kumi na mmoja waliobaki walikuwa wamelikubali neno lake au ujumbe Wa Kimasihi, na kwa sababu hiyo akawatangaza kuwa “safi.” Kwa mfano, katika upande wa kaskazini katika Kapernaumu, wakati Yesu alipowauliza mitume hao, “Je! ninyi mwataka kuondoka?” Simoni Petro alijibu: “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima Wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”​—Yohana 6:67-69.

21. Kwa hiyo, “matawi” hayo ya kimtume yalikuwa safi kutokana na mambo gani, nayo maneno ya Yesu yaliyosemwa kwao faraghani yalikuwa na matokeo gani kwao?

21 Kwa hiyo hakukuwa na vitawi vya kutoamini vilivyokauka katika mitume washikamanifu. Hakukuwa na miche yenye kuhangaisha ya mafundisho ya Kiyahudi yasiyo ya maandiko kati yao. Walikuwa wakitumikia kusudi la huyu “Mtakatifu wa Mungu” kwa nafsi yote. Walimwamini kuwa ndiye “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” (Mt. 16:16) Katika pindi nyingine, Petro alimwambia hivi: “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” (Mt. 19:27) Kwa sababu ya maamuzi kama hayo, maneno ya Yesu, sana sana yakisemwa kwa mitume faraghani, yalikuwa na matokeo yenye kusafisha, yakiwaacha katika hali iliyo “safi” kiroho. “Matawi” yote yaliyoendelea kukaa katika hali hiyo “safi” yalijitoa kabisa katika kusudi hilo la pekee la “mzabibu wa kweli” wa Yehova. Hiyo ingetokeza furaha kwa Mungu na wanadamu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki