Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 7/1 kur. 22-24
  • Ayubu—Kielelezo cha Mwenendo wa Utawa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ayubu—Kielelezo cha Mwenendo wa Utawa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “NALIMWOKOA MASKINI [ALIYEONEWA] “
  • MSIBA WATOKEA
  • “TUPATE MEMA MKONONI MWA MUNGU, NASI TUSIPATE NA MABAYA?”
  • KUVUMILIA “WAFARIJI WENYE MATATA”
  • AKUBALI KUSAHIHISHWA
  • Kitabu Cha Biblia Namba 18—Yobu
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Mtu Aliye Mfano Bora Ambaye Alikubali Kusahihishwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Ayubu Alivumilia—Hata Sisi Twaweza!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Ayubu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 7/1 kur. 22-24

Ayubu—Kielelezo cha Mwenendo wa Utawa

‘MTU yule ana subira kama ya Ayubu.’ Ni jambo la kawaida kusikia usemi huo hata leo. Masimulizi ya Biblia juu ya Ayubu yanafahamika ulimwenguni pote, na kuna sababu nzuri ya hilo. Kuhusu Ayubu, Mungu alisema hivi: “Hapana mtu aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na uelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.” (Ayubu 1:8; 2:4) Namna Biblia inavyomwonyesha Ayubu inatoa kielelezo cha mwenendo wa utawa unaofaa kuigwa.

Ayubu alikuwa akiishi Usi, kwa wazi sehemu ya nchi katika kaskazini ya Uarabu. Vifungu vingi vya maneno katika kitabu cha Ayubu vinaonyesha kwamba aliishi nyakati za wazee wa ukoo, pengine wakati Israeli ilipokuwa utumwani Misri. Kwa habari ya hali ya Ayubu maishani, twasoma hivi: “Walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng’ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”​—Ayubu 1:1-3.

Msingi wa mwenendo wa Ayubu usiolaumika na ulionyoka ulikuwa moyo mweupe wa mawazo, makusudi na tamaa. “Nilifanya agano na macho yangu,” akasema Ayubu. “Basi nawezaje kuwangalia msichana?” (Ayubu 31:1) Kwa kuwa mzee huyo wa ukoo alimpenda sana mke wake mwenyewe, lilikuwa jambo lisilowazika kwake ‘kuotea mlangoni pa jirani yake’ kusudi afanye uzinzi na mke wake mtu huyo. (Ayubu 31:9-12) Ingawa alikuwa tajiri sana, Ayubu alikataa kuweka uhakika wake katika utajiri. (Ayubu 31:24, 25) Kwa sababu ya uaminifu wake kwa Mungu, moyo wake haukuwa na nafasi ya ibada ya sanamu ya jua, mwezi na viumbe vingine vya kimbinguni ibada ambayo ilikuwa ya kawaida katika siku hizo.​—Ayubu 31:26-28.

“NALIMWOKOA MASKINI [ALIYEONEWA] “

Akiwa mmojawapo wa wazee walioketi kitako katika lango la mji ili kuangalia mambo ya mji, hakuwa na suto. Yeye anasimulia hivi:

“Nalimwokoa maskini aliyenililia; yatima naye, na yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia. Baraka yake yeye aliyekuwa karibu na kupotea ilinijia nikaufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha. Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa miguu kwa aliyechechemea. Nalikuwa baba kwa mhitaji, na daawa ya mtu nisiyemjua naliichunguza. Nami nilivunja taya za wasio haki, na kumpokonya mawindo katika meno yake.”‏ —Ayubu 29:12, 13, 15-17.

Hivyo, Ayubu alionyesha fadhili kama hizo katika kushughulika kipekee na watu mmoja mmoja. Watumishi wa nyumba yake walitendewa kama binadamu. (Ayubu 31:13-15) Walio fukara, wajane, yatima na wale wenye kuumia kwa sababu ya kuhitaji mambo ya lazima maishani walipata uwezo mwingi wa kuwategemeza katika Ayubu. (Ayubu 31:16-21) Kwa wale waliomtendea kwa uadui Ayubu hakulipa kisasi wala kuwatakia maovu yawapate.​—Ayubu 31:29, 30.

Hata hivyo, Ayubu anafahamika hasa kwa ajili ya sifa nyingine ya kimungu. Mwandikaji wa Biblia Yakobo anaitaja, akisema hivi: “Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa [Ayubu].” (Yak. 5:11, HNWW) Ayubu alijionyeshaje kuwa kielelezo cha uvumilivu wa kimungu?

MSIBA WATOKEA

Bila onyo la mbele, Ayubu alikumbwa na msiba. Ulikuja ukifuatana mmoja baada ya mwingine. Mzee huyo hakuweza kupata nafuu baada ya msiba kutokea kabla ya mwingine kutokea. Kwa kufuatana, alipoteza ng’ombe, punda wa kike, kondoo na ngamia kwa kikundi cha Waseba, umeme na Wakaldayo. (Ayubu 1:13-17) Kisha ikaja ripoti kwamba wana na mabinti wake wote walikuwa wameuawa.​—Ayubu 1:18, 19.

Wewe ungeonaje iwapo misiba kama hiyo ingekupata mmoja baada ya mwingine. Ni jambo la kusifika namna Ayubu alivyoitikia. Mahali pa kumkasirikia Mungu, yeye alitamka hivi: “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; [Yehova] alitoa, na [Yehova] ametwaa; jina la [Yehova] na libarikiwe.”​—Ayubu 1:21.

Lakini Ayubu angepaswa kuvumilia magumu zaidi. Kisha alipigwa kwa “majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.” (Ayubu 2:7, 8) Hali hii ya kuketi kwa majonzi ilikuwa kwa sababu ya mateso na huzuni nyingi. Akitaja juu ya hali yenye kuchukiza ya maradhi yake, Ayubu alitamka hivi: “Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? lakini usiku huwa mrefu; nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke. Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena.”​—Ayubu 7:4, 5.

“TUPATE MEMA MKONONI MWA MUNGU, NASI TUSIPATE NA MABAYA?”

Watu ambao hapo kwanza walivutiwa na Ayubu wakaanza kumgeuka kwa kumkataa kabisa. “Wakaao nyumbani kwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni.” (Ayubu 19:15) Kuhusu mke wake na ndugu zake, Ayubu alitangaza hivi: “Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, nami ni machukizo kwa ndugu zangu.”​—Ayubu 19:17.

Hata wahalifu na watu waliokataliwa na ujamii walimshutumu Ayubu. Akionyesha tofauti kubwa kati ya hali yake ya kwanza ya fanaka, Ayubu alitangaza hivi: “Nikakaa kama mkuu wao. Nikakaa kama mfalme katika jeshi la askari, mfano wa awafarijiye hao waombolezao. Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanyia mzaha, ambao baba zao niliwadharau hata kuwaweka na mbwa wa kundi langu. Na sasa nimekuwa wimbo wao [wa dhihaka], Naam, nimekuwa simo kwao. Wao hunichukia, na kujitenga nami, hawaachi kunitemea mate usoni.”​—Ayubu 29:25–30:1, 9, 10.

Mateso ya Ayubu yalikuwa makali sana hata kwamba akatamani kifo kiwe jambo la kumweka huru kutokana na mateso. “Laiti ungenificha kuzimuni [kaburi],” akapaza sauti “ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita, na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!”​—Ayubu 14:13.

Hata mke wa Ayubu alifikia hatua ya kumwambia hivi: “Ukufuru Mungu, ukafe.” (Ayubu 2:9) Walakini hata katika maumivu na huzuni nyingi Ayubu alikataa kuchukua ile ambayo ingeweza kuonekana kuwa ‘njia rahisi ya kutokea.’ Mahali pake, alimjibu mke wake hivi: “Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? —Ayubu 2:10.

Kulingana na habari ya Kimaandiko, misiba yote hiyo Ayubu aliletewa na Shetani Ibilisi kwa ruhusa ya Mungu. Shetani alidai kwamba kupenda sana ufanisi wa mali ndiko peke yake kulikomwongoza Ayubu amche Mungu. Ibilisi alitoa shtaka kwamba iwapo Mungu ‘angenyosha mkono wake’ juu ya Ayubu, kwa kufanya mambo yawe mabaya kwake, yeye ‘angemkufuru Mungu mbele ya uso wake.’ (Ayubu 1:11; 2:4, 5) Lakini katika jambo hilo Ibilisi alithibitishwa kuwa mwongo.

KUVUMILIA “WAFARIJI WENYE MATATA”

Jaribu la uvumilivu wa Ayubu lingekuwa kubwa zaidi. Yeye alitembelewa na wenzi watatu, Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi na Sofarj Mnaamathi. Inaelekea walikuja ‘kumlilia Ayubu na kumtuliza.’ (Ayubu 2:11) Lakini ziara hiyo haikuwa ya kufariji kamwe. Wenzi hao walisisitiza kwamba ugonjwa wa Ayubu ulikuwa adhabu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya dhambi nzito. (Ayubu 4:7-9; 8:11-19; 20:4-29; 22:7-11) Kwa maoni ya Elifazi, Bildadi na Sofari, hali za mtu, ziwe ni za kufanikiwa au mkasa, ni wonyesho wa kufaa kwa mtu kiadili. Wao walisadiki kwamba maradhi ya Ayubu yalikuwa ushuhuda wa kwamba mwenendo wake ulikuwa wa kulaumika na kwamba apaswa kutubu.

Ayubu hakupata faraja yo yote kutokana na mashtaka yao ya uongo. “Nimesikia mambo mengi kama hayo. Ninyi nyote ni wafariji wenye matata! . . . Iwapo nafsi yenu ingekuwa panapo nafsi yangu, je! ningekuwa mwerevu katika kuwapinga ninyi kwa maneno, na je! ningewatikisia ninyi kichwa changu? Ningewatieni nguvu kwa maneno ya kinywa changu.”​—Ayubu 16:2, 4, 5, NW.

Mzee huyo wa ukoo mwaminifu alinena waziwazi kwa kukataa maoni ya kwamba watu wenye haki huishi wakati wote katika fanaka na bila masumbufu hali waovu wakati wote wanataabika na kupungukiwa na vitu na kupatwa na maradhi. Yeye aliuliza hivi: “Mbona waovu wanaishi, na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu? Kizazi chote kinathibitika nao machoni pao, na wazao wao mbele ya macho yao. Nyumba zao zi salama pasina hofu, wala fimbo ya Mungu haiwapigi. Fahali wao [waovu] huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; ng’ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba.”​—Ayubu 21:7-10; tazama pia mistari 29-31 na Zaburi 73:1-14.

Kwa kuwa shtaka la Ibilisi kwamba Ayubu angemlaani Mungu msiba ukitokea halikujulikana na mzee huyo wa ukoo, alifadhaishwa na badiliko la ghafula la hali. Hivyo, pindi fulani Ayubu alihangaikia sana kutetea ukamilifu wake mwenyewe. Kwa mfano, alipokuwa amekazwa sana na maono ya ndani Ayubu alipaza sauti hivi:

“Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; sitajizuia na kuugua kwangu; nitanena kwa uchungu wa roho yangu. Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa; nionyeshe sababu ya wewe kushindana nami. Je! ni vema kwako wewe kuonea, na kuidharau kazi ya mikono yako, na kuyaangazia mashauri ya waovu?” (Ayubu 10:1-3) “Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhamlimu, lakini sisikiwi; naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, na kutia giza katika mapito yangu.”​—Ayubu 19:6-8.

Walakini, semi hizo zisimfanye mtu afikiri kwamba Ayubu aliacha kutumainia haki ya Mungu katika kushughulika kwake na wanadamu. Tofauti yake, yeye aliamini kabisa kwamba ingawa waovu walifanikiwa kwa muda mfupi huku wenye haki wakiteseka, mwishowe Mungu angerekebisha hali hiyo. Kwa habari ya “sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu,” Ayubu akatangaza hivi: “Watoto wake wakiongezeka ni kwa upanga; na wazao wake hawatashiba chakula. Hao watakaosalia kwake watazikwa katika kufa, wala wajane wake waliofiwa na waume hawataomboleza. Ajapokusanya fedha kama mavumbi, na kujifanyia mavazi kama udongo kwa wingi; humkini kuyatengeza, lakini wenye haki watayavaa, nao wasio na hatia watazigawanya hizo fedha.”​—Ayubu 27:13-17.

Ayubu hakukubaliana wakati wo wote na kuwaza kwa wenzake kwamba kuteseka ni ushuhuda hakika wa kutokuwa na kibali ya Mungu. Wala hakukubaliana na dokezo la Elifazi kwamba Mungu hawaamini watumishi wake, wa kimalaika au wa kibinadamu. (Ayubu 4:18, 19) Tofauti yake, Ayubu alisisitiza kwamba Mungu alikuwa anamfahamu yeye kuwa mtu mkamilifu na angetenda kwa ajili yake kwa kumkomboa kutokana na hali zenye msiba ambazo alikuwa ameingia ndani yake.​—Ayubu 16:18, 19; 19:23-27.

AKUBALI KUSAHIHISHWA

Hata hivyo, lilikuwa jambo la hakika kwamba Ayubu alikuwa amekuwa mwenye kuhangaikia haki yake mwenyewe kupita kiasi. Maandishi ya Kimaandiko yanasimulia kwamba “zikawaka hasira za huyo Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, katika jamaa ya Ramu, juu ya Ayubu, kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu.” (Ayubu 32:2) Elihu alimkaripia Ayubu, akitoa maoni yake kwamba “Mungu hatatenda mabaya, wala Mwenyezi hatapotosha hukumu.” (Ayubu 34:12) Akimfuata Elihu, Yehova mwenyewe “akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli.” (Ayubu 38:1) Wote wawili, Elihu na zaidi kabisa Yehova, walionyesha kwamba ushuhuda wa kazi ya mikono ya Mungu na kuongoza kwake uumbaji wote kunazidi sana kuwaza kwa wanadamu.

Kwa kushindwa na jambo hilo, Ayubu alikata shauri kwamba alizungumza pasipo kufahamu namna Mungu alivyokuwa akishughulika naye. “Tazama, mimi si kitu kabisa,” akasema Ayubu “nikujibu nini? mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu.” (Ayubu 40:4, 5) Baada ya Yehova kumhoji Ayubu juu ya hekima Yake isiyopimika inayoonekana katika wanyama walioumbwa, Ayubu alitamka hivi: “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona. Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu katika mavumbi na majivu.”​—Ayubu 42:2, 5, 6.

Kama zawadi ya uvumilivu wa Ayubu, Yehova alimrudishia afya yake, na kumbariki kwa mali aliyokuwa nayo mbeleni maradufu na kuyaongeza maisha yake kwa miaka mingine 140 zaidi. “Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.”​—Ayubu 42:10, 16, 17.

Ayubu ni mfano mzuri kwa waabudu wa Mungu leo. Alipatwa na mateso yenye kuumiza kwa sababu asizozijua wakati huo, hata hivyo akakataa kumwonea Mungu uchungu. Ingawa hakufahamu kwa nini alipaswa kutaabika, alikuja kutambua kwamba lo lote Mungu analoruhusu lazima liwe na kusudi lenye faida.

Je! hukubali kwamba kitabu cha Ayubu kinatoa mengi yenye ubora mwingi kwa waabudu wa Mungu leo? Sababu gani usichukue wakati ukisome chote mapema ikufaavyo?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki