Kutokuwamo Kwa Kikristo Vita ya Mungu Ikaribiapo
“Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa [Yehova] amemtuma kweli kweli.”—Yer. 28:9.
1. Ni kwa sababu gani maneno ya Yeremia 27:9 yanayopinga kupiga ramli yanalingana sana na jinsi hali ya ulimwengu ilivyo leo?
“LAKINI, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wala wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu, wanaowaambia, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli.” Maneno hayo ya zamani za kale katika siku za Milki ya Babeli yanapatana sana na namna hali ya ulimwengu ilivyo leo. Sababu gani hivyo? Kwa sababu ulimwengu bado unajaa wenye ndoto, waganga, wabashiri na wachawi. (Yer. 27:9) Makao makuu ya ulimwengu, kama vile Washington D.C., yana sifa mbaya sana kwa ajili ya wabashiri wake, nao wanasiasa wenye wasiwasi wanawaendea hawa. Kwa sababu hawa waganga, wabashiri, wachawi na wafasiri wa ndoto na watabiri wa mambo ya wakati ujao wanawashauri wakuu wa serikali, watu hao wenye kujishughulisha na mambo ya siri wanaweza kuwa na matokeo yenye maana sana katika siasa za ulimwengu. Hata hivyo, watu hao hawawi wakijiingiza moja kwa moja katika siasa.
2. Je! Biblia, kwa sababu ya kutabiri juu ya matukio ya ulimwengu, inajiingiza katika siasa, nalo ni jibu gani kwa ulizo hilo linalotolewa katika 1 Yohana 2:15-17?
2 Kuna kitabu cha zamani kinachowaonya wasomaji wake wajiepushe na kila namna ya mambo ya siri walakini kina matabiri mengi kuhusu matukio ya ulimwengu katika karne yetu ya 20. Kina mengi ya kusema juu ya siasa za wakati wetu. Lakini, kwa sababu ya hili, je! kitabu hiki kinajiingiza katika siasa za wakati wetu? Je! kitabu hiki kinawatia moyo wasomaji wake wajiingize katika siasa za wanadamu ili wawaingilie watawala wa kisiasa? Wale wanasiasa ambao wangetaka kukishtakia kitabu hicho, Biblia Takatifu, jambo hilo, twawajibu, Hapana! Katika kimojawapo cha vitabu vya mwisho vya Biblia, mtume Mkristo Yohana anaandika hivi:
“Msiwe mkipenda wala ulimwengu wala vitu vilivyomo katika ulimwengu. Mtu ye yote akipenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo katika yeye; kwa sababu kila kitu kilichomo katika ulimwengu—tamaa ya mwili na tamaa ya macho na kujionyesha kwa mtu mali yake—hakitokani na Baba, bali chatokana na ulimwengu. Tena, ulimwengu unapita na ndivyo na tamaa yake, lakini yeye anayefanya mapenzi ya Mungu anadumu milele.”—1 Yohana 2:15-17.
Kitabu cha mwisho kabisa cha Biblia, ambacho vilevile kiliandikwa na mtume uyu huyu Yohana, kinaeleza namna ulimwengu huu pamoja na siasa zake utapitilia mbali.
3. Viongozi wa kidini wanawahimiza Wakristo wawe na maoni gani juu ya siasa, nao wanawataja nani kama mifano ya Biblia kutegemeza madai yao?
3 Walakini, kuna viongozi wa kidini, hata mapapa, wazee wa kanisa na maaskofu wakuu, wanaotoa sababu za kupinga kutokuwamo kwa Kikristo na kusema kwamba ni wajibu wa kila Mkristo kushiriki katika siasa za ulimwengu huu. Kama mifano ya kuunga mkono msimamo wao, wanawataja manabii Waebrania, kama vile Yeremia mwana wa Hilkia wa karne ya saba kabla ya Wakati wa Kawaida wetu. Kwa kweli, maneno ya Yeremia 27:9, yaliyotajwa mwanzoni mwa makala hii, yalikuwa sehemu ya yale ambayo Yehova Mungu alimwambia Yeremia awaambie wajumbe waliotoka katika ufalme wa Edomu, Moabu, Amoni, Tiro na Sidoni. (Yer. 27:1-4) Hivyo, basi, kwa kuwa “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” katika Har–Magedoni inakaribia sasa kwa haraka sana, ebu na tuchunguze namna Yehova alivyomtumia Yeremia katika wakati huo wa zamani. Je! mfano wa Yeremia unawaruhusu Wakristo wa kweli wa leo wavunje kutokuwamo kwa Kikristo na kujiingiza katika siasa za ulimwengu za namna yo yote? Na tuchunguze.
4. Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Yehoyakimu, Yehova kupitia kwa Yeremia alisema angelifanya nini hekalu na Yerusalemu chini ya hali fulani?
4 Twaanza hadithi yetu katika mwaka 628 K.W.K., au miaka 21 kabla Yerusalemu haujaharibiwa na Wababeli. Huu ndio uliokuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Yohayakimu, mfalme wa tatu wa mwisho wa Yerusalemu. Katika mwaka wa nne baada ya hapo Yeremia alitoa unabii wake juu ya Mfalme Nebukadreza wa Babeli na juu ya “kikombe” cha Yehova ambacho kingenyweshwa zaidi ya wafalme 20 pamoja na falme kutia na Edomu, Moabu, Amoni, Tiro na Sidoni. (Yer. 25:1-3) Nabii huyo anatupa tarehe ya mambo hayo, akisema hivi:
“Mwanzo wa kumiliki kwake, Yehoyakinii mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa [Yehova], kusema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya [Yehova], useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya [Yehova]; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja. Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao. Nawe utawaambia, [Yehova] asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu, kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza; basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.”—Yer. 26:1-6.
5. Ni kwa sababu gani kwa kutoa ujumbe huo uliotangulia kutajwa, Yeremia hakuwa akichanganya ukuhani na siasa?
5 Yeremia alikuwa kuhani, na hata hivyo, kwa kutii amri hii ya kimungu, yeye hakuwa akichanganya ukuhani na siasa za kitaifa. Yeye alikuwa tu akitoa onyo kutoka kwa Yehova kwa faida ya taifa hilo. Yeye aliwaachia watawala wa kiserikali pamoja na raia zake wajibu wa kutii onyo hilo la kimungu. Yehova Mungu alikuwa na haki pamoja na wajibu wa kuonya ufalme wa Yuda kwa kuwa watu wake walikuwa katika agano la kitaifa pamoja naye akiwa Mungu wao. Katika Sheria yake aliyowapa kupitia kwa Musa alilionya taifa hilo juu ya matokeo ya kuvunja agano hili kati ya Mungu na wanadamu. Kwa hiyo nabii wa Mungu hakuwa akijaribu kuchanganya ukuhani na siasa, bali alikuwa tu akitoa onyo kwa watu hawa kutoka kwa Mungu ambaye walikuwa na agano pamoja naye. Wakiendelea kuvunja agano hili, hekalu lao huko Yerusalemu lingelipoteza sanduku la agano kama vile tu Shilo ulivyokuwa umelipoteza.
6. Jamii ya Yeremia haijiingizi katika siasa za Jumuiya ya Wakristo kwa sababu haikuagizwa na Yehova kufanya nini, na kuhusiana na jumuiya hiyo, jamii hiyo inatii maneno gani ya Yesu?
6 Yeremia hakuwa akiwawekea mfano viongozi wa kisasa wa dini za Jumuiya ya Wakristo wajiingize katika siasa za kitaifa. Leo wale wa jamii ya Yeremia wanajua kwamba hawana haki ya kujiingiza katika siasa za taifa lo lote au mwungano wo wote wa mataifa, hata yale mataifa ya Jumuiya ya Wakristo. Wanajua kwamba, yajapokuwapo madai yake, Jumuiya ya Wakristo haimo katika agano na Yehova. Yaweza kudai kuwa katika lile agano jipya lililopatanishwa na Yule aliye mkuu zaidi kuliko Musa, Yesu Kristo, walakini mambo ya hakika hufunua uongo wa dai hilo. Hivyo, wale wa jamii ya Yeremia wanajua kabisa kabisa kwamba hawajaagizwa na Yehova Mungu wayaongoze mataifa ya Jumuiya ya Wakristo au kushiriki katika siasa za mataifa kama hayo. Kutangazia Jumuiya ya Wakristo pamoja na mataifa yasiyo ya Kikristo onyo kwa uaminifu kutoka kwa Yehova si kushiriki katika siasa za kilimwengu. Wao hawapendi “wala ulimwengu wala vitu vilivyomo katika ulimwengu,” bali wanashikamana na maneno ya Yesu: “Wao si wa ulimwengu.” (Yohana 17:14, 16; 1 Yohana 2:15, NW) Wakishikamana sana na kutokuwamo wao wanajiepusha na mambo ya kila namna ya siasa.
TENDO LA KIDINI
7. Kulingana na Yeremia 26:12-15, Yeremia alisema nini alipokuwa akimaliza kujitetea kwake mbele ya mahakma ya Yerusalemu?
7 Wale makuhani wengine pamoja na wanaoitwa “manabii” walimpeleka Yeremia mbele ya baraza ya wakuu mahakimu na mbele ya watu mlangoni pa hekalu. Walimshitakia maneno ya kufitini serikali. “Mtu huyu amestahili kufa,” wakasema, “kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu.” (Yer. 26:7-11) Akimaliza kujitetea kwake, Yeremia aliiambia baraza ya hukumu ya Yerusalemu hivi: “Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia; itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wakaaji wake; kwa maana ni kweli [Yehova] amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia.”—Yer. 26:12-15.
8. Ni kwa njia gani viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo wametenda kuelekea jamii ya Yeremia sawa-sawa na vile “watukuzaji wa taifa” wa Yerusalemu walivyotenda?
8 Lo! namna walivyoionyesha roho ya utukuzo wa taifa hawa waliokuwa wakimtafutia Yeremia kifo! Ilipaswa kuichochea baraza hiyo, kama vile maombi kama ayo hayo ya kutukuza taifa katika baraza nyingine za hukumu yamefanya katika nyakati za karibuni. Ombi la Yehova wageuze njia zao hawakulijali. Hatia yao mbele Zake wakaiachilia, wakituliza dhamiri zao. Kumekuwako visa vinavyofanana na hicho vilivyohusu jamii ya Yeremia ya kisasa. Viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wametoa ombi kama hilo kwamba hatua ya haraka ichukuliwe. Wameongoza katika kufanya madai yenye ghasia kwamba jamii ya Yeremia iuawe, hivyo waache kuchomwa na dhamiri zao mbaya.
9. Kwa habari ya Yeremia, je! wakuu hao mahakimu walishindwa na mkazo wa kidini, nao walitaka kujiepushaje na msiba?
9 Kati ya wakuu walioshughulikia kumwokoa Yeremia kutokana na hukumu ya kifo alikuwa Ahikamu mwana wa Shafani. Wakuu hao hawakushindwa na mkazo wa kidini. Walitambua kwamba kwa kweli Yeremia alikuwa mnenaji wa Yehova. Wao hawakutaka Yehova awahukumu kuwa na hatia ya kumwaga damu isiyo na hatia ya mtumishi wake mwaminifu. Walitoa hukumu iliyompendelea Yeremia: Hana hatia! Kujitetea kwake kuliwaweka katika hali ya kuweza kufikiria mifano mingine iliyopata kutokea kweli kweli. Kwa mfano, walikuwa kama miaka 100 karibu na yale ambayo Mika alikuwa ametabiri juu ya Yuda na Yerusalemu. Mfalme Hezekia alijiepusha na hatia ya damu kwa kutomhukumia Mika kifo kwa kutumia maneno yenye kufikiriwa kuwa ya kufitini na yenye kudhuru Serikali. Kwa hiyo, wazee wakatoa sababu za kushughulikia kesi ya Yeremia kwa uangalifu, wakisema: “Na sisi tungetenda mabaya makuu juu ya [nafsi] zetu.”—Yer. 26:16-19, 24; Mik. 3:9-12.
10. Mwenendo wa Mfalme Yehoyakimu kuhusiana na Urija ulitofautianaje na ule wa Mfalme Hezekia?
10 Tofauti na Mfalme Hezekia aliyetii onyo la Yehova kupitia kwa Mika alikuwako huyu kining’ina (mwana wa kizazi cha nne) wa Hezekia ambaye wakati huo alikuwa katika mwaka wake wa kwanza katika kiti cha enzi cha Yerusalemu, Yehoyakimu mwenyewe! Alimwaga damu mwaka wa kwanza wa utawala wake kwa kumwua Urija mwana wa Shemaya. Ili ajiokoe na hasira ya Mfalme Yehoyakimu, nabii Urija alikuwa amekimbilia Misri. Walakini, bila ya mapatano yo yote pamoja na Misri ya kumrudisha Urija, mfalme huyo mwenye kutaka kisasi alituma wanaume wakamwinde Urija na kumrudisha kwa nguvu mpaka nchi ya Yuda afie imani yake. (Yer. 26:20-23) Hivyo baadaye katika mwaka uo huo wa kwanza wa mfalme huyo mpya, Yeremia alikuwa na sababu zaidi ya kutabiri kama alivyotabiri, kwa amri ya Yehova. Kwa habari ya jambo hili inapaswa kuangaliwa kwamba Farao Neko ndiye aliyekuwa amemfanya Yehoyakimu mfalme juu ya Yuda. (2 Fal. 23:34, 35) Hivyo inawezekana Farao Neko alishirikiana na Mfalme Yehoyakimu katika kitendo hicho cha kuihalifu sheria.
11. Hivyo Yehoyakimu alijiletea msiba gani?
11 Yehoyakimu alijiletea msiba yeye mwenyewe. Katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, Mfalme Nebukadreza aliuzingira Yerusalemu akamfanya Yehoyakimu mfalme kibaraka kwa mamlaka mpya ya ulimwengu ya Babeli. Miaka mitatu baadaye Yehoyakimu alipatwa na kifo kisichotazamiwa. Maiti yake ilitupwa nje ya kuta za Yerusalemu apate “maziko ya punda.” Ilitukia kama vile Yeremia alivyokuwa ametabiri. (Yer. 22:18, 19; 2 Nya. 36:5-8; 2 Fal. 24:1-6) Vibaya kama nini!
12. Kama vile Yeremia wa zamani, jamii ya Yeremia, ya kisasa imeokolewaje na kifo mikononi mwa viongozi wa dini?
12 Kama vile Yeremia mwana wa Hilkia, jamii ya Yeremia ya karne yetu ya 20 imeokolewa na kifo. Si katika visa vyote, na si katika nchi zote baraza za hukumu zimekubaliana na madai yenye uchungu ya sehemu yenye nguvu ya dini za Jumuiya ya Wakristo. Kumekuwako mahakimu ambao wametambua haki na uhuru wa kidini wa jamii ya Yeremia, ambayo, inawakilisha hapa duniani, tengenezo la Yehova Mungu lililo kama mke. Kwa hiyo yaliyotukia yanafanana na yaliyofananishwa katika Ufunuo 12:15, 16. Sehemu ya “nchi” ya kidemokrasi yenye kupendwa na wengi iliwasaidia wajumbe wa “mwanamke” wa Mungu ikazuia jitihada za vibaraka wa kidini wa Shetani Ibilisi za kuimeza jamii ya Yeremia katika uharibifu wa milele.
13. Wale wa jamii ya Yeremia wanaendelea kutangaza nini, pasipo kukubali washindwe kuhusiana na swala gani?
13 Wale wa jamii ya Yeremia wanaendelea kutangaza yote ambayo Mungu anawaamuru watangazie mfano wa kisasa wa Yuda na Yerusalemu, pamoja na sehemu zote nyingine za kisiasa za hii taratibu ya mambo. Hata ingawa katika sehemu nyingine wanalazimika kwenda “chini-chini,” wao hawajaribu kupindua serikali zilizosimamishwa ili kulazimisha yale wanayosema yatimie. Wao wanapinga sana mikazo yo yote ya kuwafanya wakubaliane na chama hiki cha kisiasa au kile. Wanakataa kuachilia msimamo wao wa kutokuwamo kwa Kikristo.
14. Jamii ya Yeremia inatambua kwamba vita ni ya nani na baada ya vita hiyo, dunia itakuwa mahali pa namna gani pa kuishi?
14 Hivyo, bila kujiingiza katika mambo ya kisiasa, wanajiweka wenyewe pasipo kuwa “wa ulimwengu.” Wao wanajua vizuri sana kwamba Yehova Mungu Mwenye Nguvu Zote anaweza kujiangalia mwenyewe. Vita ni yake! Si juu yao kupigana! Wao wanasimama imara katika kutokuwamo kwa Kikristo, wakiwa na uhakika kwamba “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” imekaribia, kwa kuwa majeshi ya mashetani yasiyoonekana wakiwa na uwezo wao wa uaguzi yanawakusanya watawala wa kidunia kwenye hali ya ulimwengu iitwayo kwa mfano Har–Magedoni. (Ufu. 16:13-16) Kwa hiyo jamii ya Yeremia inafurahi kwa kuwa kutokuwamo kwao kwa Kikristo kusiko na woga kunaunga mkono enzi kuu ya ulimwengu wote ya Yehova. Lo! jinsi dunia itakavyokuwa mahali pazuri kwa jamii ya Yeremia na Wakristo wenzao wasiokuwamo watakapokuwa wamekwisha shuhudia ushindi wa enzi kuu ya Yehova katika Har–Magedoni!
MPANGO WA HILA JUU YA MTUMISHI-MFALME WA YEHOVA
15. Ni kwa sababu gani huu ndio wakati wa mpango wa hila wa mataifa yote ulio mkubwa zaidi katika historia yote ya wanadamu, nao Ufunuo 14:12 wasema hiyo itamaanisha nini kwa Wakristo wenye kuwogopa Mungu?
15 Hata hivyo, huu ndio wakati wa kujaribiwa kwa Wakristo kama wale wa Biblia kwa habari ya kutokuwamo na ukamilifu wao. Huu ndio wakati wa mpango wa hila wa mataifa yote ulio mkubwa zaidi katika historia yote ya kibinadamu, kwa kuwa sasa ndio wakati wa Umoja wa Mataifa, ambao leo una washiriki 151. Sababu gani kuuita Umoja wa Mataifa mpango wa hila wa mataifa yote? Kwa sababu ni tengenezo la wanadamu la kutenda kinyume cha utawala wa ufalme wa Yehova kupitia kwa Kristo, na kuuzuia kwa muda mrefu iwezekanavyo. Ni nani atakayeshinda? Ufalme wa Yehova wa kimasihi au Umoja wa Mataifa? Usalama na amani ya watu wote vinahusika. Ukitabiri namna kipindi cha kuwapo kwa Umoja wa Mataifa ukiwa chombo cha kulinda ulimwengu kingekuwa chenye kujaribu, Ufunuo 14:12 wasema hivi: “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.”—Linganisha Isaya 8:12, 13.
16. Ni mpango gani wa hila uliokuwako karne 19 zilizopita, nao utimizo wake mdogo wa Zaburi 2:1-4 ulielekeza mbele kwenye nini?
16 Karne 19 zilizopita kulikuwako mpango wa hila au jitihada za pamoja za mataifa yote kumpinga Kristo mwenyewe, Mungu akaruhusu jambo hili ili Yesu apate kufia imani. (Matendo 3:13; 4:27; 13:28, 29; 1 Tim. 6:13) Jambo hili lilikuwa limetabiriwa katika Zaburi 2:1-4. Zaburi hii pamoja na utimizo wake mdogo karne 19 zilizopita ilikuwa ikionyesha mbele kwenye mpango wa hila wa mataifa yote juu ya Yehova na Kristo wake katika wakati huu wakati ambapo haki kamili ya “ufalme wa dunia” ni yao wote wawili.—Ufu. 11:15-18.
17. Mashahidi wa Yehova wanatambua kwamba tengenezo la ulimwengu lililopo linatenda kinyume cha nani, nao leo wanashikamana na msimamo gani uliochukuliwa katika mwaka 1919?
17 Wakristo wa kweli watatambua kwamba mpango wa hila uliopo unampinga Yehova na Kristo wake. Kwa hiyo wataendelea kuvumilia katika kutokuwamo kwao kama kule kwa Kristo, wakishikilia msimamo wao waliochukua huko nyuma katika mwaka 1919 katika kusanyiko la Intemational Bible Students Association huko Cedar Point, Ohio, (U.S.A.), kuutetea ufalme wa Yehova kupitia kwa Kristo kuliko Ushirika wa Mataifa uliokusudiwa, na ambao sasa mahali pake pamechukuliwa na Umoja wa Mataifa, tengenezo la amani na usalama wa ulimwengu. Yeremia angechukua msimamo kama wao leo, kwa kuwa yeye alitoa onyo lililoongozwa na Mungu kuhusu mpango wa hila kama huo juu ya “mtumishi” wa Yehova wa kifalme.
18. Ni nini Yeremia aliambiwa ajifanyie katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Yehoyakimu, naye angezipeleka kwa nani pamoja na ujumbe?
18 Hivyo, unabii wa Yeremia, sura ya 27, una maana ya kisasa kwetu sisi. Humo maandishi ya nabii huyo yasema hivi:
“Mwanzo wa kumiliki kwake Yoyakimu, mwana wa Yosia, mufalme wa Yuda [katika mwaka 628 K.W.K.], neno hili likakuja kwa Yeremia, kutoka kwa [Yehova], kusema: [Yehova] ameniambia hivi: Ujifanyie vifungo na kongwa, uzitie juu ya shingo yako; kisha uzipeleke kwa mufalme wa Edomu, na mufalme wa Moabu, na mufalme wa wana wa Amoni, na mufalme wa Tiro, na mufalme wa Sidoni, kwa mikono ya wajumbe watakaofika Yerusalemu kwa Zedekia, mufalme wa Yuda. Uwaagize waende kwa bwana zao, na kuwaambia: [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Mutawaambia bwana zenu maneno haya.”—Yer. 27:1-4, ZSB.
19. Kulingana na andiko la kawaida la Kiebrania, Yeremia alipokea ujumbe kutoka kwa Yehova mwaka gani, naye alichukua hatua juu yake wakati gani?
19 Twaona kwamba hapa wafalme wawili wanatajwa kuwa wakitawala juu ya Yuda na Yerusalemu, kwanza Yehoyakimu, kisha ndugu yake Zedekia, ambaye alitawala baada ya Yehoyakimu na mwanawe Yehoyakini. Ikiwa jina Yehoyakimu ni sahihi katika Yeremia 27:1, basi Yeremia alipata unabii huu katika mwaka 628 K.W.K. akauweka kwa miaka 11 kabla ya kutenda juu yake. Walakini hati tatu za Kiebrania pamoja na tafsiri ya Kishamu na ya kiarabu ya Yeremia 27:1 husema “Zedekia” mahali pa “Yoyakimu,” na hivi ndivyo tafsiri nyingi za kisasa za Biblia huonyesha mambo kuwa.a Kwa vyo vyote, inaonyeshwa kwamba Yeremia alichukua hatua katika kutii amri ya Yehova katika wakati wa utawala wa Mfalme Sedekia wakati ambapo wajumbe kutoka nchi tano jirani, Edomu, Moabu,! Amoni, Tiro, na Sidoni, walipokuja Yerusalemu kushughulika na Mfalme Sedekia. Kufikia wakati huu Nebukadreza alikuwa amekuwa mfalme wa Babeli angaa miaka minane naye alikuwa amekwisha kumhamisha Mfalme Yehoyakini mpaka Babeli na kuweka amu wake Sedekia juu ya kiti cha enzi cha Yerusalemu. Akiwa mfalme kibaraka, ilimpasa Sedekia kuitii Babeli.
20. Kuja kwa wajumbe hao watano kulifananisha tendo gani, na ni kwa sababu gani wakaambiwa wasisikilize maneno ya wenye kupiga ramli?
20 Kuja kwa wajumbe kutoka katika nchi tano jirani lilikuwa tendo lililopangwa pamoja. Ulikuwa mwendo wa kupatana kufanya shauri pamoja. Kutokana na yale ambayo Yeremia aliambiwa awaambie wajumbe hawa, ni wazi kwamba kulikuwako mpango wa hila wa kutokeza uasi wa mwungano juu ya Mfalme Nebukadreza. Wenye kubashiri na wapiga ramli walipendelea uasi huo. Ndiyo sababu; Yeremia aliambiwa awaambie wajumbe hao hivi: “Lakini, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu, wanaowaambia, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli; maana wanawatabiria uongo, ili kuwatoa ninyi mbali na nchi yenu; niwafukuze mkaangamie.”—Yer. 27:9, 10.
21. Huko nyuma, mashetani yalikuwa yakiyahimiza mataifa yaliyohusika yafanye nini?
21 Kama vile leo mashetani wanavyowaongoza watawala wa kisiasa kwenye Har–Magedoni, kwenye“vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi,” ndivyo huko nyuma mashetani ao hao walivyokuwa wakiwahimiza watawala wa kisiasa wa nchi ambamo kutoka hizo wajumbe walitoka wakaja kubuni uasi wa mwungano juu ya “mtumishi” wa Yehova, Nebukadreza. (Ufu. 16:13-16) Ni jambo linalopatana na akili kwamba, mataifa hayo hawakupinga wakati Mfalme Sedekia wa Yuda alipoasi katika mwaka wa tisa wa utawala wake.
22. Wakati Yeremia alipowapelekea wajumbe hao ujumbe kutoka kwa Yehova, ni kwa sababu gani Yeremia hakuwa akijiingiza katika siasa, naye Yehova alikaziaje enzi yake kuu katika ujumbe huo?
22 Wakati Yeremia alipopeleka ujumbe kutoka kwa Yehova kwa wajumbe hao waliotoka katika mwungano huo wa mataifa matano, yeye hakuwa akijiingiza katika siasa, kwa kuwa Mungu wake, Yehova, alikuwa “mfalme wa mataifa” naye alikuwa akiyafanyia mataifa hayo jambo jema kwa kuwapa onyo lililokuwa la maana sana kwa taifa zima. Akikazia juu ya enzi yake kuu ya ulimwengu wote, Yehova alimwambia Yeremia awaambie hivi:
“Mimi nimeiumba dunia hii, wanadamu na wanyama walio juu ya uso wa nchi, kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulionyoshwa; nami nawapa watu kama inipendezavyo. Na sasa nimetia nchi hizo zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie. Na mataifa yote watamtumikia, yeye, na mwanawe [Evil-merodaki], na mwana wa mwanawe [Belshaza], hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye.”—Yer. 27:5-7; 2 Fal. 25:27; Dan. 5:1, 11, 18, 22.
23. Utumwa kwa Babeli ungekuwa wa urefu gani, nalo ni jambo gani ambalo lingelipata taifa lo lote ambalo lingepinga amri ya Yehova?
23 Kwa hiyo, kulingana na amri ya Yehova, ungekuwa muda mrefu—kwa kweli, miaka 70—wakati ambapo mataifa ambayo yangekuwa chini ya Milki ya Babeli yangeichukua nira ya utumwa. Utumwa huo ulifananishwa na vifungo na nira ambazo Yehova alimwambia Yeremia ajifanyie na kuwapa wajumbe wa nchi za kigeni waliotembelea Mfalme Sedekia. Uasi wa mataifa hayo haungevunja amri ya Mungu:
“Na itakuwa, taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadreza, huyo mfalme wa Babeli, . . . mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema [Yehova], hata nitakapokuwa nimewaangamiza kwa mkono wake.”—Yer. 27:8.
24. Ni kwa sababu gani lazima Mtumishi-Mfalme wa Yehova, Yesu Kristo, atawale sasa katikati ya adui zake?
24 Leo, wakati wa jamii ya Yeremia, na vilevile huko nyuma katika wakati wa Mfalme Sedekia, lingekuwa jambo bora zaidi kutii shauri la Bwana Mwenye Enzi Kuu wa ulimwengu wote mahali pa kuyatii mashetani. (Yer. 27:9-11) Bila shaka sisi hatutaki kutegwa katika mpango wa hila wa mataifa yote juu ya Mtumishi-Mfalme wa Yehova, Yesu Kristo. Watawala wa kisiasa, sana sana wale wa Jumuiya ya Wakristo, wamepashwa habari kwa kutangaziwa mara nyingi na jamii ya Yeremia, walakini watawala hao wanapendelea kukaa katika Umoja wa Mataifa. (Yer. 27:12-15; Ufu. 17:12, 13) Wanashikilia sana enzi kuu zao za kitaifa na kukataa kabisa kutia shingo zao chini ya nira ya kifalme ya Mtumishi-Mfalme wa Yehova. Kwa kuwa hawauoni kwa uzito mwisho wa Majira ya Mataifa katika mwaka 1914, watawala wa kisiasa hawakubali kwamba wanafanya mpango wa hila wa duniani pote juu ya utawala wa duniani pote wa Mtumishi-Mfalme wa Yehova. Walakini, kama vile Sedekia alivyoruhusiwa awe mfalme juu ya Yuda na “mtumishi” wa Yehova, Nebukadreza, ndivyo ilivyo sasa kwa habari ya watawala wa kisiasa, kutia na wale wa Jumuiya ya Wakristo. Wameruhusiwa waendelee kuongoza mambo ya kisiasa tangu mwaka 1914. Hivyo, Mtumishi-Mfalme wa Yehova lazima sasa atawale katikati ya adui zake, wale wanaopanga hila juu yake.
25. (a) Kwa sababu ya watawala kukataa kutii, lazima sasa jamii ya Yeremia iwaendee nani na ujumbe? (b) Ikiwa manabii wale waliokuwa wakitabiri juu ya faraja ya mapema walitoka kwa Yehova, waliambiwa waombe nini kuhusu vyombo vilivyokuwa vimesalia?
25 Kwa kuwa watawala wa kisiasa wanaonyesha kwamba hawatatia shingo zao chini ya “nira” ya Mtumishi wa Yehova, Mwanawe aliyeketishwa juu ya kiti cha enzi mbinguni, jamii ya Yeremia yapaswa ifanye nini? Wawaendee watu, mmoja mmoja. Lazima jamii ya Yeremia iwafunulie watu, wale watu wanaofanya mpango wa hila.
“Msisikilize maneno ya manabii wenu, wanaowatabiria, wakisema, Tazameni, vyombo vya nyumba ya [Yehova], baada ya muda kidogo, vitaletwa tena toka Babeli; maana wanawatabiria uongo. Msiwasikilize; mtumikieni mfalme wa Babeli, mkaishi; kwani mji huu kufanywa ukiwa? Lakini ikiwa hao ni manabii, ikiwa neno la [Yehova] liko kwao, basi na wamwombe [Yehova] wa majeshi, kwamba vyombo vile vilivyosalia Yerusalemu, visiende Babeli.”—Yer. 27:16-18.
26. Mahali pa vyombo hivyo kurudishwa mapema, ni jambo gani lingevipata vyombo vilivyosalia, kulingana na usemi wa Yehova?
26 Katika Yerusalemu bado hekalu pamoja na nguzo zake lilikuwa linasimama. Uani mwake lile bakuli kubwa la kuogea lililoitwa “bahari” lilikuwapo pamoja na mabakuli mengine madogo madogo na vyombo vingine vingi vilivyokuwa vikitumiwa na makuhani na Walawi. Namna gani juu ya vyombo hivi vyote vya hekalu?
“[Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za vyombo vilivyobaki katika nyumba ya [Yehova], na katika nyumba ya mfalme wa Yuda, na hapa Yerusalemu; Vitachukuliwa mpaka Babeli, navyo vitakaa huko, hata siku ile nitakapovijilia, asema [Yehova] hapo ndipo nitakapovileta tena, na kuvirudisha mahali hapa.”—Yer. 27:19-22.
27. (a) Usemi wa Yehova ulimaanisha nini kuhusia na ule mpango wa hila wa mataifa yote? (b) Kwa hiyo ni mwendo gani utatuwezesha kushiriki katika matunda ya ushindi wa amiri-jeshi mkuu wa Yehova katika Taratibu Mpya?
27 Usemi huu wa Yehova ulikuwa na maana gani? Hii: Mpango wa hila wa mataifa yote juu ya utawala wa “mtumishi” wa Yehova ungeshindwa. Manabii hao wa kidini pamoja na wabashiri waliokuwa wakitabiri matukio lazima waonekane kuwa wa uongo, wakiwaongoza vibaya watu hao wenye kuamini uongo kwenye uharibifu. Kutokuwaamini kutamaanisha usalama wetu. Tumaini letu halipaswi kuwa katika Umoja wa Mataifa au tengenezo jingine lo lote la mataifa yote bali katika ufalme wa Yehova kupitia kwa Mtumishi-Mfalme wake mwenyewe, Yesu Kristo. Katika kushikamana na msimamo wetu wa kutokuwamo kwa Kikristo katika siasa na vita vya ulimwengu huu, tutatia shingo zetu chini ya nira ya yule ambaye amewekwa na Yehova, yule anayeungwa mkono naye akiwa amiri-jeshi mkuu wake katika “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” inayokuja katika Har–Magedoni. Jambo hili litatuwezesha kushiriki katika matunda ya ushindi wake wenye utukufu katika taratibu mpya ya Yehova yenye haki.
[Maelezo ya Chini]
a Tazama tafsiri ya Union Version; Revised Standard Version; na Good News Bible.