Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w81 12/1 kur. 3-4
  • Unaweza Kuzuia Hasira Yako

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Unaweza Kuzuia Hasira Yako
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KUIZUIA HASIRA
  • Ninaweza Kuzuiaje Hasira Yangu?
    Amkeni!—2009
  • Jinsi ya Kudhibiti Hasira
    Amkeni!—2015
  • Kwa Nini Udhibiti Hasira Yako?
    Amkeni!—1997
  • Ninawezaje Kudhibiti Hasira Yangu?
    Vijana Huuliza
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
w81 12/1 kur. 3-4

Unaweza Kuzuia Hasira Yako

MWANAMUME mmoja alikuwa akiendelea na shughuli yake ya siku. Kwa ghafula, mpigo wake wa damu uliongezeka. Mboni za macho yake zikapanuka. Mkazo wake wa damu ukaongezeka. Sura yake ya usoni ikabadilika kisha akaanza kuhema-hema. Dawa-dawa za mwili wake zilianza kufanya kazi kwa njia yenye mabadiliko. Kulitukia nini? Je! alikuwa na kifafa? Hapana, mwanamume huyo alikuwa amekasirika tu.

Wakati watu wanapokasirika, badiliko la utu linatukia, kisha wanaelekea sana kupatwa na mambo yasiyopendeza. Kijana mmoja wa kike hatasahau hata siku moja wakati ule ambao yeye alishindwa kuzuia hasira yake. Wakati huo ulikuwa siku ya arusi yake. Alipokuwa akiondoka mahali palipokuwa na karamu akiwa na mume wake mgeni, alibishana naye juu ya jambo fulani. Halafu akaendesha gari akilipitisha juu yake na kumkanyaga, akamwua—msiba mkubwa looo kwa sababu ya kushindwa kujizuia.

Biblia, pia, inatoa habari za kwamba dhambi nyingi zimetokana na kukasirika. Kumbuka, Kaini “aliwaka kwa hasira kubwa” akamwua Habili, ndugu yake mdogo. Halafu alikuwako Mfalme Herode mwovu ambaye “alighadhabika sana” akaagiza vivulana vichanga viuawe katika Bethlehemu na ujirani wa mji huo.​—Mwa. 4:5-8, NW; 2:16-18.

Kwa hiyo, “mishtuko ya ghafula ya hasira” imepangwa ndani ya Biblia kama ‘kazi ya mwili,’ ambayo lazima Wakristo wajitahidi sana kuishinda. (Gal. 5:19, 20, NW) Kiasi ambacho tunaweza kuzuia hasira yetu kinaonyesha kidogo kadiri ya maendeleo tuliyo nayo kama Wakristo. Ndiyo sababu wanaume wanaotatizwa sana katika upande huu hawatumiwi kama wazee katika kundi la Kikristo.​—Tito 1:7.

Basi, je! haimpasi kamwe Mkristo kujisikia akiwa na hasira? Biblia inatuambia kwamba nyakati nyingine Yehova anakasirika. (Zab. 110:5) Yesu alikasirika au akaudhika sana kwa sababu ya kufa ganzi kwa Mafarisayo na ukosefu wao wa kuonyesha huruma. (Marko 3:4-6) Kwa hiyo, huenda Mkristo akajisikia amekasirika ikiwa, kwa mfano, anaona jina la Yehova likiletewa sifa mbaya au mwanadamu mwenzake akitendwa kwa ukatili. Lakini yeye anashauriwa hivi: “Mwe na hasira, ila msitende dhambi.” (Efe. 4:26) Wakati hasira inapoendelea bila kuzuiwa, halafu mtu anashindwa kujiweza, ndipo dhambi inapoelekea kutokea.

Kumbuka kisa cha Simeoni na Lawi, wana wa Yakobo mzee wa ukoo. Dina dada yao aliingiliwa kwa nguvu na mwanamume kijana jina lake Shekemu wa mji wa karibu. Je! hiyo ilikuwa sababu nzuri ya kuwa na hasira? Hakika. Lakini hatua iliyochukuliwa na ndugu zake ilipita kiasi. Wao waliwaua wanaume wote katika mji huo, kutia ndani na Shekemu.​—Mwa. sura ya 34.

Hiyo inaonyesha jambo la maana. Mara nyingi kunakuwa na sababu halisi ya kumchochea mtu akasirike. Lakini kushindwa kujiweza kunaweza kumwongoza mtu aseme maneno na kufanya matendo anayokuja kujutia baadaye. Tena hakuwi na tatizo moja bali mawili: kule kuudhika kwa kwanza halafu tendo lenye hasira linalofuata. Mara nyingi inakuwa kwamba kule kuhamaki kwa hasira ndiko mtu anakokumbuka kwa muda mrefu kuliko kuudhiwa kulikomfanya awe na hasira. Katika kisa cha Simeoni na Lawi, wewe unafikiri ni jambo gani lililokumbukwa zaidi na wakaaji wa majimbo hayo—ni kule kuingiliwa kwa nguvu kwa Dina, au ni kuuawa kwa wanaume wote wa mji huo?

Kwa upande mwingine, kuzuia hasira, hata mtu anapochochewa kukasirika, kunaweza kutokeza mambo mazuri. Kwa mfano, mwanamke fulani Mkristo alikuwa mke wa mtu asiyeamini aliyekuwa mcheza kamari. Mume huyu aliponda pesa nyingi za jamaa kwa kucheza kamari. Siku moja akamwambia mkewe kwamba anakwenda akauze samaki. Wakati alipokaa bila kurudi kwa muda fulani, mkewe alikwenda kumtafuta, akamkuta, si akiuza samaki, bali akiwa katikati ya mchezo wenye makelele mengi wa kamari ya ki-China uitwao MahJongg. Weee, acha jambo hilo lichochee hasira! Hata hivyo yeye hakumgombeza mumewe mbele ya rafiki zake. Halafu mwishowe mume alipofika nyumbani, mke wake alimweleza kwa utulivu tu matatizo ambayo jamaa ilikuwa ikipata kutokana na mchezo wake mbaya. Mume alivutwa na mfano huo wa “roho ya upole na utulivu.” Aliuacha mchezo wake wa kamari na mwishowe akawa Mkristo.​—1 Pet. 3:1-4.

KUIZUIA HASIRA

Wakristo wanashauriwa hivi: “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu.” (Efe. 4:31) Ni kweli kwamba watu wanatofautiana. Wengine ni watulivu sana, na wengine wamezaliwa wakiwa watu wa hasira kali-kali. Hata hivyo, watu wengi ambao wanaonekana kuwa watulivu wanaweza kueleza kwamba wakati mmoja wao pia walipatwa na tatizo la kujiweza. Walakini, walilitatua kwa kufuata mashauri mazuri ya Maandiko, kama yale yaliyo kwenye Zaburi 4:4; Mithali 15:1 na 22:24; na Warumi 12:18.

Katika habari hii, ni vizuri kukumbuka jinsi sifa ya upendo inavyoweza kutusaidia. Hakuna mtu anayependa awe ndiye wa kuonyeshwa “ghadhabu na hasira na kelele.” (Efe. 4:31) Kwa hiyo, ikiwa kweli ‘tunampenda jirani yetu kama nafsi yetu,’ hatutataka kuwatenda wenzetu mambo hayo. (Mt. 22:39) Mzazi mwenye kushindwa kuzuia hasira anaweza kumshtua sana mtoto mdogo. Mzee wa Kikristo aliyewekwa mwenye kufanya ivyo hivyo anaweza kufanya matokeo ya kazi yake nzuri kundini yawe ya bure. Huenda mtu akasema: ‘Ah, hiyo ndiyo hali yangu. Sina la kufanya.’ Lakini Biblia inasema: “Upendo . . . huvumilia mambo yote. Upendo haushindwi kamwe.” (1 Kor. 13:4-8, NW) Upendo mwingi sana kwa wenzetu utatusukuma tujitahidi kuondoa maelekeo yo yote ya kuwa na hasira kali-kali.

Jambo la mwisho, tena la maana sana, Wakristo wanaweza kuomba Mungu awasaidie kupitia roho takatifu yake. Sifa kama upendo, amani, ustahimilivu na upole—ambazo zinatusaidia tuweze kuuondoa ukosefu wetu wa kujiweza—ni matunda ya ile roho. (Gal. 5:22-24, NW) Kwa hiyo ikiwa wewe binafsi una tatizo la kuwa na hasira mbaya, mbona usimsihi sana Yehova Mungu akusaidie? Mwombe roho yake ikutie nguvu uzuie maoni yako ya moyoni. Kwa msaada wa Yehova, unaweza kufaulu!

Naam, lazima tuepuke kuwa ‘wepesi wa kukasirika,’ kwa kuwa “hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.” (Yak. 1:19, 20) Hasira mbaya inaweza kutufanya tuonekane kuwa watu wa upuzi, inaweza kuharibu uhusiano wetu na wengine na inaweza kuonyesha hatuna upendo. Kwa sababu ya kuacha kujiweza wakati mmoja, Musa hakuruhusiwa kuiingia Nchi ya Ahadi. (Hes. 20:9-13) Usiruhusu ukosefu wa kujiweza ukuharibie baraka zako. Bali, sikuzote yakumbuke maneno ya Mfalme Daudi: “Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Maana watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojao [Yehova] ndio watakaoirithi nchi.”​—Zab. 37:8, 9.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki