Neno la Mungu Li Hai
Mungu Anatumia Watu wa Cheo Kidogo
MAKAO ya Amosi ni katika Tekoa, mji ambao uko kilomita 16 kuelekea upande wa kusini wa Yerusalemu. Upande wa mashariki kuna jangwa la Yuda, lenye vilima mviringo visivyozaa kitu ambavyo vimekatwa-katwa kwa mabonde, na magenge. Wakati wa majira ya mvua, eneo hilo linazalisha majani machache. Hapa ndipo Amosi anafanya kazi yake ya mchungaji wa kondoo wa cheo kidogo. Vilevile anafanya kazi ya pindi kwa pindi akiwa mtunzaji-mikuyu, kuchuna au kuchoma-choma matunda hayo ili kuharakisha kuiva kwayo na kuzidisha ukubwa na utamu wayo.—Amosi 1:1; 7:14, 15.
Akiwa bado anafanya kazi yake ya uchungaji, Amosi anaitwa akatumike akiwa nabii wa Yehova. Akiongozwa na roho ya Mungu, yeye anaelekea upande wa kaskazini na kuingia katika eneo la ule ufalme wa makabila 10 wa Israeli. Kwa ujasiri, Amosi anatangaza ujumbe wa kuhukumiwa maangamizi kwa nyumba ya kifalme ya Yeroboamu, mwana wa Yoashi, na pia anatabiri juu ya kuhamishwa kwa Israeli.—Amosi 6:7; 7:9, 11.
Huko Betheli, makao ya ibada ya ndama, utabiri wa Amosi unamhangaisha sana kuhani Amazia mwenye kuabudu sanamu. Akitaka kumwogopesha nabii wa Yehova, yeye anamwambia hivi: “Ewe mwona, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme.”—Amosi 7:12, 13.
Akitiwa ujasiri na roho ya Mungu, Amosi anasimama imara. “Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii”; ndivyo anavyosema, “bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye [Yehova] akanitwaa; katika kufuatana na kundi; [Yehova] akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.” Kisha anamtangazia Amazia hukumu itakayompata kwa ajili ya kuupinga ujumbe wa Mungu: “Mke wako atakuwa kahaba mjini [aingiliwe na askari wa majeshi yenye kushambulia] na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba [na wale watakaokuja kuiteka nchi hiyo]; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi [nje ya nchi ya Israeli].”—Amosi 7:14-17.
Kuchaguliwa kwa Amosi awe nabii wa Yehova katika karne ya tisa K.W.K. kunaonyesha kwa mkazo kwamba Mweza Yote hategemei wenye hekima wa ulimwengu ili kuitimiza kazi yake. Hata leo kusudi la Mungu linatimizwa vizuri kwa kuwatumia wenye cheo kidogo ambao wana nia ya kuongozwa na roho yake. Nao wamekuwa bila woga kama nini katika kulitangaza jina lake na ufalme! Kwa njia hiyo wenye hekima wanaaibishwa. Kwa njia hiyo Yehova Mungu anathibitisha hekima yao haihitajiwi. Uwezo mbalimbali wanaojivunia unaonyeshwa kuwa haufai kitu.—1 Wakorintho 1:26-31.