Neno la Mungu Li Hai
Je! Unyofu wa Moyo Peke yake Utampendeza Mungu?
MAMBO mabaya sana yamefanywa katika jina la dini. Mwone Stefano hapa, mwanafunzi wa Yesu Kristo. Anauawa!
Wauaji wa Stefano ni watu wenye kufuata dini sana. Mmoja wao ni Saulo, ndiye yule-e-e akitunza mavazi yale. (Matendo 7:58-60) Yeye alisema hivi baadaye: “Nilikuwa nikifanya maendeleo mengi zaidi katika dini ya Kiyahudi kupita wengi wa umri wangu.” Hata hivyo, mahali pa kumfanya awe mtu mzuri zaidi, Saulo alisema kwamba dini yake ndiyo iliyokuwa na hatia ya hali yake ya “kutesa kundi la Mungu.”—Gal. 1:13, 14, NW.
Saulo aliwatesa Wakristo katika Yerusalemu kwa kuwavamia nyumbani mwao, na kuwaburuta nje na kuwaweka gerezani. (Matendo 8:3) Walakini hakuachia hapo. Vilevile alianza kwenda Damasko kuwakamata Wakristo huko.—Matendo 9:1, 2.
Hata hivyo, anapokuwa njiani, jambo lenye kutokeza sana linatokea. Kama unavyoweza kuona, mwangaza kutoka angani unamulika kumzunguka Saulo naye anaanguka kwenye ardhi. Sauti yasema hivi: “Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?”
“Ni nani wewe, Bwana?” Saulo anauliza.
“Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa,” ndilo jibu. (Matendo 9:3-5, HNWW) Yesu anasema hivyo kwa sababu Saulo anapowatesa wafuasi wa Yesu, Yesu anaona kama kwamba ni yeye anayeumizwa. Muda mfupi baadaye awa mshiriki wa kundi la Kikristo na, baada ya muda mfupi, anajulikana kuwa mtume Paulo.
Tunaweza kujifunza somo la maana katika hayo. Saulo alikuwa mnyofu moyoni, akiwa anaamini kwamba alikuwa akimpendeza Mungu kwa kuwatesa Wakristo. (Matendo 22:3, 4; Yohana 16:2) Walakini hilo halikufanya yale aliyokuwa akifanya yawe haki. Alihitaji kubadili dini ili apate kibali ya Mungu. Baadaye yeye aliandika juu ya wengine waliokuwa wanyofu moyoni, walakini ambao hawakuwa wakimpendeza Mungu. Tatizo lao lilikuwa nini?
Paulo anaeleza hivi: “Nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa [sahihi].” (Rum. 10:2) Ndiyo, pamoja na unyofu wa moyoni, maarifa sahihi ya Neno la Mungu yanahitajiwa. Iwapo mtu hajui kweli ya mambo, huenda akafanya mambo mabaya sana. Kwa hiyo ni jambo la maana kama nini tupate maarifa sahihi ya makusudi ya Mungu!—1 Tim. 1:13; Yohana 17:3.